Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Utatuzi wa kuchafuliwa mazingira unahitaji kazi na bidii na si kampeni na propaganda

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amekutana na wafanyakazi wa Idara ya Hifadhi ya Mazingira ambapo amesema kuwa utatuzi wa matatizo ya mazingira kama uchafuzi wa hewa, vimbunga vya vumbi na uvamizi wa misitu, nyika na malisho na maeneo ya umma unahitaji mipango, tadbiri na ufuatiliaji wa kweli na wa mara kwa mara wa vyombo husika. Amesisitiza kuwa kulinda mazingira ni wadhifa muhimu wa dola unaopaswa kutekelezwa kwa kutayarishwa hati ya kitaifa ya mazingira na kufungamanishwa na miradi yote ya ujenzi na viwanda na vilevile kwa kutambuliwa kitendo cha kuharibu mazingira kuwa ni kosa la jinai.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mtazamo wa Uislamu kuhusu umuhimu wa kulinda ardhi na utajiri wa umma wa ardhi na akasema: Uislamu na dini za Mwenyezi Mungu daima zinasisitiza udharura wa mwanadamu kujihisi kuwa ana majukumu ya kulinda mazingira na mlingano baina ya mwanadamu na mazingira, kwani sababu ya kujitokeza matatizo ya mazingira ni kuvurugwa mlingano huo.

Ayatullah Khamenei amesema changamoto ya mazingira ni ya dunia nzima. Ameashiria athari za muda mrefu za masuala ya kulinda mazingira na akasema: Uzoefu wa nchi mbalimbali umeonesha kuwa, masuala mengi yanayohusiana na uchafuzi wa mazingira yanaweza kutatuliwa.

Ametoa mfano wa uchafuzi wa hewa katika miji mikubwa na vimbunga vya vumbi na mchanga na akasema kuwa matatizo hayo yanaweza kutatuliwa kwa kuwa na subira na ufuatiliaji unaohitajika.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema suala la kulinda mazingira si suala la serikali hii au ile na wala si suala la mtu huyu au yule, kundi hili au lile, bali ni kadhia ya nchi na taifa zima na wananchi wote wanapaswa kushirikiana kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wake.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hewa, maji na ardhi ni vitu vitatu muhimu katika suala la mazingira. Ameongeza kuwa ili kuweza kutatua masuala kama ya uchafuzi wa hewa katika miji mikubwa, vimbunga vya vumbi na mchanga na vilevile uhaba wa maji na kuharibika kwa ardhi, kuna ulazima wa kufanyika kazi kwa bidii zaidi na ufuatiliaji wa mara kwa mara kuliko kufanya kampeni.

Ayatullah Khamenei amesema misitu na nyika ni sawa na mapafu ya kupumua miji na sababu za kulinda na kuhifadhi ardhi na ameeleza kusikitishwa mno na uvamizi unaofanywa na watu wanaonyemelea fursa dhidi ya misitu na maliasili hususan katika maeneo ya kaskazini mwa Iran. Amesema vyombo husika vinapaswa kukabiliana vikali na wavamizi wa misitu wanaotumia visingizio mbalimbali kama ujenzi wa mahoteli na kuvutia watalii, ujenzi wa vyuo vya kidini na sababu nyingine ambazo kidhahiri zinaonekana kukubalika.

Amevitaja vitendo vya kuvamia na kutwaa ardhi na hata maeneo ya milimani na vilevile ujenzi wa nyumba katika miinuko kweye siku za hivi karibuni kuwa ni miongoni mwa mambo ya kuumiza na kusikitisha na akasema: Sheria inapaswa kuvitambua vitendo kama hivi kuwa ni kosa la jinai na watu wanaohusika na uhalifu huo wafuatiliwe kisheria bila ya huruma; vilevile kama kuna taasisi zilizozembea basi wahusika na uzembe huo wachukuliwe hatua kali.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa kulinda mazingira ni wadhifa wa dola na kuongeza kuwa, kutayarisha hati ya kitaifa ya kulinda mazingira, kufungamanishwa suala la kulindwa mazingira na miradi yote ya ujenzi, viwanda na biashara, kurekebishwa na kutazamwa upya sheria kwa ajili ya kutambua suala la kuharibu mazingira kuwa ni kosa la jinai na kuimarishwa usimamizi makini kuwa ni miongoni mwa njia muhimu za kulinda mazingira na kukabiliana na watu wanaowania fursa za kutaka kujifaidisha na wale wanaovunja sheria.

Ayatullah Khamenei ameutaja mchango wa wananchi katika kulinda mazingira na vilevile suala la kueneza utamaduni wa kulinda mazingira katika jamii kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa kuwa ni jambo muhimu na kuongeza kuwa: Yaliyokuwa lazima kuelezwa yamesemwa hii leo na tangu sasa wananchi wanapaswa kutoa hukumu kwamba ni chombo na taasisi gani zinazotekeleza wajibu wao katika kulinda mazingira na ni zipi hazifanyi bidii na hazichukui hatua kutosha katika uwanja huo.       

 

 

    

700 /