Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Amijireshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Iran:

Kusimama kidete taifa la Iran kukabiliana na njama za mabeberu kumeikasarishi Marekani

Leo asubuhi (Jumtano) kumefanyika sherehe za kumaliza masomo wanachuo wa Chuo Kikuu cha Malezi na Mafunzo ya Uafisa wa Kijeshi cha Imam Husain AS. Sherehe hizo zilizohudhuriwa na Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Amirijeshi Mkuu wa Vikosi vyote vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimefanyika wakati huu wa kukaribia Khordad 3 (Mei 24) siku ya kuadhimisha ukombozi wa mji wa Khorramshahr (wa kusini Magharibi mwa Iran) katika operesheni iliyoliletea fakhari kubwa taifa la Iran iliyojulikana kwa jina la Baytul Muqaddas.

Mwanzoni kabisa mwa kuingia kwenye uwanja wa sherehe hizo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekwenda kwenye maziara ya mashahiri waliopotea na kuwasomea Faatiha mashahidi wa vita vya kujihami kutakatifu, akimuomba Mwenyezi Mungu awapandishe daraja za juu za utukufu.

Baada ya hapo, amekagua vikosi mbali mbali vya askari waliokuwa wamepanga gwaride kwenye medani hiyo.

Ayatullah Khamenei vile vile amezungumza kwa karibu na majeruhi wa vita waliokuwepo kwenye medani hiyo na kutoa shukrani zake za dhati kwao.

Katika hotuba fupi aliyoitoa kwenye sherehe hizo, Ayatullah Udhma Khamenei  ameitaja hatua ya kulelewa vijana waumini, walioshikamana na dini, wanamapinduzi, watafiti na wataalamu wa fani mbali mbali katika Chuo Kikuu cha maafisa wa kijeshi cha Imam Husain AS kuwa ni mfano wa wazi wa njia na mbinu za Mapinduzi ya Kiislamu na huku akiashiria namna taifa la Iran lilivyosimama imara kukabiliana na mfumo wa kibeberu wa kuigawanya dunia katika makundi mawili ya madola ya kibeberu na mataifa yanayofanyiwa ubeberu amesisitiza kuwa: Leo kambi ya kiistikbari imehamakishwa mno na maendeleo ya kila namna ya taifa la Iran na ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambayo yamepatikana bila ya kuitegemea Marekani wala madola mengine ya Magharibi, bali kwa kutegemea nguvu na uwezo wake wa ndani. Amesema: Sisi tunayajibu madola hayo kwa kukumbushia maneno yale yale maarufu ya Shahid Beheshti kwamba: Kufeni na hamaki zenu!

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuwepo mbinu mpya mpya kila siku katika Jamhuri ya Kislamu kuwa ni jambo muhimu na la kimsingi sana na huku akiashiria wasiwasi waliokuwa nao baadhi ya watu katika miaka ya huko nyuma kuhusu baadhi ya mambo amesema: Kama ambavyo tulisema wakati huo, Mapinduzi ya Kiislamu yamefanikiwa kuyashinda mambo hayo waliyokuwa na hofu nayo watu hao na hivi sasa kizazi cha vijana na wanamapinduzi kote nchini Iran kinatoa bishara njema na yenye matumaini makubwa ya kimaendeleo.

Ayatullah  Khamenei vile vile amewakumbusha vijana wa Iran wanaoshikamana vilivyo na dini, nukta nyingine moja akisema: Kizazi hicho cha vijana kina wajibu wa kuzingatia njia za kuufikia upeo mkubwa wa mbele, nao ni upeo wa kuunda ustaarabu mpya wa Kiislamu na waache kufikiria mustakbali wa karibu na miguu yao. 

Aidha amesisitiza kuwa, Uislamu ndiyo njia pekee ya kuweza kumkomboa mwanadamu kutokana na majeraha na mashambulizi ya matukio tofauti ya karne nyingi sasa na kwamba Uislamu ndiyo njia pekee ya kuweza kumletea mwanadamu ufanisi na mafanikio yake ya kweli.

Ameongeza kuwa: Vijana waumini na wanaoshikama vilivyo na dini, ndio watakaojenga mustakbali wa nchi hii na ndio nguzo kuu za kuweza kuleta ustaarabu huo mpya wa Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu ameashiria pia changamoto mbali mbali unazokumbana nazo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema: Watu wenye muono wa mbali, mwenye mwamko na mashujaa kamwe hawaogopeshwi na kuwepo changamoto, bali wanachofanya wao ni kuangalia suhula na uwezo uliopo na baadhi ya wakati huangalia hata uwezo uliofubaa na ulioacha kufanya kazi wa ndani, na kustafidi nao vizuri.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameitaja sababu kuu ya kuwepo changamoto hizo kuwa ni uwezo wa maendeleo, uimara na nguvu zinazoongezeka kila leo za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu akisisitiza kuwa: Taifa la Iran kutokana na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa miaka 35 sasa linakabiliana na tabia ovu, mbaya na ya kuchefua moyo ya kambi ya mabeberu duniani ambayo imeigawa dunia katika makundi mawili, kundi la madola yanayofanya ubeberu na kundi la mataifa yanayofanyiwa ubeberu na ni kwa sababu hiyo ndio maana madola ya kiistikbari na ya kibeberu duniani yakiongozwa na Marekani yanahamakishwa sana na maendeleo ya taifa la Iran.

Ameongeza kuwa: Tab’ani kusimama kidete taifa la Iran kumeyafanya mataifa mengine ulimwenguni yavutiwe na taifa hili na hata serikali nyingi duniani zinafurahishwa na namna Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inavyosimama imara kukabiliana na madola ya kibeberu na zinalisifu taifa la Iran kwa hilo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekitaja kitendo cha madola ya kibeberu cha kuzusha na kuzumbua masuala kama nyuklia, haki za binadamu na masuala mengine na kuyatumia dhidi ya taifa la Iran kuwa ni kisingizio tu kinachotumiwa na madola hayo bila ya kuwa na mashiko yoyote. Amesema, njama za madola hayo ambayo yanatumia visingizio na mashinikizo hayo kutaka kulizuia taifa la Iran lisisimame kupambana na madola hayo, haziwezi kuzaa madunda kwani kamwe taifa la Iran halitositisha mapambano yake ya kupigania haki.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Taifa la Iran limeonyesha nguvu na uwezo wake katika medani tofauti na limethibitisha kivitendo kuwa inawezekana kupata maendeleo ya kielimu, kijamii na ushawishi wa kimataifa pamoja na heshima ya kisiasa bila ya kuitegemea Marekani.

Amesisitiza pia kuwa: Taifa la Iran limeshajichagulia njia yake iliyo sahihi na litaendelea mbele na njia yake hiyo na kwamba mataifa yaliyo mengi duniani yako pamoja na taifa la Iran.

Kiongozi Maudhamu amegusia pia njama za kila siku za madola ya kibeberu yanayodhibiti vyombo vya habari na kuzuia mataifa mengine duniani yasipate habari kuhusiana na hatua kubwa za maendeleo na mafanikio ya kila namna linayoyapata taifa la Iran na kuongeza kuwa: Licha ya kuwepo njama zote hizo, lakini leo hii idadi kubwa sana ya watu duniani wana imani na wanalitegemea taifa la Iran na wanalipongeza.

Ayatullahil Udhma Khamenei amekosoa kutumiwa istilahi za uongo za kujiita jamii ya kimataifa katika kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ameongeza kuwa: Sisi pia tunapaswa kutumia istilahi hizo hizo zinazotumiwa na mabeberu kusuta uongo wa madola hayo kwani ukweli wa mambo ni kuwa, madola hayo yanayojiita ni jamii ya kimataifa, si jamii ya kimataifa, bali ni madola machache tu ya kibeberu yanayodhibitiwa na makampuni na mashirika ya Wazayuni ndiyo yaliyojipachika jina hilo la jamii ya kimataifa.

Vile vile amesisitiza kuwa: Jamii ya kimataifa ni mataifa ya dunia yanayodhulumiwa na madola ya kibeberu ambayo kutokana na mashinikizo ya madola hayo ya kiistikbari, hayana uthubutu wa kupinga ubeberu wao, lakini kama yatapata fursa basi bila ya shaka yoyote yatatangaza upinzani wao dhidi ya mabeberu.

Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: Jamii ya kimataifa ni wasomi, wanafikra, watu wenye fikra huru na watu wanaowapendelea kheri wenzao duniani.

Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake kuwa Chuo Kikuu cha maafisa wa kijeshi cha Imam Husain AS ni kituo muhimu kwa ajili mafunzo na kupata elimu na kufanya utafitifi na vile vile kupata mafunzo ya kimapinduzi na utaalamu wa kijeshi pamoja na kuwa na mtazamo wa mbali na kujijenga kimaanawi.

Aidha amewataka wanachuo vijana wa Chuo Kikuu hicho kujua thamani ya kupata fursa hiyo muhimu kama ambavyo pia amewataka wakuu na wahadhiri wa chuo hicho nao watumie vizuri kadiri inavyowezekana fursa hiyo muhimu.

Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakhutubu vijana wa Iran akiwaambia: Nchi na mustakbali wake ni wenu nyinyi vijana, jiwekeni tayari kwa ajili ya kuvifikia vilele vya juu na vya mbali vya ufanisi na kufanya kazi kubwa kubwa.

Katika sherehe hizo, Meja Jenerali Muhammad Ali Jaafari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, miongoni mwa kazi za daima zinazofanywa na jeshi la SEPAH ni kuzalisha nguvu mpya kila siku, kupanua uwezo wa kuepusha kushambuliwa na kuongeza uwezo wa kuwa tayari kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu kwa hali zote na kuongeza kuwa: Chemchemu na chimbuko kuu la nguvu zinazojizalisha zenyewe ndani kwa ndani za SEPAH ni nguvu kazi ya watu waumini, werevu na wanamapinduzi.

Kwa upande wake, Admirali Morteza Safari, Kamanda wa Chuo Kikuu cha Imam Husain AS ametoa ripoti fupi  ambayo ndani yake amebainisha ratiba, mipango na hatua za kielimu na kiutamaduni za Chuo Kikuu hicho.

Katika sherehe hizo, makamanda kadhaa, wahadhiri, wakufunzi, wakurugenzi, wahitimu na wanachuo bora wa Chuo Kikuu cha Imam Husain AS wamepokea zawadi zao kutoka kwa Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; Ayatullah Udhma Khamenei. Aidha mwakilishi wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Imam Husain AS amepata fakhari ya kupandishwa cheo katika sherehe hizo.

Miongoni mwa ratiba zilizokuwepo kwenye sherehe za leo za kula kiapo cha kijeshi cha wanachuo wa Chuo Kikuu cha maafisa wa kijeshi cha Imam Husain AS ilikuwa ni kuendesha mpango wa mambo yanayotakiwa kuwemo kwenye “umma mmoja.”

Vile vile katika sherehe hizo, wanachuo wa Chuo Kikuu cha maafisa wa kijeshi cha Imam Husain AS wameendesha ratiba zilizoonyesha uwezo wao mbali mbali wa kijeshi.

Mwishoni mwa sherehe hizo, vikosi mbali mbali vilivyokuwepo katika uwanja huo, vimepita kwa gwaride mbele ya Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

700 /