Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Amirijeshi Mkuu:

Makubaliano ya Iran na 5+1 yawe ya awamu moja na yajumuishe vitu vyote

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya KiislamuAyatullah Ali Khamenei leo asubuhi (Jumapili) ameonana na makamanda na wafanyakazi wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu na akibainisha sababu na lengo kuu la uadui wa miaka 36 na unaondelea hadi hivi sasa wa Wamarekani na kosa lao la kimahesabu kwa ajili ya kutaka kulipigisha magoti na kulidhalilisha taifa la Iran. Amegusia miamala na hatua za kimantiki na zenye ushahidi madhubuti za Iran katika mazungumzo ya nyuklia na miamala isiyo ya kimantiki na ya ushinikizaji ya upande wa pili na kusisitiza kuwa: Siku ya Bahman 22 (Februari 11 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu) Taifa la Iran litaonesha kwamba haliwezi kukubaliana na ubeberu na litatoa kipigo kwa mdhalilishaji yeyote yule.

Katika mkutano huo ambao umefanyika sambamba na maadhimisho ya siku ya kihistoria ya kutangaza bay'a na utiifu wa majimui ya maafisa na wafanyakazi wa Jeshi la Anga la Iran kwa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu), tarehe 19 Bahman mwaka 1357 Hijria Shamsia (Februari 8, 1979), Ayatullah Ali Khamenei amelitaja tukio hilo kuwa ni muhimu sana lenye madhumuni na shabaha zitakazobakia milele. Ameongeza kuwa: Hatua hiyo ya kishujaa ya maafisa na wafanyakazi wa Jeshi la Anga la Bahman 19, 1357, ilionesha haki na mvuto wa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yaliweza kuvuta imani za ndani kabisa ya nyoyo za askari wa Jeshi la Anga la wakati huo la kifalme ambalo lilikuwa mboni ya jicho ya Marekani.

Vilevile amesisitizia ulazima wa kuelewa na kuulinda uhakika humo muhimu na baada ya kuashiria baadhi ya matukio muhimu kama vile ushawishi mkubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, mataifa mengine duniani yalipata hamasa na kuvutiwa na ujumbe wa mapinduzi hayo hasa baada ya kuona ushujaa na kusimama kidete taifa la Iran ambalo limesimama hadharani kukabiliana na ubeberu wa Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Katika upande wa pili pia, madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani, tangu siku ya kwanza kabisa ya Mapinduzi (ya Kiislamu ya Iran) hayajaacha kuchukua hatua wala mashinikizo ya kuizima harakati hiyo adhimu ilinayozidi kupata nguvu siku hadi siku na kwamba uadui huo unaendelea hadi leo hii.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Uadui wa Marekani na madola ya kibeberu na kiistikbari hauwalengi watu maalumu, bali unalenga asili na msingi wa harakati na misimamo pamoja na kusimama kidete sambamba na kupigania ukombozi na heshima taifa zima la Iran.

Aidha amekumbushia matamshi ya baadhi ya wanasiasa wa Marekani katika miaka ya hivi karibuni ambayo yamejaa chuki na bugudha dhidi ya taifa la Iran na kusema: Wanasiasa hao wa Marekani wamehamakishwa na kusimama imara taifa la Iran na kwamba lengo asili la Marekani na wenzake ni kutaka kulipigisha magoti na kulidhalilisha taifa la Iran na hapana shaka kuwa wamefanya kosa na wamepotea katika mahesabu yao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja sababu kuu ya kushindwa mtawalia na mara kwa mara Wamarekani katika masuala ya eneo la Mashariki ya Kati hususan Iran kuwa ni makosa yao hayo ya kimahesabu na kupotea kwao kiistratijia na kuongeza kwamba: Moja ya mifano ya makosa yao hayo, ni matamshi ya siku chache zilizopita ya kiongozi mmoja Mmarekani aliyeseme kuwa, Wairani wamefungwa mikono katika mazungumzo ya nyuklia na kwamba eti hawafurukuti.

Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza kuwa: Siku ya Bahman 22 (mwaka huu inasadifiana na Jumatano Februari 11, 2015) mtaona namna taifa la Iran litakavyojitokeza kwa wingi kuadhimisha siku hiyo na hapo itajulikana kama madai ya kiongozi huyo wa Marekani ya kwamba taifa la Iran limefungwa mikono, ni ya kweli au la.

Vilevile amesema: Mikono ya wananchi na viongozi wa Iran haijawahi kufungwa hata mara moja na wamelithibitisha kivitendo jambo hilo na katika siku za usoni pia watatumia ubunifu na ushujaa wao kuzidi kulithibitisha suala hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Upande ambao kwa hakika umekwama na hauwezi kufurukuta ni Marekani na matukio yote ya eneo hili (la Mashariki ya Kati) na ya nje ya eneo hili yanathibitisha uhakika huo.

Ayatullah Ali Khamenei ameashiria pia kufeli siasa za Marekani katika nchi za Syria, Iraq, Lebanon, Palestina na hususan Ghaza, Afghanistan na Pakistan na vilevile kushindwa Marekani huko Ukraine na amewakhutubu Wamarekani akiwaambia: Ni nyinyi ambao mumekuwa mukifeli na kushindwa mfululizo na mtawalia, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tayari imeshasonga mbele na haiwezi kufananishwa kamwe na miaka thelathini na kitu iliyopita.

Pia ameashiria maendeleo makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu katika nyuga za sayansi, elimu na teknolojia na kwenye masuala mbalimbali ya kijamii, masuala ya kimataifa na vilevile ushawishi mkubwa wa kieneo na kupenya misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu katika nyoyo za vijana na kuongeza kuwa: Kutokana na kuwa na utajiri na akiba yenye thamani kubwa ya uzoefu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasonga mbele kwa nguvu zote na Wamarekani ambao wameshindwa kung'oa mzizi na msingi wa mapinduzi haya matukufu hivi sasa wanalazimika kukubaliana na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kwamba wapangaji wa masuala ya kisiasa, kiusalama, kiuchumi na kiutamaduni wa maadui, hawaweza kuzuia maendeleo hayo ya Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia mazungumzo ya nyuklia na njama za wanaolitakia mabaya taifa la Iran na maadui wenye inadi wanaoeneza propaganda chafu za kwamba eti Iran imekwama katika jambo hilo, na amezungumzia nukta kadhaa muhimu kuhusiana na mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea hivi sasa baina ya Iran na kundi la 5+1.

Nukta ya kwanza kabisa iliyoashirishwa na Ayatullah Khamenei ni kukubaliana kwake na asili ya mwafaka na makubaliano ambapo amesema: Mimi ninaafikiana na makubaliano ambayo yatatekelezwa lakini sikubaliani na makubaliano "maovu."

Vilevile ameashiria matamshi ya mara kwa mara ya Wamarekani wanaosema kuwa, "kutoafikiana ni bora kuliko mwafaka mbovu" na kuongeza kuwa: Sisi pia tuna mtazamo huo huo! Tunaamini kwamba, kutoafikiana ni bora kuliko mwafaka ambao utakuwa na madhara kwa manufaa ya taifa na ambao utaandaa uwanja wa kudhalilishwa taifa kubwa la Iran.

Juhudi zisizosita za viongozi na timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran za kumpokonya adui silaha ya vikwazo ni nukta ya pili iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake hiyo na kuongeza kuwa: Kama kutafikiwa makubaliano na kupitia mwafaka huo akapokonywa adui silaha yake ya vikwazo, hilo litakuwa ni jambo zuri sana, lakini kama makubaliano hayatofikiwa, kila mtu atambue kuwa, kuna njia nyingi ndani ya Iran za kuweza kupunguza nguvu za silaha hiyo ya vikwazo.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Kama vitu tulivyo navyo tutavizingatia kwa namna inayotakiwa, kwa hima na jitihada kubwa, basi hata kama hatutaweza kumpokonya kikamilifu adui silaha ya vikwazo, lakini tutaweza kuivunja nguvu na kuikata makali silaha hiyo.

Nukta ya tatu iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ilikuwa ni kuhusiana na mienendo ya kimantiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na miamala isiyo ya kimantiki na ya kiistikbari ya upande wa pili wa mazungumzo hayo.

Ayatullah Khamenei amegusia pia matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kwamba maana ya mazungumzo ni kufikia pande mbili kwenye nukta ya pamoja na kusema kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana si sahihi kwa upande mmoja wa mazungumzo kuwa na mwenendo usioingilika akilini wa kushinikiza kila unachotaka kikubaliwe bila ya kuzingatia matakwa ya upande wa pili.

Ameongeza kuwa: Miamala ya Wamarekani na ya baadhi ya nchi chache za Ulaya zinazowafuata kibubusa Wamarekani katika mazungumzo hayo si ya kimantiki, bali madola hayo yana matarajio ya kuchupa mipaka yakitarajia kuwa matakwa yao yote lazima yakubaliwe wakati ambapo huo sio mwenendo wa mazungumzo.

Ayatullah Aki Khamenei amekutaja kusimama kidete viongozi wa Iran mbele ya tabia ya kupenda makuu upande wa pili kuwa ni suala sahihi kikamilifu na huku akiashiria muamala wenye mashiko na wa kimantiki wa Jamhuri ya Kiislamu katika vipindi tofauti ikiwa ni pamoja na kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu (vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) na hatua ya Iran ya kulikubali azimio nambari 598 la Umoja wa Mataifa na vilevile maamuzi ya kimantiki ya Jamhuri ya Kiislamu katika masuala mbalimbali baada ya vita hivyo amesema kuwa: Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unatumia mantiki pia katika mazungumzo yake ya nyuklia, lakini upande wa pili wa mazungumzo hayo hauna mantiki yoyote bali unafaya mambo yasiyoingilika akilini ukitumia mabavu kufanikisha matakwa yake.

Amesisitiza kuwa: Kamwe taifa la Iran haliwezi kukubali kufanyiwa ubeberu na linapinga miamala ya kupenda makuu na vitendo visivyo vya kimantiki.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena amesema: Mimi ninaunga mkono kuendelea na mazungumzo na kufikiwa makubaliano mazuri na ni jambo lisilo na shaka hata chembe kwamba taifa la Iran nalo halipingi makubaliano yoyote ambayo yatachunga itibari, izza na heshima ya taifa hilo. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Inabidi heshima, hadhi, taadhima, thamani na maendeleo ya Iran yalindwe katika mazungumzo hayo kwani taifa hili halina kawaida ya kukubaliana na ubeberu wa upande wa pili, ni sawa tu upande huo uwe Marekani au watu mengine wowote.

Vilevile ameashiria baadhi ya mijadala iliyozushwa kuhusiana na makubaliano ya awamu kwa awamu na kupendekezwa kuweko kwanza makubaliano juu ya misingi mikuu na baada ya kupita muda kuweze kufikiwa makubaliano kuhusu vitu vidogo vidogo na kusema: Makubaliano ya namna hiyo hayakubaliki na sababu yake ni kuwa, kutokana na uzoefu tulio nao kuhusu mienendo na miamala ya upande wa pili, kufikia makubaliano katika masuala makuu tu kutafanywa wenzo wa upande huo wa pili wa kutolea visingizio vya mara kwa mara kuhusu vitu vidogo vidogo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kwamba: Kama kutafikiwa makubaliano, basi inabidi makubaliano hayo yawe ya awamu moja na ndani yake yajumuishe vitu vyote, vikuu na vidogo vidogo.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Vipengee vya makubaliano hayo navyo vinapaswa kuwa wazi, bayana na wadhiha bila ya kuhitaji kutafsiriwa na kuaguliwa.Vipengee vya makubaliano hayo havipaswi kuwa kwa namna ambayo upande wa pili ambao una kawaida ya kutatiza mambo katika mazungumzo, utashindwa kupata kisingizio cha kutumia vibaya au kukwepa kutekeleza vipengee vya makubaliano hayo.

Ameongeza kuwa: Inshaallah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, siku ya tarehe 22 Bahman (Februari 11 siku ya kufikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu) taifa la Iran litatoa pigo kwa kila mtu ambaye anadhamiria kulidhalilisha taifa hili.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Taifa zima la Iran na wote wenye uchungu na nchi wanakubaliana kwamba heshima ya taifa ni muhimu mno kwa nchi, kwani inapokosekana heshima ya taifa, usalama na maendeleo nayo yatakosekana, hivyo heshima ya taifa lazima ilindwe na kwamba viongozi nchini mwetu nao wanalitambua jambo hilo.

Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei amesema: Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, taifa la Iran litajitokeza kwa wingi, kwa nguvu na kwa nia moja mmoja kwenye maandhimisho ya Bahman 22 na kumpigisha magoti adui.

Mwanzoni mwa mkutano huo, Brigedia Jenerali, Rubani, Hasan Shah Safi, Kamanda wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa pongezi na baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya tarehe 19 Bahman (Februari 8) siku ilipochukuliwa hatua na maafisa wa Jeshi la Anga la Iran ya kihistoria ya kutangaza bay'a na utiifu wao kwa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) na ametoa ripoti fupi kuhusiana na uwezo, nguvu na hatua za kimaendeleo za jeshi hilo.

Brigedia Jenerali Shah Safi ametaja baadhi ya kazi muhimu zilizofanywa na Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni pamoja na kubuni, kutengeneza na kuboresha mshabaha wa kupaa na ndege, kupata uwezo na utaalamu wa kubuni na kutengeneza madege makubwa yasiyo na rubani, kuanzisha, kukarabati na kutengeneza upya aina mbalimbali za ndege za kisasa, kuzifanya za kileo zaidi zana zilizopo nchini za kijeshi pamoja na kuzalisha na kuviandalia kufanya kazi vifaa vya ndege vya kurushia makombora na kuyaandaa kwa ajili ya operesheni makombora ya kiistratijia kwa kutumia uwezo wa ndani ya Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu. Amesema suala hilo linathibitisha kushindwa makucha ya vikwazo vya zana za ulinzi wa anga na ni bishara njema ya kudhihiri mlingano mpya katika mizani ya masuala ya kiulinzi kwenye eneo hili.

Kabla ya mkutano huo, Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei ameonana kwanza na makamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye mkutano wa peke yao na huku akiashiria nafasi nyeti, nzito na iliyojaa hatari ya jeshi hilo la anga la Jamhuri ya Kiislamu katika majimui ya mfumo wa kiulinzi wa Iran na kuongeza kuwa: Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linategemea uchumi unaotokana na kazi za kiutaalamu za elimu na teknolojia na jambo hilo linathibitisha umuhimu mkubwa wa jeshi hilo katika suala zima la kukabiliana na vitisho mbalimbali.

 

700 /