Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Tukabiliane na hujuma dhidi ya Uislamu kwa kuarifisha Uislamu halisi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo Alkhamisi amekutana na Mwenyekiti na wawakilishi wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran ambapo amesema kutekelezwa Uislamu kamili ndiyo takwa la Mwenyezi Mungu na lengo kuu la utawala wa Jamhuri ya Kiislamu hapa nchini. Ameashiria udharura wa kuoneshwa Uislamu halisi mbele ya njama za mabeberu za kutaka kueneza hofu kuhusu Uislamu katika mataifa mbalimbali na akasema: Kuna udharura wa kujiepusha na mtazamo wa kijuujuu wakati wa kuchunguza sababu na njia za kukabiliana na changamoto zilizopo na kuchunguza kwa kina sababu za mambo mbalimbali ili kuweza kuyaendesha vyema na kwa njia za kimantiki.

Ayatullah Khamenei amezungumzia pia sifa na huduma za Ayatullah Muhammad Yazdi na kuongeza kuwa, kuchaguliwa kwake kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Wataalamu ni hatua mwafaka. Amesema kuwa uchaguzi huo ulikuwa makini na bila ya makelele na unaweza kuwa kigezo cha kuigwa na taasisi nyingine.

Akitumia aya za Qur’ani Tukufu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Uislamu unataka kutekelezwa misingi na sheria zote za dini. Amesema kuwa katika mafundisho ya Uislamu hakuna kitu kinachoitwa dini ya kiwango cha chini, kwa msingi huo kuna ulazima wa kutekelezwa vipengee vyote na kamili vya Uislamu na kufanya bidii na harakati ya kudumu katika njia hiyo.

Ayatullah Khamenei amesisitiza udharura wa kulindwa na kuimarishwa pande zote za Uislamu katika “sura” na “sira” yake na kuongeza kuwa: Kulinda sira ya Uislamu kuna maana kwamba Uislamu, malengo na thamani vinapaswa kuwekwa mbele katika mazingira yote ya harakati ya nchi, wananchi na viongozi, na kutayarishwa mipango mizuri ili kuhakikisha jambo hilo linatimia. Amesisitiza kuwa watu wote hapa nchini wanapaswa kufanya harakati katika njia hiyo.

Ayatullah Khamenei amewataja mabeberu wa kimataifa kuwa ndiyo kizuizi kikuu cha harakati ya kuelekea kwenye Uislamu kamili na kuongeza kuwa: Hujuma inayofanywa na vyombo vya kipropaganda na kisiasa vya Wazayuni ili kueneza hofu kuhusu Uislamu ni kielelezo cha woga wao wa kutokemezwa maslahi yao haramu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia baadhi ya matamshi ya maadui wa utawala wa Kiislamu hapa nchini wanaosema wanataka kubadili mwenendo wa Jamhuri ya Kiislamu na si kubadili utawala huo na kusema: Maana ya kubadili mwenendo wa utawala wa Kiislamu ni kulifanya taifa la Iran lishindwe kufanya harakati ya kuelekea kwenye malengo na thamani zake na kutekeleza Uislamu kamili, na lengo hilo kwa hakika lina maana ya kubadili utawala na kuangamiza sira ya dini katika harakati ya umma ya utawala wa Kiislamu ambako mara hii kunafanyika kwa kutumia njia hiyo.

Amesema kuna udharura wa kujiepusha na misimamo isiyo ya kimantiki katika kukabiliana na hujuma ya kuwatisha watu kuhusu Uislamu na akasema: Propaganda za kueneza hofu baina ya watu kuhusu Uislamu kwa hakika ni tarjumi na kielelezo cha hofu na woga wa madhalimu wa kimataifa mbele ya Uislamu wa kisiasa na Uislamu uliopo hivi sasa katika maisha ya mataifa mbalimbali ambao taifa la Iran ndilo linalobeba bendera ya harakati ya kuuimarisha.

Ayatullah Khamenei amesema inawezekana kubadili hujuma hiyo dhidi ya Uislamu na kuifanya fursa nzuri badala ya kuwa tishio. Ameongeza kuwa jitihada za kudumu za kuyatisha mataifa mbalimbali na vijana kuhusu Uislamu zinazusha swali katika fikra za walimwengu kwamba, ni nini sababu ya hujuma na mashambulizi hayo yote dhidi ya Uislamu?

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kutoa majibu sahihi ya swali hilo kupitia njia ya kuonesha Uislamu halisi kwa mataifa mbalimbali kuna baraka nyingi na kuongeza kuwa: Tunapaswa kufanya bidii na juhudi kubwa katika njia hiyo.

Akibainisha Uislamu halisi, Ayatullah Ali Khamenei amesema: Kufundisha Uislamu unaotetea watu wanaodhulumiwa na kukabiliana na madhalimu kunawahamasisha vijana na kuwafahamisha kwamba Uislamu una mipango na ratiba ya kivitendo ya kuwatetea watu wanaodhulimiwa na wasio na makimbilio.

Ayatullah Khamenei amesema sifa nyingine za Uislamu halisi ni kutetea akili na mantiki, kukabiliana na mitazamo finyu na fikra mgando na kupambana na hurafa. Ameongeza kuwa tunapaswa kuarifisha Uislamu wa kushikamana na mafundisho ya dini mkabala wa kutojali mafundisho hayo, Uislamu unaokuwa katika maisha ya watu mkabala wa Uislamu wa kisekulari, Uislamu unaokuwa rehema kwa matu dhaifu na Uislamu wa kupigana jihadi dhidi ya mabeberu; kwa njia hiyo tubadili mradi wa kuwatisha watu kuhusu Uislamu na kuufanya fursa ya kulingania Uislamu halisi kwa mataifa mbalimbali.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria changamoto zilizopo kati ya Iran na Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya ikiwemo kadhia ya nyuklia na akasema: Kuna ulazima wa kuchunguza chanzo cha changamoto na matatizo yaliyopo kwa kujiepusha na mitazamo ya kijuujuu, na kwa utaratihu huo tuweze kupata njia ya kimantiki ya ufumbuzi.

Ametolea mfano matatizo yaliyosababishwa na vikwazo na kuongeza kuwa: Upembuzi yakinifu unaonesha kuwa, sababu ya matatizo tuliyosababishiwa na vikwazo ni utegemezi wa nchi kwa mafuta na uchumi unaodhibitiwa na serikali na kutoshirikishwa wananchi katika masuala ya kiuchumi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuliza maswali kadhaa muhimu akisema: Je, kama tusingefanya uchumi na maisha ya wananchi yategemee pato la mafuta na tukajiepusha kuendeleza makosa ya kipindi cha mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu ya kuweka mambo yote mikononi mwa serikali na badala yake tukawashirikisha ipasavyo wananchi katika shughuli za kiuchumi, adui angeweza kusababisha matatizo haya kwa kutumia vikwazo vya mafuta na vikwazo dhidi ya taasisi za serikali?

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa kama tungetibu mambo hayo kwa njia hii matatizo yangetatuliwa na wala hatutakuwa na haja ya mapenzi na huruma ya adui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria ufanisi wa mtazamo huo wa kina na kimantiki katika kukabiliana na changamoto za wazi na zisizo wazi mkabala wa mabeberu duniani ikiwemo kadhia ya nyuklia na akasema: Timu ya nyuklia iliyochaguliwa na Rais wa Jamhuri ni nzuri, aminifu, inayokubalika na inachapa kazi kwa bidii; hata hivyo nina wasiwasi kwa sababu upande wa pili unatumia hadaa, ujanja, hila na kusaliti.

Ameashiria makosa yanayofanyika mara kwa mara kwamba watu wenye nguvu na uwezo hawana haja ya kufanya hila na hadaa na kusema: Baadhi wanadhani kuwa Marekani yenye nguvu na uwezo mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi haina haja ya kufanya hadaa; lakini kinyume na dhana hiyo Wamarekani wanahitaji sana hila na hadaa na hivi ndivyo wanavyofanya; ukweli huu unatutia wasiwasi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kuwa macho mbele ya hila na hadaa za Wamarekani na kusema :Wamarekani daima hutumia lugha kali na ya kufurutu mipaka unapokaribia wakati ulioainishwa kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo ili kufikia malengo yao, kwa msingi huo kuna haja ya kuwa macho.

Ayatullah Khamenei amezungumzia pia matamshi ya kipuuzi na yanayochukiza yaliyotolewa na Wamarekani katika wiki na siku za hivi karibuni na kusema: Mjinga mmoja wa Kizayuni alitoa hotuba huko, na ili kujitenga naye maafisa wa Marekani walitoa matamshi ambayo ndani yake waliituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi; hakika maneno haya ni kichekesho.

Amesema Wamarekani na waitifaki wao katika Mashariki ya Kati wameanzisha kundi habithi na katili zaidi la kigaidi yaani Daesh na mengine mfano wake na wanandelea kuyapa misaada na wakati huo huo wanalituhumu taifa la Iran na utawala wa Kiislamu kuna unaunga mkono ugaidi!

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia uungaji mkono wa waziwazi wa serikali ya Marekani kwa utawala bandia na wa Kizayuni wa Israel na kusema: Washington inaiunga mkono na kuisaidia kwa hali na mali serikali ambayo imekiri rasmi kufanya ugaidi na wakati huo huo inaituhumu Jamhuri ya Kiislamu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa barua iliyoandikwa hivi karibuni na maseneta wa Marekani (kwa viongozi wa Iran) ina vielelezo vingi vya kuporomoka maadili ya kisiasa katika mfumo wa utawala wa Marekani. Ameongeza kuwa: Kwa mujibu wa sheria zilizokubalika kimataifa, nchi zote huendelea kuheshimu ahadi na makubaliano yao na (pande nyingine) hata baada ya kuondoka serikali iliyokuwa madarakani na kushika hatamu serikali nyingine, lakini maseneta wa Marekani wametangaza rasmi kwamba, iwapo serikali ya sasa ya nchi hiyo itaondoka basi makubaliano yake na pande nyingine pia yatakuwa bure bilashi; je, hiki si kielelezo cha kuporomoka maadili ya kisiasa na kusambaratika ndani kwa ndani mfumo wa utawala wa Marekani?  

Ayatullah Ali Khamenei ameongeza kuwa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanatambua vyema kazi yao na iwapo tutafikia makubaliano wanajua jinsi ya kufanya ili hapo badaye serikali ya Marekani isiwezi kujinasua kwenye makubaliano hayo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amemkumbuka na kumuenzi marehemu Ayatullah Mahdavi Kani na kusema kuwa alikuwa mwanazuoni aliyefanyia kazi elimu yake na mwenye jitihada zilizokuwa na taathira. Ayatullah Khamenei amemuombea dua na maghufira mwanazuoni huyo.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran alitoa ripoti kuhusu kikao cha 17 cha baraza hilo. Ayatullah Muhammad Yazdi amesema kuwa miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na mwenendo wa mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1, masuala ya ndani ya nchi na ulazima wa kutekelezwa sera za uchumi wa kimapambano, kujiepusha na nara tupu, ripoti kuhusu nafasi ya Uislamu katika hali ya sasa duniani, hujuma dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi na wasiwasi uliopo kuhusu masuala ya kiutamaduni.

   

                     

700 /