Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Imam Ali Khamenei:

Dunia nzima inapaswa kuwasaidia kwa silaha wananchi wa Palestina

Mvuto wa sikukuu ya Idul Fitr umeongezeka maradufu leo kutokana na kuswaliwa Swala ya Idi katika kila kona ya Iran ya Kiislamu huku wananchi waumini wenye mshikamano thabiti wa Iran wakiwa wamejitokeza kwa wingi kwenye misikiti na maeneo mbalimbali ili kutekeleza ibada hiyo tukufu wakimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa taufiki ya kutimiza mwezi wa taqwa na ibada, mwezi mtukufu wa Ramadhani. Katika ibada hiyo ya kimaanawi ambayo kitaifa imesaliwa katika eneo la "Muswala" wa Tehran, Waislamu wa Tehran wamejumuika kwa wingi kwenye eneo hilo mapema leo asubuhi na kutekeleza kwa ufanisi mkubwa swala hiyo iliyongozwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika hotuba ya kwanza aliyoitoa baada ya Swala na Idi, Ayatullah Ali Khamenei ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa sikukuu hii adhimu na kuzitaja majalisi nyingi za Qur'ani Tukufu, dhikri na kulisha masikini pamoja na tawasali na sadaka nyingi zilizotolewa katika kipindi kizima cha mwezi mtukufu wa Ramadhani pamoja na mikesha iliyojaa nuru ya Laylatul Qadr na kujitokeza kwa wingi mno wananchi wa Iran katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds kuwa ni mambo ambayo yamepelekea kupatikana rehema na baraka za Allah. Ameongeza kuwa: Uhakika huo wenye mvuto wa aina yake umelifanya taifa la Iran litekeleze kwa mafanikio makubwa ibada za mwezi uliojaa baraka wa Ramadhani na kuingia kwa furaha kubwa katika idi tukufu ya Fitr.

Ayatullah Khamenei ametumia hotuba yake ya kwanza kutoa nasaha kwa matabaka yote ya wananchi wa Iran walinde na kuendeleza mambo mazuri waliyoyapata katika mwezi uliojaa baraka wa Ramadhani na ameashiria nasaha zake za mwaka jana za kuitaka jamii kujizoesha kula futari nyepesi. Ameongeza kuwa: Kwa bahati nzuri mwaka huu kumeshuhudiwa suala la kutolewa futari nyepesi katika mitaa, barabara na vituo vikuu vya umma na vya kidini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amewausia wananchi akisema: Masuala kama hayo yanasaidia katika kuupa sura yake halisi mtindo wa maisha ya Kiislamu na kuufanya upanue wigo wake kwa haraka sana.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Quds kuwa yameonyesha hima kubwa waliyo nayo wananchi wa Iran na huku akiashiria kushiriki kwa wingi mno watu wa matabaka yote hususan akina mama na watoto wao katika maandamano ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Quds amesisitiza kuwa: Kwa insafu na kwa hakika, maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Quds yalifanyika kwa ufanisi mkubwa sana na kwamba taifa azizi la Iran limewaonesha kwa mara nyingine walimwengu kuwa ni taifa hai lenye misimamo isiyotetereka hata kidogo.

Ayatullah Ali Khamenei ameifanya hotuba yake ya pili katika Swala hiyo ya Idi iwe maalumu kwa ajili ya kuzungumzia kadhia ya Ghaza kutokana na umuhimu mkubwa wa matukio yanayoendelea hivi sasa katika ukanda huo.

Amesema kadhia ya Ghaza ndilo suala nambari moja katika ulimwengu wa Kiislamu na ulimwengu mzima wa ubinadamu.

Vilevile ameashiria namna watoto wadogo, malaika wa Mungu wanavyouliwa kwa umati na Wazayuni katika ukanda huo na jinsi akinamama wa eneo hilo wanavyoteseka na kutwishwa misiba ya kila aina na kusisitiza kuwa: Mbwa mwitu katili na mla nyama za watu anayejulikana kwa jina la utawala wa Kizayuni, anaendelea kufanya jinai kubwa mno hivi sasa huko Ghaza na kwamba watu wenye hisia za utu wana jukumu la kusimama kukabiliana na jinai za utawala huo katili unaofyonza damu za wanadamu.

Ayatullah Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kugusia nukta tatu muhimu kuhusiana na kadhia ya Ghaza.

1- Umuhimu wa kulaaniwa na kuadhibiwa Wazayuni wanaotenda jinai pamoja na waungaji mkono wao.

2- Kupongeza mapambano na kusimama kidete kunakostahiki kupigiwa mfano kwa wananchi wa Ghaza.

3- Ulazima wa kutiwa nguvu na kupewa silaha taifa la Palestina.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja jinai za wazi wazi zinazofanywa na viongozi wa utawala wa Kizayuni huko Ghaza kuwa ni uangamizaji wa kizazi na ni maafa makubwa katika historia na kusisitiza kuwa: Watenda jinai hizo pamoja na madola ya kibeberu yanayowasaidia na kuwaunga mkono watenda jinao hao, wote wanapaswa kulaaniwa katika kona zote za dunia na inabidi waadhibiwe kwa jinai zao hizo, ni sawa tu watenda jinai hao wawe bado wako madarakani au wawe wameshaporomoka na wameshaondoshwa madarakani na kwamba hilo ndilo jambo ambalo watu wenye utu na ubinadamu duniani wanapaswa kulipigania.

Subira na uvumilivu wa hali ya juu mno na wa kupigiwa mfano pamoja na muqawama unaostahiki kupongezwa na kusifiwa wa wananchi wa Ghaza, ni nukta ya pili muhimu iliyogusiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba hiyo ya pili ya Sala ya Idi.

Amesema, wananchi wa Ghaza wanaishi katika eneo ambalo limefungiwa njia zote na limezingirwa kila upande huku hata hizo suhula chache walizo nazo zikishambuliwa usiku na mchana tena kiuadui mkubwa na adui muovu Mzayuni ambaye ni khabithi, najisi na asiye na chembe ya huruma, lakini pamoja na hayo wananchi wa ukanda huo wanaonyesha ushujaa mkubwa na muqawama wa kipekee.

Ayatullah Khamenei ametaja mapambano na nguvu za kusimama kidete za wananchi madhulumu wa Ghaza kuwa ni somo kubwa kwa watu wote na kuongeza kuwa: Muqawama huo usiotasawirika unaonesha nguvu za kusimama kidete anazoweza kuwa nazo mwanadamu na namna nguvu za muqawama za taifa fulani zinavyoweza kuwa kubwa mno. Amesema, hatimaye wananchi hao kwa taufiki na msaada wa Mwenyezi Mungu wataweza kumshinda adui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria njama za utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake wahalifu yaani Marekani na Ulaya za kutaka kuwalazimisha wananchi wa Ghaza wakubali usitishaji vita wenye madhara kwao na wenye manufaa kwa watenda jinai Wazayuni na waungaji mkono wao na kusema kuwa, hadi kufikia sasa tayari adui jibwa mtenda jinai, anajuta kujiingiza kwenye kinamasi huko Ghaza na ndio maana anatafuta usimamishaji vita kwa kila hali na hizo ni dalili za wazi kuwa muqawama umeshinda.

Ameongeza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana waungaji mkono wa watenda jinai Wazayuni nao wakawa wanafanya kila njia kutaka kuwabebesha wananchi wa Ghaza usitishaji vita ili kuuokoa utawala huo katili.

Vilevile amebainsha nukta ya tatu ambayo ni njama za viongozi wa kisiasa wa kambi ya kiistikbari akiwemo Rais wa Marekani za kutaka kuzipokonya silaha harakati za Hamas na Jihadul Islami za Palestina na kuongeza kuwa: Lengo la kutaka kuupokonya silaha muqawama ni kutaka kuwafanya Wazayuni waweze kuingamiza Palestina wakati wowote wanaopenda na Wapalestina wasiwe na uwezo wa kufanya lolote wala kujihami kwa njia yoyote ile.

Mwishoni mwa khutba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Kinyume na zilivyo njama na mitazamo ya waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni unaoua watoto wadogo na malaika wa Mungu, ulimwengu mzima ukiwemo ulimwengu wa Kiislamu una jukumu wa kulisaidia na kulipa silaha taifa la Palestina kadiri unavyoweza ili liweze kujihami mbele ya mashambulizi ya Wazayuni.

 

700 /