Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Amirijeshi Mkuu:

Kuna watu wanajifanya kutoa maoni kuhusu uchaguzi wa Iran wakati watu hao hao wanafanya jinai kwenye jela ya Guantanamo

Leo asubuhi (Jumatatu) kumefanyika sherehe za kuhitimu mafunzo wanachuo wa Chuo Kikuu cha malezi na maafisa wa kijeshi cha cha Imam Hussein AS zilizohudhuriwa na Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amirijeshi Mkuu wa Vikosi Vyote vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sherehe hizo zimefanyika sambamba na siku za maadhimisho ya ukombozi wa Khorramshahr.

Wakati wa kuingia kwenye uwanja wa sherehe hizo, Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekwenda kwenye eneo walipozikwa mashahidi wa Iran wa vita vya kujihami kutakatifu na kuwasomea Faatiha pamoja na kuwakumbuka kwa wema na kuwaombea dua mashahidi wote wa vita vya kujihami kutakatifu.

Baada ya hapo Amirijeshi Mkuu wa Vikosi Vyote vya Ulinzi vya Iran amekagua vikosi vilivyokuwa vimepanga paredi kwenye uwanja huo.

Katika hotuba yake kwenye sherehe hizo, Ayatullahil Udhma Khamenei, ameitaja hatua kubwa ya hamasa na ya shauku kubwa ya taifa la Iran katika uchaguzi ujao wa Juni 14 kwamba inatoa bishara njema ya kupatikana mafanikio na matunda makubwa zaidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini.

Vile vile amewausia wananchi wa Iran kuwa makini sana katika kusikiliza matamshi, ahadi na kaulimbiu za wagombea wapendwa ili waweze kumjua na kumchagua mtu anayefaa zaidi kwa ajili ya kumpa jukumu la kuwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Vile vile Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amewausia kwa kusisitiza wagombea katika uchaguzi ujao wa Rais nchini Iran akiwataka wajiuepushe kikamilifu na kuchochea mizozo na wazingatie wajibu wa kuitia nguvu misingi na misimamo ya kimantiki na ya heshima ya Jamhuri ya Kiislamu.

Vile vile amewataka wajiepushe na kuchupa mipaka, kuwapaka matope watu wengine na tabia zisizo sahihi katika kampeni zao. Pia amesisitiza kuwa: Kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, kesho ya nchi na taifa hili ni kesho inayong’aa, yenye heshima na ambayo itakuwa ni kigezo chema kwa mataifa mengine ya dunia.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Sisi hatujui ni mgombea gani atachaguliwa kuwa Rais wa baadaye wa Iran na hatujui Mwenyezi Mungu Mtukufu atazielekeza nyoyo za wananchi upande wa mgombea gani lakini tunajua vizuri kwamba wananchi watajitokeza kwa wingi na kwa hamasa kubwa katika upigaji kura; kujitokeza ambako kutakuwa ni kutangaza uwepo wenye nguvu wa taifa la Iran katika medani ya harakati na kasi kubwa ya kuelekea kwenye kufanikisha malengo makuu.

Amesema: Bila ya shaka yoyote jambo hilo litaanda uwanja wa kushuhudiwa hadhi, kinga na heshima ya kimataifa kwa Iran na kwa taifa la nchi hii kama ambavyo pia jambo hilo litawafurahisha marafiki na kuwakasirisha maadui wa taifa hili.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameashiria pia propaganda za watu wanaolitakia mabaya taifa la Iran zenye lengo la kuwavunja moyo wananchi wa Iran ili kuwafanya wasishiriki kwa wingi kwenye zoezi hilo la uchaguzi na kuongeza kuwa, sababu ya kushuhudiwa propaganda hizo kubwa za maadui ni kuwa maadui hao wanatambua vyema kwamba, kama wananchi wa Iran watajitokeza vilivyo katika medani na kuonesha hamasa yao kubwa katika medani hiyo, basi jambo hilo litakuwa na madhara makubwa kwa maadui wa taifa hili.

Vile vile ameashiria matamshi ya viongozi wa Marekani kuhusu uchaguzi wa Iran na kuongeza kuwa: Kuna watu wanajifanya kutoa maoni yao kuhusu uchaguzi wa Iran wakati watu hao hao wanafanya jinai kwenye jela ya Guantanamo na ndege zao zisizo na rubani zinaendelea kufanya mauaji katika vijiji vya watu maskini na wanyonge huko Pakistan na Afghanistan.

Amesemema: Ni watu hao hao ambao wamezusha vita vingi katika eneo hili na kuuunga mkono kibubusa na kwa kila namna utawala wa Kizayuni ambao kila leo unatenda jinai kubwa dhidi ya binaadamu. Amesema vitendo hivyo vimewafedhehesha na kuwaaibisha watu hao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, matamshi ya ukosoaji yanayotolewa na watu hao dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ambao ni mfumo wenye heshima na fakhari kubwa, hayana hata thamani ya kujibiwa na wala hayawashughulishi wananchi na viongozi wa Iran.

Hata hivyo amesema, matamshi ya watu hao ni funzo kwa taifa la Iran kwani yanaonesha ni jinsi gani uchaguzi wa Iran ulivyo muhimu na nyeti sana kwao.

Ayatullahil Udhma Khamenei amekumbusha pia kuwa: Kambi ya maadui mara zote imekuwa ikizusha makelele mengi wakati unapofanyika uchaguzi nchini Iran katika kipindi chote hiki cha miaka 34 ya tangu kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini lakini mara zote njama zao zimeshindwa na kwamba kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mara hii pia taifa kubwa la Iran litatoa pigo jingine kubwa kwa maadui hao.

Aidha amewataka wananchi wa Iran kuwa macho, kuwa makini na kufanya tathimini vizuri kuhusu matamshiu, ahadi na misimamo ya wagombea wapendwa na kusisitiza kuwa: Wananchi wanapaswa kumpa nafasi kubwa zaidi mtu ambaye ataandaa uwanja wa kupatikana hadhi na heshimu katika mustakbali wa Mapinduzi ya Kiislamu na wa nchi ya Iran na ambaye ana uwezo wa kutatua matatizo yao na kusimama imara na kwa nguvu kubwa mbele ya kambi ya maadui na kuifanya Jamhuri ya Kiislamu kuwa kigezo kizuri cha kufuatwa na wanyonge duniani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia tofauti ya mitazamo ya wananchi kuhusu wagombea na kuongeza kuwa, tofauti hizo za mitazamo na mapenzi ya wananchi kuhusu wagombea inabidi ziwe za salama na zisije zikapelekea watu kugombana na kuzozana.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kuna njia nzuri na makini za kisheria nchini Iran kwa ajili ya kuchagua na kuteua mtu wa kushika nafasi ya juu ya utendaji (yaani serikali) na ambalo ni jukumu nyeti na muhimu sana, na kwamba sheria hizo ndizo zitakazotumika kufanikisha jambo hilo, hivyo tofauti za mitazamo hazipaswi kupewa nafasi ya kuzusha uadui kati ya watu.

Vile vile ametoa nasaha kadhaa kwa ajili ya wagombea kwenye uchaguzi wa Rais wa Iran unaotarajiwa kufanyika tarehe 14 mwezi ujao wa Juni akisema: Wagombea wapendwa nao wanapaswa kufanya kampeni zao kwa hamasa, shauku na ghera lakini wakati huo huo wajiepushe na ugomvi na mizozo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Hapa ndipo kinapoonekana kipaji na usanifu wa mambo yaani kuweko ushindaji mkubwa na hamasa na harakati na majadiliano moto moto wakati wa uchaguzi lakini wakati huo huo harakati hizo zichungwe vizuri zisije zikazusha mizozo na ugomvi.

Nasaha nyingine zilizotolewa na Ayatulla Udhma Khamenei kwa wagombea wa uchaguzi wa Rais wa Iran ni namna ya kufanya kampeni zao na matumizi na gharama zake.

Amesisitiza kuwa, wananchi watawapima wagombea hao kwa kuangalia kampeni zao za uchaguzi na namna walivyotumia fedha na kutochupa mipaka katika matumizi hayo na kwamba wagombea ambao katika kampeni zao watatumia fedha za Baytulmal (hazina ya nchi) au fedha zenye chembe chembe za haramu za baadhi ya watu, hawataweza kuwavutia wananchi na wala hawataweza kuwafanya wananchi wawape kura zao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Jambo lililo muhimu katika kampeni za uchaguzi na kaulimbiu pamoja na ilani za wagombea ni kuhakikisha kuwa kaulimbiu hizo zinaimarisha msimamo wa heshima, sahihi, wa hekima, busara na unaongilika akilini wa Mapinduzi ya Kiislamu na wa mfumo wa Kiislamu nchini Iran.

Ayatullahil Udhma Khamenei vile vile amesisitiza kuwa: Inabidi watu wachukue tahadhari kubwa ili Mungu apishie mbali, wasije wakatoa mwanya na fursa kwa maadui wa nje na hata wa ndani ya kutumia vibaya fursa hiyo, kwani adui anafanya njama ili kuwavunja moyo wananchi na kuwakatisha tamaa na kwa bahati mbaya kuna baadhi ya koo na ndimi na kalamu za watu wasiomuogopa Mwenyezi Mungu ndani ya Iran zinakariri na kutia nguvu matamshi ya maadui.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake aliyoitoa mbele ya wanachuo, wahadhiri na makamanda wa Chuo Kikuu cha maafisa wa kijeshi cha Imam Hussein Alayhis Salaam cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Amirijeshi Mkuu wa Vikosi Vyote vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia pia sifa bora na maalumu za wanachuo wa Chuo Kikuu hicho na kuongeza kuwa: Moja ya mambo ya lazima katika kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu, ni kuwa na ufahamu sahihi na wa kina kuhusu misingi ya kifikra na usuli za Mapinduzi ya Kiislamu na kushikamana vilivyo na misingi hiyo.

Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Katika kipindi chote hiki cha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wametokezea watu ambao waliingia kwenye medani bila ya kuwa na welewa wa kina kuhusu misingi ya kifikra ya Mapinduzi hayo na ndio maana baada ya watu hao kukumbwa na dhoruba fulani, walibadilisha njia na kutoka nje ya njia ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullahil Udhma Khamenei amelitaja jambo jingine la lazima kwa ajili ya kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu kwamba ni kuwa na ufahamu wa kina kuhusu historia ya mapinduzi hayo na kuongeza kuwa: Kwa hakika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ni misingi yake yenyewe ya kifikra na jinsi misingi hiyo ilivyopata uzoefu baada ya kushinda katika mitihani mbalimbali kwenye medani ya amali na vitendo.

Vile vile ameashiria jinsi vyombo vya habari vya maadui vinavyoshikilia na kung’ang’ania sana baadhi ya nukta dhaifu na ndogo ndogo na kuzikuza kwa makumi ya mara nukta hizo na ametahadharisha kuwa: Lengo la vyombo hivyo ni kujaribu kufifiliza na kusahaulisha uzoefu bora na wa mafanikio ambao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeupata na kujaribu kuonesha kuwa misingi ya kifikra ya Mapinduzi ya Kiislamu si sahihi katika upande wa utekelezaji wake, hivyo wananchi wote na hasa vijana wanapaswa kuhakikisha kuwa wana welewa na ufahamu wa kina na mkamilifu kuhusu historia ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Amirijeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Iran amesisitiza pia kuwa, moja ya majukumu muhimu ya viongozi na makamanda wa Chuo Kikuu cha Imam Hussein AS na vile vile wakuu na wahadhiri wa Vyuo Vikuu vingine vyote nchini Iran ni kuwaelimisha wanachuo historia ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameongeza kuwa, iwapo kizazi chipukizi na cha vijana kitakuwa na ufahamu sahihi na wa kina kuhusu historia ya mapinduzi ya Kiislamu, basi jambo hilo litaandaa uwanja mzuri kwa ajili ya mustakbali bora na wenye matumaini mazuri.

Vile vile amesema, tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi hivi sasa, hatua yoyote iliyochukuliwa na mapinduzi haya imekuwa na bishara njema kuhusu hatua ya baadaye na ni kwa sababu hiyo ndio maana Mapinduzi haya ya Kiislamu hayajawahi kukwama hata mara moja katika mambo yake na wala hayajawahi kutumbukia kwenye shimo la kukata tamaa na kupoteza matumaini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Siku zote faraja na njia ya harakati kuelekea kwenye malengo makuu na matukufu imekuwa wazi mbele yetu na iwapo itaonekana kwamba katika baadhi ya wakati hatukuweza kupata maendeleo yaliyotakiwa hiyo ilitokana na udhaifu na uvivu wetu wenyewe na wala jambo hilo halikutokana na kufungika njiambele yetu.

Katika sherehe hizo, Meja Jenerali Muhammadali Jafari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ameashiria jinsi jeshi hilo lilivyoongeza uwezo wake wa ulinzi na kutia nguvu uwezo wa ndani wa jeshi hilo kwa ajili ya kuonesha radiamali inayofaa na yenye taathira kubwa mbele ya kila aina ya vitisho vya adui na amesisitiza kuwa: Kuongeza umaanawi, kutia nguvu itikadi za kidini na maarifa ni miongoni mwa ratiba za usomeshaji na ufundishaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuna mfumo kamili na uliokusanya mambo mengi wa usomeshaji na malezi ambao unafanya kazi hivi sasa katika vituo vya mafunzo vya jeshi la Sepah.

Naye Admirali Morteza Safari, Kamanda wa Chuo Kikuu cha Imam Hussein AS ametoa ripoti kuhusu mipango na ratiba za kielimu, kimafunzo, kiutamaduni na za kijeshi za Chuo Kikuu hicho.

Aidha katika sherehe hizo majimui ya makamanda, wahadhiri, wakufunzi na wanachuo bora wa Chuo Kikuu cha Imam Hussein AS wamepokea zawadi kutoka kwa Amirijeshi Mkuu wa Vikosi Vyote vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullahil Udhma Khamenei ambapo mwakilishi wa wanachuo wa chuo hiyo naye amepata fakhari ya kupandishwa cheo.

Katika sherehe hizo pia wanachuo wa Chuo Kikuu cha Imam Hussein AS wameonesha kivitendo mpango maalumu wa kijeshi uliopewa jina la “Fastaqim kamaa umirta.”

Mazoezi ya kijeshi yaliyofanywa na wanachuo wa Chuo Kikuu cha Imam Hussein AS ilikuwa ni sehemu nyingine ya ratiba za sherehe hizo.

Mwishoni mwa sherehe hizo vikosi mbali mbali vya kijeshi vilivyokuwepo kwenye uwanja wa sherehe hizo vimepita kwa gwaride mbele ya Amirijeshi Mkuu wa Vikosi Vyote vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 

700 /