Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ujumbe wake wa mwaka mpya:

Mwaka mpya wa 1394 Hijria Shamsia naupa jina la “Serikali na Wananchi, Mshikamano na Maelewano”

Katika ujumbe wake uliotolewa kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1394 Hijria Shamsia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amelitakia heri na mwaka mpya taifa la Iran na mataifa yote yanayoadhimisha sikukuu ya Nowruz na kuupa mwaka mpya jina la Mwaka wa Serikali na Wananchi, Mshikamano na Maelewano.

Ayatullah Khamenei ameashiria suala la kusadifiana kuanza mwaka mpya na siku za kukumbuka tukio chungu la kufa shahidi Bibi Fatimatu Zahra (as) na kusema: Mapenzi ya taifa letu kwa Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) yanaandamana na mambo ya lazima kuyafanya na nina yakini kwamba, wananchi watayachunga na kuyatekeleza. Ni matarajio kwamba mwaka mpya utaandamana na baraka za Bibi Fatima, na kumkumbuka mtukufu huyo kutakuwa na taathira kubwa na za kubakia siku zote katika maisha ya wananchi.

Katika mtazamo wake wa kiujumla kwa masuala ya mwaka 1394, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuna udharura wa kuwepo ushirikiano mpana kati ya serikali na wananchi na kusisitiza kuwa: Ili kuweza kutekeleza kaulimbiu ya mwaka 1394 yaani “Serikali na Wananchi, Mshikamano na Maelewano”, kuna ulazima wa pande hizo mbili za kaulimbiu hii yaani taifa azizi, kubwa, shujaa, angavu, lenye maarifa na hima la Iran, na serikali inayohudumia wananchi kuaminiana na kushirikiana kwa dhati.

Ayatullah Khamenei ameashiria matarajio ya taifa la Iran katika mwaka mpya na akasema: “Maendeleo ya kiuchumi”, “nguvu na izza ya kieneo na kimataifa”, “harakati kubwa ya kielimu kwa maana yake halisi”, “uadilifu wa mahakama na wa kiuchumi” na zaidi ya yote hayo “Imani na masuala ya kiroho” ni mambo makubwa tunayotarajia kwa ajili ya taifa la Iran katika mwaka huu, na matakwa na matarajio haya yote yanaweza kupatikana na hayako nje ya uwezo wa taifa adhimu la Iran na siasa za utawala wa Kiislamu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kwa kusema kuwa, sharti la kupatikana matarajio makubwa ni ushirikiano na mshikamano wa pande mbili za serikali na wananchi na akaongeza kuwa: Serikali inahudumia wananchi, na wananchi ni waajiri wa serikali, na kadiri ushirikiano kati ya serikali na taifa unavyozidi, kazi zitaboreka na kuwa nzuri zaidi; kwa msingi huo serikali inapaswa haswa kulikubali taifa na kutambua thamani, umuhimu na uwezo wa wananchi, vilevile taifa linapaswa kuiamini serikali ipasavyo.

Akitathmini kiwango cha kutimizwa kaulimbiu ya mwaka 1393 Hijria Shamsia, Ayatullah Khamenei amesema mwaka uliopita uliandamana na changamoto na maendeleo ya nchi na kuongeza kuwa: Kaulimbiu ya “Azma ya Kitaifa na Uendeshaji wa Kijihadi” ilichaguliwa kwa ajili ya mwaka 1393 kwa kutilia maanani changamoto hizo, na taifa letu pia limeonesha hima na azma yake kubwa katika kustahamili baadhi ya matatizo na kwa kuhudhuria kwa wingi katika minasaba mbalimbali muhimu ikiwemo maandamano ya tarehe 22 Bahmar (11 Februari wakati wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu), Siku ya Kimataifa ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani) na katika maandamano makubwa ya siku ya Arubaini (ya Imam Hussein AS).

Kuhusu uendeshaji na uongozi wa kijihadi, Ayatullah Khamenei amesema suala hilo limefanyika katika baadhi ya maeneo na kuongeza kuwa: Mahala popote panapokuwapo uongozi na uendeshaji wa kijihadi maendeleo pia yamekuwapo. Hata hivyo amesema, azma ya kitaifa na uendeshaji wa kijihadi si makhsusi kwa ajili ya mwaka uliopita wa 1393 Hijria Shamsia bali pia vinahitajiwa na taifa azizi la Iran kwa ajili ya mwaka huu na miaka yote inayokuja.    

 

       

700 /