Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni mfano wa kutimia ahadi ya kudhihiri mwokozi

Katika wakati huu wa kukaribia maadhimisho matukufu ya siku ya kuzaliwa kutakatifu kwa mwokozi wa ulimwengu na kizazi cha mwanadamu, Imam wa Zama, Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake); Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo (Jumatano) amekagua maonyesho ya mjumuiko wa bidhaa na uzalishaji wa kielimu na kiutafiti wa Taasisi ya Darul Hadith. Wakati wa kutembelea maonyesho hayo, kumeonyeshwa stashahada (diploma) ya Imam Mahdi AS ambayo imeandaliwa kwa hima ya taasisi hiyo.

Baada ya kukagua maonyesho hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba mbele ya watafiti, maafisa na wafanyakazi wa taasisi hiyo ya Darul Hadith na kitengo cha ufatifi wa Qur'ani na Hadithi na sambamba na kutoa shukrani zake za dhati kwa kuandaliwa stashahada ya Imam Mahdi AS amelitaja jambo hilo kuwa ni mfano mzuri sana wa kugundua mapengo yaliyopo na kuchanganua mambo kwa njia sahihi lakini pia shtashahada hiyo ni hadiya yenye thamani kwa jamii ya Kiislamu na jamii ya kielimu katika wakati huu wa sikukuu ya Nusu ya Shaaban, (siku ya kuzaliwa Imam Mahdi AS).

Ameongeza kuwa: Maudhui ya "Mahdawiyyat" (yaani itikadi juu ya Imam Mahdi AS) na kudhihiri Imam wa Zama (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ambayo lazima itatimia kwani kutokana na kutimia ahadi zote za Mwenyezi Mungu katika kipindi chote cha historia, kunamfanya mwanadamu awe na yakini kwamba kutimia kwa ahadi hii kubwa nako ni jambo lisiloepukika.

Ameutaja ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran kuwa ni sehemu moja ya kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu kunakompa yakini mwanadamu ya kutimia ahadi zote za Allah na kuongeza kuwa: Ni nani aliyekuwa akitasawari kwamba katika eneo hili nyeti mno na katika nchi hii muhimu sana na katika sehemu hii ambayo ilikuwa ikitawaliwa na utawala uliokuwa unapata uungaji mkono kamili wa madola makubwa kimataifa, yangeliweza kupata ushindi Mapinduzi ambayo yamesimama juu ya msingi wa dini, fikihi na sheria za Kiislamu?

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo kwa kuashiria mfano mmoja uliomo ndani ya Qur'ani Tukufu akisema: Wakati Qur'ani Tukufu, inapohadithia kisa cha kipindi cha utotoni mwa Nabii Musa AS, inasema kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimpa ahadi mbili mama wa Nabii huyuo mtukufu. Moja ya ahadi hizo ilikuwa ni kwamba angelimrejeshea mama huyo mwanawe huyo ambaye alimwamrisha amuweke kwenye kisusu na kumuacha aburutwe na maji mtoni na ahadi nyingine ilikuwa ni kwamba mwanawe huyo ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na angelipewa utume afikapo ukubwani.

Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea kusema: Mwenyezi Mungu alifanikisha ahadi Yake ya kwanza kwa mama yake Nabii Musa AS katika kipindi kifupi tu baada ya hapo na kufanikishwa ahadi hiyo kukazitia yakini nyoyo kuhusiana na ulazima wa kutimia ahadi ya pili kubwa zaidi baada ya miaka mingi.

Vilevile ameashiria kwamba, kuwa na itikadi na Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) na hatima ya safari ya msafara wa mwanadamu katika dunia hii, ni moja ya sehemu muhimu sana za itikadi kuhusu dunia zilizomo kwenye dini za Mitume waliopewa vitabu.

Ameongeza kuwa: Dini zote za Mitume waliopewa vitabu zinaamini kuwa, msafara wa mwanadamu utafikia mwisho, na mwisho huo utakuwa mzuri, wenye kuvutia nyoyo na kuridhisha mitima ambapo moja ya sifa muhimu zaidi za mwisho huo ni kutawala kikamilifu uadilifu ndani yake.

Amesema, msafara wa mwanadamu tangu mwanzoni wa kuumbwa kwake umekuwa ukipita kwenye njia nzito zilizojaa panda shuka, njia za tambarare na zilizojaa matope na kinamasi, na kuna siku utafikia kwenye njia nyeupe na ya wazi na kwamba njia hiyo nyeupe na ya wazi itafikiwa wakati atakapodhihiri mwakozi wa ulimwengu, Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesisitiza kuwa, kuandaliwa mazingira mazuri kwa ajili ya kipindi cha Imam Mahdi AS si jambo ambalo linaweza kufanyika kwa kushitukiza na kwa mara moja. Ameongeza kuwa: Katika kipindi hicho pia vita baina ya kheri na shari katika tabia na maumbile ya mwanadamu vitaendelea kuwepo na vita baina ya watu wazuri na watu wabaya vitaendelea lakini hali ya kipindi hicho itakuwa kwa namna ambayo mazingira ya kuweza wanadamu kuwa watu wazuri na kufanikishwa uadilifu yatakuwa yako mengi mno.

Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja mwisho wa safari ya msafara wa mwanadamu kwamba utakuwa ni mwisho uliojaa matumaini na kusisitiza kuwa: Kusubiri faraja ya Imam Mahdi AS ni kusubiri kwenye matumaini na kunakozitia nguvu nyoyo na kwamba kuwa na moyo wa kusubiri ni moja ya milango mikubwa sana ya faraja kwa jamii ya Kiislamu.

Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amemshukuru Hujjatul Islam Walmuslimin Reyshahri na wahadhiri na watafiti wa taasisi ya Darul Hadith kwa juhudi zao za kuandaa stashahada ya Imam Mahdi AS.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadi Reyshahri, Mkuu wa Taasisi ya Kielimu na Kiutamaduni wa Darul Hadith ametoa ripoti fupi na sambamba na kuashiria hatua ya kuonyeshwa hadharani stashahada ya Imam Mahdi (AS) katika wakati huu wa kukaribia maadhimisho ya kuzaliwa mtukufu huyo, amekutaja kufanyika utafiti wa kina kuhusu itibari ya vyanzo muhimu, kutegemea zaidi na zaidi vyanzo vya Kishia na Kisuni, kufanyia tathimini ya kina hoja na dalili zisizo za kunukuu za itikadi ya "Mahdawiyyat," suala la kuzingatia muundo wa kijamii na kuteua vizuri mambo, kuwa na ubainishaji na uchambuzi pamoja na ukosoaji na kufanyia uchanganuzi mitazamo tofauti, kubainisha itikadi za dini nyinginezo kuhusiana na mwokozi wa ulimwengu, kutoa muhtasari na kutafiti ripoti zinazopingana, kuyapatia majibu maswali, shubha na mambo yenye utata na kutoa tahadhari kuhusu mambo yaliyopotoshwa, kuwa ni miongoni mwa sifa kuu za stashahada ya Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).

700 /