Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu katika dakika za awali za kupiga kura:

Mustakbali wa nchi na ufanisi wa wananchi unategemea kushiriki wananchi katika uchaguzi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, mapema leo asubuhi (Ijumaa) ameshiriki katika duru ya kumi na moja ya uchaguzi wa Rais wa Iran na duru ya nne ya uchaguzi wa Mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji nchini kwa kupiga kura katika eneo jongefu la kupigia kura la nambari 110 katika Husainia ya Imam Khomeini (MA) mjini Tehran.

Wakati akishiriki katika kupiga kura, Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa sikukuu za mwezi huu mtukufu wa Shaaban na kusema pia kuwa, mahudhurio makubwa ya wananchi, kushiriki kwa wakati unaofaa watu wote kwa pamoja na kwa hamasa na shauku kubwa katika uchaguzi huo ni jambo lenye umuhimu mkubwa.

Vile vile amesisitiza kuwa: Wananchi wapendwa wa Iran wanapaswa kuingia kwenye medani ya uchaguzi kwa hamasa na shauku kubwa na wajue kuwa, mustakbali wa nchi yao na ufanisi wa taifa lao unategemea kujitokeza kwao kwa wingi katika uchaguzi kama ambavyo unategemea pia aina ya mtu wanayemchagua.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja athari kubwa na za kimsingi za kushiriki wananchi kwenye uchaguzi katika mustakbali wa nchi kuwa ndizo zilizowapelekea maadui wa Iran kufanya propaganda kubwa, nyingi mno na za kila sekunde dhidi ya kushiriki wananchi katika uchaguzi huo na kuongeza kuwa, maadui wamefanya njama kubwa ili kujaribu kuwavunja moyo wananchi na kuwafanya wawe na mtazamo mbaya kuhusu uchaguzi huu na hivyo wasishiriki kupiga kura na ili kufanikisha njama zao hizo wamekwenda mbali zaidi ya kutumia vyombo vya habari na mara hii wanasiasa na watu wakubwa wa nchi za Magharibi wa kambi ya adui walikuwa wanapinga waziwazi kujitokeza wananchi wa Iran katika uchaguzi.

Aidha ameashiria matamshi ya viongozi wa Marekani waliosema kuwa wao hawakubaliani na uchaguzi wa Iran na kusisitiza kwamba, kamwe wananchi wa Iran hawashughulishwi na maneno ya maadui bali siku zote wao wenyewe ndio wanaoamua wafanye nini, kitu gani kina maslahi kwao na kwa nchi yao na jambo gani halina maslahi kwao na ndio maana miaka yote hii wamekuwa wakishiriki vilivyo katika chaguzi mbalimbali nchini na wataendelea kufanya hivyo.

Ayatullahil Udhma Ali Khamenei vile vile amewataka wananchi wajitokeze kwenye kupiga kura katika wakati wa awali kabisa wa kuanza zoezi hilo na kuongeza kwamba: Hakuna mtu yeyote, hata watu wangu wa karibu anayejua kura yangu mimi inakwenda kwa nani na kwamba ni jukumu la wananchi kufanya uchunguzi na kuamua wao wenyewe mtu wa kumpa kura zao.

Amma kuhusiana na uchaguzi wa Mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa yeye katika uchaguzi huu amewapigia kura watu 31 ambapo baadhi yao anawajua vizuri na wengine ni kutokana na kutegemea orodha fulani ya wagombea.

Aidha ameelezea matumaini yake kuwa matokeo ya uchaguzi wa leo yatakuwa ni kheri kwa nchi na wananchi na yatapelekea taifa la Iran kupata ufanisi na ustawi wa kimaada na kimaanawi.

Vile vile amewakhutubu waendeshaji wa uchaguzi huo akisema kwa kusisitiza kwamba. kura za wananchi ni dhamana na ni haki ya watu juu ya mabega ya maafisa wa uchaguzi na watu wanaohesabu kura, hivyo inabidi kufanyike umakini wa hali ya juu sana katika kutekeleza jukumu hilo.

700 /