Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Amirijeshi Mkuu:

Maadui wanachafua jina la Uislamu kwa kuunda makundi yanayoua watu wasio na hatia

Sherehe za nane za kuhitimu masomo, kula viapo na kupandishwa vyeo wanafunzi wa vyuo vikuu vya maafisa wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, zimefanyika leo asubuhi (Jumatatu) mbele ya Ayatullah Ali Khamenei, Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya Jeshi la Ulinzi la Iran katika Chuo Kikuu cha maafisa wa jeshi cha Imam Ali AS.

Mwanzoni mwa kuingia kwake katika uwanja wa sherehe hizo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekwenda kwenye maziara ya mashahidi na sambamba na kuwasomea al Fatiha mashahidi hao, amemuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awapandishe daraja za juu za utukufu, mashahidi wa vita vya kujihami kutakatifu (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya taifa la Iran).

Baada ya hapo, Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya jeshi la Iran, amekagua vikosi mbalimbali vilivyokuwa vimepanga paredi katika uwanja huo.

Katika sherehe hizo, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, vikosi vya ulinzi vya Iran ni nguzo muhimu za nguvu za nchi na kusisitiza kuwa: Mambo ya lazima ya kuvifanya vikosi vya ulinzi kuwa na uimara na nguvu za kweli ni kujipamba kwa imani, busuri, muono wa mbali, ari, kutotetereka na kuhisi wajibu wa kutekeleza vilivyo majukumu sambamba na kuwa na nguvu kazi iliyojiimarisha vilivyo kwa mafunzo bora na zana za kisasa.

Vilevile amesema dunia ya leo ina kiu ya kupata ujumbe wa ukombozi wa dini ya Uislamu wa kweli na kuongeza kuwa: Wanaoutakia mabaya Uislamu na mabeberu wa dunia wanafanya njama za kutumia sanaa, siasa, mifumo ya kijeshi na kila walicho nacho ili kuzuia sauti ya Uislamu wa kweli isiwafikie walimwengu, lakini tayari sauti hiyo imeshafika kulikokusudiwa na dalili zake ni namna madola ya kibeberu yanavyozidi kutiwa hofu na dini hiyo tukufu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia pia ulazima wa kulifuatilia vilivyo, kwa kina na si kijuu juu suala la kuviimarisha kwa kila namna vikosi vya ulinzi nchini Iran na kuongeza kuwa: Kuwa na idadi kubwa ya askari na masomo na zana nyingi za kisasa za kijeshi si jambo pekee linalovifanya vikosi vya ulinzi vya nchi kuwa na nguvu, bali vikosi hivyo vinapaswa kujipamba kimaanawi, nia ya kweli, kuelewa vilivyo uhakika na kuhisi wajibu wa kutekeleza vilivyo majukumu yao na kujua vyema stratijia na misimamo inayopaswa kuchukuliwa.

Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Iran ameashiria pia uwezo wa kimaanawi na ustadi wa kielimu na umahiri wa ubunifu na nia ya kweli uliooneshwa na vikosi vya ulinzi vya Iran katika kipindi cha miaka minane ya kujihami kutakatifu na kuongeza kuwa, dunia inavizingatia na kuviangalia kwa jicho la kina vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuvipa uzito wa hali ya juu kwani dunia inajua kuwa popote pale patakapohitajika suala la kuonyesha uwajibika na uimara wa kijeshi, basi vikosi vya ulinzi vya Iran vitajitokeza kwa nguvu, kwa uimara wa hali ya juu na kwa sura bora kabisa.

Vilevile ameashiria mambo mengi ya kujivunia ya Chuo Kikuu cha Maafisa wa Kijeshi cha Imam Ali AS na mashahidi watukufu wa vikosi vya ulinzi vya Iran wakiwa ni nguzo muhimu ya nguvu za Iran na kuwahutubu viongozi wa vyuo vikuu vya maafisa wa kijeshi akiwaambia: Jiimarisheni zaidi katika majimui hii iliyojaa baraka ya kielimu na kijeshi kwa ajili ya kuviimarisha kila kukicha vikosi vya ulinzi ambavyo ni moja ya nguzo muhimu za nchi na kama wanavyofanya vijana watafiti na wasomi nchini ambao wamefanya mambo ya kustaajabisha katika uwanja wa kielimu na ubunifu, nyinyi pia tumieni vizuri umahiri wa kielimu na vipaji vya ubunifu kutoa kila leo vitu vipya vyenye manufaa katika upande wa kijeshi ili kuifanya taasisi ya kijeshi nchini Iran iwe katika vilele vya juu kabisa vya ubora.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, hivi sasa mwanadamu anahitajia mno ujumbe wa Uislamu wa taifa la Iran kuliko wakati mwingine wowote na kuongeza kuwa, wapenda makubwa na mabeberu wa dunia, wana woga na wasiwasi mkubwa wa kuzidi kuenea ujumbe wenye kutia uhai wa Uislamu wa kweli ambao unatishia maslahi ya mabeberu hao na wanatumia kila walicho nacho hususan sanaa ili kuzuia mafundisho ya kweli ya Uislamu yasiwafikie watu duniani.

Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kuunda makundi yenye silaha na kuyapachika jina la Uislamu au dola la Kiislamu na kuyatumia makundi hayo kuua kwa umati watu wasio na hatia kuwa ni mfano mwingine unaotumiwa na maadui wa Uislamu kueneza chuki dhidi ya Uislamu ili ujumbe wa dini hiyo tukufu usiwafikie walimwengu na kuongeza kuwa: Ujumbe wa Uislamu wa kweli unalingania ubinadamu, ni ujumbe wa ufanisi, heshima, kulinda hadhi ya mwanadamu na kuishi kwa amani na usalama na kwamba wasioutakia mema Uislamu hawataki mataifa ya dunia yapate ujumbe huo mtukufu wa Uislamu.

Aidha amewahutubu wanachuo wa Chuo Kikuu cha Maafisa wa Kijeshi cha Imam Ali AS akiwasisitizia kwamba: Kizazi cha vijana kilichokutangulieni nyinyi kiliubeba ujumbe wa Uislamu wa kweli kupitia medani za vita, siasa na Mapinduzi na kuwafikishia walimwengu. Hivi sasa nyinyi ambao mumerithi yale yaliyopiganiwa na mashahidi hao watukufu, mnapaswa kufanya jitihada zenu zote kufuata nyayo za watu hao watukufu kuwafikishia walimwengu ujumbe huo.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Brigedia Jenerali Fouladi, Kamanda wa Chuo Kikuu cha Maafisa wa Kijeshi cha Imam Ali AS sambamba na kumkaribisha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ripoti fupi kuhusu ratiba na kazi za masomo na malezi kwenye Chuo Kikuu hicho katika masuala mbalimbali kama vile kuimarisha imani, muono wa mbali na kushikamana na dini pamoja na kunyanyua ubora wa masomo na kuyafanya kuwa ya kisasa na kuimarisha vipaji na ubunifu wa hali ya juu.

Katika sherehe hizo Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewapa zawadi makamanda, wahadhiri, wahitimu, wanachuo bora wa vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi pamoja na mmoja wa mama wa mashahidi, na amewapandisha pia cheo mwakilishi wa wanachuo wapya pamoja na wahitimu wa masomo katika vyuo vikuu vya maafisa hao wa kijeshi.

Katika sherehe hizo, wanachuo wa vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi wameonesha mazoezi mbalimbali ya kijeshi katika uwanja huo.

Mwishoni mwa sherehe hizo, vikosi vilivyokuwepo kwenye uwanja huo vimepita kwa gwaride mbele ya jukwaa alilokuwepo Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei.

700 /