Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kuonesha masuala ya kimaanawi katika michezo kunadhihirisha istiqama ya taifa la Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo asubuhi (Jumatano) ameonana na mabingwa na wanamichezo wengine walioshiriki katika mashindano ya Asia na Para Asia huko Incheon, Korea Kusini na huku akiashiria nafasi ya ushindi unaopatikana kwenye medani mbalimbali za michezo katika kuleta hisia za kujivunia kitaifa wananchi, amekutaja kusimama kidete kimaanawi kunakofanywa na wanamichezo na mabingwa katika kuhifadhi na kueneza matukufu na nara za kidini mbele ya mamilioni ya watu kuwa ni jambo muhimu mno na kusisitiza kwamba: Istiqama na kusimama kidete huko kimaanawi katika nyuga za kimataifa kunaitangaza, kunaiarifisha na kunaonesha uimara, kusimama kidete na istiqama ya taifa la Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa shukrani nyingi sana kutokana na ushindi na medali walizopata wanamichezo wa Iran katika mashindano ya Asia na Para Asia na kulitaja suala la kutambua fakhari za taifa na vile vile kuwepo moyo wa fakhari ya kitaifa kati ya wananchi kuwa kunaandaa harakati za kuelekea kwenye fakhari kubwa zaidi na kuongeza kuwa: Mtu unapoona kwamba kijana fulani mwanamichezo analikabidhi taifa medali yake aliyoipata kwenye mashindano fulani na kuona fakhari kufanya hivyo jambo ambalo kwa hakika linaingiza furaha katika nyoyo za watu, ni kitendo kizuri mno cha kimichezo.

Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia namna hisia na mitazamo ya watu inavyoelekezwa mno kwa ushindi wa mwanamichezo na kuongeza kuwa: Mienendo na miamala ya mwanamichezo baada ya kuwa bingwa inapaswa kuwa ni kulitangaza taifa, utamaduni na shakhsia ya kitaifa pamoja na istiqama ya kimaanawi ya taifa la Iran.

Ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu istiqama ya kimaanawi akisema: Katika dunia hii ambayo suala la kupiga vita dini na heshima kuwa ajenda kuu ya vituo na taasisi za kimataifa na vyombo vya habari duniani, suala la utamaduni na ukosefu wa heshima ni mambo ambayo yameenea sana duniani na kwamba kitendo cha mwanamichezo kijana wa Kiirani cha kuonesha madhihirisho ya umaanawi kwa hakika ni kutangaza uwezo wa kusimama kidete kimaanawi taifa la Iran mbele ya wimbi hilo kubwa la upotofu na upotoshaji duniani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa pia nasaha kadhaa.

Kujiepusha na uvunjaji sheria katika nyuga za kimataifa na vile vile katika nyuga za ndani na za michezo na ulazima wa kuchukuliwa hatua kali watu wanaohalifu sheria, ni nasaha za kwanza kabisa zilizotolewa na Ayatullah Udhma Khamenei katika mkutano huo.

Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Kukabiliana na wanaohalifu sheria hakupaswi kufanyika kwa woga na kuwaonea haya watu, kwani kuhalifu amri si jambo linalokubalika kabisa hata likifanywa na mtu yeyote yule awe kiongozi au mtu wa kawaida, iwe imefanywa na watu wenye ushawishi au wasio na ushawishi iwe uhalifu huo umefanywa na watu wanaopata ushindi katika siasa au mabingwa katika michezo au watu muhimu kielimu na kiviwanda, wote wanapaswa kuheshimu sheria.

Amesema, mapenzi ya watu kwa wanamichezo na hasa wale wanaopata ushindi na kuwa mabingwa, ni fursa nzuri ya kuwa kigezo kwa vijana na kuongeza kuwa: Harakati yoyote nzuri inayofanywa na bingwa wa michezo, hupelekea kuongezeka milioni ya harakati kama hizo na kuenea mambo ya kheri katika jamii.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuwa bingwa na kupendwa na watu ni upanga wa nchi mbili; kama mtu atashikamana vizuri na inavyotakiwa na mambo hayo, huwa ni jambo zuri sana, lakini kama atashindwa kuchunga vizuri mambo hayo, huwa ni hatari sana.

Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amegusia ripoti iliyotolewa na Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran kuhusu ulazima wa kuwekwa vipaumbele katika masuala mbalimbali na kusisitiza kuwa: Sambamba na kuunga mkono michezo ya kupigania kupata ushindi, michezo ya watu wengi kwa pamoja nayo ni muhimu kutiliwa nguvu kwani michezo ya aina hiyo huifanya jamii kuwa salama kiafya.

Mwishoni mwa hotuba yake, amezungumzia namna taifa la Iran linavyopata ushindi katika medani mbalimbali zikiwemo medani za kielimu na kimaadili na kuongeza kuwa, kujenga moyo wa kuwa bingwa na kupata ushindi katika medani tofauti hivi sasa kumekuwa ni jambo muhimu sana nchini Iran na inabidi jambo hilo lizidi kupewa umuhimu na kutiliwa nguvu.

Mwanzoni mwa mkutano huo, Bw. Goudarzi, Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran amegusia namna wanamichezo wa Iran walivyon'gara, walivyopata ushindi na kuwa mabingwa katika mashindano ya Asia na Para Asia na kusema kuwa: Kaulimbiu na nara ya "Michezo salama, umaanawi na kulitangaza taifa" kuwa ndiyo ajenda kuu ya harakati na shughuli za kimichezo za Iran akiongeza kuwa: Kuleta mizani sawa katika mtazamo wa michezo ya watu wote na ile ya kupigania ushindi na ubingwa, kulipa umuhimu maalumu suala la kupanua michezo ya akinamama, kufanya juhudi za kueneza utamaduni wa Kiislamu - Kiirani na kupunguza udhibiti na mkono wa serikali kuwa ni miongoni mwa kazi zilizofanywa na Wizara ya Michezo na Vijana ya Iran katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

 

700 /