Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Njia ya kuhitimishwa mgogoro wa Yemen ni kusitishwa mashambulizi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei amesema leo katika mazungumzo yake na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki aliyeko safarini hapa nchini kwamba mwamko wa Kiislamu ndiyo sababu kuu ya wasiwasi wa maadui wa Uislamu. Ayatullah Khamenei ameashiria njama na mipango ya maadui kwa ajili ya kukabiliana na mwamko wa Kiislamu na akasema: Hii leo Marekani na Wazayuni wanafurahishwa na hitilafu za ndani katika baadhi ya nchi za Waislamu na njia ya utatuzi wa matatizo hayo ni ushirikiano wa nchi za Kiislamu na kuchukuliwa hatua za kivitendo na zinazofaa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amezungumzia maslahi ya pamoja ya Iran na Uturuki ya kuimarishwa zaidi uhusiano wa pande hizo mbili na akasema: Nguvu ya kila moja kati ya nchi za Kiislamu ni nguvu ya umma mzima wa Kiislamu, na siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ni kuona nchi za Kiislamu zikiimarishana na kujiepusha kudhoofishana. Amesisitiza kuwa kuimarishwa uhusiano wa Iran na Uturuki kutasaidia kufikiwa lengo hilo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Sisitizo la siku zote la Iran ni kwamba nchi za Waislamu hazifaidi lolote kwa kuitegemea Magharibi na Marekani na hii leo inaonekana wazi kwamba, matokeo ya hatua za Magharibi katika Mashariki ya Kati yamekuwa na madhara kwa Uislamu.

Ameashiria matukio yanayojiri katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati na harakati za kikatili za makundi ya kigaidi huko Iraq na Syria na akasema: Kama kuna mtu asiyeona mkono wa nyuma ya pazia wa adui katika matukio hayo basi anajihadaa yeye mwenyewe.

Akitilia mkazo zaidi ukweli huo, Ayatullah Khamenei ameashiria furaha ya Marekani na Wazayuni kutokana na hali ya sasa ya Mashariki ya Kati na akasema: Wazayuni na nchi nyingi za Magharibi hususan Marekani zinafurahishwa na hali hii na hazina azma ya kumaliza suala la Daesh.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mifano kadhaa ya ukatili na unyama usio na kifani wa kundi la Daesh na nia ya mwanzoni ya kundi hilo ya kutaka kudhibiti mji wa Baghdad na kuhoji kwamba, ni kina nani wanaolisaidia kundi hilo kwa mali na silaha?

Ameongeza kuwa, ni wazi kwamba wageni hawataki suala hilo litatuliwe na kwa msingi huo nchi za Kiislamu zinawajibika kuchukua uamuzi wa kutatua tatizo hilo lakini inasikitisha kuona kwamba, hakuchukuliwi uamuzi unaofaa wa pamoja.

Ayatullah Khamenei amesema kadhia ya Yemen ni mfano mwingine wa matatizo mapya ya ulimwengu wa Kiislamu na kuhusu njia ya utatuzi wa tatizo hilo amesema: Msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu nchi zote ikiwamo Yemen unapinga uingiliaji wa kigeni katika mambo ya ndani ya nchi nyingine; kwa msingi huo kwa mtazamo wa Tehran, njia ya utatuzi wa mgogoro wa Yemen ni kusitishwa mashambulizi na uingiliaji wa kigeni dhidi ya taifa hilo, na ni Wayemeni pekee ndio wanaopaswa kuchukua maamuzi kuhusu mustakbali wa nchi yao.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema tukio adhimu la mwamko wa Umma wa Kiislamu na kiu ya mataifa mbalimbali ya kutaka kujua dini hiyo ndiyo sababu kuu ya wasiwasi wa maadui. Ameongeza kuwa: Mkabala wa mwamko huo, maadui wa Uislamu walianza mashambulizi yao muda mrefu uliopita na ukweli wa kusikitisha ni kuwa, baadhi ya tawala za Waislamu zinafanya usaliti na kutoa fedha na suhula zao kwa adui.

Baada ya hapo Ayatullah Khamenei amezungumzia hali ya Iraq na misaada ya Jamhuri ya Kiislamu kwa taifa hilo kwa ajili ya kuzuia magaidi wasidhibiti nchi hiyo na akasema: Iran haina majeshi nchini Iraq lakini kuna uhusiano wa kihistoria, wa kina na wa karibu sana baina ya mataifa ya Iran na Iraq.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuombea dua ya kupata nguvu na heshima Umma wa Kiislamu na akasema: Iran iko tayari kubadilishana maoni na fikra kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya Mashariki ya Kati.

Kwa upande wake Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na mwenyeji wake, Rais Hassan Rouhani, kwamba katika safari yake ya sasa hapa nchini viongozi wa nchi hizi mbili wamechunguza masuala ya pande mbili na kuzungumzia uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na masuala ya eneo hili.

Ameashiria uhusiano wa Tehran na Ankara katika sekta ya nishati na akasema: Kumeundwa Baraza la Ushirikiano wa Kiuchumi la Iran na Uturuki, na mawaziri wa pande mbili wametakiwa kufuatilia suala hilo na kutimiza matarajio yaliyopo kama kupanua kiwango cha biashara ya pande mbili hadi dola bilioni 30 kwa mwaka.

Rais wa Uturuki amesisitiza udharura wa kutatuliwa matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu bila ya uingiliaji kati wa nchi za Magharibi na akaongea kuwa, kuna matatizo mengi katika eneo hili ambayo yanapaswa kutatuliwa kwa kusaidiana. Amesisitzia kuwa hakuna haja ya kusubiri Wamagharibi kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo.

Rais Erdogan amelaani jinai zinazofanywa na kundi la Daesh na kusisitiza kuwa yeye hawatambui wapiganaji wa kundi la Daesh kuwa ni Waislamu na kwamba amechukua misimamo dhidi ya kundi hilo.   

 

         

700 /