Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kaulimbiu ya "Sisi Tunaweza" ionyeshwe kivitendo kwa wananchi

Hotuba iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei katika kikao cha wanachama wa kamati ya maandalizi ya Siku ya Taifa ya Wahandisi hapo tarehe 6/11/93 Hijria Shamsia (26 Januari 2015) ilisambazwa leo asubuhi katika kongamano lililofanyika kwenye ukumbi wa Mnara wa Milad mjini Tehran.

Katika kikao hicho Ayatullah Khamenei aliashiria uwanja mpana wa kazi za kihandisi na mchango mkubwa wa wahandisi vijana katika vipindi mbalimbali na akasema: Katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu (vita vilivyoanzishwa na Saddam Hussein wa Iraq dhidi ya Iran) wahandisi wetu walikuwa askari waliosabilia nafsi zao na walitumia nguvu, sanaa na bongo zao zote na kubuni vitu vipya kila siku.

Amezitaja juhudi na matunda ya kisayansi ya wahandisi hapa nchini baada ya vita vya kujitetea kutakatifu na pia mahudhurio yao katika nafasi nyeti kuwa ni jambo muhimu na akasisitiza kuwa: Inabidi mfanye jitihada kubwa kuhakikisha kwamba kaulimbiu ya "Sisi Tunaweza" inaoneshwa kwa wananchi kivitendo. Vilevile ametilia mkazo suala la kutambua mapungufu na mahitaji ya nchi na kufanya kazi ambazo hazijatekelezwa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia madhara ya uingizaji wa bidhaa kiholela hapa nchini na vilevile magendo na akasema: Hii leo mashinikizo ya uingizaji wa bidhaa kutoka nje unaiumiza nchi na kunatolewa takwimu za kustaajabisha kuhusu kiwango cha bidhaa zinazoingizwa nchini kwa njia za magendo. Hata hivyo amesisitiza kuwa, si jambo la kimantiki pia kufungua rasmi njia ya kuingiza bidhaa kwa wingi nchini kwa kisingizio cha kuzuia magendo na kupata faida ya ushuru wa forodha. 

Amewaambia wahandisi hapa nchini kwamba: Fanyeni bidii ili matunda na bidhaa za vijana wenye vipawa, waumini na bingwa hapa nchini zisimezwe na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Ayatullah Ali Khamenei ameashiria matamshi ya katibu wa kikao hicho kuhusu uchumi wa kimapambano na kukaririwa sana jambo hilo katika hotuba za maafisa wa serikali na wanaharakati wa nyanja mbalimbali na akasema: Kukariri maneno matupu hakuwezi kufua dafu bali jambo hilo linapaswa kuchunguzwa ipasavyo katika Bunge na Serikali na kuangalia nini kimefanyika kuhusu uchumi wa kimapambano na nini kinapaswa kufanyika.         

700 /