Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Vikwazo viondolewe baada tu ya kufikiwa makubaliano

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo (Jumamosi) katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 1934 Hijria Shamsia amehutubia hadhara kubwa ya makumi ya maelfu ya wananchi waliokwenda kuzuru Haram ya Imam Ali bin Mussa Ridha (as) katika uwanja wa Imam Khomeini. Katika hotuba hiyo muhimu, Ayatullah Khamenei ametoa maelezo kuhusu kaulimbiu ya mwaka mpya ya “Serikali na Wananchi, Mshikamano na Maelewano” na kusisitiza juu ya wadhifa wa pande mbili wa uungaji mkono wa wananchi kwa serikali halali na ya kisheria na ulazima wa viongozi wa serikali kuwa na kifua kipana na kustahamili ukosoaji wa kimantiki. Ameashiria nguzo nne kuu za jengo la mfumo wa Kiislamu, fursa na changamoto zinazoukabili mfumo huo na akasema: Kupanga malengo na viongozi kuweka ratiba na mipango kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na msaada wa kila mwananchi hususan wadau wa sekta ya uchumi na vyombo vya habari kwa uchumi wa taifa ni wadhifa mkubwa na wa watu wote. Amesisitiza kuwa hii leo uwanja wa uchumi ni uwanja wa mpambano makhsusi unaohitajia harakati ya kijihadi kwa msingi wa kujumuisha pamoja uwezo, ubunifu wa ndani na kutumia nyenzo, mbinu na sera makhsusi za mpambano huo.

Kuhusu mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Nchini Iran hakuna mtu anayepinga utatuzi wa kidiplomasia wa maudhui hii ya nyuklia lakini katika upande mwingine taifa la Iran, maafisa wa serikali na timu ya mazungumzo ya Iran haitalegeza kamba mbele ya misimamo ya kutwishwa na mabavu ya Marekani na itafanikiwa katika mtihani huo mkubwa.

Ayatullah Khamenei ameashiria aya ya Qur’ani Tukufu na kutaja mambo manne yaani “Swala, Zaka, kuamrisha mema na kukataza maovu” kuwa ni vigezo na nguzo nne za jengo la utawala wa Kiislamu. Ameongeza kuwa: Mwenyezi Mungu Mtukufu ameahidi kulinusuru na kulisaidia taifa lenye sifa hizo na kuliondoa chini ya udhibiti wa watawala madhalimu. Amesema kuwa kila kimoja kati ya vigezo hivyo kina upande wa mtu binafsi na wa kijamii na vilevile taathira kubwa katika kujenga mfumo wa Kiislamu.

Akiashiria upande unaohusiana na mtu binafsi wa ibada ya Swala katika saada na ufanisi wa mwanadamu muumini, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Wakati huo huo Swala ina upande wa kijamii na inatayarisha mazingira ya kuziunganisha nyoyo za Waislamu katika wakati mmoja na kuelekea kwenye kituo kimoja.

Vilevile amesema Zaka inatayarisha uwanja mzuri wa kuimarika moyo wa kutoa na ukarimu katika nafsi ya mwanadamu na kueleza faida za kijamii za ibada hiyo akisema: Katika upande wa kijamii Zaka inaonesha kuwa, Mwislamu anajitambua kuwa anawajibika mbele ya jamii ya Kiislamu, masikini, watu wasiojiweza na wenye haja.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuamrisha mema na kukataza maovu ndiyo msingi wa sheria zote za Uislamu. Amongeza kuwa: Waumini wote popote pale walipo duniani wanawajibika kuielekeza jamii upande wa mema na mambo mazuri na kutahadharisha kuelekea upande wa maovu na machafu. Amesema kuwa, suala linalopaswa kupewa umuhimu mkubwa zaidi ni kuamrisha jema kubwa zaidi ya yote, yaani kuanzisha na kulinda utawala wa Kiislamu.

Amesema, kulinda heshima ya taifa la Iran, kuimarisha utamaduni, kulinda maadili, kulinda mazingira ya ndani ya familia, kuzidisha na kulea kizazi cha vijana, kutayarisha mazingira bora ya maendeleo ya nchi, kustawisha uchumi na uzalishaji, kueneza maadili ya Kiislamu katika jamii nzima, kupanua elimu na teknolojia kutekelezwa uadilifu mahakamani na katika uchumi, kufanya juhudi kwa ajili ya umoja wa Kiislamu, kuinua juu taifa na uwezo na nguvu ya Umma wa Kiislamu ni miongoni mwa mema mengine makubwa zaidi ambayo wananchi wote wanawajibika kufanya jitihada za kuhakikisha yanatimia.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameashiria baadhi ya vielelezo vya maovu makubwa ikiwa ni pamoja na kuporomoka kiutamaduni, kuwasaidia maadui, kudhoofisha utawala na utamaduni wa Kiislamu, kudhoofisha uchumi, elimu na teknolojia na akasema: Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala alikuwa wa kwanza na Mtume (saw) na Maimamu maasumu katika kizazi chake walikuwa mstari wa mbele zaidi katika kuamrisha mema na kukataza maovu, na ni wajibu kwa waumini wote popote pale walipo katika ulimwengu wa Kiislamu kutekeleza faradhi hiyo ya Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei ameendelea kwa kutoa ufafanuzi kuhusu kaulimbiu ya mwaka mpya (wa Hijria Shamsia) yaani “Serikali na Wananchi, Msikamano na Maelewano” na akasema kwamba, kuchaguliwa kwa kaulimbiu hiyo kumefanyika kwa kutilia maanani vigezo hivyo vinne vikuu na kwa ajili ya msikamano wa kitaifa na kijamii wa wananchi wote katika mfumo wa Kiislamu. Amesema kuwa: Uislamu unataka kuwepo mshikamano na maelewano na kusaidiana kati ya mirengo yote ya jamii; kwa msingi huo kila serikali inayokuwa madarakani katika mfumo wa Kiislamu inapaswa kuungwa mkono na kusaidiwa na wananchi wote hata wale ambao hawakuipa kura zao.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuna udharura wa kuwepo umoja na mshikamano wa wananchi na serikali hususan wakati nchi inapokabiliana na changamoto kubwa na akaongeza kuwa: Hii leo ni wajibu wa kila mwananchi kuwasaidia na kuwaunga mkono maafisa na viongozi wa nchi na serikali.

Amesema kushirikiana na kuzisaidia serikali zinazokuwa madarakani katika Jamhuri ya Kiislamu ni msingi thabiti na wa daima. Akibainisha zaidi udharura wa suala hilo amesema: Dukuduku kuu na la msingi la serikali zote ni kutatua matatizo ya wananchi na nchi kadiri ya uwezo; hivyo wananchi wote wanapaswa kuzisaidia serikali kwa ajili ya kutatua matatizo hayo.

Ayatullah Khamenei amesema, kura za wananchi wengi zinatayarisha uwanja wa “uhalali wa kisheria wa serikali” na akaongeza kuwa: Si muhimu kiwango cha idadi ya watu waliompigia kura Rais wa Jamhuri, bali kila serikali iliyochaguliwa kwa kiwango chochote cha kura nyingi za wananchi huwa halali kwa mujibu wa katiba, na wananchi wanapaswa kuisaidia serikali halali kadiri wanavyoweza.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, katika anga hiyo ya ushirikiano na msaada, haki za pande mbili zinalindwa na kuheshimiwa. Ameashiria pia suala la wakosoaji, jinsi ya kueleza ukosoaji na jinsi ya kuamiliana na wakosoaji.

Amezungumzia mwenendo wa kawaida yaani “kuwepo kundi la wakosoaji” wa kila serikali na kusema: Serikali ya sasa pia kama zilivyokuwa serikali za kabla yake ina wakosoaji na hakuna tatizo kwa baadhi ya watu wasiokubaliana na mbinu, mwenendo na sera za serikali kuikosoa, lakini ukosoaji unapaswa kufanyika kwa misingi ya mantiki.

Ayatullah Khamenei amesema: Mimi mwenyewe pia nimekuwa nikizikosoa serikali mbalimbali zinazoshika madaraka hapa nchini na sikuacha kutoa maoni yangu popote pale panapohitajika kukosolewa lakini nilieleza mitazamo yangu kwa njia nzuri na inayofaa.

Akieleza mipaka ya “ukosoaji wa kimantiki”, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Ukosoaji haupasi kufanyika kwa njia ambayo itaondoa imani ya wananchi kwa viongozi wanaofanya kazi na kulifanya taifa lisiwaamini viongozi, vilevile haupaswi kuambatana na udhalilishaji na mbinu za kuzusha mivutano.

Amesema mwenendo wa udugu wa Kiislamu, mshikamano na upendo ni miongoni mwa vigezo vya dharura wakati wa kukosoa utendaji wa serikali na kuongeza kuwa, mambo haya yanazihusu pande zote, na viongozi wa nchi katika mihimili mitatu mikuu ya dola pia wanalazimika kulinda mipaka hiyo na kuwa na mwenendo mzuri, usio wa kudunisha wala kudhalilisha kwa wakosoaji wao, kwa sababu hatua yoyote ya viongozi kuwadunisha wapinzani ni kinyume na tadbiri, hekima na busara.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Siwataki wananchi azizi kupuuza au kuacha kusimamia utendaji wa serikali, bali nawahimiza kujali masuala ya nchi na ninasisitiza kuwa, mienendo sawa iwe ya wananchi au ya viongozi, isiwe ya kuchafuana au kuambatana na udunishaji na udhalilishaji.

Amesema kuwa si kosa kuwepo watu wanaoeleza wasiwasi na dukuduku zao kuhusu masuala muhimu ya nchi na hakuna kizuizi chochote katika hilo, lakini suala hilo halipaswi kuwa na maana ya kutoa tuhuma na kupuuza juhudi na huduma zilizofanywa; katika upande mwingine pia serikali na waungaji mkono wake hawapaswi kuwadunisha na kuwadhalilisha wale wanaoeleza wasiwasi na dukuduku zao kuhusu utendaji wa serikali.

Akieleza mwenendo wake wa daima wa kuzihami serikali zote zilizotangulia, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Vilevile ninaihami na kuiunga mkono serikali ya sasa, lakini simpi mtu yeyote cheki nyeupe iliyosainiwa, bali ninatoa hukumu na kuamiliana na serikali hizo kulingana na utendaji wao.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia fursa kubwa na changamoto zilizopo na kusema: Kwa mipango mizuri na inayofaa na kwa kutumia vyema uwezo wetu, tunaweza kushinda changamoto hizo kwa taufiki yake Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei amesema nguvu kazi hodari na yenye ubunifu ambayo sehemu yake kubwa inaundwa na vijana, na kushikamana wananchi na vijana hao na mfumo wa Kiislamu ni miongoni mwa fursa kubwa za nchi. Ameongeza kuwa, licha ya mashambulizi makubwa ya vyombo vya habari yanayofanywa na wageni dhidi ya vijana wa nchi hii ili kuwavunja moyo kuhusu mustakbali au kuwafanya wakabiliane na mfumo wa Kiislamu au kutojali mambo ya nchi, lakini makumi ya mamilioni ya vijana hawa kote nchini wanamiminika mitaani katika siku ya tarehe 22 Bahman (siku ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu) na kuonesha mapenzi yao makubwa kwa mfumo wa Kiislamu na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu.

Amesema kuwa maendeleo ya kisayansi ya kipindi hiki cha vikwazo ni miongoni mwa fursa kubwa za Iran na kuongeza kuwa, maendeleo mbalimbali ya kisayansi katika miaka ya hivi karibuni hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutekelezwa miradi mikubwa na migumu ya kiviwanda kama mradi wa awamu ya 12 wa Pars Kusini na kuzinduliwa zana mpya na za kuwastaajabisha maadui katika mazoezi ya kijeshi ya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu, hayo yote yamefanyika katika kipindi ambacho wanaoitakia mabaya Iran wanadhani kuwa wameiwekea nchi hii vikwazo vya kulemaza.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amevitaja vikwazo vya sasa dhidi ya Iran pia kuwa ni fursa licha ya matatizo yake yote na akatoa maelezo kuhusu changamoto zinazoukabili mfumo wa Kiislamu. Amesema kuwa, miongoni mwa changamoto kubwa za sasa za Iran ni suala la uchumi wa taifa na utatuzi wa matatizo ya kiuchumi na kimaisha ya wananchi na kwamba suala hilo linahitaji harakati na kazi kubwa.

Ayatullah Khamenei amekumbusha tahadhari yake ya miaka kadhaa iliyopita kuhusu njama za adui za kujielekeza kwenye suala la uchumi na udharura wa kuwa tayari viongozi wa nchi kwa ajili ya kukabiliana na njama hizo na akasema: Wanaolitakia mabaya taifa la Iran wanasema waziwazi kwamba, lengo la mashinikizo ya kiuchumi ni la kisiasa yaani kuwafanya wananchi waichukie Jamhuri ya Kiislamu na kuvuruga usalama wa taifa kwa kuwapambanisha wananchi na serikali na utawala wa Kiislamu.

Amesisitiza kuwa ili kuweza kukabiliana na changamoto hiyo kunahitajika umoja na mshikamano wa makundi yote na viongozi na kulipa umuhimu mkubwa suala la uchumi. Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu amebainisha mambo manne.

Jambo la kwanza lililobainishwa na Ayatullah Khamenei ni ulazima wa kuwepo harakati ya kijihadi ya kukabiliana na siasa za kiadui za Marekani katika medani ya mpambano wa kiuchumi. Katika uwanja huo ameashiria mitazamo ya aina mbili iliyopo hapa nchini kuhusu jinsi ya kutatua matatizo ya kiuchumi.

Amesema: Mtazamo mmoja hapa nchini unaamini kuwa maendeleo na ustawi wa kiuchumi unapaswa kudhaminiwa kwa kutumia uwezo na suhula za ndani ya nchi ambazo hadi sasa hazijapewa mazingatio ya kutosha au hazijatumiwa kabisa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, mtazamo wa pili ni ule unaokabiliana na huo wa kwanza na unaamini kuwa, ustawi na maendeleo ya kiuchumi yanaweza kupatikana kwa kuelekeza macho yetu nje ya mipaka ya nchi; kwa msingi huo tunapaswa kubadilisha siasa zetu za nje na kufanya mapatano na mabeberu na kukubali dhulma zao ili matatizo ya kiuchumi yatatuliwe!

Ayatullah Khamenei amesema, mtazamo huu wa pili ni makosa kabisa, tasa na usio na faida.

Akifafanua sababu za makosa ya mtazamo huu wa pili, amesema kuwa: Vikwazo vya sasa vya Magharibi dhidi ya taifa la Iran ni ushahidi wa wazi wa makosa ya mtazamo unaoamini kuwa, ustawi wa kiuchumi utapatikana kwa kujielekeza nje ya nchi, kwani madola ya kigeni hayana mpaka wowote katika kuzitwisha nchi nyingine mitazamo na dhulma zao, mbali na kuwa zinaanzisha baadhi ya masuala ya ghafla na yasiyotarajiwa kama njama ya kupunguza bei ya kimataifa ya mafuta na kutoa pigo kwa uchumi wa Iran.

Ayatullah Khamenei amongeza kuwa, hii leo watu wanaolitakia mabaya taifa la Iran wanafanya juhudi za kuimarisha na kutia nguvu mtazamo wa pili na kwa sababu hiyo Rais wa Marekani alisema katika ujumbe wake wa Nowroz (mwaka mpya wa Kiirani) akiwaambia wananchi wa Iran kwamba: “Iwapo mtakubali matakwa yetu katika mazungumzo ya nyuklia kutapatikana kazi na ustawi wa kiuchumi nchini Iran”.

Amesisitiza kuwa, kujielekeza nje ya nchi kwa ajili ya kutatua matatizo ya  kiuchumi hakuwezi kuwa na matunda kwa msingi huo tunapaswa daima kutumia suhula na uwezo wa ndani; na uchumi wa kimapambano uliokaribishwa na wataalamu wote wa uchumi unalenga katika suhula na uwezo wa ndani ya nchi na taifa.

Suala la tatu lililotajwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu masuala ya kiuchumi ni ulazima wa viongozi kuwa na malengo na sera na kutokukwama katika masuala ya sasa tu.

Ayatullah Khamenei amesema, lengo kubwa zaidi linalopaswa kupewa umuhimu na viongozi na wananchi katika mwaka huu ni kutoa mazingatio makhsusi kwa suala la kuimarisha uzalisha wa ndani. Amebainisha njia za kuimarisha uzalisha wa ndani na kusema: Kuhami taasisi ndogo na za kati, kuimarisha kazi na harakati za taasisi za elimu msingi, kuanzisha harakati ya kupunguza uuzaji wa malighafi, kusahilisha uwekezaji, kupunguza uingizaji wa bidhaa za matumizi kutoka nje ya nchi na kupambana na magendo ndiyo njia za kuhami uzalisha wa ndani. Amesema kuwa benki zinaweza kuwa na mchango nzuri au kusababisha uharibifu katika kadhia hii, kwa msingi huo maafisa waandamizi wa mabenki hapa nchini wanapaswa kulizingatia vilivyo suala hili.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kufanya kazi hizi ni kugumu sana na wakati huo huo amesema: Viongozi wa nchi wanalazimika kufanya kazi hizo ngumu, kwa sababu suala la uchumi na ustawi wa kiuchumi lina umuhimu mkubwa.

Ayatullah Khamenei amesema, mchango wa wawekezaji na wananchi katika kuhami uzalishaji wa ndani una taathira kubwa na kusisitiza kwamba, miongoni mwa njia za kuimarisha uzalishaji wa ndani ni kuelekeza mitaji katika uzalishaji na utumiaji wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na kujiepusha na israfu.     

Akibainisha suala la nne na la mwisho kuhusu maudhui ya uchumi wa taifa amesema: Vikwazo ndiyo wenzo pekee wa adui kwa ajili ya kukabiliana na taifa la Iran, hivyo iwapo tutapanga mipango yetu kwa njia sahihi na kwa kutegemea nguvu za ndani ya nchi, athari za vikwazo zitapungua na mwishowe havitakuwa na taathira yoyote.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, iwapo viongozi wa serikali, wananchi wote na wadau wa masuala ya uchumi watafanya hima na vyombo vya habari vya umma vikasaidia, mutaona kuwa vikwazo havitaweza kuzuia maendeleo ya taifa la Iran.

Baada ya hapo Ayatullah Ali Khamenei amezungumzia kadhia ya mazungumzo ya nyuklia na kueleza nukta kadhaa.

Ameashiria sera na mipango iliyoratibiwa kwa uangalifu mkubwa ya upande wa pili katika mazungumzo hayo ambao unadhibitiwa na Marekani na akasema: Wamarekani wanahitajia sana mazungumzo haya, na hitilafu zao za ndani zinatokana na kuwa, upande unaoipinga serikali ya sasa ya Marekani hautaki kuona alama nzuri za mazungumzo hayo zikisajiliwa kwa jina la chama hasimu.

Ameashiria pia ujumbe wa Nowruzi wa Rais wa Marekani na matamshi yake yasiyo ya kweli katika ujumbe huo na akasema: Katika ujumbe huo Rais wa Marekani amesema nchini Iran kuna watu wanaopinga utatuzi wa kidiplomasia wa maudhui ya nyuklia; maneno haya ni urongo, kwa sababu nchini Iran hakuna mtu anayepinga utatuzi wa kadhia ya nyuklia kupitia njia ya mazungumzo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, jambo linalopingwa na taifa la Iran ni sera za mabavu na za kutaka kulazimisha mitazamo ya serikali ya Marekani, na taifa la Iran linaendelea kukabiliana nazo.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, viongozi, timu ya mazungumzo na taifa la Iran halitakubali kamwe sera za kimabavu na kidhalimu za Marekani.

Amesisitiza tena kuwa, mazungumzo ya sasa ya Iran na Marekani ni kuhusu maudhui ya nyuklia peke yake na si jambo lolote jingine. Amesema: Katika masuala ya ndani na ya kieneo na maudhui ya silaha hatutafanya mazungumzo na Marekani, kwa sababu siasa za nchi hiyo katika eneo hili ni kuzusha machafuko, kuvuruga amani na kukabiliana na mataifa ya eneo hili na mwamko wa Kiislamu, jambo ambalo ni kinyume na siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia matamshi ya mara kwa mara ya Wamarekani kwamba vikwazo dhidi ya Iran havitaondolewa ila baada ya kufikiwa makubaliano na kuchunguzwa mwenendo na utendaji wa Iran na kusema, hiyo ni hadaa. Amesema kuwa, maneno kama haya hayakubaliki, kwa sababu suala la kuondolewa vikwazo ni sehemu ya mazungumzo na si matokeo yake; hivyo basi kama alivyosema waziwazi mheshimwa Rais wa Jamhuri, vikwazo vinapaswa kuondolewa mara moja baada tu ya kufikiwa makubaliano.

Vilevile Ayatullah Khamenei ameashiria matamshi ya Wamarekani wanaosema kuwa, maamuzi ya Iran katika kila makubaliano yanayotarajiwa yanapaswa kuwa ya kudumu na yasiyoweza kutenguliwa na akasema: Maneno hayo pia hayakubaliki, kwa sababu iwapo wao wenyewe wanajipa haki ya kuweka tena vikwazo kwa kutumia kisingizio cha aina yoyote baada ya kufikiwa makubaliano, hakuna sababu inayoifanya Iran ikubali hatua ambazo haziwezi kuangaliwa upya na kutenguliwa.

Amesema teknolojia ya nyuklia nchini Iran imekuwa elimu ya ndani ya  nchi na iliyoenea baina ya wananchi na inapaswa kustawishwa zaidi, kwani maendeleo na kustawi zaidi ni sehemu ya kila teknolojia.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia madai ya Wamarekani wanaosema kwamba Iran inafanya jitihada za kupata silaha za nyuklia na kusema: Wao wenyewe wanaelewa vyema kwamba katika mazungumzo haya tumeheshimu sheria zote za kimataifa na maadili ya kisiasa wala hatujavunja ahadi na kuwa na tabia za kinyonga; lakini katika upande ule wa pili, Wamarekani wamevunja ahadi, kughushi, kubadili misimamo na kuwa na undumakuwili katika misimamo na matamshi yao.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa mwenendo wa Wamarekani katika mazungumzo ya nyuklia unapaswa kuwa darsa na ibra kwa wananchi wa Iran na kuongeza kuwa, mwenendo wa Marekani pia ni ibra kwa wanafikra wa ndani ya nchi ili wapate kujua tunakabiliana na nani katika mazungumzo na vilevile kujua mwenendo wa Marekani.

Ameashiria pia vitisho vya Marekani vya uwezekano wa kuzidisha vikwazo au kufanya mashambulizi ya kijeshi iwapo hakutafikiwa makubaliano na kusema: Vitisho hivyo havilitii hofu wala woga taifa la Iran na litashinda mtihani huu mkubwa kwa mafanikio kamili.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, taufiki na msaada wa Mwenyezi Mungu ndiyo sababu kuu ya mafanikio ya taifa la Iran katika njia hiyo. Ameongeza kuwa, serikali na taifa la Iran lina kazi kubwa ikiwa ni pamoja na suala la umoja wa Kiislamu, kuyasaidia mataifa yanayodhulumiwa na kueneza satua na ushawishi wa kiroho wa Uislamu katika eneo hili, jambo ambalo bendera yake kwa sasa inashikwa na taifa la Iran.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Ayatullah Khamenei amezungumzia historia ya Nowruzi na kusema, sherehe za sasa za Nowruzi ni “ubunifu makini wa Kiislamu”. Ameongeza kuwa, Nowruzi ya jadi na kale ilikuwa sherehe ya wafalme na fursa ya masultani na watawala kwa ajili ya kuonesha adhama yao ya kidhahiri kwa mataifa, lakini Wairani Waislamu walibadilisha kalibu na mfumo huo kwa maslahi yao wenyewe.

Amesema hakika ya Nowruzi ni “hakika ya wananchi” na kuongeza kuwa, Nowruzi ya sasa si Nowruzi ya kijadi na kale bali ni “Nowruzi ya Kiirani na Nowruzi ya taifa la Kiislamu” ambalo limeweza kujitengenezea rasilimali ya kufanya harakati kuelekea kwenye malengo yake ya kimaanawi na kiroho kupitia kalibu ya sherehe hiyo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa maeneo yenye msongamano mkubwa zaidi wa watu na harakati nyingi hapa nchini katika siku hizi za sherehe ya Nowruzi na kuanza mwaka mpya ni Haram tukufu za Maimam watoharifu katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw) na watoto wao.

Ayatullah Khamenei ameashiria suala la kusadifiana siku ya kukumbuka tukio chungu na kufa shahidi Bibi Fatimatu Zahra (as) na sikukuu ya Nowruzi na kusema: Kwa kutilia maanani mtazamo makini wa Wairani kuhusu Nowruzi, sherehe za Nowruzi na mwaka mpya hazipaswi kupingana na heshima ya siku ya kufa shahidi mwanamke bora zaidi duniani, Bibi Fatimatu Zahra (as).

700 /