Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Nguvu inayotakikana katika Uislamu inapaswa kuambatana na uadilifu na urehemevu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo (Jumapili) amehutubia hadhara ya washiriki katika kongamano la makamanda, wakurugenzi na viongozi wa vitendo vya itikadi na siasa wa Jeshi la Polisi na kusema kuwa, jeshi hilo ni dhihirisho la kujitawala na usalama wa Jamhuri ya Kiislamu. Amesisitiza kuwa jukumu kubwa zaidi la Jeshi la Polisi ni kuleta amani ya mtu binafsi, ya jamii, ya kimaadili na ya kinafsi katika jamii. Ameongeza kuwa sharti la kuweza kuleta amani ni kuwa na nguvu Jeshi la Polsi lakini nguvu hiyo inapaswa kuandamana na uadilifu, murua na urehemevu. 

Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewapongeza hadhirina kwa kuingia mwezi wa Shaaban na kusema: Mwezi huu ni fursa yenye thamani kubwa kwa ajili ya kujikurubisha kwenye thamani za Mwenyezi Mungu na kutakasa nafsi, na ni utangulizi wa kufika kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani. Vilevile amewausia wananchi wote kufaidika zaidi na baraka za miezi hiyo.

Ayatullah Khamenei amesema: Umuhimu wa kuleta na kudumisha usalama- kama jukumu kuu la Jeshi la Polisi- unaonesha umuhimu wa asasi hiyo. Ameongeza kuwa, suala la kuleta amani si propaganda na maneno matupu bali kuwepo kwa amani kunapaswa kuhisiwa na wananchi.

Akibainisha kuwa Jeshi la Polisi halipaswi kutosheka na kiwango chochote katika sehemu mbalimbali za kuimarisha amani na usalama kama usalama wa barabarani, usalama wa miji, mipaka na vituo mbalimbali, amesema kuwa kudhamini usalama wa kinafsi na kifikra wa jamii ni miongoni mwa vipengee na masuala yenye umuhimu mkubwa. Ameongeza kuwa: Kukabiliana na hali ya ukosefu wa usalama wa kifikra na kinafsi katika jamii kama wasiwasi wa familia kuhusu usalama wa watoto wao wanapokuwa mitaani na katika mabustani kutokana na uwezekano wa kuvutwa watoto hao upande wa dawa za kulevya, au wasiwasi wa kutumbukia vijana katika ufuska na mambo maovu, kuna umuhimu mkubwa zaidi kuliko kukabiliana na usalama wa kimwili, na kuna ulazima wa kukabiliana kwa nguvu zote na ukosefu kama huo wa usalama na amani.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuzungukazunguka mitaani baadhi ya vijana walioleweshwa na ghururi ya utajiri wakiwa na magari ya kifahari ni miongoni mwa vielelezo vya uvunjivu wa amani ya kifikra ya kinafsi katika jamii. Ameongeza kuwa, Jeshi la Polisi linapaswa kuwa na mipango kwa ajili ya masuala yote yanayovunja amani na usalama na kukabiliana nayo.  

Ayatullah Khamenei amesema, sharti la kuweza kuleta amani katika jamii ni kufanya kazi kwa nguvu Jeshi la Polisi na kongeza kuwa: Jeshi la Polisi ni dhihirisho la kujitawala na usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa msingi huo linapaswa kuwa na nguvu lakini nguvu hiyo haina maana ya kudhulumu na harakati isiyokuwa na kidhibiti wala mipaka.

Amesema: Iran haitaki kuwa na nguvu ya polisi ya kihollywoodi na jamii za Kimagharibi na Kimarekani na kuongeza kuwa, nguvu kama hiyo si tu kwamba haileti usalama, bali pia inasababisha ukosefu wa usalama na amani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema miamala na mwenendo wa polisi ya Marekani dhidi ya watu weusi ni mfano wa nguvu ya kidhalimu. Amesema: Katika nchi ya Marekani ambayo kwa sasa Rais wake ni mtu mweusi, watu weusi (wenye asili ya Afrika) wanadhulumiwa, kupuuzwa na kudunishwa na polisi; mwenendo ambao unasababisha machafuko na ukosefu wa amani.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa nguvu inayotakikana katika mfumo wa utawala wa Kiislamu ni nguvu inayoambatana na uadilifu, murua na urehemevu; kama ambavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwingi wa rehma na Mwenye kurehemu na wakati huo huo hutoa adhabu iumizayo.

Vilevile ametilia mkazo udharura wa kuheshimiwa sheria wakati wa kuamiliana na wananchi na ndani ya asasi ya Jeshi la Polisi na akasema: Kutokana na upana na ukubwa na mawasiliano ya Jeshi la Polisi na wananchi, suala la kuwa na askari wasafi katika asasi hii lina umuhimu mkubwa sana kwa kadiri kwamba, polisi mmoja mchapakazi na mwenye msimamo imara anaweza kuwa sababu ya heshima na hadhi ya mfumo wa Kiislamu mbele ya macho ya watu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo ulazima wa kuimarishwa zaidi masuala ya kiitikadi na kimaadili na vilevile kuinua juu kiwango cha elimu na ubunifu wa kisayansi ndani ya Jeshi la Polisi na amewataka maafisa wa sekta mbalimbali kushirikiana na jeshi hilo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amelishukuru Jeshi la Polisi kwa uchapakazi wake mzuri hususan katika siku za sikukuu ya Nowruz.

Kabla ya hotuba ya Amiri Jeshi Mkuu, Brigedia Ashtari ambaye ni Kamanda wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa ripoti kuhusu shughuli na mipango ya jeshi hilo na kusema: Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo ni pamoja na ongezeko la kufichua uhalifu mkubwa, kudumishwa mapambano dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya, kuzidishwa utayarifu wa polisi kwa ajili ya kudhibiti mipaka, kupungua kwa asilimia 7 majanga yanayosababishwa na ajari za barabarani, kupanuliwa zaidi mawasiliano ya Jeshi la Polisi na wasomi, harakati ya ustawi mkubwa zaidi katika sayansi na teknolojia na kulinda thamani za Mapinduzi ya Kiislamu.

700 /