Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Amiri Jeshi Mkuu wa Iran:

Iran inapaswa kuzidisha uwezo wake wa kujihami siku baada ya siku

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo ametubua hadhara ya makamanda, wafanyakazi na familia za mashahidi wa jeshi la Iran akiliamuru kulinda, na kuimarisha muono wake wa mbali na mwelekeo wa kidini na kimapinduzi, kuzidisha uwezo wa kujihami na wa kisilaha na kuwa tayari kiroho. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi na haitakuwa tishio kwa eneo hili na nchi jirani lakini itajibu uchokozi wa aina yoyote kwa nguvu zake zote.

Katika mkutano huo uliofanyika kwa mnasaba wa kuadhimisha Siku ya Jeshi na Hamasa ya Kikosi cha Jeshi la Nchi Kavu hapa nchini, Amir Jeshi Mkuu amelipongeza jeshi hilo na kusema kuwa, uamuzi wa kuipa siku ya tarehe 29 Farvardin (Aprili 18) jina la Siku ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ni miongoni mwa ubunifu wa hayati Imam Khomeini katika kipindi cha mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mkabala wa njama za baadhi ya makundi za kutaka kuliangamiza jeshi hilo. Ameongeza kuwa: Jeshi hili limebakia hai kwa nguvu zote kutokana na umakini na kuwa macho kwa Imam Khomeini na limekuwa na mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na katika vita vya miaka 8 ya kujihami kutakatifu na kuiletea nchi fahari na hamasa kubwa.

Kiongozi wa Mapinduzi wa Kiislamu amesema kuwa tarehe 29 Farvardin ina maana ya kusimama wima jeshi kwa kutumia miguu ya Mapinduzi ya Kiislamu na katika njia ya kuhudumia malengo ya wananchi. Ameongeza kuwa, miongoni mwa sifa za Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ni kushikamana kwake na kanuni na mafundisho ya dini.

Ayatullah Khamenei ameashiria kuwa majeshi mengi duniani huwa hayaheshimu kanuni za kimataifa na kanuni za kibinadamu wakati yanapopata ushindi au kushindwa na akasema: Mfano wa wazi kabisa wa ukweli huo ni mwenendo wa madola makubwa hususan Marekani ambayo haiheshimu wala kujali kanuni za kimataifa na vigezo vya kibinadamu na inafanya jinai za kila aina.

Ametayaja matukio ya Yemen, vita vya Gaza na vita vya Lebanon kuwa ni mifano ya kutofungamana na kuheshimu sheria za kimataifa na kusema: Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu daima linafungamana na kuheshimu kanuni na sheria za kimataifa na kamwe halichupi mipaka wakati wa ushindi wala halitumii nyenzo na mbinu zilizopigwa marufuku wakati wa hatari.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Sisitizo la Jamhuri ya Kiislamu kwamba haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia ni katika fremu hii na kwa mujibu wa kushikamana kwake na mafundisho ya dini.

Ayatullah Khamenei ameashiria propaganda na tuhuma zinazosema kuwa Iran inaingilia masuala ya nchi za eneo hili na kusema: Tuhuma hizo ni kinyume na ukweli, kwa sababu Iran haiingilii masuala ya nchi nyingine na wala haitafanya hivyo.

Amesema: Tunawachukia mno wale wanaowashambulia raia, wanawake na watoto na tunaamini kwamba, watu hao hawaujui kabisa Uislamu na ubinadamu; pamoja na hayo hatuingilii masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, sifa ya kushikamana na misingi ya Uislamu na sheria za Mwenyezi Mungu ndiyo sababu kuu ya kupendwa jeshi la Iran baina ya wananchi. Ameongeza kuwa sifa nyingine ya jeshi hilo ni kuinua na kuzidisha uwezo na utayarifu wake wa kujilinda na wa zana na silaha zake, suala ambalo linafanyika kutokana na ilhamu ya aya ya Qur’ani Tukufu inayosema: “Na waandalieni nguvu kadiri muwezavyo..”.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, mafanikio na maendeleo ya kijeshi na ya kujihami ya jeshi la Iran pamoja na maendeleo makubwa ya kielimu na kiteknolojia hapa nchini ni ya aina yake na ni miongoni mwa mafanikio makubwa zaidi. Ameongeza kuwa, maendeleo na uwezo huo umepatikana wakati Iran ikiwa chini ya mashinikizo na vikwazo visivyo na kifani na ikikabiliwa na uhaba wa vyanzo, jambo ambalo ni mafanikio makubwa sana na lazima yaendelezwe kwa kasi kubwa.

Amesema wanaolitakia mabaya taifa la Iran wanachukizwa na maendeleo ya kiulinzi ya jeshi la Iran na wanafanya jitihada za kusimamisha maendeleo hayo na akaongeza kuwa, kwa msingi huo wameelekeza mashinikizo yao yote ya kipropaganda katika maudhui hii hususan katika maendeleo ya Iran katika utengenezaji wa makombora na ndege zisizo na rubani; lakini mantiki sahihi inayotegemea aya ya Qur’ani inatwambia kwamba mwenendo huu unapaswa kudumishwa kwa nguvu zote.

 Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria vitisho viovu vya Marekani na kusema: “Baada ya kukaa kimya kwa muda sasa, afisa wao mmoja hivi karibuni alizungumzia tena chaguo zilizoko mezani. Kwa upande mmoja Wamarekani wanajigamba hivyo na katika upande mwingine wanasema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kusimamisha maendeleo yake katika sekta ya ulinzi; maneno ambayo ni ya kipumbavu.”  

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitakubali maneno haya ya kipumbavu na taifa la Iran limethibitisha kuwa iwapo litashambuliwa litajihami kwa nguvu zote na kusimama kidete kama ngumi madhubuti mbele ya mvamizi na mchokozi asiye na mantiki.

Amir Jeshi Mkuu ameliambia jeshi kwamba: Taasisi zote kuanzia Wizara ya Ulinzi, Jeshi la Taifa hadi Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) zinapaswa kuzidisha uwezo na utayarifu wao wa kijeshi, wa kujihami, uratibu wa masuala ya vita siku baada ya siku, na kuwa tayari kiroho, na hii ni amri rasmi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa moyo wa vikosi vya jeshi hapa nchini uko juu sana na kuongeza kuwa, licha ya kupata maendeleo makubwa katika masuala ya kiulinzi na kijeshi, Jamhuri ya Kiislamu haitakuwa tishio kwa nchi za eneo hili na majirani zake.

Ameashiria pia ngano zilizobuniwa na Wamarekani, watu wa Ulaya na nchi vibaraka wao kuhusu eti juhudi za Iran za kutaka kutengeneza silaha za nyuklia na kuidhihirisha Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni tishio na akasema: Tishio kubwa zaidi la dunia na Mashariki ya Kati ni Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao wanavamia na kuingilia mambo ya kila eneo na kufanya mauaji bila ya kufungamana au kujali sheria yoyote, kanuni za kibinadamu au za kidini.

Ameyataja matukio ya Yemen na himaya ya Marekani na nchi za Magharibi kwa mvamizi kuwa ni mfano wa mwenendo unaohatarisha amani ya dunia na akasema: Tofauti na madola yasiyo na mipaka, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitambua amani kuwa ni neema kubwa zaidi ya Mwenyezi Mungu na inasimama kidete na kulinda amani na usalama wake na wa nchi nyingine.

Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa wadhifa muhimu zaidi wa maafisa wa jeshi la polisi ni kulinda amani ya nchi, mipaka na maisha ya wananchi.  

Kabla ya hotuba ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Meja Jenerali Salehi ambaye ni Kamanda Mkuu Majeshi ametoa hutuba fupi kuhusu maadhimisho ya Siku ya Jeshi na kusema: Jeshi la kimapinduzi na la kihizbullahi la Jamhuri ya Kiislamu liko tayari kikamilifu kwa ajili ya kulinda mipaka ya Iran na kulinda maslahi ya kistratijia ya nchi hii.

Meja Jenerali Salehi amesema kuwa jeshi la Iran halitambui chaguo lolote ghairi ya izza na heshima na liko tayari kutengeneza hamasi nyingine ya kudumu katika hali yoyote ile.

700 /