Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu katika hotuba za Swala ya Idil Fitr:

Wazayuni wanafurahishwa na hali mbaya ya Misri, Iraq na nchi nyingine za Kiislamu zilizokumbwa na hitilafu

Taifa la waumini na lenye umoja na mshikamano la Iran leo limeshiriki kwa wingi katika Swala ya Idil Fitri kote nchini na kumshukuru Mwenyezi Mungu SW kwa kukamilisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mjini Tehran Swala ya Idi iliyohudhuriwa na mamilioni ya watu imeongozwa na Ayatullah Imam Ali Khamenei katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran na kilomita kadhaa katika mitaa ya kandokando yake.  

Katika hotuba za Swala ya Idi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amelipongeza taifa la Iran na Waislamu wote duniani kwa mnasaba wa kuwadia Idil Fitri na kusema ibada na funga ya mwezi wa Ramadhani ya wananchi katika siku hizi zenye joto kali na ndefu za kiangazi imemridhisha Allah na kuwapa hisia za furaha ya kimaanawi na kiroho wananchi. Ayatullah Khamenei amesema ana matumaini kwamba Mwenyezi Mungu muweza atalipa taifa taufiki ya kulinda matunda ya juhudi zake kubwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema moja ya jihadi kubwa za wananchi wa Iran katika mwezi uliomalizika wa Ramadhani ni kushiriki kwao kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds. Amesema mahudhurio hayo makubwa ya taifa zima yamethibitisha tena uhai na kusimama kidete kwa taifa la Iran katika moja kati ya masuala muhimu ya dunia na historia ya Uislamu na kwa hakika ni muhali kuweza kueleza umuhimu mkubwa wa harakati hiyo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema miongoni mwa kazi nzuri nzuri naz a kupongezwa zilizofanyika katika mwezi wa ramadhani ni kupanuliwa na kuenezwa suna ya ada ya kutoa futari misikitini na mitaani. Amekosoa israfu na ubadhirifu katika futari za baadhi ya watu na kusema: Ni vyema kwa watu wenye nia ya kutoa sadaka katika mwezi wa Ramadhani kutilia maanani suna na ada hiyo ya kutoa futari za kawaida zisizo za israfu katika misikiti na maeneo ya umma.

Katika hotuba ya pili ya Swala ya Idi, Ayatullah Khamenei amewataka Waislamu wote kuwa na taqwa na ucha Mungu katika maeneo na matendo yao na vilevile kuwa wacha Mungu katika misimamo yao ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Akibainisha  baadhi ya matukio muhimu ya Iran na Mashariki ya Kati, Imam Khamenei amesema miongoni mwa matukio hayo muhimu ni uundwaji wa serikali mpya nchini Iran. Amesema kwa baraka zake Mwenyezi Mungu na hima na juhudi kubwa matakwa hayo ya kisheria yaametekelezwa kwa njia bora.

Ayatullah Khamenei amemtakia taufiki na mafanikio Rais mpya wa Iran.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amefanya ulinganisho baina ya matukio ya Iran na nchi za kaskazini mwa Afrika na magharibi mwa Asia na kusema kuwa, inasikitisha kwamba kinyume na hali ya kufurahisha nchini Iran, matukio na hali ya eneo la nchi za Kiislamu inatia wasiwasi.

Ameashiria dhulma na ukandamizaji unaendelea kufanywa na Wazayuni dhidi ya taifa la Palestina na kusema: Miongoni mwa masaibu ya dunia ya sasa ni uungaji mkono wa madola yanayodai kutetea haki za binadamu na demokrasia kwa jinai za waziwazi za utawala ghasibu wa Israel.

Ayatullah Ali Khamenei ameashiria tukio la kuanza tena mazungumzo kati ya serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Wazayuni na kusisitiza kwamba, hapana shaka kuwa mazungumzo haya kama yalivyokuwa ya kabla yake, hayatakuwa na natija isipokuwa kukanyagwa zaidi haki za Wapalestina na kuwahamasisha Wazayuni kutenda jinai zaidi.

Imam Khamenei vilevile amegusia madai ya Marekani kuwa ni mpatanishi katika mazungumzo hayo na kusema Marekani imejionesha waziwazi kuwa upande wa Wazayuni maghasibu na ni wazi kuwa hali hiyo itakuwa na madhara kwa Wapalestina.

Ameutaka ulimwengu wa Kiislamu kutokaa kimya mbele ya dhulma hiyo kubwa na kulaani matendo ya mbwa mwito mkali wa Kizayuni na waungaji mkono wake wa kimataifa.

Imam Khamenei ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali mbaya ya Misri na kusema kuwa, uwezekano wa kutokea vita vya ndani nchini Misri umepata nguvu zaidi na suala hilo ni maafa.

Amelitaka taifa kubwa la Misri, makundi mbalimbali, shakhsia wakubwa wa kisiasa na maulama wa Misri kutaamali na kutafakari vyema matokeo mabaya ya hali ya sasa nchini humo na kuhoji kwamba, je hali ya sasa ya Syria, athari hatari za vita vya ndani na matokeo mabaya sana ya kuwepo vibaraka wa nchi za Magharibi na Israel na magaidi katika maeneo mbalimbali kwenye ulimwengu wa Kiislamu havitoshi kuwa ibra na mafunzo kwa Wamisri?

Ayatullah Khamenei amelaani vikali kuuawa kwa wananchi huko Misri na akasema matamshi makali yanayotolewa na makundi mbalimbali dhidi ya mwenzake hayana faida yoyote na iwapo kutatokea vita vya ndani basi jambo hilo litatumiwa kama kisingizio cha madola ya kigeni kuingilia mambo ya ndani ya Misri na kusababisha balaa kubwa wa taifa la nchi hiyo.

Amesisitiza juu ya udharura wa kutiliwa maanani demokrasia na matakwa ya wananchi na amewataka wananchi, makundi mbalimbali ya kisiasa na kidini, wasomi na maulama wa Misri kutatua mgogoro wa nchi hiyo na wasiwaruhusu wageni kuingilia mambo yao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameitaja hali ya Iraq kuwa ni ya kusikitisha na akasema: Nchini Iraq kuna serikali iliyochaguliwa na wananchi lakini madola makubwa na vibaraka wao wa kanda hii hawaridhishwi na serikali hiyo.

Amesema hapana shaka kuwa ugaidi na mauaji yanayotokea nchini Iraq yanafanyika kwa misaada ya kifedha na kisiasa ya baadhi ya nchi za kanda hii na za nje ya eneo hili ili kuvuruga hali ya mambo nchini humo na kuzuia ustawi na maendeleo yake.

Mwishoni mwa hotuba zake, Ayatullah Ali Khamenei amesema, Wazayuni wanafurahishwa sana na hali ya kusikitisha ya Misri, Iraq na nchi nyingine zilizokumbwa na hitilafu na ukosefu wa amani na kuongeza kuwa, wanasiasa, makundi ya kisiasa na matabaka mbalimbali ya wananchi, Shia na Suni, Waarabu na Wakurdi wanapaswa kutilia maanani matokeo mabaya ya hitilafu za ndani na kuelewa kwamba, vita vya ndani vinaharibu miundombinu na mustakbali wa nchi yao.

        

 

700 /