Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Kushuka kwa bei ya mafuta ni harakati ya kisiasa isiyo ya kiuchumi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo jioni (Jumamosi) ameonana na Rais Nicolas Maduro wa Venezuela na sambamba na kuisifu misimamo na hatua zilizochukuliwa na Venezuela katika kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel, ameitaja sababu inayoifanya kambi ya kiistikbari na kibeberu iifanyie uadui na kuishinikiza Venezuela kuwa ni msimamo wake huo wa kishujaa, wenye taathira na wa kiistratijia katika eneo la Amerika ya Latini na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina azma ya kweli na isiyotetereka ya kuimarisha na kuongeza ushirikiano wake wa pande zote na Venezuela.

Ayatullah Udhma Khamenei aidha amemtaja hayati Hugo Chaves, Rais wa zamani wa Venezuela kwamba alikuwa ni rafiki mzuri wa Iran na huku akiashiria uhusiano wa karibu uliokuwepo baina ya nchi hizi mbili amemwambia Rais Maduro kwamba: Na wewe pia umeendeleza ushirikiano huo katika kipindi cha uongozi wako na umefanikiwa kwa ushujaa mkubwa kushinda matatizo na njama zinazofanywa na maadui.

Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kupungua vibaya bei ya mafuta tena katika kipindi kifupi ni harakati ya kisiasa isiyo ya kiuchumi na kuongeza kuwa, maadui wetu wa pamoja wanatumia mafuta kama silaha ya kisiasa, na ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba wana mkono pia katika kupungua vibaya na kiasi chote hiki bei ya mafuta duniani.

Aidha ameunga mkono makubaliano yaliyofikiwa baina ya Marais wa Iran na Venezuela kwa ajili ya kufanya kazi kwa pamoja katika kukabiliana na kuporomoka bei ya mafuta duniani na kuongeza kuwa: Tab'an ushirikiano wa nchi hizi mbili haumalizikii tu katika suala la bei ya mafuta na inabidi kiwango cha mabadilishano ya kibiashara pamoja na uwekezaji ambacho hivi sasa ni cha kiwango cha chini sana, kiongezwe.

Ayatullah Udhma Khamenei aidha ameipongeza Venezuela kwa muqawa na misimamo na hatua zake za kishujaa kieneo na kimataifa na kuongeza kuwa: Nchi za Amerika ya Latini kwa kweli ndicho kiini cha mikakati na stratijia ya Venezuela, na kwamba malengo matukufu ya Venezuela yameyaamsha mataifa mengi ya eneo hilo na hilo bila ya shaka ndilo lililoifanya Marekani iifanyie uadui serikali na wananchi wa Venezuela.

Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia misimamo mizuri sana ya serikali ya Venezuela wakati wa vita vya siku 51 vya Ghaza na vilevile matamshi ya Rais wa Venezuela katika mazungumzo hayo ya leo na kuongeza kuwa: Utawala wa Kizayuni unachukiza sana duniani na hasa kati ya watu wa eneo letu hili na kwamba msimamo wako wa kishujaa dhidi ya utawala wa Kizayuni, umewafanya watu wengi wa eneo hili wafurahi na kukupenda sana.

Aidha ameiombea dua za kheri na mafanikio serikali ya Venezuela na kumwambia Rais Maduro kwamba: Hivi sasa wewe ni kijana na una azma na nia ya kweli ya kufanikisha malengo matukufu ya nchi yako, na napenda uelewe kuwa, msimamo usiotetereka wa Jamhuri ya Kiislamu nao ni kuendeleza na kuongeza ushirikiano wake na nchi yako ambao umeanza miaka mingi nyuma na kwamba kuendelezwa na kustawishwa uhusiano huo ni kwa faida ya nchi zote hizi mbili.

Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameshukuru misaada na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nchi yake na kusema: Katika matamshi yake, Bw. Hugo Chaves siku zote alikuwa akikumbushia miongozo yako na alikuwa akiliheshimu kwa namna ya kipekee taifa la Iran, pamoja na nafasi ya kihistoria ya Iran na sisi pia kama alivyokuwa Bw. Chaves, tunaihesabu Iran kuwa ni nyumbani petu.

Amesema, kuelewana na kuaminiana nchi hizi mbili ni rasilimali yenye thamani kubwa kwa ajili ya kuimarisha na kustawisha uhusiano wa pande zote na kuongeza kuwa: Inabidi tuchukue hatua za kweli na kufanya mapinduzi katika ustawi wa uhusiano wa nchi zetu mbili kwa kutumia uwezo na suhula nyingi zilizopo katika nchi hizi.

Rais wa Venezuela pia amegusia kuporomoka vibaya bei ya mafuta duniani na kusema: Tunafanya juhudi za kuleta msimamo wa pamoja katika kudhibiti bei ya mafuta kati ya nchi wanachama wa Opec na nchi nyinginezo zinazosafirisha mafuta nje ikiwemo Russia ili kupitia ushirikiano wa pamoja na kwa kutumia njia za kisasa, iwezekane kurejea bei ya mafuta katika kiwango chake kinachotakiwa.

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Rais wa Venezuela amezungumzia kadhia ya Palestina na kusisitiza kuwa: Palestina ni moja ya malengo matukufu na ya asili ya utu na ubinadamu na kwamba taifa na serikali ya Venezuela inajihisi kuwa na deni katika malengo matakatifu ya Palestina na tuna yakini kwamba kuna siku Palestina itakombolewa.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela pia amesema: Palestina ni muhanga wa siasa za kiistikbari, za kibeberu na za uangamizaji za dola la Marekani na kwamba serikali ya nchi hiyo ya kibeberu siku zote inafanya njama ya kuficha sura yake ya kibeberu na iliyo dhidi ya ubinadamu, kwa walimwengu.

 

700 /