Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Tamaa ya adui kuwa Iran itawekea kikomo mipango yake ya makombora na ujinga wa mwisho

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumapili) ametembelea makao makuu ya kikosi cha anga na anga za mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kukagua maonyesho ya mafanikio mbali mbali ya kikosi hicho.

Katika maonyesho hayo, kumeonyeshwa zana, vyombo na vifaa mbali mbali vya kisasa vilivyobuniwa na kutengenezwa na kikosi hicho katika nyuga tofauti kama za kubuni na kutengeneza ndege za kisasa zisizo na rubani, mifumo ya makombora dhidi ya manowari na makombora ya balestiki, mifumo ya kujilinda kwa makombora na mifumo mgingine mbali mbali ya kiulinzi pamoja na aina kwa aina ya rada na vituo vikuu vya uendeshaji wa zana, vyombo na mifumo hiyo.

Eneo la kuonyesha mafanikio na maendeleo ya kikosi cha anga na anga za mbali cha SEPAH katika uwanja wa kutengeneza na kubuni aina kwa aina ya ndege zisizo na rubani, ndilo behewa la kwanza lililotembelewa na Kiongozi Muadhamu ambaye pia ndiye Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika eneo hilo, kumeonyeshwa ndege zisizo na rubani aina ya Shahid 129, Shahid 125, Shahid 121 na mifumo ya kuongoza na kuendesha vyombo hivyo na injini za ndege zinazoweza kuongozwa kwa mbali, zana za kisasa ambazo zote zimebuniwa na kutengenezwa na wataalamu na wanasayansi wa Iran.

Kuonyeshwa ndege ya kisasa kabisa isiyo na rubani na isiyoonekana na rada aina ya RQ170 ambayo ni mfano kamili wa ndege ya Kimarekani iliyochukuliwa ngawira na Iran na kutengenezwa modeli ya Kiirani ya ndege hiyo ilikuwa ni miongoni mwa sehemu muhimu zaidi za eneo hilo la maonyesho.

Wataalamu na wanasayansi wa kikosi cha anga na anga za mbali cha SEPAH katika kipindi cha karibu miaka miwili wamefanikiwa kutengeneza modeli ya Kiirani ya ndege ya kisasa kabisa isiyo na rubani ya Kimarekani aina ya RQ170.

Kiongozi Mapinduzi ya Kiislamu amepewa ufafanuzi wa kutosha kuhusu hatua zinazopitiwa katika kutengeneza ndege hiyo ya kisasa kabisa isiyo na rubani, namna sehemu mbali mbali za ndege hiyo aina ya RQ170 zilivyopangiliwa ikiwa ni pamoja na jinsi inavyorekebisha data zake na kuzihifadhi kwa malengo maalumu, namna kanali ya mawasiliano ya kisatalaiti ya ndege hiyo inavyofanya kazi, kuchambua namna inavyokwepa rada, kutolewa na kukarabatiwa vyombo vyake vya ndani na kompyuta inayoongoza urukaji wa ndege hiyo pamoja na kukarabati na kufunga injini ya ndege hiyo ya Kimarekani.

Behewa la makombora ya ardhi kwa ardhi ya kikosi cha anga na anga za juu cha SEPAH ni sehemu ya pili iliyotembelewa na Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika maonyesho hayo.

Kwenye sehemu hiyo yalikuweko makombora ya balestiki ya kuangamiza manowari, makombora ya Zilzal, makombora ya Ghuba ya Uajemi, Zilzal ya Mvua, Hormoz 1 na 2, makombora ya Cruse, Fajr 5, Ra’ad 301 na Sijjil ambayo hatua zote za utengenezaji wake, kuanzia fikra hadi utengenezaji na uzalishaji wake, zote zimefanywa na wataalamu wa Kiirani.

Vile vile leo na kutokana na kutembelewa na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, kumeonyeshwa mfumo mpya wa ulinzi wa Khordad Tatu ambao umebuniwa na kutengenezwa na wataalamu wa Kiirani. Mfumo huo wa kiulinzi ambao kubuniwa na kutengenezwa kwake kumechukua mwaka mmoja na nusu, una uwezo wa kulinda masafa ya kilomita 50 na kugundua kwa wakati mmoja shabaha nne tofauti na kupiga makombora manane kwa sekunde moja.

Mfumo wa kiulinzi wa Tabas, kituo kikuu cha uendeshaji na udhibiti, aina kwa aina ya mifumo mingine ya kiulinzi, Ra’ad 1 na 2 na aina kwa aina ya rada za kisasa ni mafanikio mengine ya kikosi cha anga na anga za juu cha jeshi la SEPAH la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoonyeshwa kwenye maonyesho hayo.

Aina kwa aina ya rada zikiwemo rada za kisasa za Kavosh, vituo vikuu vya udhibiti na uendeshaji wa rada hizo na kuendesha vita vya elektroniki ni uwezo na maendeleo mengine ya kikosi hicho cha anga na anga za juu cha SEPAH yaliyotembelewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.  

Baada ya kutembelea maonyesho ya maendeleo ya kikosi cha anga na anga za juu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba fupi mbele ya makamanda wa ngazi za juu wa SEPAH na Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu pamoja na baadhi ya makamanda na wataalamu na wanasayansi wa kikosi hicho cha anga na anga za juu cha SEPAH. Amesema, amefurahi mno kuona maendeleo makubwa yaliyopigwa kupitia maonyesho hayo na kusisitiza kwamba: Somo kubwa linalopatikana kwenye maonyesho hayo ni kutiliwa nguvu vipaji na uwezo wa taifa la Iran wa kuingia kwenye medani mbali mbali ngumu sana na medani nyinginezo ambazo adui ameamua kulipiga marufuku taifa hili lisiingie.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Maonyesho hayo yanatupa sisi viongozi wote ujumbe wa uwezo na nguvu za ndani ya taifa letu na yanatutangazia wazi wazi kuwa “Tunaweza.”

Vile vile ameelezea kusikitishwa kwake na baadhi ya maafisa ambao hawaupi uzito mkubwa ujumbe wa uwezo na nguvu za ndani ya taifa na kusema kuwa: Inasikitisha kuona kuwa kuna baadhi ya maafisa wanashindwa kuuona na kuudiriki ujumbe huo.

Kiongozi Muadhamu vile vile ameyataja mambo matatu ya “vipaji, uwezo na azma na nia ya kweli” kuwa ni sababu kuu za taifa kuwa na uwezo na nguvu na kusisitiza kwamba: Katika kipindi cha miaka yote hii iliyopita, tumeweza kupata matunda mazuri katika kila medani tuliyoingia na kutuliza akili ndani yake na kuwa na azma ya kweli ya kufanikisha tuliyoyakusudia.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Mimi siku zote ni mpenzi wa ubunifu katika siasa za nje na ninapenda mazungumzo na nasaha zangu ninazozitoa kila siku kwa maafisa husika ni kwamba katika siasa za nje na mabadilishano ya kimataifa, kadiri watakavyofanya juhudi na ubunifu, watambue kuwa, hawapaswi kuyakwamisha mahitaji ya nchi na baadhi ya masuala kama vile vikwazo katika mazungumzo hayo.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, viongozi nchini wanapaswa kutafuta njia nyingine za kutatulia suala la vikwazo na wasikwamishe mahitaji ya nchi katika suala hilo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja maonyesho ya kikosi cha anga na anga za juu cha SEPAH kuwa ni mfano wa kivitendo wa faida za kutumia vipaji na uwezo wa taifa la Iran pamoja na kuzikusanya pamoja nia na azma za wenye nia na uwezo wa maendeleo nchini na kusema kwa kusisitiza kuwa: “Lazima tuamini na tutambue kuwa tunaweza.”

Ayatullah Khamenei amesisitiza pia kuwa tatizo kubwa la mataifa ya dunia ni kutokuwa na taarifa kuhusiana na uwezo wao na kuongeza kwamba: Tatizo la taifa la Iran hadi kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilikuwa ni hilo hilo na kwamba taifa hili lilikuwa halijui kuwa linao uwezo wa kufanya mambo makubwa makubwa kama ambavyo hadi hivi sasa pia kuna baadhi ya watu hawatambui kuwa tunao uwezo wa kufanya lolote tunaloamua na kulitilia nia ya kweli!

Vile vile ameitaja majimui ya vijana na wabunifu ndani ya vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni kigezo kizuri kwa sekta nyinginezo zote nchini na kusisitiza kuwa: Katika upande wa masuala ya kiuchumi pia tunaweza kutatua masuala mengi sana kwa kutegemea uwezo na vipaji vyetu vya ndani kama ambavyo huko nyuma pia tumepata uzoefu mzuri wa jambo hilo.

Kiongozi Muadhamu vile vile amesema, sababu kuu ya kuwepo uadui wa kila namna dhidi ya Iran ni kwa sababu taifa hili limeamua kuwa huru na limeamua kushikamana na Uislamu na Qur’ani Tukufu.

Ameongeza kuwa: Uislamu na Qur’ani inayataka mataifa ya Waislamu yajitegemea na yasimame juu ya miguu yao wenyewe na yategemee utambulisho wao wa Kiislamu – Kibinadamu na kuwa na imani na nia nzuri na Mwenyezi Mungu Mtukufu na kutosalimu amri mbele ya dhulma na uporaji wa mabeberu wa kimataifa. Hivyo maadamu taifa la Iran litaendelea kushikamana na Uislamu na Qur’ani na malengo yake makuu matukufu, basi uaduia wa kambi ya mabeberu na waistikbari dhidi ya taifa hili nao utaendelea kuwepo.

Ayatullah Khamenei vile vile amesisitiza kuwa: Kambi ya kibeberu inafanya njama za kulipigisha magoti taifa la Iran, kulikwamisha na kulilazimisha kurudi nyuma, lakini kamwe haitafanikiwa kulifikia lengo lake hilo la kiuadui.

Vile vile ameashiria matamshi yasiyo ya kimantiki na yasiyoingia akilini ya upande wa Magharibi katika mazungumzo na Iran kuhusiana na sisitizo lao la kuitaka Iran iwekee ukomo mipango yake ya makombora na kusema kuwa: Wamagharibi wana tamaa ya kuona Iran inawekea mipaka na ukomo mipango yake ya makombora katika hali ambayo daima Wamagharibi hao hao wanatoa vitisho vya kijeshi dhidi ya Iran, ndio maana tunasema, kuwa na tamaa ya aina hiyo ni ujinga na upumbavu wa mwisho.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema kwa kusisitiza kuwa, miamala isiyo ya kimantiki ya Wamagharibi inaonesha kushindwa kwao kikamilifu kukabiliana na taifa la Iran na kuongeza kuwa: Kikosi cha anga na anga za juu cha SEPAH kinapaswa kuendelea mbele na kwa umakini wa hali ya juu na mipango na ratiba zake zote na kisitosheke na maendeleo kiliyo nayo hivi sasa.

Ayatullah Khamenei pia amesisitiza kuwa, kikosi hicho cha anga na anga za mbali cha SEPAH kina wajibu wa kuhakikisha kuwa kinafikia hatua ya kuzalisha kwa wingi uvumbuzi na uwezo wake mbali mbali na kusema kwa msisitizo mkubwa kwamba: Suala hili ni wajibu na ni jukumu la watu wote na kwamba maafisa na viongozi wote wa kijeshi wanapaswa kuelekeza juhudi zao zote upande huo na viongozi wa serikali nao wanapaswa kuunga mkono na watambue kuwa hilo ni miongoni mwa majukumu yao makuu.

Vile vile ameashiria kuendelea adui kupiga hatua za maendeleo sambamba na maendeleo ya Iran na kuongeza kuwa: Lazima taifa la Iran lijipangie mambo yake kwa namna ambayo wakati wote liwe linapunguza mwanya uliopo baina yake na adui katika upande huo na katika zile medani ambazo mwanya uliopo ni mdogo, taifa la Iran lihakikishe linampiku adui katika medani hizo.

Mwishoni mwa hotuba yake, Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekumbushia nukta hii kuwa, taifa la Iran linapaswa kutegemea vipawa na vipaji vyake ndani na kustafidi kivitendo na uwezo na vipaji hiyo na kuomba msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kutochoka wala kughafilika hata chembe kuomba hidaya na auni ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Brigedia Jenerali Haji Zadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga na Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ametoa ripoti fupi kuhusiana na mafanikio na maendeleo ya kikosi hicho katika medani za makombora, ndege zisizo na rubani, ulinzi wa anga, rada na vituo vikuu vya udhibiti na uendeshaji mambo na kusema: Watalaamu na wanasayansi wa kikosi cha anga na anga za mbali cha SEPAH wamefanikiwa kuondoa vizuizi vilivyosababishwa na vikwazo katika masuala yake ya ufundi na teknolojia kwa namna ambayo leo hii nguvu na uwezo wa makombora ya Iran unashika nafasi ya kwanza katika eneo zima la Mashariki ya Kati na unashika nafasi ya saba duniani.

Amesisitiza kuwa: Maonyesho ya leo katika eneo hilo ni sehemu ndogo sana tu ya uwezo wa walinzi wa Uislamu nchini na kama adui atafanya kosa lolote lile la kuichokoza Iran, basi atapata somo ambalo hataweza kulisahau milele maishani mwake.

Brigedia Jenerali Haji Zadeh ameongeza kuwa: Vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu katika upande wa kijeshi vimetumia miongozo ya Amirijeshi MKuu wa vikosi vyote vya ulinzi nchini na kufanikiwa kushinda vikwazo vyote na inatarajiwa kuwa viongozi na maafisa wa sekta nyinginezo pia zikiwemo za kiuchumi, wataweza kuvifanya vikosi vya ulinzi kuwa kigezo kizuri kwao na kutumia mbinu hizo kushinda vikwazo na vitisho vyote vya adui.

Vile vile mwanzoni mwa kuingia kwenye Makao Makuu ya Kikosi cha Anga na Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekwenda kwenye maziara ya mashahidi katika makao makuu hayo na kuwasomea Faatiha mashahidi wa vita vya kujihami kutakatifu na kumuomba Mwenyezi Mungu awapandishe daraja za juu za utukufu.

 

700 /