Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Maendeleo katika sekta ya nano yawe kigezo cha maendeleo katika sekta nyingine

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo asubuhi (Jumamosi) ametembelea maonyesho ya mafanikio ya teknolojia ya nano ya Iran katika Husainia ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) mjini Tehran kwa muda wa saa moja na nusu na kuona kwa karibu mchakato wa jitihada na maendeleo makubwa ya kielimu ya wanasayansi na wasomi vijana wa Iran katika teknolojia ya nano.

Katika maonyesho hayo ambapo Dk Sattari, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya sayansi na teknolojia alikuwa amefuatana na Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kumeonyeshwa maendeleo ya hivi sasa kabisa na matunda ya karibuni kabisa ya watafiti wa Iran katika sekta ya nano yakiwa na ubora wa hali ya juu na yenye matumizi mengi. Baadhi ya vitu vilivyoonyeshwa kwenye maonyesho hayo ni matumizi ya teknolojia ya nano katika madawa, afya na matibabu, katika sekta ya nguo na vitambaa, namna nano inavyoweza kutumika na kuleta faida kubwa katika masuala ya kilimo, maji na matumizi ya viwandani, katika utengenezaji wa vinu na majengo, kwenye sekta ya mafuta na nishati na katika utengenezaji wa magari. Muda wote wahusika wa vitengo mbalimbali vilivyotembelewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu walikuwa wanatoa maelezo kuhusu vitengo husika.

Baada ya kutembelea maonyesho hayo, Ayatullah Khamenei ametoa hotuba fupi mbele ya wahadhiri, watafiti na watu wanaohusiana na sekta ya nano nchini Iran akiyataja mafaniko makubwa yaliyopatikana katika sekta hiyo kuwa ni mfano na ni kielelezo cha maendeleo katika sekta nyingine nchini Iran na kusisitiza kuwa: Maendeleo na mafanikio hayo yanaonesha kuwa, wakati majimui na kikundi cha watu wenye mapenzi na kitu fulani wanapokusanyika pamoja na kufanya kazi za kiutaalamu, kwa ari na kwa moyo mmoja katika uga maalumu, basi matokeo ya jambo hilo ni kuonekana wazi maendeleo na mapinduzi katika sekta hiyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja sharti la kuweza kuendelea kushuhudiwa mafanikio kama hayo kuwa ni kulinda sababu za mafanikio husika. Baada ya hapo  amebainisha sababu mbalimbali za kuweza kupatikana maendeleo ya kielimu hususan katika sekta ya nano.

Amesema kwamba, kuwa na mipangilio makini, kuweko uthabiti na uimara katika uongozi na uendeshaji wa mambo, kueneza utamaduni na kulifanya suala hilo likubalike katika jamii kwa lengo la kutafuta na kugundua vipaji vilivyo bora, ni miongoni mwa njia bora za kuweza kulindwa maendeleo katika sekta ya teknolojia ya nano. Amesisisitiza kwamba: Njia nyingine bora ya kuweza kuendelea kuwa na maendeleo katika sekta hiyo ni kutoruhusu kujipenyeza masuala ya kisiasa katika masuala ya kielimu na kiutafiti.

Ayatullah Ali Khamenei amelitaja suala la kutoingiwa na ghururi na majivuno na kutotosheka na maendeleo yaliyofikiwa kuwa ni jambo jingine muhimu la kuweza kuendeleza harakati yenye kasi kubwa ya kielimu nchini Iran na kuongeza kuwa: Ni sawa kwamba leo hii kiwango cha vipaji vya vijana wa Kiirani na kasi ya kielimu nchini Iran ni kubwa sana ikilinganishwa na wastani wa kasi hiyo duniani, na ushahidi wa jambo hilo ni kuona kuwa Iran ni ya saba duniani katika maendeleo ya teknolojia ya nano, lakini inabidi kasi hiyo iongezwe na kuweza kuziba haraka mapengo yaliyosababishwa na kubakishwa nyuma kimaendeleo taifa hili.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuashiria uadui wa madola makubwa ya kibeberu dhidi ya taifa la Iran na kusema kwamba uadui huo unatokana na sera huru za kisiasa, kijamii na kifikra za taifa la Iran. Amesema: Uadui huo huwa unajitokeza katika nyuga na nyanja mbalimbali, hivyo inabidi kuimarisha uwezo wetu kila uchao na kuhakikisha tunakuwa na nguvu zaidi na zaidi kadiri siku zinavyosonga mbele.

Vilevile ameashiria udharura wa kuelekezwa bidhaa na maendeleo ya teknolojia ya nano upande wa biashara na katika soko la matumizi na kuzalisha utajiri akisisitiza kuwa: Moja ya mambo makubwa na muhimu yanayoweza kudhamini kuendelea kushuhudiwa maendeleo katika sekta ya nano ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaona athari za kazi zenu za kielimu na kiutafiti katika maisha yao ya kila siku.

Ayatullah Khamenei amegusia pia ripoti zinazohusiana na tofauti kubwa iliyopo baina ya bajeti ya Iran katika sekta ya teknolojia ya nano na bajeti za nchi nyinginezo katika sekta hiyo na amemkhutubu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya sayansi na teknolojia akimtaka alipe uzito wa hali ya juu zaidi suala hilo.

700 /