Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya mkusanyiko mkubwa wa wananchi katika Haram toharifu ya Imam Khomeini (MA):

Imani thabiti ya Imam Khomeini kwa Mwenyezi Mungu, kwa wananchi na kwake yeye mwenyewe iliandaa uwanja wa kupatikana ushindi na maendeleo ya kupigiwa mfano taifa la Iran

Idadi kubwa isiyo na kifani ya wananchi waumini na wanapinduzi kutoka kila pembe ya Iran, leo wamekutanika kwenye mkusanyiko adhimu na uliojaa hamasa katika Haram toharifu ya Imam Khomeini (MA) mjini Tehran na kwa mara nyingine kutangaza utiifu wao kwa kipenzi chao huyo aliyetangulia mbele ya Haki, Imam Khomeini (MA) ambaye ni kamba madhubuti ya umoja na utukufu wa taifa na viongozi wa Iran.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehutubia mkusanyiko huo mkubwa na kusema kuwa, imani ya Imam Khomeini kwa Mwenyezi Mungu, imani yake kwa wananchi na kujiamini kwake yeye mwenyewe binafsi kuliandaa uwanja wa kupatikana ushindi, kupiga hatua za kimaendeleo Mapinduzi ya Kiislamu na kuweza mapinduzi haya kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Aidha ametoa nasaha muhimu sana kuhusiana na uchaguzi wa unaotarajiwa kufanyika Juni 14 nchini Iran akiwahutubu wananchi na wagombea katika uchaguzi huo muhimu akisema: Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, siku kumi nyingine taifa la Iran litakwenda kujenga hamasa kubwa na litatoka kwa ufakhari mkubwa katika mtihani mkubwa wa Juni 14.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameitaja harakati ya kihistoria ya Khordad 15, 1342 (Hijria Shamsia, Juni 5, 1963 Milaadia) kwamba ilikuwa ni kipindi muhimu mno katika historia ya Iran na kuongeza kuwa: Baada ya kukamatwa Imam Khomeini (MA) na watawala wa wakati huo wa Iran hatua iliyochukuliwa na maafisa usalama wa utawala huo wa kidikteta baada ya Imam kutoka hotuba tarehe 3 Juni mwaka 1963, kulizuka harakati adhimu ya wananchi tarehe 5 Juni mwaka huo katika miji ya Tehran, Qum na katika miji mingine kadhaa ya Iran jambo ambalo lilionesha ni kiasi gani wananchi wa Iran walivyokuwa wameshikamana na wanavyuoni na maraji’i wa kidini dhidi ya utawala wa taghuti.

Kiongozi Muadhamu vile vile amesisitiza kwamba mshikamano madhubuti uliokuwepo baina ya wanavyuoni wa kidini na wananchi ulidhamini kufikia kileleni harakati zao na hatimaye kufanikisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Wakati wananchi wanapoingia kwenye medani, na hisia na fikra zao kutiwa nguvu na mwamko maalumu, basi harakati hiyo hupata uwezo wa kusonga mbele na hatimaye kupata ushindi.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameashiria pia jinsi sura ya ukatili na ukandamizaji mkubwa ya taghuti ilivyojitokeza wazi wazi katika tukio la Khordad 15, 1342 (Juni 5, 1963) na kuongeza kuwa: Moja ya nukta muhimu za tukio hilo ni jinsi jumuiya na taasisi za kimataifa zinazodai kutetea haki za binaadamu zilivyonyamazia kimya jinai hiyo na hakuna upinzani wala malalamiko yoyote yaliyosikika yakifanywa na taasisi na jumuiya hizo.

Vile vile amesisitiza kuwa: Licha ya kuweko masuala yote hayo, Imam Khomeini (MA) alisimama peke yake tab’an akiwa na uungaji mkono wa wananchi na kujitokeza katika historia na mbele ya watu wote akiwa kiongozi wa kidini na wa kiroho aliye na misimamo imara isiyotetereka.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria imani tatu muhimu alizokuwa nazo Imam Khomeini (MA) na kusisitiza kuwa: Imani kwa Mwenyezi Mungu, imani kwa wananchi na kujiamini yeye mwenyewe, imani zote hizo tatu alikuwa nazo Imam kwa maana halisi ya neno na zilionekana kwa uwazi katika misimamo ya Imam na harakati zake zote.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Imam Khomeini (MA) alizungumza na watu kwa udhati wa moyo wake na wananchi nao wakamuitika labeka kwa roho na nafsi zao na wakajitokeza katikati ya medani ya mapambano, wakapambana kiume katika medani hiyo na hivyo kuifanya harakati hiyo ianze pole pole kuelekea kwenye ushindi na hatimaye ikafanikiwa kupata ushindi kamili bila ya msaada wa nchi yoyote ile.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi kuhusu imani tatu kuu na muhimu mno alizokuwa nazo Imam Khomeini (MA) yaani imani kwa Mwenyezi Mungu, imani kwa wananchi na kujiamini yeye nafsi yake na kuongeza kuwa: Imam alikuwa akimwamini Mwenyezi Mungu kwa udhati wa moyo wake na alikuwa na yakini na kutimia ahadi za msaada wa Mwenyezi Mungu na ni kwa sababu hiyo ndio maana alifanya harakati na mambo yake yote kwa lengo moja tu la kumridhisha na kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.

Ameongeza kuwa: Imam aidha alikuwa akiwaamini na kuwategemea mno wananchi na ni kwa imani hiyo ndio maana wananchi waumini, werevu na mashujaa wa Iran wakathibitisha kivitendo kwamba kama watakuwa na kiongozi bora na mstahiki basi wanaweza kung’ara  mithili ya jua katika medani tofauti.

Ayatullahil Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, kwa mtazamo wa Imam, wananchi ni watu azizi zaidi na maadui ni watu wanaopaswa kuchukiwa zaidi na imani hiyo ni moja ya sababu kuu za kusimama kwake kidete Imam kukabiliana na mabeberu ambao walikuwa wanalifanyia uadui taifa na wananchi wa Iran.

Kiongozi Muadhamu ametoa ufafanuzi kuhusu sifa maalumu ya tatu ya Imam Khomeini (MA) yaani kujiamini yeye mwenyewe na kuimaini nafsi yake akisema: Imam alihuisha imani ya “Sisi tunaweza” katika moyo wa taifa la Iran na kupelekea kudhihiri na kujitokeza uwezo wa dhati wa taifa la Iran katika nyuga tofauti.

Vile vile ameashiria misimamo ya kishujaa ya Imam Khomeini (MA) katika kukabiliana na utawala wa kidikteta wa Kipahlavi wa nchini Iran, misimamo yake katika kipindi cha mapinduzi, misimamo yake wakati wa vita vya kujihami kutakatifu na katika kukabiliana na madhalimu na wakandamizaji duniani na kuongeza kuwa: Misimamo isiyotetereka na kujiamini ambako kulionekana wazi katika maneno na matendo na maamuzi ya Imam Khomeini pole pole ilianza kuonekana pia kwa wananchi na kulilibadilisha taifa hili kuwa kigezo cha istikama na muono wa mbali.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ilikuwa ni chini ya kivuli hicho cha kujiamini na ushujaa mkubwa aliokuwa nao ndio maana Imam hakuwahi hata mara moja kukumbwa na hisia za kukata tamaa na atiati hadi katika lahadha na sekunde za mwisho za uhai wake uliojaa baraka. Amesema, ushahidi wa hayo unaonekana zaidi pale tunapozingatia kwamba miongozo aliyokuwa akiitoa katika miaka ya mwisho ya uhai wake ilikuwa ni yenye nguvu zaidi na ya kimapinduzi zaidi kuliko hata misimamo yake ya katika miaka ya mwanzoni mwa harakati yake.

Aidha ametoa ufafanuzi kuhusu matunda ya imani ya taifa la Iran na kaulimbiu kuu ya Imam Khomeini yaani “Sisi tunaweza” na kuongeza kuwa: Taifa la Iran likiwa chini ya kivuli cha kujiamini, lilifanikiwa kuweka pembeni tabia na hisiza za kuvunjika moyo na kukata tamaa zilizokuwa zimelitawala taifa hili katika kipindi cha utawala wa Kifalme na mahala pake kuweka matumaini na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kufanikiwa kupata fakhari kubwa mbalimbali katika nyuga tofauti na kwa njia hiyo kuweza kuwa kigezo cha utukufu na maendeleo kwa mataifa mengine.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu baada ya hapo ametaja baadhi ya baraka zilizopatikana nchini Iran kutokana na sifa hizo tatu za Imam Khomeini (MA) chini ya kivuli cha kuwa na imani thabiti na Mwenyezi Mungu, kuwaamini wananchi na kujiamini yeye mwenyewe.

Ametaja baadhi ya baraka hizo kuwa ni pamoja na kuokoka taifa la Iran kutoka katika utegemezi duni na wa kudhalilishwa na Marekani na Uingereza, kupinduliwa viongozi mafisadi, wasaliti na mafuska nchini Iran na mahala pake kuchukuliwa na viongozi walioshikamana na dini na wanaochaguliwa kidemokrasia kwa kura za wananchi, kubadilika Iran kutoka nchi iliyobaki nyuma kimaendeleo na kuwa nchi yenye kasi kubwa ya maendeleo ya kielimu ambayo kasi yake hiyo ni mara 11 zaidi ya wastani wa kimataifa wa maendeleo pamoja na kupata Iran maendeleo ya kupigiwa mfano katika nyuga za ujenzi, za kielimu, tiba na elimu ya juu.

Hata hivyo Ayatullahil Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa maendeleo hayo ambayo taifa la Iran limeyapata katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, hayapaswi kupewa fursa ya kuwafanya watu waghururike na kukumbwa na majivuno bandia.

Amesisitiza kuwa: Kama sisi tutajilinganisha na Iran ya kipindi cha taghuti, tutaona kuwa hivi sasa tumepiga hatua kubwa za kimaendeleo, lakini wakati tunapojilinganisha na “Iran ya Kiislamu inayotakiwa” ambayo jamii yake ni jamii yenye heshima, ustawi wa hali ya juu, maadili bora, imani na umaanawi, tutaona kuwa bila ya shaka yoyote bado tuna safari ndefu ya kuweza kufikia kwenye Iran hiyo ya Kiislamu.

Vile vile amesisitiza kuwa: Njia hii ndefu lakini yenye fakhari nyingi tunaweza kuivuuka kwa kujipamba kwa sifa zile zile tatu alizokuwa nazo Imam Khomeini (MA), na kwamba kutokana na taifa la Iran kuwa na vijana waumini, na kwa kujipamba kwa sifa hizo tatu, tunao uwezo wa kufikia haraka kwenye vilele vya juu vya Iran ya Kiislamu inayotakiwa.

Kiongozi Muadhamu amesisitiza pia kwamba upeo ulio mbele ya taifa la Iran ni upeo uliojaa matumaini na kuongeza kuwa: Taifa la Iran tayari lina ramani ya njia ya kulifikisha huko, nayo ni ile ile misingi ya Imam Khomeini (MA).

Ayatullah Khamenei vile vile amesema: Misingi ya Imam inapatikana katika hotuba zake zilizochapishwa na zilizonudhumiwa na katika wasia wake na kwamba ni misingi hiyo ndiyo ambayo ililibadilisha taifa lililokuwa tegemezi la lililokuwa limebaki nyuma kimaendeleo la Iran kuwa taifa lenye maendeleo na fakhari kubwa, huru na lisilotegemea madola mengine.

Aidha amekumbushia nukta nyingine moja akisema: Watu ambao wanataja jina la Imam na ambao wanashikamana naye wanapaswa waiamini na kuiitakidi pia msingi wa “ramani ya njia” wa Imam kwani uhakika wa Imam unaweza kujulikana na kutekelezwa kwa kupitia misingi, usuli na ramani ya njia ya azizi huyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kubainisha misingi ya Imam kwenye nyuga tofauti kwa kuzungumzia misingi ya Imam Khomeini katika “Siasa za Ndani” na kusema: Kutegemea rai na kura za wananchi, kudhamini umoja na mshikamano wa taifa, kuzifanya siasa hizo kuwa za kidemokrasia na za maamuzi ya wananchi bila ya viongozi wake kuwa watu wa anasa, kushikamana viongozi na maslahi ya taifa na kufanya kazi kwa bidii na idili kubwa kwa ajili ya kuiletea maendeleo nchi ni miongoni mwa usuli na misingi ya Imam Khomeini (MA) katika upande wa siasa za ndani.

Amma kuhusiana na misingi ya Imam Khomeini (MA) katika siasa za nje, Ayatullahil Udhma Khamenei amesema: Kusimama kidete katika kupambana na siasa za kibeberu na za kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine, kufanya udugu na mataifa ya Waislamu, kuwa na uhusiano wa usawa na nchi zote za dunia ukitoa nchi ambazo zimelielekezea taifa la Iran ncha za upanga, kupambana na Uzayuni, kupambana kwa ajili ya ukombozi wa Palestina, kuwasaidia watu wanaodhulumiwa na kusimama imara mbele ya madhalimu, ndiyo iliyokuwa misingi ya Imam Khomeini katika siasa za nje.

Aidha ameashiria misingi ya Imam Khomeini katika upande wa masuala ya utamaduni akisema: Misingi ya Imam katika suala hili ni: Kupinga utamaduni wa Magharibi wa kuruhusu mambo yote bila ya kuchunga misingi ya dini, kupinga kuwa na fikra mgando na zisizokubali mabadiliko, kupinga ria na kujionesha katika kushikamana na dini, kutetea vilivyo na bila ya kutetereka maadili na hukmu za Kiislamu na kupambana na uenezaji wa ufuska na ufisadi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu misingi ya Imam Khomeini katika upande wa “Uchumi” kuwa ni pamoja na kutegemea uchumi wa kitaifa, kujitosheleza, uadilifu wa kiuchumi, uzalishaji na usamabazaji, kulindwa tabaka la watu maskini, kukabiliana na utamaduni wa kibepari, kuheshimu milki, kazi na vitega uchumi vya watu, kutomezwa na uchumi wa kimataifa pamoja na kuwa huru na kuwa na istiklali katika uchumi wa kitaifa. Amesema, hiyo ndiyo misingi ya kiuchumi ya Imam Khomeini (MA).

Ayatullahil Udhma Khamenei aidha amesisitiza kuwa: Matarajio ya Imam kwa viongozi nchini Iran daima na siku zote yalikuwa ni kuongoza nchi kwa uwezo na usimamiaji mzuri na kwa busara na hekima ya hali ya juu na wakati wote alikuwa akiwahimiza viongozi nchini kutekeleza kivitendo mambo hayo.

Huku akisisitiza kuwa misingi hiyo ndiyo ramani ya njia ya Imam Khomeini (MA) amesema: Taifa la Iran lenye imani thabiti, uwezo wa kila nui na vipaji vya kila namna pamoja hima ya vijana wake na kwa kutumia ramani ya njia ya Imam Khomeini, inaweza kuendeleza kwa kasi kubwa zaidi na kwa uwezo wa hali ya juu zaidi njia iliyovuukwa na taifa hili katika kipindi cha miaka 34 iliyopita na kuweza kuwa kigezo cha kweli na kamili kwa ajili ya mataifa mengine ya Waislamu.

Kiongozi Muadhamu amezungumzia pia uchaguzi nyeti na muhimu mno wa duru ya 11 ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kujadili nukta kadhaa kuhusu suala hilo.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameutaja uchaguzi kuwa ni dhihirisho la imani zote tatu alizokuwa nazo Imam Khomeini (MA) na kuongeza kuwa: Uchaguzi ni dhihirisho la kuwa na imani na Mwenyezi Mungu kwani inabidi kutekeleza jukumu la kidini la kuainisha mustakbali wa nchi kupitia kushiriki kwenye uchaguzi.

Vile vile amesema: Uchaguzi ni dhihirisho la kuwa na imani na wananchi kwani wananchi wenyewe ndio wanaochagua viongozi wa kuongoza nchi yao kupitia uchaguzi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema: Uchaguzi aidha ni dhihirisho la kujiamini kwani kila kura inayotumbukizwa kwenye sanduku la kupigia kura kwa hakika huwa ni sawa na kushiriki na kuhusika katika maamuzi ya nchi.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameitaja maudhui muhimu zaidi katika uchaguzi kuwa ni kuleta hamasa ya kisiasa na kushiriki kwa wingi na kwa hamasa kubwa wananchi kwenye masanduku ya kupigia kura akisisitiza kwamba: Kura yoyote ile ambayo wananchi wataipiga kumpa mgombea yeyote yule kati ya wagombea wanane wa urais, kwanza kabisa ajue kuwa kura hiyo ni kwa ajili ya Jamhuri ya Kiislamu na ni kura ya kuonyesha kuwa na imani na faida za uchaguzi.

Vile vile amesema: Kura hiyo katika daraja ya pili inakwenda kwa mtu ambapo kila mtu kulingana na mtazamo wake anaamua kumchagua mgombea fulani kwa kumuona anafaa zaidi kumpa dhamana ya kuongoza masuala ya utendaji nchini.

Kiongozi Muadhamu pia ameashiria njama zinazofanywa na maadui za kujaribu kuubadalisha uchaguzi wa Iran kuwa kitisho dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini na kusema kuwa: Maadui wana hamu ya kuona kuwa uchaguzi nchini Iran imma unakuwa chapwa usio na mvuto wa aina yoyote ile au wazushe fitna baada ya uchaguzi kama walivyofanya mwaka 2009 lakini maadui wanajidanganya katika njama zao kwani inaonekana kuwsa hadi hivi sasa bado hawajalijua taifa la Iran na inaonekana wameshaisahau tarehe 9 Dei (Disemba 30, 2009).

Vile vile amesisitiza kuwa: Kwa taufiki ya Mwenyeziu Mungu na tofauti kabisa na wanavyotaka maadui, uchaguzi wa Juni 14 Inshaallah utakuwa fursa kubwa kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislanmu ya Iran.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Maadui wanadhani kwamba, kuna wingi wa watu walionyamaza kimya na ambao wanaipinga Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran wakati ambapo wamesahau jinsi wananchi wa Iran walivyojitokeza kwa wingi mno katika maadhimisho ya Bahman 22 mwaka huu (siku zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran) na kwamba katika kipindi chote hiki cha miaka 34 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kundi kubwa na adhimu la wananchi wa Iran limekuwa likijitokeza kwenye maandamano mbalimbali ya kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu na kupiga nara za “Mauti kwa Marekani.”

Aidha amesisitiza kuwa watu wanaolitakia mabaya taifa la Iran na wapangaji wa sera zao wanafanya njama mbalimbali dhidi ya uchaguzi wa Iran kama vile kujaribu kuwafanya watu wasijitokeze kwa wingi kwenye uchaguzi huo au kueneza propaganda mbaya za kudai kuwa eti matokeo ya uchaguzi huo yameshapangwa tangu zamani na eti chaguzi nchini Iran hazifanyiki kwa uhuru na haki na kuhoji akisema: Umeona wapi katika dunia hii wagombea wa uchaguzi wote, wale maarufu na wale wasiojulikana kabisa wakipewa fursa sawa kabisa na vyombo vya habari vya taifa ili waweze kutangaza sera zao kwa uhuru na kwa uwazi kabisa bila ya bugdha wala kunyimwa hata kidogo haki hiyo, ghairi ya nchini Iran?

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Nchini Marekani na katika nchi nyingine za kibepari, kama mgombea si mwanachama wa vyama viwili au vitatu hivi vya kisiasa, na kama mamafia wenye utajiri na nguvu na kanali za Wazayuni hazitamuunga mkono, haiwezekani kabisa kwa mgombea katika nchi hizo kuweza kufanya kampeni zake za uchaguzi.

Ayatullah Khamenei ameitaja sheria kuwa ndiyo marejeo ya mwisho na ya kweli katika mchakato wa uchaguzi nchini Iran na kusisitiza kuwa: Katika Jamhuri ya Kiislamu kitu pekee kinachotawala mchakato wa kuingia kwenye uchaguzi ni sheria na ni kwa mujibu wa sheria ndipo baadhi ya watu wanapata fursa ya kuingia kwenye uchaguzi na wengine hawapati fursa hiyo kama ambavyo pia mchakato wa kuainisha watu waliotimiza sifa za kugombea nao unafanyika kwa mujibu wa sheria kikamilifu.

Ameongeza kuwa: Adui aliye nje ya Iran anafumbia macho uhakika huo na badala yake anaamua kueneza propaganda za uongo na kwa bahati mbaya baadhi ya koo na kalamu zisizo na taqwa za ndani ya nchi nazo zinakariri na kurudia rudia propaganda hizo za maadui wa nje ya Iran.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Taifa la Iran kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu litajitokeza kwa wingi mno katika uchaguzi huo likiwa na imani thabiti na hivyo kutoa jibu kali kwa njama zote hizi za maadui.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake kuhusu uchaguzi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakhutubu wagombea kwenye uchaguzi huo akiwapa nasaha kadhaa.

Amesisitiza kuwa, waheshimiwa wagombea wana ruhusa ya kukosoa jambo lolote wanalopenda lakini wakati huo huo wazingatie kuwa maana ya kukosoa si kukosa insafu na wala si kukanusha kazi zote zilizofanyika huko nyuma na pia si kupaka matope watu wengine bali ukosoaji maana yake ni kuonyesha mapungufu yaliyopo kwa nia njema na kwa ajili ya kutatua matatizo hayo na kuzidisha kasi ya hatua za kimaendeleo.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameongeza kwamba: Ijapokuwa vyombo vya habari vya kibeberu vinafanya njama kwa chuki na uadui wa wazi na bila ya shaka vitajaribu kuyaonesha maneno yake hayo kuwa yanawalenga wagombea maalumu wa uchaguzi huo lakini ukweli wa mambo ni kuwa matamshi yake hayo hayamlengi mgombea au wagombea fulani tu, bali yanawahusu wagombea wote.

Ameongeza kuwa: Lengo la kukosoa kitu si kukanusha mambo mazuri yaliyofanyika hivyo watu wanaotaka kupata imani za wananchi hawapaswi kukanusha kazi nzuri na kubwa zilizofanywa na serikali ya hivi sasa na serikali nyingine za huko nyuma na ambazo zimeifanya Iran kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Ayatullah Khamenei ameashiria pia matatizo ya kiuchumi ikiwemo ughali wa bidhaa na mfumuko wa bei na kuongeza kuwa: Matarajio ya taifa na sisi sote ni kuwa mtu atakayechaguliwa na wananchi katika uchaguzi wa Juni 14 ataweza kutatua matatizo yaliyopo ya kiuchumi lakini wagombea katika kutangaza sera na mipango yao ya kiuchumi, wanapaswa kufanya hivyo bila ya kukanusha kazi nzuri zilizofanyika nchini hadi hivi sasa katika uwanja huo.

Nasaha nyingine kuhusu uchaguzi zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu kwa wagombea wanane wa uchaguzi wa Juni 14 wa Urais nchini Iran ni kwamba wagombea hao wasitoe ahadi ambazo hazitekelezeki.

Amewakhutubu wagombea katika uchaguzi huo akisema: Zungumzeni kwa namna ambayo hamtakuja kuwaonea haya wapiga kura wenu iwapo mwezi Juni mwakani maneno yenu yaliyorekodiwa yatarushwa hewani, na wala hamtalazimika kutoa visingizio hivi na vile kujitetea.

Ayatullahil Udhma Khamenei amesema pia kuwa uwezo wa Rais katika Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mpana mno na ni mkubwa sana na kongeza kuwa: Mipaka pekee aliyo nayo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni “Sheria” na tab’an sheria nayo katika uhalisia wake si kitu cha kubana bali ni cha kutoa mwongozo na ni cha kuonyesha njia sahihi ya kufuata.

Baada ya hapo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mwito kwa wagombea akiwataka sambamba na kutangaza ilani na sera zao za uchaguzi watoe pia ahadi kadhaa muhimu kwa wananchi.

Amesema: Wagombea watoe ahadi kwamba watafanya kazi zao kwa mantiki, umakini, kwa bidii kubwa bila ya kuchoka na kustakimu katika kazi zao.

Vile vile amewataka watoe ahadi kuwa watatumia uwezo wote aliopatiwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Katiba kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake mazito na watoe ahadi kwamba sambamba na kuongoza masuala ya nchi, watalipa uzito wa kutosha pia suala la uchumi ambalo hivi sasa limegeuka kuwa medani ambayo maadui na mebeberu wa dunia wanaitumia kulitwisha changamoto taifa la Iran.

Vile vile amewataka wagombea hao watoe ahadi kwa taifa kuwa watajiepusha na masuala ya pembeni na kusema jambo hilo ni la dharura na ni muhimu sana.

Ameongeza kuwa: Kuna ulazima wa kutoa ahadi kwa taifa kwamba kama mtachaguliwa hamtafungua mlango wa kutumiwa vibaya fursa hiyo na watu wenu wa pembeni na marafiki zenu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka wagombea watoe ahadi kwa wananchi kuwa watazingatia kikamilifu na kulinda vilivyo manufaa ya taifa mbele ya mabeberu pamoja na ahadi nyinginezo za dharura wanazopaswa kuzitoa wagombea hao.

Ameongeza kuwa: Baadhi ya watu wanatoa uchambuzi wa kimakosa wakidai kuwa kama tunataka kupunguza hasira za adui basi tunapaswa kulegeza kamba na kufungua njia japo kidogo kwa adui lakini kuwa na fikra kama hizo ni makosa bali maana ya jambo hilo ni kufadhilisha manufaa ya mabeberu kuliko manufaa ya taifa.

Vile vile amekumbusha kuwa: Hamaki za adui zinatokana na adui kuona kuwa Jamhuri ya Kiislamu inazidi kutukuka na zinatokana na kuwa hai njia, utajo na malengo ya Imam Khomeini (MA) katika fikra na akili za wananchi wa Iran na kwamba njia pekee ya kukabiliana na jambo hilo ni kufanya jitihada bila kuchoka kwa ajili ya kutatua matatizo yaliyopo sambamba na kulinda uhuru, istiklali na nguvu za kitaifa.

Ayatullahil Udhma Khamenei amesisitiza mwishoni mwa hotuba yake kuwa: Siku kumi zijazo, itawadia siku ya mtihani mkubwa kwa taifa la Iran na ni matumaini yetu kuwa kwa baraka, taufiki na msaada wa Mwenyezi Mungu, taifa la Iran litajenga hamasa kubwa iliyojaa baraka na yenye matunda yanayong’ara na litatoka katika mtihani huo mkubwa wa Mwenyezi Mungu kwa ufakhari na mafanikio makubwa.

Mwanzoni mwa maadhimisho ya kumbukumbu hizo, Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Hasan Khomeini, mfawidhi wa Haram Tukufu ya Imam Khomeini (MA) ametoa hotuba fupi na kuitaja harakati ya Khordad 15, 1342 (Juni 5, 1963 Milaadia) kwamba ulikuwa mwanzo wa harakati adhimu ya Imam Khomeini na kuongeza kuwa: Wakati wa kuanza harakati hiyo ya Imam mazingira yalikuwa kwa sura ambayo hakuna mtu yeyote ambaye angalau japo kidogo alifikiria tu kuwa harakati hiyo ingelipelekea kutokea Mapinduzi yenye muelekeo na fikra za kidini kupitia kwa Imam Khomeini (MA).

Amesema, sifa aliyokuwa nayo Imam Khomeini ya kumwamini kikamilifu Mwenyezi Mungu na kutawakkal Kwake, ndio uliokuwa msingi wa harakati ya kimapinduzi ya Imam na kuongeza kuwa: Imam Khomeini (MA) alianzisha harakati yake katika mazingira ambayo itikadi za kidini zilikuwa dhaifu mno mashariki na magharibi mwa dunia.

Sayyid Hassan Khomeini vile vile ameashiria uchaguzi wa Juni 14 wa nchini Iran na kusema kuwa: Ni matumaini yetu watu wa matabaka yote watajitokeza kwenye uchaguzi huo na kutekeleza vizuri jukumu lao katika wakati huu nyeti na muhimu sana.

 

700 /