Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Adui anapinga asili ya Mapinduzi ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amekutana na maelfu ya wananchi wa mkoa wa Azarbaijan Mshariki ambapo amelipongeza taifa la Iran kwa kushiriki kwa wingi katika maandamano ya tarehe 22 Bahman (11 Februari, siku ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini). Katika hotuba yake muhimu kwenye hadhara hiyo, Ayatullah Khamenei ameeleza hali ya kiuchumi ya Iran na njia za utatuzi wa mambo mbalimbali hususan udharura wa kutekelezwa sera za uchumi wa kimapambano. Ameashiria pia mivutano iliyopo, masharti ya Marekani na vikwazo vipya vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran na akasema: Taifa la Iran daima limeonesha kuwa lina idara imara, na katika suala la vikwazo taifa hili linaweza kuzima njama hizo.

Ayatullah Khamenei ameashiria ripoti sahihi na za kina zilizowasilishwa kwake kuhusu maandamano ya tarehe 22 Bahman (11 Februari) za mahudhurio makubwa ya wananchi katika maandamano ya mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita na akasema: Ulimi wangu unashindwa kulishukuru taifa kubwa la Iran na kueleza mahudhurio makubwa ya wananchi katika maandamano hayo.

Ameashiri baridi kali na mvua iliyokuwa ikinyesha katika baadhi ya miji na vilevile kimbunga cha mchanga huko Ahwaz katika mkoa wa Khuzistan (kusini mwa Iran) wakati wa maandamano hayo na kusema: Katika hali hiyo na licha ya kupita miaka 36 sasa tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, mahudhurio ya mwaka huu ya wananchi katika maandamano yalikuwa makubwa na adhimu zaidi kuliko miaka iliyopita; na suala hili halina kifani duniani.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema sababu kuu ya adhama ya maandamano ya 22 Bahman (Februari 11) ni mahudhurio ya wananchi katika medani na kushika hatamu za mambo wananchi wenyewe. Ameongeza kuwa: Wakati wowote wananchi wanapokuwapo na kushirikishwa katika masuala ya nchi, tumeshuhudia na tutaendelea kushuhudia muujiza kama huu.

Ayatullah Khamenei ametabikisha kaida hiyo pana kwenye masuala ya uchumi na kusisitiza juu ya udharura wa kushirikishwa wananchi katika masuala ya kiuchumi kwa mpangilio maalumu na kutumia uwezo wao. Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu amebainisha sababu za matatizo ya kiuchumi hapa nchini na kusema miongoni mwa sababu hizo muhimu ni mipango ya madola ya kibeberu baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa (vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran) kwa ajili ya kuzuia Iran isiwe kambi kubwa ya kiuchumi na yenye taathira kubwa katika Mashariki ya Kati na duniani.

Amesema kuwa: Wamagharibi hususan Wamarekani- kwa mipango na ratiba maalumu na kwa kutumia mbinu mbalimbali- walianza njama za kukwamisha miradi na shughuli za kiuchumi za Iran na nchi za Mashariki ya Kati na kuizunguka Iran katika kanali za kusafirisha mafura na gesi, njia za nchi kavu, anga na kanali za mawasiliano na walianza kuiwekea Iran vikwazo kimyakimya kabla hata ya kuanza masuala ya nyuklia, na mkabala huo wa kiuchumi ungali unaendelea hadi hii leo.

 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kwa hivyo katika kuyafanyia uchunguzi mazingira na matatizo ya kiuchumi nchini hatunapaswi kupuuza mipango ya adui Mmarekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinazoifuata kibubusa Marekani.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, inabidi tukabiliane vilivyo na mipango ya wanaolitakia mabaya taifa la Iran kiasi ambacho tutaweza kuzifanya njama hizo za maadui zisiwe na taathira au ziwe na taathira ndogo na kuongeza kwamba: Mbali na kuweko mipango mikubwa na endelevu ya kambi ya kibeberu, uchumi wetu una matatizo mengine mawili makubwa, nayo ni kutegemea kwake mafuta na kuendeshwa kwake na Serikali.

Amesema, kuuza mafuta ghafi na kutumia pato lake katika matumizi ya kila siku ya ndani ya nchi na kutotumia mazao mengi yanayotokana mauzo ya mafuta ni urithi mbaya tuliourithi kutoka kwa utawala wa kitaghuti (utawala wa Shah wa kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran) urithi ambao una hasara zisizoweza kufidiwa.

Ameongeza kuwa: Mbinu hiyo ndiyo njia rahisi zaidi ya kupatia pesa na kwamba baadhi ya viongozi katika vipindi mbalimbali wamekuwa wakifadhilisha kutumia sana pesa hizo zinazopatikana kirahisi kuendeshea mambo ya nchi.

Kuhusu matatizo yanayojitokeza wakati uchumi wa nchi unapoendeshwa na serikali Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ameashiria hatua ya kuwasilishwa siasa kuu za kifungu cha 24 cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran miaka michache iliyopita na sisitizo lake la wajibu wa kutekelezwa kivitendo siasa hizo na kuongeza kuwa: Viongozi hapa nchini wanafanya kazi kwa dhati na kwa moyo safi, hata hivyo juhudi hizo hazitoshi na inabidi kufanyike jitihada kubwa zaidi za kukuza uchumi.

Ayatullah Khamenei ameitaja Bahman 29 (Februari 18) kuwa inasadifiana na mwaka wa kwanza wa tangu kuwasilishwa siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete nchini Iran na kusisitiza kwamba: Uchumi wa kusimama kidete ni jambo la dharura nchini iwe ni katika mazingira ya vikwazo au nje ya mazingira ya vikwazo. Hii ina maana ya kwamba, msingi ya uchumi nchini unapaswa kupangiliwa kwa namna ambayo hautaathiriwa na mitikisiko ya mara kwa mara inayotokea duniani.

Ameongeza kuwa: Iwapo msingi wa uchumi wa nchi yetu utasimama juu ya uwezo wa wananchi na uzalishaji wa ndani na iwapo kutawekwa mipangilio makini chini ya msingi huo, basi uchumi wetu hautaathiriwa na vikwazo na kushuka bei ya mafuta na wala hakutakuwa na wasiwasi wa uchumi huo kuathiriwa na mambo mengine.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja moja ya mambo ya lazima na muhimu ya udharura wa kujitoa kwenye uchumi unaotegemea pato la kuuza nje mafuta kwamba ni kuifanya bajeti ya nchi iache kutegemea fedha hizo za mafuta.

Ameongeza kuwa: Tunapaswa kufikia kwenye nukta hiyo na ninaamini kwamba, kazi hiyo ngumu inawezekana kwa hima na kwa kuwategemea wananchi na vijana pamoja na kutegemea rasilimali na uwekezaji wa ndani ya nchi na muhimu kuliko yote kumtegemea na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye ametoa ahadi ya nusra (ya kumnusuru kila anayeinusuru dini Yake.)

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa miongoni mwa njia za kuifanya bajeti isitegemee mapato ya fedha zitokanazo na kuuza nje mafuta ni kutegemea fedha zitokanazo na kodi, uzalishaji wa ndani na biashara.

Amesema: Baadhi ya wawekezaji wakubwa ambao wanakwepa na kukimbia kulipa kodi, kitendo chao hicho ni uhalifu kwani kinaifanya nchi izidi kutegemea fedha za kuuza nje mafuta na kuandaa mazingira ya kujitokeza matatizo zaidi na zaidi ya kiuchumi.

Amelitaja suala la ulipaji kodi kuwa ni muhimu sana bali ni jambo la faradhi kisheria na kuongeza kuwa: Maafisa wa masuala ya kodi wameweka mipangilio mizuri kwa ajili ya ukusanyaji wa kodi zinazotokana na uzalishaji bidhaa na masuala ya biashara na kwamba inabidi wananchi washirikishwe vilivyo na wasaidie katika ufanikishaji wa haraka mipango hiyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, nukta nyingine muhimu ya kutatua matatizo yaliyopo ya kiuchumi ni kuongeza tija na ufanisi na kuongeza kuwa: Maana ya kuongeza ufanisi ni kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa na wakati huo huo kupandisha juu ubora wa bidhaa hizo.

Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kuweka mipango inayofaa kwa ajili ya kustafidi kadiri inavyowezekana na suhula na uwezo wa vyanzo vya ndani ya nchi kuwa ni njia nyingine ya kuweza kutatua matatizo ya kiuchumi. Baada ya hapo amegusia nukta kadhaa ili kutilia nguvu matamshi yake hayo.

Kutumia bidhaa za ndani ni nukta ya kwanza iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambapo amesema: Wananchi na watu wote wanaoipenda Iran na mustakbali wa nchi hii pamoja na taasisi zote za kiserikali zinapaswa ziache kutumia bidhaa za nje ambazo hapa nchini tunazalisha mfano wake.

Ayatullah Ali Khamenei amebainisha nukta nyingine kuwa ni ulazima wa kujiepusha na israfu na kuzuia kupotea na kutumiwa vibaya mali ya umma pamoja na kuyategemea mashirika ya elimu msingi na kupambana vilivyo na magendo na kuongeza kuwa: Inabidi kazi hizo zifanyike kwa uzito wa hali ya juu ili iwezekane kutatua matatizo yaliyopo ya kiuchumi.

Ameongeza kuwa: Katika miaka ya hivi sasa kumetolewa tahadhari na maonyo mengi na kumefanyika jitihada nyingi katika uwanja huo lakini pamoja na hayo maonyo na tahadhari hizo hazitoshi na hata jitihada zilizofanyika hadi hivi sasa ijapokuwa ni nyingi lakini nazo pia hazitoshi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia ulazima wa kulipa umuhimu mkubwa suala la kushirikishwa vilivyo wananchi na uwezo wao katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi na kuongeza kuwa: Sisi tunao uwezo wa kusimama kidete na kukabiliana na makelele na hatua zinazochukuliwa na maadui kuhusiana na vikwazo na hatimaye kuvivunja nguvu vikwazo hivyo.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Kama hatutachukua hatua zinazotakiwa na kufanya jitihada kwa nguvu kubwa zaidi katika masuala ya kiuchumi, basi matokeo yake yatakuwa ni yale yale ambayo tunayaona hivi sasa ambapo adui anaweka masharti haya na yale katika kadhia ya nyuklia na baadaye anasema kijeuri kwamba kama hamtokubali masharti yetu basi tutakuwekeeni vikwazo.

Vilevile ameashiria namna kambi ya kibeberu inavyotumia kadiri inavyoweza silaha ya vikwazo dhidi ya taifa la Iran na kusisitiza kuwa: Lengo kuu la maadui ni kulidhalilisha taifa la Iran na kukwamisha harakati adhimu ya taifa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya kuelekea kwenye ustaarabu mpya wa Kiislamu na mimi ninaamni kwamba, kata kama ikitokezea tukakubaliana na matakwa yao katika kadhia ya nyuklia, vikwazo havitaondoshwa kwani maadui hao ni wapinzani wakubwa wa asili ya Mapinduzi yenyewe ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia uwezo mkubwa sana wa vijana wa Iran hususan wanachuo mabasiji katika masuala ya nchi na katika kufanikisha malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na vilevile ameashiria vitisho vinavyotolewa na dola la kibeberu la Marekani pamoja na vikwazo vipya vya nchi za Ulaya dhidi ya Iran na kusema kuwa: Kama suala hapa ni kuwekeana vikwazo basi taifa la Iran nalo linao uwezo wa kuweka vikwazo na litafanya hivyo.

Ayatullah Ali Khamenei ameongeza kuwa: Taifa la Iran lina irada na azma thabiti na kwamba wakati wowote Jamhuri ya Kiislamu inapoingia katika jambo fulani, huonyesha kivitendo azma na nia yake ya kweli na isiyotetereka.

Amesema hatua ya Iran ya kukabiliana vilivyo na kundi la Daesh ni moja ya mifano ya azma yake hiyo kubwa na isiyotetereka. Amegusia pia uongo na ubazazi unaotumiwa na Marekani na waitifaki wake wakati wanapodai wanapambana na kijikundi hicho cha kigaidi na kusema kuwa: Wamarekani waliiandikia barua wizara yetu ya mambo ya nje na kutwambia kuwa hawaliungi mkono kundi la Daesh lakini siku chache baadaye kulisambazwa picha zinazoonesha namna Marekani inavyolisaidia kijeshi kundi hilo la Daesh.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametumia sehemu nyingine ya hotuba yake kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya hamasa ya wananchi wa Tabriz ya Bahman 29 mwaka 1356 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia sawa na Februari 18, 1978 Milaadia) na kulitaja suala la kuzijua vizuri zama, nyakati na kuchukua hatua wakati unaofaa, ushujaa na imani ya kweli kuwa ni katika sifa za kipekee za wananchi wa Azerbaijan na wa mji wa Tabriz katika nyakati tofauti na amemsifu Ayatullah Mohammad Mojtahed Shabestari, mwanachuoni mwana jihadi ambaye ana busuri na anaangalia mambo kwa mtazamo wa mbali.

Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, wananchi ndio wamiliki halisi wa Mapinduzi ya Kiislamu na nchi ya Iran na mwishoni mwa hotuba yake amesisitiza kwamba: Ni jambo lisilo na shaka kuwa, taifa la Iran litafikia vilele vya vya juu vya heshima na fakhari katika mustakbali usio mbali sana.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mojtahed Shabestari, mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyul Faqih) katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki ambaye pia ni Imam wa Swala ya Ijumaa wa mji wa Tabriz ametoa hotuba fupi na sambamba na kuashiria hamasa kubwa iliyooneshwa na taifa la Iran katika maandamano ya Bahman 22 (Februari 11 mwaka huu) amesisitiza kuwa: wananchi wenye ghera na uchungu wa Azerbaijan wana historia ya kujitokeza vilivyo katika nyuga mbali mbali nyeti kwenye historia ya Mapinduzi ya Kiislamu na hususan katika harakati yao ya Bahman 29, 1356 (Februari 18, 1978) na katika kulinda umoja wa ardhi yote ya Iran na kufanikisha ushindi wa mapinduzi matukufu ya Kiislamu.

Mwakilishi huyo wa Fakihi Mtawala katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki ameongeza kuwa: Wananchi wenye welewa mpana wa Azerbaijan kutokana na uwezo na suhula za aina yake walizo nazo katika upande wa elimu, viwanda na kuheshimu matukufu ya Kiislamu, mara zote wako mstari wa mbele kwenye jitihada za kuunda ustaarabu mpya wa Kiislamu.

              

700 /