Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Amirijeshi Mkuu wa majeshi ya Iran:

Moyo wa mapambano na kusimama kidete ni kielelezo cha heshima ya jeshi la Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, leo asubuhi (Jumapili) ameonana na majimui ya makamanda na maafisa waandamizi wa kikosi cha majini cha jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuutaja moyo wa muqawama na kusimama kidete kuwa ndilo chimbuko la heshima na itibari viliyo nayo vikosi vya ulinzi vya Iran na kuongeza kuwa, kikosi cha majini cha jeshi kinapaswa kuimarisha nguvu zake za kijeshi wakati wote kulingana na zama zinavyokwenda na wakati huo huo kujiimarisha kiimani na moyo wa kujitolea ili kulinda nafasi yake kubwa na muhimu katika kulinda usalama wa taifa, kuwalinda raia na kuimarisha ngome madhubuti iliyojiwekea nchi yao.

Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa ni jambo la dharura kutia nguvu kila uchao moyo wa kufanya kazi kwa bidii na kuweko tayari wakati wote kwa ajili ya kujitolea katika njia ya haki na kusisitiza kuwa: Somo ambalo Qur'ani Tukufu inatufunza ni kwamba, wakati inapokuwepo imani madhubuti na moyo wa kusimama kidete, basi huwezekana kupata ushindi mbele ya adui hata kama wenye imani thabiti hao watakuwa na zana chache.

Vilevile ameashiria mipaka mipana na mirefu ya majini ya Iran na jinsi adui alivyowekeza mno katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa: Vikosi vyetu vya ulinzi havipaswi kushughulishwa na mahesabu ya kisiasa, bali vinachopaswa kufanya ni kuzidisha nguvu zao na kuwa kwao tayari wakati wote na kufanyia uchunguzi kila palipo na mapungufu na kufanyia utafiti wa kina uwezo na udhaifu wa adui na kuweka stratijia na mikakati yake madhubuti kulingana na mambo kama hayo.

Ayatullah Udhma Khamenei amekitaja kipindi cha amani na usalama kuwa ni fursa nzuri sana kwa vikosi vya ulinzi kufanyia kazi masuala ya kielimu, ujenzi na kuongeza nguvu za kuzuia vitendo vya kiuadui vya maadui na kuongeza kuwa: Suala la kuzistawisha fukwe za eneo la Makran ni miongoni mwa kazi hizo za kimsingi na muhimu sana ambazo vikosi vya ulinzi kwa kushirikiana na Serikali vinapaswa kuweka ratiba na mipango inayotakiwa kwa ajili ya kuharakisha ustawishaji wa eneo hilo.

Mwishoni mwa hotuba yake, Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia namna kikosi cha majini cha jeshi la Iran kilivyojitolea muhanga mara nyingi sana katika nyakati tofauti na hususan wakati wa vita vya kujihami kutakatifu (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) na kuongeza kuwa: Kikosi cha majini cha jeshi la Iran ni fakhari ya vikosi vyote vya ulinzi nchini kama ambavyo pia ni fakhari kwa nchi na kwamba kumbukumbu za mashahidi wa kikosi hicho wakiwemo mashahidi waliojitolea kila kitu chao katika njia ya haki wakiwemo mashahidi wa hamasa ya boti ya "Peykan," daima zitaendelea kuwepo na hazitafutika katika historia ya Iran.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Admirali Habibullah Sayyari, Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sambamba na kuitukuza na kuienzi tarehe 8 Azar (siku ya hamasa ya kishujaa ya kikosi cha majini cha jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya mwaka 29 Novemba 1980 ambapo wanamapambano wa kikosi hicho walifanya operesheni ya kishujaa iliyoangamiza kabisa kisima cha mafuta cha "al Bakr wal Umayyah" cha Iran na kuzamisha majini meli kadhaa za kivita na ndege za kivita za utawala wa wakati huo wa Iraq) na kuongeza kuwa, kuongeza uimara wa kijeshi, kujiimarisha kielimu na kimaarifa, kuongeza nguvu na uwezo wa utendaji kazi na kutangaza kwa njia bora kabisa utamaduni wa Kiislamu-Kiirani katika upande wa pili wa mipaka ya Iran, uwepo wenye taathira wa kikosi hicho katika maji ya kimataifa na kuzisaidia meli za nchi nyingine na kuwekwa kikosi cha majini cha jeshi la Iran katika fukwe za Makran kwa lengo la kulistawisha na kulijenga eneo hilo, ni miongoni mwa kazi na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na kikosi cha majini cha jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
700 /