Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Jinai za Saudia nchini Yemen zinashabihiana na jinai za Wazayuni huko Gaza

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amehutubia mjumuiko mkubwa wa wanawake, washairi na wasomaji wa tungo za Ahlulbaiti wa Mtume (saw) na sambamba na kuwapongeza Waislamu kwa mnasaba wa kuadhimisha siku aliyozaliwa Bibi Fatimatu Zahra (as), amezungumzia masuala muhimu sana kuhusu mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kundi ya 5+1 na vilevile matukio ya Yemen. Amesema jinai zinazofanywa na Saudi Arabia huko Yemen zinashabihiana na zile zinazofanywa na Wazayuni katika Ukanda wa Gaza huko Palestina na kutaka jinai hizo zikomeshwe mara moja. Kuhusu mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1, amesema kuwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Iran vinapaswa kufutwa kikamilifu siku hiyo hiyo ya kufikiwa makubaliano.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza hotuba yake kwa kusema: “Baadhi wanauliza kuwa, kwa nini Kiongozi Muadhamu hajaeleza msimamo wake kuhusu mazungumzo ya hivi karibuni ya nyuklia?”

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, sababu ya kutochukua msimamo ni kuwa hakuna kitu ambacho inabidi uchukuliwe kukihusu kwa sababu maafisa wa serikali na wale wa faili la nyuklia wanasema kuwa hadi sasa hakujafanyika chochote na hakuna maudhui inayoziwajibisha na kuzipa majukumu pande mbili.

Amesema iwapo nitaulizwa: Unaunga mkono mazungumzo ya hivi karibuni ya nyuklia au unapinga”, nitasema siafiki na wala siyapingi, kwa sababu hadi sasa hakujatokea chochote.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, tatizo limo katika mazungumzo kuhusu vifungu na vipengee vyote vya ndani, kwa sababu upande wa pili ni kaidi, unakiuka ahadi zake na unasaliti na yumkini katika kipindi cha kujadili masuala yote ya ndani na madogo madogo wakaizingira nchi, taifa na timu ya mazungumzo.

Amesema kilichofanyika hadi sasa si asili ya makubaliano, si mazungumzo yanayoishia kwenye makubaliano, hakidhamini matini ya makubaliano na wala hakidhamini kwamba mazungumzo haya yataishia kwenye makubaliano; kwa msingi huo hakuna maana ya kutoa pongezi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kwa kukumbusha masuala kadhaa na kusema: Sijawahi kuwa na matumaini kuhusu kufanya mazungumzo na Marekani na suala hili halitokani na dhana zisizo na mashiko bali ni kutokana na uzoefu na tajiriba iliyopo katika uwanja huo.

Ayatullah Khamenei amesema iwapo katika mustakbali mambo yote, matukio na kumbukumbu za yaliyojadiliwa katika mazungumzo ya nyuklia zitachapishwa, watu wote wataelewa kwamba uzoefu wetu unatokana na kitu gani.

Ameongeza kuwa: Licha ya kwamba sijawahi kuwa na matumaini kuhusu suala la kufanya mazungumzo na Marekani, lakini ninaunga mkono kikamilifu mazungumzo yanayofanyika baadhi ya nyakati kama haya ya sasa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa anaunga mkono mia kwa mia makubaliano yanayolinda izza na heshima ya taifa la Iran, na kwamba kama kuna mtu anayedai kwamba kiongozi anapinga suala la kufikiwa makubaliano, basi huyo hatakuwa amesema ukweli.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, anaafiki kikamilifu makubaliano yanayodhamini maslahi ya taifa na nchi na kuongeza kuwa: Hata hivyo nimesema pia kuwa “Kutofikia makubaliano ni bora kuliko kufikia makubaliano mabaya”, kwa sababu kutokubali makubaliano ambayo yatakanyaga maslahi ya taifa la Iran na kuharibu heshima na izza ya taifa ni sharafu na hadhi, kuliko makubaliano yatakayolidunisha taifa la Iran.

Baada ya hapo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu tuhuma kwa kusema: “Wakati mwingine inasemwa kuwa mzungumzo kuhusu masuala ya ndani na madogo madogo yanafanyika kwa mujibu wa mtazamo wangu ilhali maneno hayo si sawa. Ayatullah Khamenei amesema ninawajibika kufuatilia ipasavyo mazungumzo lakini hadi sasa sijawahi kuingilia mazungumzo ya masuala madogomadogo na ya ndani na sitaingilia masuala hayo.

Amesema: Kimsingi ninamweleza Rais wa Jamhuri na katika baadhi ya mambo machache, Waziri wa Mambo ya Nje masuala makubwa, misingi na sera kuu, na mistari myekundu lakini masuala madogomadogo na ya ndani yako mikononi mwao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Nina imani kwa timu ya mazungumzo ya nyuklia na hadi sasa sina shaka na timu hiyo na Inshaallah hali itaendelea kuwa hivyo katika siku za usoni, lakini nina dukuduku kubwa kuhusu mazungumzo ya nyuklia.

Ayatullah Khamenei amesema sababu ya dukuduku hiyo ni tabia ya hadaa, kuvunja ahadi na harakati kinyume na njia sahihi ya upande wa pili na kuongeza kuwa, mfano wa mienendo hiyo ya upande wa pili umeonekana wazi, na yapata masaa mawili na nusu tu baada ya kumalizika mazungumzo, ikulu ya Marekani White House ilitoa taarifa yenye kurasa kadhaa kuhusu mazungumzo hayo na aghlabu ya vipengee vya taarifa hiyo ni kinyume na ukweli.

Amesema haiwezekani kutayarisha taarifa kama hiyo katika kipindi cha masaa mawili tu; kwa msingi huo waliandika taarifa hiyo yenye dosari, makosa na kinyume na yaliyozungumzwa wakati walipokuwa katika mazungumzo na sisi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, upande unaokabiliana na sisi unakiuka ahadi na kufanya hadaa na kuongeza kuwa, mfano mwingine ni kuwa baada ya kila duru ya mazungumzo, wao hutoa matamshi ya wazi na katika vikao makhsusi wanasema kuwa matamshi hayo yametolewa kwa ajili ya ndani ya nchi zao na kwa ajili ya kukabiliana na wapinzani, suala ambalo halina mfungamano wowote na sisi.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, wao na kwa mujibu wa methali isemayo: “Kafiri hudhania watu wote kuwa ni makafiri kama yeye”, wanasema kuwa iwapo Kiongozi wa Iran atapinga mazungumzo huo hautakuwa msimamo halisi wa Iran bali upinzani huo ni kwa ajili ya kuwaridhisha watu ndani ya nchi,; ilhani wao yaani upende wa pili, hauelewi hali halisi na ukweli wa mambo ndani ya Iran.

Amesema kuwa: Maneno yanayotolewa na Kiongozi Mkuu kwa wananchi ni kwa mujibu wa imani ya pande mbili na kama ambavyo wananchi wananiamini, mimi pia nina imani kamili kwa wananchi na ninaamini kuwa, mkono wa Mwenyezi Mungu daima uko pamoja na wananchi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mahudhurio makubwa ya wananchi katika baridi kali ya tarehe 22 Bahman (11 Februari katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu) na maandamano ya joto kali la mwezi Ramadhani katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds, yote ni kielelezo cha mkono wa Mwenyezi Mungu, na kwa msingi huo tuna imani kamili kwa wananchi, na matamshi yetu pamoja nao yanatolewa kwa msingi wa hisia hizi za ukweli na maarifa ya wananchi.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa ana dukuduku kuhusu mwenendo wa upande wa pili katika mazungumzo ya nyuklia.

Ameashiria uungaji mkono na upinzani uliopo hapa nchini dhidi ya mazungumzo hayo na kusema hakupaswi kutia chumvi na kuchukua msimamo wa haraka, lazima kuwa subira na kuona nini kitatukia.

Wakati huo huo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka maafisa wa serikali kuwaeleza wananchi hususan wasomi kuhusu masuala ya ndani ya mazungumzo hayo na kuwaeleza ukweli wa mambo, kwani hakuna kitu kinachofanyika kwa siri.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa kuwaeleza wananchi na wasomi mambo yote yanayohusiana na mazungumzo ya nyuklia ni kielelezo cha mshikamano wa viongozi wa serikali na wananchi na kusisitiza kuwa, mshikamano si kanuni bali ni suala la kutengeneza, na hali ya sasa ni fursa nzuri kwa ajili ya kujenga mashikamano na wananchi.

Ametoa pendekezo kwa viongozi wa serikali akisema: Maafisa wa serikali mbao ni watu wakweli na wanaofuatilia maslahi ya taifa wanapaswa kuwaalika wakosoaji wakubwa wa mazungumzo ya nyuklia na kuzungumza nao; iwapo kutakuwapo jambo muhimu katika maneno yao basi walitumie kwa ajili ya kudumisha vyema mazungumzo, la sivyo wawakinaishe.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hicho ni kielelezo cha mshikamano na kuzikutanisha pamoja nyoyo na matendo.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, yumkini maafisa wa serikali wakasema kuwa muda wa miezi mitatu (ulioainishwa ) kwa ajili ya kufikia makubaliano hautoshi kwa ajili ya kujadili na kusikiliza maneno ya wakosoaji; jibu la maneno hayo ni kuwa fursa ya miezi mitatu si maudhui ambayo haiwezi kubadilishwa, na hakuna tatizo lolote katika kuongezwa muda huo kama ambavyo upande wa pili katika kipindi fulani cha mazungumzo ya nyuklia ulichelewesha mazungumzo hayo kwa kipindi cha miezi saba.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kwa kusisitiza tena kwamba, mazungumzo ya Iran na Marekani yanahusu tu maudhui ya nyuklia na si maudhui nyingine yoyote. Amesema mazungumzo haya ya nyuklia ni tajiriba na uzoefu; iwapo upande wa pili utaacha kupindisha mambo kama kawaida yake, tajiriba na uzoefu huo utaendelezwa katika masuala mengine, lakini kama utadumisha mwenendo huo wa kuyumbisha mambo basi jambo hilo litaimarisha zaidi tajiriba ya awali ya Iran na kutokuwa na imani na Marekani.

Ayatullah Khamenei amekosoa baadhi ya misimamo inayotambua upande wa pili unaokabiliana na Iran kuwa ni jamii ya kimataifa na kusema: Upande unaokabiliana na Iran na kukiuka ahadi ni Marekani na nchi tatu za Ulaya na si jamii ya kimataifa. “Jamii ya kimataifa ni nchi 150 ambazo marais na wawakilishi wao wa ngazi za juu miaka kadhaa iliyopita walishiriki katika mkutano wa Tehran wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote”. Ameongeza kuwa si sahihi kusema kuwa upande unaokabiliana na Iran ni jamii ya kimataifa ambayo inapaswa kuwa na imani na sisi.

Kiongozi Muadhamu ameashiria masuala ambayo, katika vikao makhsusi, aliwataka viongozi wa serikali kuyafanyia kazi katika maudhui hii ya nyuklia na akasema: Ninasisitiza kuwa maafisa wa serikali wanapaswa kutambua kuwa matunda ya sasa ya nyuklia hapa nchini yana umuhimu mkubwa sana.

Ayatullah Khamenei amesema viwanda vya nyuklia ni jambo muhimu na la dharura kwa nchi hii na kuongeza kuwa, ni hadaa kuona baadhi ya wanaojiita wanafikra akisema: Mnataka viwanda vya nyuklia kwa kitu gani?

 

Ameashiria haja ya Iran kwa viwanda vya kisasa vya nyuklia kwa ajili ya kuzalisha nishati, dawa, kusafisha maji ya bahari na kilimo na akasema: Sifa muhimu zaidi ya viwanda vya nyuklia hapa nchini ni kuwa kupatikana kwa mafanikio hayo muhimu sana ni matokeo ya mlipuko wa vipawa vya ndani vya vijana wa Kiirani; kwa msingi huo maendeleo ya sekta hii yanapaswa kudumishwa. 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia madai yanayotolewa na nchi kadhaa zinazotenda jinai kama Marekani iliyotumia bomu la nyuklia dhidi ya binadamu na Ufaransa ambayo imefanya majaribio hatari ya silaha za nyuklia na kusema, nchi hizo zinaituhumu Iran kuwa inafanya jitihada za kutengeneza bomu la nyuklia ilhali Jamhuri ya Kiislamu na kwa mujibu wa fatuwa ya kidini na msingi wa akili na mantiki haijawahi kufanya jitihada za kutengeneza silaha hizo na wala haitafanya, na inatambua silaha hizo kuwa zinasababisha matatizo.

Ayatullah Khamenei ametaja matakwa yake mengine kwa viongozi wa serikali kuwa ni kutouamini upande unaokabiliana na Iran. Ameongeza kuwa, hivi karibuni kiongozi mmoja hapa nchini alisema waziwazi kwamba Iran haina imani na upande wa pili; huu ndio msimamo mzuri.

Amesema kuwa hatupaswi kuhadaika kwa tamasamu za upande wa pili wala kuamini ahadi zake na kwamba mfano wa wazi wa suala hilo ni misimamo na matamshi ya Rais Barack Obama wa Marekani baada ya kutolewa taarifa ya hivi karibuni.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema miongoni mwa yanayotakiwa kufanywa na viongozi wa serikali ni kusisitiza suala la kufutwa mara moja vikwazo vyote ilivyowekewa Iran na kuongeza kuwa, suala hili lina umuhimu mkubwa na vikwazo hivyo lazima viondolewe kikamilifu siku ileile ya kufikiwa makubaliano. Ayatullah Khamenei amesema iwapo vikwazo hivyo vitaondolewa kwa awamu, mazungumzo ya nyuklia hayatakuwa na maana kwa sababu lengo la mazungumzo ni kuondolewa vikwazo.

Baada ya hapo Ayatullah Khamenei amezungumzia suala la ukaguzi na kusisitiza kuwa: Abadani, hatutaruhusu kupenya katika sekta ya usalama na ulinzi wa Iran kwa kutumia kisingizio cha usimamizi, na maafisa wa kijeshi hapa nchini hawana ruhusa kabisa kuwaruhusu wageni kuingia katika masuala ya usalama wa taifa kwa kisingizio cha usimamizi na ukaguzi au kusimamisha ustawi wa masuala ya ulinzi nchini.

Amesema kuna ulazima wa kuimarishwa zaidi uwezo wa kiulinzi wa Iran katika masuala ya kijeshi. Vilevile mazungumzo hayo hayapaswi kutia doa uungaji mkono wetu kwa ndugu zetu wanamapambano katika pembe mbalimbali za dunia.

Kuhusu njia ya kusimamia miradi ya nyuklia ya Iran, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Mbinu yoyote ya usimamizi isiyo ya kawaida inayoifanya Iran kuwa kesi makhsusi katika upande huo haikubaliki, na usimamizi unapaswa kubakia katika mipaka ya usimamizi wa kawaida unaotumika duniani kote, na sio zaidi.

 

Tahadhari nyingine iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ilikuwa ni kuhusiana na udharura wa kuendelea na ustawi wa kiufundi katika miradi ya nyuklia ya Iran. Amesisitiza kwamba: Ustawi wa kielimu na kiufundi inabidi uendelee katika upeo wake mbalimbali. Tab'an yumkini timu ya mazungumzo ya nyuklia inapaswa kuelewa pia kuwa, inabidi ikubaliane na baadhi ya mipaka, na hakuna tatizo katika suala hilo, lakini kwa hali yoyote ile, maendeleo na ustawi wa kiufundi unapaswa kuendelea na kusonga mbele kwa nguvu kubwa zaidi.

Ayatullah Khamenei amesisitiza pia kwamba: Kudhaminiwa matakwa hayo ni jukumu la wafanya mazungumzo hayo na inabidi watumie mitazamo na fikra za wataalamu waaminifu na hata mitazamo ya wakosoaji ili kupata mbinu sahihi za kuendelea na mazungumzo hayo.

Baada ya hapo Ayatullah Khamenei amegusia katika sehemu nyingine ya hotuba yake, matukio na mabadiliko muhimu ya nchini Yemen na kusisitiza kuwa: Kitendo cha Wasaudia cha kuivamia Yemen ni kosa na tayari wamepanda mbegu ya bida'a katika eneo hili.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja mashambulio ya serikali ya Saudia huko nchini Yemen hivi sasa kuwa yanashabihiana na jinai za Wazayuni huko Ghaza, Palestina na baada ya hapo ameanza kuzungumzia pande mbili muhimu za suala hilo.

Ameitaja hatua ya kulivamia na kuanza kulishambulia taifa la Yemen kuwa ni jinai, ni mauji ya kimbari na ni suala ambalo watendaji wake wanapaswa kufuatiliwa kisheria kimataifa na kuongeza kuwa: Kuwaua watoto wadogo, kuharibu nyumba za watu, kuangamiza miundombinu na utajiri wa taifa fulani, ni jinai kubwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Ni jambo lisilo na shaka hata chembe kuwa Wasaudia watapata hasara na madhara katika kitendo chao hicho na kamwezi hawatopata ushindi kwenye mashambulizi yao hayo.

Aidha Udhma Khamenei amesema kuhusu kushindwa Wasaudia katika mshambulizi yao huko Yemen kwamba: Dalili za kushindwa huko ziko wazi, kwani nguvu za kijeshi za Wazayuni ni kubwa zaidi ikilinganishwa na za Wasaudia, na eneo la Ghaza nalo ni eneo dogo tu ikilinganishwa na nchi kubwa na pana ya Yemen, lakini pamoja na hayo, Wazayuni wameshindwa kuidhibiti Ghaza, wakati ambapo Yemen ni nchi kubwa na pana, yenye makumi ya mamilioni ya watu (Vipi Wasaudia na uwezo huo walio nao wataweza kuidhibiti nchi kama hiyo?)

Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba: Ni jambo lisilo na shaka hata chembe kuwa Wasaudia watapa pigo kwenye mashambulizi yao hayo na "pua zao zitarambishwa mchanga" huko Yemen.

Aidha ameashiria historia ya Wasaudia katika masuala yanayohusiana na siasa za nje na kusema: Sisi tuna hitilafu za mitazamo katika masuala mbali mbali ya kisiasa na Wasaudia, lakini pamoja na hayo mara zote tulikuwa tukisema kuwa, Wasaudia ni makini na wanafanya mambo kwa hekima katika siasa zao za nje. Hata hivyo hivi sasa vijana wachache wasio na uzoefu wamehodhi masuala ya nchi hiyo na hivi sasa wanaufanya upande wa ukatili uuzidi nguvu upande wa umakini na ule wa kujidhihirisha kwa sura nzuri Saudia huko nyuma, na kwamba jambo hilo bila ya shaka yoyote ni kwa madhara ya nchi hiyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakhutubu viongozi wa serikali ya Saudi Arabia akiwaambia: Harakati yenu hii haikubaliki katika eneo hili na ninakutahadharisheni kuwa, mnapaswa kuacha mara moja kutenda jinai huko Yemen.

Baada ya hapo, Ayatullah Khamenei amegusia namna Marekani inavyoilinda na kuiunga mkono serikali ya Saudi Arabia na kuongeza kuwa: Hii ndiyo tabia ya Marekani, siku zote haiko pamoja na watu wanaodhulumiwa. Badala ya kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa, siku zote Marekani inamuunga mkono dhalimu. Lakini Wamarekani nao watapata pigo katika jambo hili na siasa zao zitafeli tu.

Vilevile ameashiria madai ya eti Iran kuingilia mgogoro wa Yemen na kusema: Ndege zao zinazotenda jinai zimeondoa usalama na amani kabisa katika anga ya Yemen na baadaye wanaeneza propaganda na kutoa madai ya kipumbavu ambayo Mwenyezi Mungu hakubaliano nayo, wala mataifa ya dunia na wala sheria za kimataifa. Wanafanya jinai zote hizo huko Yemen na hapo hapo wanadai kuwa huko si kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo na badala yake wanaituhumu Iran kwa mambo yasiyo sahihi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, taifa la Yemen ni taifa lenye historia kongwe, na lina uwezo wa kutosha wa kujiainisha lenyewe utawala linaoutaka na kwa mara nyingine akasisitiza kuwa: Serikali ya Saudia inapaswa kuachana mara moja na jinai zake zinazosababisha maafa makubwa huko Yemen.

Ayatullah Khamenei pia amesema kuwa, hatua ya awali iliyokusudiwa na madola yanayolitakia mabaya taifa na wananchi wa Yemen ilikuwa ni kuifanya nchi hiyo isiwe na serikali yenye nguvu sawa sawa kabisa na walivyofanya huko Libya kwa kuitumbukiza nchi hiyo kwenye hali mbaya na ya kusikitisha mno. Aidha amesema: Kwa bahati nzuri hatua hiyo ya kwanza ya njama hiyo ya kiadui dhidi ya Yemen imefeli, kwani vijana wenye imani thabiti, wenye uchungu na nchi yao na walioshikamana vilivyo na njia ya Amirul Muminin (Imam Ali as) , iwe ni Waislamu wa Kishia au wa Kisuni, wa Kizaidi au wa Kihanafi, wote wamesimama kidete kupambana na njama hiyo na katika siku za usoni pia vijana hao watafelisha njama zote za maadui wa Yemen.

Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei ametumia fursa hiyo kumkumbuka kwa wema, marhum Aahi, msoma kasida na mashairi ya Ahlulbait AS aliyekuwa ameshikamana vyema na mafundisho ya watukufu hao, aliyekuwa na msimamo usiotetereka, mpigania kheri na aliyefanya jitihada zisizochoka katika nyuga mbali mbali bila ya kuchoka na hapo hapo akawakumbusha wasoma kasida na mashairi ya Bwana Mtume SAW na Ahlulbait AS mambo kadhaa muhimu.

Kujua thamani ya kujitokeza kwa wingi mno vijana katika "majalis" za kuwakumbuka na kuwaenzi Ahlulbait Alayhimus AS na wajibu wa kueneza mafundisho ya kidini na mtindo wa maisha ya Kiislamu na kuwaelekeza walengwa kwenye kutekeleza ipasavyo majukumu yao ya kidini ilikuwa ni nukta ya kwanza kabisa iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiwakumbusha wajibu wao wasoma kasida za Ahlulbait AS.

Kujiepushe na mambo yasiyo sahihi na yaliyopotoshwa na kutilia nguvu imani sahihi ndani ya nyoyo za vijana ni jukumu jingine ambalo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakumbusha wasoma kasida za Ahlulbait AS.

     

700 /