Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Ninaunga mkono harakati za kidiplomasia za serikali

Sherehe ya kuapishwa na kupewa vyeo wanafunzi waliohitimu vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanyika mapema leo ikihudhuriwa na Amiri jeshi Mkuu wa majeshi yote Ayatullah Ali Khamenei katika Chuo Kikuu cha Jeshi la Anga cha Shahid Sattari.

Baada ya kuwasili chuoni hapo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikwenda moja kwa moja kwenye mnara wa kumbukumbu ya mashahidi wa jeshi na kusoma al Fatiha akiwaombea maghufira na daraja za juu peponi. Baada ya hapo Amiri Jeshi Mkuu amekagua vikosi vya majeshi.

Ayatullah Khamenei amehutubia hadhara hiyo akisema kuwa, kuingia katika vikosi vya jeshi shupavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni fahari kubwa kwa vijana. Ameashiria  ulazima wa kuimarishwa utayarifu na hali ya kujihami ya vikosi vya jeshi sambamba na kuimarisha Mfumo wa Kiislamu na umoja wa kitaifa na akasema kuwa: "Tunaunga mkono harakati za kidiplomasia za serikali ikiwemo safari iliyofanywa hivi karibuni huko New York, kwani tuna imani na serikali inayowahudumia wananchi na tuna matumaini nayo; hata hivyo  baadhi ya yaliyotokea katika safari ya New York hayakupasa kufanyika kwa sababu tunaitambua serikali ya Marekani kuwa haiaminiki, ni yenye kiburi, haina mantiki na haiheshimu ahadi zake."

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Tuna imani na viongozi wetu na tunawataka wapige hatua imara kwa umakini na kwa kutilia maanani pande zote na wala wasisahau maslahi ya taifa."

Ayatullah Khamenei amesema muundo wa Mfumo wa Kiislamu wa Iran uko imara na kuongeza kuwa, masuala makuu yaliyolinda mapinduzi na taifa na kuwa sababu ya maendeleo tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini ni kutiliwa maanani malengo aali ya utawala wa Kiislamu na izza ya kitaifa; kwa msingi huo ni wajibu kwa viongozi na wananchi wote kulinda izza na utambulisho wa taifa.

Ameashiria jinsi Mfumo wa Kiislamu wa Iran usivyokuwa na imani na Marekani na akasema serikali ya Marekani iko katika makucha ya Wazayuni. Ameongeza kuwa kwa hakika serikali ya Marekani inafanya harakati katika upande wa kudhamini maslahi ya Wazayuni na inaushurutisha ulimwengu mzima huku yenyewe ikiwa inashurutishwa na utawala wa Kizayuni.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa taifa la Iran si tishio kwa nchi yoyote na kusema kuwa, uimara wa vikosi vya jeshi la Iran ni sababu muhimu ya kulinda usalama wa Mfumo wa Kiislamu. Ameongeza kuwa vikosi vya Iran ikiwa ni pamoja na jeshi, Sepah (Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi), Basij (jeshi la kujitolea la wananchi) na jeshi la polisi vinapaswa kuwa ngome imara mbele ya njama za maadui.

Amiri Jeshi Mkuu wa Iran ameashiria vitisho vya kukirihisha vinavyotolewa mara kwa mara na maadui wa taifa la Iran na kusema: "Watu wote wenye tabia ya kutoa vitisho vya maneno dhidi ya Iran wanapaswa kuelewa kwamba, jibu letu kwa chokochoko za aina yoyote litakuwa kali na zito."

Ayatullah Khamenei amesema taifa la Iran limeonesha ungangari wake katika kulinda thamani na maslahi yake na vilevile limeonesha hamu ya kuwepo amani, maelewano na kuishi kwa usalama kwa sababu mambo hayo mawili yanakwenda sambamba.

Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei amepongeza ushujaa na kujitolea kwa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan Jeshi la Anga katika kipindi chote cha miaka minane ya kujihami kutakatifu.

Baada ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu, Brigedia Jenerali Shah Saffi ambaye ni Kamanda wa Jeshi la Anga amemkaribisha Ayatullah Khamenei na kusema kuwa, mbali na kutoa mafunzo ya teknolojia mpya na sayansi ya kisasa, vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi hapa nchini pia vimeweka mafunzo ya kidini na kiitikadi katika ajenda zake kuu. Ametoa ripoti fupi kuhusu mipango ya kistratijia ya jeshi hilo na kutangaza kuwa, liko tayari kulinga mipaka ya anga ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

        

700 /