Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Iran inatambua usalama na maendeleo ya Afghanistan kuwa ni usalama na maendeleo yake

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khameni alasiri ya leo amemkaribisha Rais wa Afghanistan ofisini kwake. Ayatullah Khamenei ameashiria uhusiano na mambo mengi ya kiutamaduni na kihistoria yanayozikutanisha pamoja nchi hizo mbili na kusema, mchango wa maulama na wana fasihi wa Afghanistan katika kustawisha na kueneza maarifa ya Kiislamu na lugha ya Kifarsi ni mkubwa na muhimu. Ameongeza kuwa mbali na nguvu kazi na utajiri wa kiutamaduni, Afghanistan ina utajiri wa maliasi na vyote hivyo  vinapaswa kutumiwa kwa ajili ya kustawisha zaidi kiwango cha ushikiano wa nchi hizi mbili.

Ayatullah Khamenei ametilia mkazo udharura wa kuwepo irada imara na azma thabiti ya kuimarishwa ushirikiano na mshikamano kati ya Iran na Afghanistan na akasema: Wamarekani na baadhi ya nchi za eneo hili hazitambui uwezo wa Afghanistan na haziafiki mshikamano na ushirikiano wa nchi mbili, lakini Iran inatambua usalama na maendeleo ya jirani yake, Afghanistan, kuwa ni usalama na maendeleo yake.

Amekumbusha maendeleo makubwa ya Iran katika nyanja mbalimbali za kielimu, kiteknolojia, kiutamaduni na kidiplomasia kama uwanja mzuri wa ushirikiano wa nchi mbili na akasema, masuala yaliyoko baina ya nchi hizi mbili kama suala la wahajiri, maji, usafirishaji na usalama pia yanaweza kutatuliwa, na masuala yote hayo yanapaswa kufuatiliwa kwa nguvu zaidi na kisha kuchunguzwa na kutatuliwa kwa mujibu wa jedwali na kipindi maalumu.

Kuhusu suala muhimu la wahajiri, Ayatullah Khamenei ameashiria mamia ya wahajiri wa Kiafghani wanaopata elimu hapa nchini Iran katika ngazi mbalimbali na akasema: Wananchi wa Afghanistan ni watu wenye vipawa na hodari na vipawa hivyo vinapaswa kutumiwa vyema katika kutafuta elimu kwa sababu wasomi wa Kiafghani wanahitajika sana kwa ajili ya kuijenga upya nchi yenu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Tehran ni nyumba ya ndugu zetu Waafghani. Ameashiria pia uhusiano na urafiki wa kudumu na wa siku nyingi wa Iran na nchi hiyo jirani na akaeleza matumaini ya kuongezeka mafanikio na uwezo wa ndani wa nchi hiyo siku baada ya siku.

Katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Rais Hassan Rouhani, Rais Muhammad Ashraf Ghani wa Afghanistan ameeleza kufurahishwa na safari yake mjini Tehran na kuzungumzia mifungamano mikubwa ya kihistoria na kiutamaduni iliyopo baina ya Iran na Afghanistan. Amesema lengo lao ni kuifanya Afghanistan kuwa kituo kikuu cha mawasiliano na usafirishaji katika eneo hili na kupata nafasi yake ya awali kama njiapanda ya mawasiliano katika eneo hili.

Rais wa Afghanistan amesema, kwa sasa nchi mbili zinakabiliana na hatari zinazoshabihiana na fursa za pamoja na kuongeza kuwa, Kabul ina irada ya kustawisha zaidi uhusiano wa pande mbili na kwamba juhudi zaidi zinapaswa kufanyika kwa ajili ya kuimarisha masuala ya pamoja.

Rais Ashraf Ghani amesema, lengo la siasa za serikali ya Afghanistan ni kubadili migongano na mapigano ya ndani na kuyafanya medani ya ushirikiano. Kuhusu uhusiano wa pande mbili, ameashiria baadhi ya matatizo yaliyopo kama suala la ugaidi, dawa za kulevya, wahajiri na maji yaliyopo kwenye mpaka wa nchi hizi mbili na akasema: Masuala yaliyopo baina ya nchi mbili hizi yatatatuliwa kwa idara ya kisiasa ya pande mbili na kwa mujibu wa jedwali lanye wakati maalumu lililotayarishwa katika safari hii.

Rais wa Afghanistan amesema, katika suala la magendo ya dawa za kulevya, Iran ndiyo iliyopata madhara zaidi. Ameongeza kuwa, hakuna nchi yoyote jirani iliyolipa umuhimu mkubwa suala la hatari ya dawa za kulevya kama ilivyofanya Iran na vilevile hakuna nchi inayopambana na dawa hizo kama Iran. Amesisitiza kuwa Afghanistan iko tayari kupambana na balaa hilo linaloangamiza watu kwa ushirikiano wa Iran.

Rais wa Afghanistan ameashiria juhudi za kustawishwa uhusiano wa nchi mbili katika nyanja za usafirishaji, uwekezaji na ushirikiano wa kiutamaduni na kiuchumi na akamwambia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba: Chini ya uongozi wako wa busara, Iran imethibitisha utambulisho wake wa kihistoria na nina matarajio kwamba kutokana na uongozi wako wa busara kutashuhudiwa maendeleo katika ushirikiano wa nchi mbili.      

700 /