Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Taifa la Iran halina haja ya kuaminiwa na Marekani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo asubuhi (Alkhamisi) ameonana na wajumbe wa Baraza Kuu la Basiji na wawakilishi wa matabaka mbalimbali ya Basiji na huku akiashiria udharura wa kuwa na hisia za wajibu wa kutekeleza majukumu yao ya kibinadamu na ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu na kuwa na busuri na muono wa mbali kwamba ni nguzo mbili kuu za tafakuri wa kimantiki ya Basiji, ameishukuru timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na jitihada zake kubwa na kulipa kwake uzito wa hali ya juu suala hilo na kutotetereka katika mazungumzo hayo. Vilevile ameashiria namna taifa la Iran lisivyo na haja ya kuonesha nia njema kwa Marekani na kuongeza kuwa, hatupingi kuongezewa muda mazungumzo hayo kwa dalili zile zile zilizotufanya tusipinge kufanyika asili ya mazungumzo yenyewe. Tab'an tunakubaliana na maamuzi yoyote yale ya kimantiki na ya kiadilifu, lakini tunajua pia kuwa, ni dola la Marekani ndilo lililo na haja sana na kufikiwa makubaliano kwani itapata madhara kama hakutafikiwa makubaliano yoyote na hata kama itatokezea mazungumzo hayo yashindwe kufikia mwafaka, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitapata madhara.

Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, siri ya mafanikio makubwa ya Basiji katika medani mbalimbali pana na kubwa ni kujipamba kwake kwa fikra sahihi na madhubuti, pamoja na kujipamba kielimu na kimantiki na kufanya kazi kwa mapenzi na kwa nia ya kweli. Ameongeza kuwa, msingi wa awali na mkubwa zaidi wa fikra ya Basiji na ambaoo chimbuko lake ni misingi madhubuti ya dini ya Kiislamu, ni kuhisi wajibu wa kutekeleza majukumu ya kibinadamu na ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mtu binafsi, kwa ajili ya familia, kwa ajili ya jamii na kwa ajili ya wanadamu wote.

Ameongeza kuwa: Msingi wa pili wa fikra ya Basiji ambao unakamilisha msingi wa kwanza na ambao ni sharti la lazima ni kuwa na mtazamo wa mbali, mpana na wa kuangalia mambo katika uhalisia wake kwa maana ya kuzijua vizuri zama na vitu vya kuvipa kipaumbele, kuwajua vizuri marafiki na maadui na kuzijua vyema mbinu na njia za kukabiliana na adui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kukosekana busuri na muono wa mbali kuwa kunaandaa uwanja za kutumbukia katika makosa, utovu wa welewa na kufahamu mambo vibaya na kwenda pogo. Amesisitiza kuwa: Watu wasio na busuri na mtazamo wa mbali ni kama wale maskini ambao walitumbukia kwenye mtego wa fitna ya mwaka 88 (Hijria Shamsia - yaani machafuko ya mjini Tehran ya mwaka 2009) ambao wanafanya mambo yao kwenye anga zilizogubikwa na vumbi na hivyo si tu wanamsaidia adui, bali hata wanawalenga na kuwatia matatizoni pia marafiki.

Ayatullah Khamenei vilevile amesisitiza kwamba, kuwa na hisia za kuhisi wajibu wa kutekeleza vizuri majukumu bila ya kuwa na busuri na muono wa mbali ni jambo la hatari mno na kuongeza kuwa: Kuna baadhi ya watu katika kipindi cha mapambano kabla ya Mapinduzi (ya Kiislamu ya nchini Iran) na katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, ni kweli wamekuwa wana hisia za wajibu wa kutekeleza ipasavyo majukumu yao lakini hawana muono wa mbali na mwishowe watu hao wameiletea madhara harakati ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, Mapinduzi na nchi.

Ameashiria pia namna alivyokuwa anasisitizia mno umuhimu wa kuwa na muono wa mbali wakati wa fitna ya mwaka 88 na kuongeza kuwa: Kuna baadhi ya watu tangu siku hizo walikuwa wanachukia wanapoona kunasisitiziwa suala la kuwa na muono wa mbali, lakini mimi hadi leo hii ninasisitizia udharura wa kuwa na muono wa mbali kwani kadiri majukumu ya mtu yanavyokuwa mengi na makubwa na ikawa mtu huyo hana busuri na muono wa mbali, ndivyo hatari zake zinavyokuwa kubwa zaidi na mtu wa namna hiyo kamwe hawezi kuaminika.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria namna Imam Khomeini Khomeini alivyokuwa na muono wa mbali mno na wa wazi katika nyakati na vipindi tofauti na namna alivyobainisha njia na kuweka wazi misimamo inayotakiwa kuchukliwa katika masuala yote na kuongeza kuwa: Imam wetu mtukufu Mwenyezi Mungu amrehemu alitoa amri ya kuundwa Basiji kama ambavyo pia alionyesha msimamo, njia na lengo kuu la kuundwa Basiji na kusema: Ifokeeni Marekani kwa kadiri ya uwezo wenu.

Vilevile ameashiria matamshi maarufu ya Imam Khomeini  aliposema, "Kuulinda mfumo (wa Jamhuri ya Kiislamu) ndio wajibu mkubwa zaidi kuliko wajibu wowote mwingine" na kuongeza kuwa: Wale watu ambao wameshindwa kuelewa maneno hayo ya Imam (quddisa sirruh) kuna wakati walifanya makosa ya kutisha.

Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei ametoa muhtasari wa matamshi yake katika sehemu hiyo ya hotuba yake na kuongeza kuwa: Haipasi kuacha hata kwa sekunde moja kuhisi wajibu wa kutekeleza majukumu ukiwa ndio msingi mkuu wa tafakuri ya Basiji, na vilevile kuwa na busuri na muono wa mbali, likiwa ni sharti la lazima la msingi huo mkuu wa fikra ya Basiji.

Amesisitiza kwamba, ni kwa kuwa na mtazamo huo ndipo tutakapoweza kutoa maana halisi na ya kina ya Basiji. Ameongeza kuwa: Mtu yeyote anayefanya kazi zake kwa nia ya kweli na kwa kuwa na hisia za wajibu wa kutekeleza majukumu huku akiwa amejipamba kwa sifa ya kuwa na busuri na mtazano wa mbali, huyo ni Basiji katika sehemu yoyote aliyo. Hivyo tunaweza kusema kuwa, idadi kubwa mutlaki ya wananchi wa Iran, ni Mabasiji.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an kambi kuu ya wigo huo adhimu ni kikosi cha muqawama cha Basiji ambacho kinapaswa kutoa ilhamu ya nidhamu, mafunzo, malezi, harakati na kuwepo imara katika nyuga na medani zote.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, wigo wa kazi za Basiji hauna mwisho na hauna mipaka na kuongeza kuwa: Nyuga za ulinzi, nyuga za ujenzi wa nchi, siasa, uchumi, sanaa, sayansi na teknolojia, jumuiya za kidini na kwa hakika nyuga zote nyingine ni medani za kuwepo Basiji ndani yake.

Vilevile amesisitiza kuwa, katika medani zote hizo kuna vigezo vikuu na vielelezo vya wazi vya Mabasiji ndani yake na kuongeza kuwa: Watu hao wenye vipawa katika nyuga mbalimbali za kielimu na kiutafiti wameingia kwenye medani tofauti kutoka ndani ya Basiji hususan katika ule wakati ambao adui alifanya njama kwa ukhabithi mkubwa za kulifungia taifa la Iran milango yote na kuwazuia wagonjwa wa Iran kupata dawa za mionzi. Wakati huo shahid Shahriyar na wenzake walifanya jitihada kubwa za kibasiji na kufanikiwa kurutubisha urani kwa asilimia ishirini na kuzalisha sahani za fueli nyuklia zilizokuwa zinahitajika (kwa ajili ya matibabu ya mionzi).

Ayatullah Udhma Khamenei aidha ameashiria nukta nyingine muhimu na kuongeza kuwa: Ni tafakuri ya Basiji ambayo iliasisiwa na Imam wetu mtukufu (quddisa sirruh) ndiyo ambayo leo hii imeenea hadi nje ya mipaka ya Iran na kufika kwa mataifa mengine ambapo hivi sasa ni mithili ya harufu njema ya maua ya msimu wa machipuo, hakuna mtu yeyote anayeweza kuizuia.

Ameongeza kwamba: Upepo mwanana unaoleta uhai na nguvu mpya wa fikra ya Basiji hivi sasa yanaonekana matunda yake katika nchi za Iraq, Syria, Lebanon na Ghaza huko Palestina na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu katika mustakbali si wa mbali sana, utavuma pia katika Quds tukufu na Masjidul Aqsa.

Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ni kwa kuzingatia mambo hayo na ni kwa baraka za tafakuri ya Basiji ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ni taifa lisiloshindika.

Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Hatua ya wingi mutlaki wa wananchi wa Iran ya kuwa Mabasiji ndiyo sababu ya kutoshindika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu lakini hilo halina maana ya kwamba sasa watu wajipweteke, wajisahau na waghafilike na mitihani na kutojipanga inavyopasa kukabiliana na hali tofauti.

Amesisitiza kwamba: Msimamo mkuu wa harakati ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni kupambana na ubeberu na dola la kiistikbari la Marekani na hakupaswi kuweko uvivu wa aina yoyote ile katika jambo hilo au kufanyika makosa ndani yake. Amesema: Tab'an sisi hatuna tatizo na wananchi au na nchi ya Marekani, bali tatizo letu sisi ni ubeberu na kupenda makuu watawala wa Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu kuongezewa muda mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la tano ongeza moja kwamba: Dalili ile ile ambayo imetufanya tusipinge asili ya kufanyika mazungumzo ni dalili hiyo hiyo ndiyo inayotufanya tusipinge kuongezewa muda mazungumzo hayo lakini hapa inabidi tubainishe pia nukta kadhaa.

Amesema, timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran inafanya jitihada kubwa, inayachukulia kwa uzito wa hali ya juu mazungumzo hayo, ina uchungu wa nchi, iko imara na inafanya mambo yake kimantiki na kuongeza kuwa: Kwa haki na kwa insafu, timu ya Iran imesimama imara mbele ya ubeberu, na tofauti na upande wa pili, siku zote ina msimamo mmoja ulio wazi na haibadilishi badilishi maneno yake kama unavyofanya upande wa pili.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia namna Marekani ilivyo na misimamo ya kindumilakuwili na kuongeza kuwa: Katika vikao vya faragha na katika barua zao, utawaona Wamarekani wanasema kitu fulani na wanapokwenda mbele ya kadamnasi ya watu wanabadilisha maneno yao na kusema kitu kingine.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria matokeo ya ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ya "kidiplomasia, kisiasa na vyombo vya habari" vya pande zinazofanya mazungumzo na Iran na kuongeza kuwa, nyuma ya kila anayefanya mazungumzo na Iran kuna jeshi jingine kubwa linaloutia nguvu na kuusaidia upande huo, na Marekani ndiyo yenye tabia mbaya zaidi huku Waingereza wakiwa ndio wanaofanya maudhi makubwa zaidi.

Ameongeza kuwa, Tunapoyaangalia mazungumzo hayo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la tano ongeza moja tutaona kuwa, kama mazungumzo hayo hayatafanikiwa, pande zote zinazofanya mazungumzo hayo zitapata madhara likiwemo pia taifa la Iran lakini watakaopata madhara makubwa zaidi ni Wamarekani.

Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Tunaamini kwa yakini na kwa ushahidi madhubuti kwamba lengo hasa la uistikbari ni kulizuia taifa la Iran lisinawiri, lisiwe imara na lisizidi kuwa na nguvu.

Amesema, suala la nyuklia ni kisingizio tu kinachotumiwa na mabeberu kwa nia ya kufanikisha malengo hayo na kuongeza kuwa: Tab'an waistikbari wana na visingizio vingine, lakini lengo kuu la vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi ambayo ndiyo silaha kuu inayotumiwa na mabeberu hao, ni kuzuia ustawi na maendeleo ya Iran.

Aidha amekutaja kukiri vyombo vya habari vya Magharibi kuhusu kupungua umaarufu wa Rais wa Marekani, kushuka mno idadi ya watu walioshiriki kupiga kura katika uchaguzi wa hivi karibuni wa Marekani na matukio ya Ferguson huko Marekani kuwa ni katika dalili na ushahidi mwingine unaoonesha kuwepo mpasuko mkubwa baina ya wananchi na serikali ya Marekani na huku akibainisha namna serikali ya Washington inavyohitajia mno mazungumzo ya nyuklia amesema: Kwa kuzingatia matatizo hayo yanayoongezeka kila leo, viongozi wa Marekani ndio walio na haja kubwa ya kupata mafanikio na ushindi mkubwa katika jambo fulani (ili wapunguze makali ya matatizo waliyo nayo ndani ya Marekani).

Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Lakini tofauti na Marekani, kama mazungumzo hayo yatashindwa kufikia mwafaka, kwetu sisi "mbingu hazitaanguka juu ya ardhi" (mambo yetu sisi hayataharibika) kwani tayari tuna utatuzi wa mambo yetu, nao ni uchumi wa kusimama kidete.

Amesema, katika kipindi kifupi tu, uchumi wa kusimama kidete umepunguza mashambulizi ya adui na kuongeza kuwa: Kama wanavyoamini wataalamu wa mambo, ni kwamba, mtazamo na fikra hiyo itaimarika na kufikia katika vilele vya juu vya harakati adhimu ya taifa la Iran katika kipindi cha kati na kirefu kijacho.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa pia matamshi ya baadhi ya viongozi wa Marekani waliyoyatoa baada ya kuongezewa muda mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 na kuongeza kuwa: Wamarekani wanadai kuwa, Iran lazima ivutie imani ya jamii ya kimataifa. Amma katika matamshi yao hayo kuna nukta mbili ni ghalati kikamilifu na si sahihi hata chembe.

Ameongeza kuwa: Nukta ya kwanza ni kwamba, nchi hizo chache ambazo zimejikuza na kujipa jina la jamii ya kimataifa, zinajaribu kuthibitisha madai yao hayo kwa kudharau uwepo wa nchi nyingine dunia kama vile wanachama 150 wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande wowote NAM na mabilioni ya watu duniani ambao kimsingi hao ndio wanaopasa kuitwa jamii ya kimataifa.

Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Nukta ya pili ni kwamba, sisi hatuna haja kabisa ya kutafuta imani ya Marekani na kimsingi sisi hatutaki kabisa kuvutia imani yake kwani jambo hilo halina umuhimu wowote kwetu sisi.

Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Hao ni mabeberu na sisi hatuwezi kamwe kuwa kitu kimoja na mabeberu.

Aidha amegusia nukta nyingine iliyomo kwenye matamshi ya viongozi wa Marekani kuhusiana na udharura wa kulinda usalama wa Israel chini ya kivuli cha mazungumzo ya nyuklia na kusisitiza kuwa: Hili nalo litambueni kwamba Israel itazidi kukosa usalama na amani, ni sawa tu makubaliano ya nyuklia yafikiwe au yasifikiwe.

Hapo hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an hata katika jambo hilo pia, viongozi wa Marekani hawasemi kweli kwani wanachotafuta viongozi hao wa Marekani ni maslahi na usalama wao binafsi tu na si usalama wa Israel.

Ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo akisema, lengo kuu la viongozi wa Marekani ni kuhakikisha kuwa hawaiudhi kanali ya kimataifa ya mabepari wa Kizayuni kwani kanali hiyo inawapa rushwa, fedha na utawala na kama kanali hiyo itapinga, basi viongozi hao watakuwa hatarini, watafedheheshwa na hata wanaweza kuuawa.

Vilevile ameashiria namna viongozi wa Iran walivyo wakweli mbele ya wananchi wao na kugusia msimamo imara na usiotetereka wa kitaifa walio nao wananchi wa Iran katika kukabiliana na ubeberu wa waistikbari na kuongeza kuwa: Kama katika mazungumzo hayo ya nyuklia kutatolewa maneno ya kimantiki na kuchukuliwa maamuzi ya kiadilifu na yanayoingilika akilini, sisi tutakubaliana nayo, lakini Iran, kuanzia kichwani hadi kwenye unyayo, kuanzia kwa matabaka ya wananchi wake hadi viongozi, itasimama kidete na haitotetereka mbele ya siasa za kupenda makuu za mabeberu.

Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakumbuka Mabasiji nukta kadhaa.

Amewausia kujipamba kwa sifa za upole, kuhimili mambo, ukweli, unyofu, kuimarisha nafsi zao kiimani, ushujaa, kujitolea, kujiweka mbali na kiburi, kuzuia kujipenyeza ndani yao fikra ya kujiona duni pamoja na kutoruhusu kuzorota kiimani na kielimu katika kukabiliana na vishawishi na wasiwasi mbalimbali, kuzingatia wajibu wa kujenga na kuimarisha matabaka yote katika Basiji na kuupa umuhimu udharura wa kuweko mfungamano na mawasiliano ya karibu baina ya matabaka hayo ya Basiji.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, ni jambo la dharura kwa Serikali kusaidia ustawi wa Basiji na kuongeza kuwa: Msingi mkuu wa uchumi wa kusimama kidete ni kuimarisha na kutia nguvu uzalishaji wa ndani na kwamba viongozi serikalini wanapaswa kusaidiana na Basiji katika kufanikisha jambo hilo.

Kabla ya miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Meja Jenerali Muhammadali Jafari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, Basiji iko tayari wakati wote kutekeleza ipasavyo majukumu na wajibu wake na kusisitiza kuwa: Majimui adhimu ya Basiji imearifisha muundo mpya kwa ajili ya kupanua uwezo wa watu wenye vipaji katika jamii ikiwa ni katika kujipanga na kujiimarisha upya kwa nia ya kuimarisha, kueneza na kutia nguvu fikra ya Mapinduzi ya Kiislamu katika jamii ambapo taasisi kubwa zaidi katika muundo huo mpya wa majimui hiyo adhimu ni Baraza Kuu la Basiji.

Naye Brigedia Jenerali Muhammad Reza Naqdi, Mkuu wa Taasisi ya Basiji ya Wanyonge ametoa hotuba fupi na huku akiashiria kuundwa Baraza Kuu la matabaka mbalimbali ya Basiji ya Wanyonge amesema: Baraza hilo linafanya juhudi, sambamba na kubainisha misimamo na kuleta fikra za pamoja, kufungua na kusahilisha njia za maendeleo ya haraka ya Mapinduzi ya Kiislamu.

700 /