Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Matakfiri wanapigana na Waislamu badala ya kupambana na Wazayuni

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo (Jumanne) amehutubia hadhara ya maulamaa, wanavyuoni, wasomi na wageni walioshiriki kwenye Kongamano la Kimataifa la Mirengo ya Kitakfiri kwa Mtazamo wa Maulamaa wa Kiislamu na kusema kuwa kufufuliwa  makundi ya kitakfiri katika miaka ya hivi karibuni ni tatizo lililopandikizwa na mabeberu katika ulimwengu wa Kiislamu. Ameashiria harakati za mrengo habithi wa kifakfiri zinazotumikia malengo ya Marekani, madola ya kikoloni na utawala wa Kizayuni wa Israel hususan njama za makundi hayo za kujaribu kuwasahaulisha Waislamu suala muhimu zaidi la ulimwengu wa Kiislamu yaani kadhia ya Palestina na Msikiti wa Aqsa na kusisitiza kuwa, kuanzisha mwamko wa kielimu, kimantiki na wa pande zote kwa ajili ya kung'oa mizizi ya mrengo unaowakufurisha Waislamu wengine, kuwazindua Waislamu kuhusu njama za siasa za kibeberu za kutaka kuhuisha mrengo huo na kulipa umuhimu mkubwa suala la Palestina ni miongoni mwa nyadhifa na wajibu mkubwa zaidi unaopeswa kupewa kipaumbele na maulamaa wa ulimwengu wa Kiislamu.

Mwanzoni wma hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewapongeza Ayatullah Makarim Shirazi, Ayatullah Jaafar Subhani na maulamaa wengine wa Qum waliofanya jitihada kubwa za kuitisha kongamalo hilo la kimataifa na kuanzisha harakati kubwa ya kielimu kati ya maulamaa wa ulimwengu wa Kiislamu ya kukabiliana na mrengo wa kitakfiri. Asema: Katika kuchunguza mrengo huu hatari unaokufurisha Waislamu wengine kuna ulazima wa kutiliwa maanani maudhui kuu ambayo ni kuanzisha mapambano ya pande zote dhidi ya mrengo uliohuishwa tena wa kitakfiri ambao ni mkubwa zaidi kuliko kundi moja tu linaloitwa Daesh, bali kwa hakika Daesh ni tawi moja la mti huo muovu.

Baada ya hapo Ayatullah Khamenei amezungumzia nukta nyingine muhimu na kusema: Mrengo wa kitakfiri na nchi zinazouunga mkono zinatumikia kikamilifu malengo ya mabeberu yaani Marekani, madola ya kikoloni ya Ulaya na utawala wa Kizayuni, kwa kutumia vazi la Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mifano kadhaa ya kuonesha jinsi makundi hayo yanavyotumikia malengo ya ubeberu na kukabiliana na ulimwengu wa Kiislamu. Amelitaja suala la kujaribu kupotosha harakati ya mwamko wa Kiislamu kuwa ni ushahidi wa kwanza wa kuthibitisha kwamba fikra ya kitakfiri inatumikia malengo ya mabeberu na kuongeza kuwa: Mwamko wa Kiislamu ni harakati iliyo dhidi ya Marekani, udikteta na vibaraka wa Marekani lakini makundi ya kitakfiri yamezuka ili kukabiliana na harakati hiyo adhimu iliyo dhidi ya ubeberu na kuifanya kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na mauaji ya Waislamu kwa Waislamu.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, mstari wa mbele wa mapambano ya Waislamu wa eneo hili ni Palestina inayokaliwa kwa mabavu, lakini makundi ya kitakfiri yamegeuza mstari huo na kuingia kwenye mitaa na miji ya nchi za Iraq, Syria, Pakistan na Libya na kwamba hiyo ni moja ya jinai kubwa sana zisizoweza kusahaulika zinazofanywa na makundi hayo ya kitakfiri.

Amesema, kupotosha harakati ya mwamko wa Kiislamu ni kuitumikia Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni pamoja na mashirika yao ya kijasusi. Ameongeza kuwa: Ushahidi mwingine unaothibitisha kwamba vitendo vya makundi hayo vinatumikia malengo ya mabeberu ni kwamba wanaoendesha fikra hiyo ya kitakfiri hawasemi lolote dhidi ya utawala wa Kizayuni bali wanafikia hata kushirikiana na utawala huo dhidi ya Waislamu. Lakini hao hao utawaona wako mstari wa mbele katika vitendo vya kutoa pigo kwa nchi na mataifa ya Waislamu.

Ayatullah Khamenei amevitaja vitendo vya kuangamiza miundombinu yenye thamani kubwa ya nchi za Kiislamu vinavyofanywa na makundi hayo yanayoeneza fitna katika ulimwengu wa Kiislamu kuwa ni mfano mwingine unaothibitisha kwamba makundi hayo yanatumikia malengo ya maadui wa Uislamu na kuongeza kuwa: Hatua nyingine ya kihabithi zaidi ya makundi ya kitakfiri ni kupotosha sura halisi ya Uislamu ambayo ni dini ya upendo, ya kimantiki, ya kufanya mambo kwa kutumia busara na ya kuhurumiana, na kuonesha picha za jinai kubwa zinazofanywa na makundi hayo kama za kuchinja watu wasio na hatia, kupasua mwili na kutoa moyo wa Muislamu na kuutafuna tafuna kwa meno mbele ya kamera tena kwa jina la Uislamu!

Amesema, ushahidi mwingine wa kwamba makundi ya kitakfiri yanayotumikia malengo ya mabeberu ni kutojali kwao hata kidogo jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika mashambulizi yake ya siku 50 huko Ghaza na kuwaacha peke yao Wapalestina katika mashambulizi hayo ya Ghaza. Ameongeza kuwa, ushahidi mwingine ni namna makundi hayo ya kitakfiri yanavyopotosha hamasa na mwamko walioupata vijana wa ulimwengu wa Kiislamu baada ya kutokea mwamko wa Kiislamu katika ulimwengu huo na inasikitisha kuona kuwa makundi hayo yanatumia vibaya hamasa hizo za vijana wa Kiislamu kwa ajili ya kuua Waislamu wengine wasio na hatia.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja mfano mwingine kuwa ni hatua ya hivi karibuni na ambayo imekuwa ikikaririwa mara kwa mara ya ndege za Marekani kulirushia silaha za kijeshi kundi linaloitwa Daesh huko Iraq na kusisitiza kuwa: Pamoja na hayo yote Marekani inadai kuwa imeunda muungano wa kupambana na Daesh, jambo ambalo kwa hakika ni uongo wa wazi kwani lengo kuu la muungano huo ni kuhakikisha kwamba fitina ya vita na mapigano kati ya Waislamu inaendelea kuwepo, lakini hawataweza kufikia malengo yao hayo.

Baada ya hapo, Ayatullah Ali Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia majukumu makubwa ya maulamaa wa ulimwengu wa Kiislamu katika kipindi cha sasa na kuongeza kuwa: Moja ya malengo hayo ni maulamaa hao wa madhehebu mbalimbali kuleta mwamko wa kielimu, wa kimantiki na mkubwa kwa ajili ya kung'oa kikamilifu mizizi ya fikra ya kitakfiri.

Amesema: Mrengo huo wa kitakfiri unatumia kaulimbiu ya uongo ya kudai kuwa ni Salafus Salih, hivyo inabidi kutumia lugha ya dini, elimu na mantiki kuthibitisha kuwa Salafus Salih iko mbali kabisa na vitendo vya mrengo huo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Inabidi vijana wasio na hatia waliotumbukia katika mtego wa mrengo huo habithi waokolowe kupitia mwamko huo wa kielimu na kimantiki, na kwamba hilo ni jukumu linalopaswa kufanywa na maulamaa.

Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kuamsha watu kuhusiana na nafasi ya siasa za Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni katika kufufua mrengo huo wa kitakfiri kuwa ni moja ya majukumu makubwa ya maulamaa katika nchi za Waislamu na kuongeza kuwa: Jukumu la tatu muhimu la maulamaa ni kuipa umuhimu wa hali ya juu kadhia ya Palestina na Masjidul Aqsa na kuzuia kusahauliwa kadhia hiyo ambayo ndilo suala muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu.

Vilevile ameashiria uamuzi wa hivi karibuni wa Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni la kudai kuwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni ya Mayahudi na kuongeza kuwa: Utawala wa Kizayuni wa Israel unapigania kuiteka kikamilifu Quds na Masjidul Aqsa na kuzidi kuwadhoofisha Wapalestina. Amesisitiza kuwa mataifa yote ya Kiislamu pamoja na maulamaa, wanapaswa kuzitaka tawala za nchi zao kulipa umuhimu mkubwa suala la Palestina.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hatua iliyochukuliwa na Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) ya kutangaza siasa za kuiunga mkono Palestina na kuufanya adui utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa: Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, serikali na wananchi wote wa Iran, wote kwa pamoja wana msimamo mmoja katika suala zima la kuiunga mkono Palestina na kuutambua utawala wa Kizayuni  kuwa ni adui na kwamba hawajakwenda kinyume na njia hiyo iliyochorwa na Imam Khomeini kwa miaka 35 iliyopita.

Ayatullah Khamenei amesisitiza pia kuwa taifa na vijana wa Iran wanawaunga mkono wananchi wa Palestina kwa moyo wao wote na ni wapenzi wa mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa: Alhamdulillah kwa uwezo na taufiki ya Mwenyezi Mungu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikufungwa na mipaka ya hitilafu za kimadhehebu na kama ambavyo inaisaidia Hizbullah ya Waislamu wa Kishia huko Lebanon, vivyo hivyo inazisaidia Hamas, Jihadul Islami na makundi mengine ya Waislamu wa Kisuni huko Palestina na kwamba itaendelea kutoa misaada kwa makundi hayo.

Amesema, kuwatia nguvu ndugu zetu wa Kipalestina huko Ghaza ni mfano wa wazi wa misaada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wa Palestina na kusisitiza kuwa: Kama ambavyo tumetangaza huko nyuma, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan nao inabidi uzatitiwe kwa silaha na uwe na uwezo wa kujilinda, na bila ya shaka yoyote jambo hilo litatendeka.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, maadui wa ulimwengu wa Kiislamu ni dhaifu mno hivi sasa kuliko huko nyuma na huku akiashiria matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama ziliyo nayo nchi za Ulaya na vilevile matatizo makubwa na mabaya zaidi iliyo nayo Marekani katika masuala ya maadili, masuala ya kisiasa husuasan masuala ya mali na kifedha pamoja na kuporomoka hadhi ya heshima ya Marekani na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni nao ni dhaifu mno hivi sasa ikilinganishwa na huko nyuma. Amesema utawala huo ndio ule ule ambao katika miaka ya huko nyuma ulikuwa ukijigamba kuwa unapigania kuunda dola kubwa linaloanzia Mto Nile hadi Mto Furat, lakini hivi sasa katika vita vya siku 50 vya Ghaza, ilitumia nguvu na uwezo wake wake na ikashindwa kuangamiza mahandaki na njia za chini ya ardhi za Hamas na Jihadul Islami.

Ayatullah Khamenei amekumbushia matatizo na kushindwa maadui wa Uislamu katika eneo la Mashariki ya Kati hususan katika nchi za Iraq, Syria na Lebanon na kusema kuwa: Mfano mwingine wa udhaifu wa adui ni kadhia ya nyuklia ya Iran. Amesema Marekani na nchi nyingine za kikoloni za Ulaya zote zimekusanyika pamoja ili kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika suala la nyuklia lakini zimeshindwa na zitaendelea kushindwa katika siku za usoni.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Alizadeh Mousavi, Katibu wa Kongamano la Mirengo ya Kufurutu Ada na Kitakfiri kwa Mtazamo wa Maulamaa wa Kiislamu ametoa ripoti fupi kuhusiana na namna kongamano hilo lilivyofanyika kwa ufanisi na kusema kuwa: Katika siku mbili za kongamano hilo, kuliundwa kamati mbalimbali za kitaalamu na kiistratijia na kuchunguza na kutafakari kwa kina mizizi ya makundi ya kitakfiri, masuala yao ya kisiasa na vilevile njia za kuweza kung'oa mizizi ya fikra nzima ya kitakfiri.

Vilevile amegusia namna kulivyofanyika vikao vingine mbalimbali kabla ya kongamano hilo katika nchi za Syria na Pakistan na kuwasilishwa zaidi ya makala 700 kwa sekretarieti ya kongamano hilo. Ameongeza kuwa: Kongamano hilo liliwakutanisha pamoja maulamaa 315 wa ulimwengu wa Kiislamu na kwamba makala 144 bora zilizoandikwa kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu, zimekusanywa na kuchapishwa katika jildi nane za vitabu.

700 /