Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Ufunguo wa kutatua matatizo ya kiuchumi uko ndani ya nchi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei asubuhi ya leo (Jumatano) amekutana na maelfu ya wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ambapo ameeleza nyadhifa za maafisa wa serikali, asasi na vyombo mbalimbali vinavyojihusisha na masuala ya uzalishaji wa ndani ya nchi. Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza udharura wa kupambana ipasavyo na ubadhirifu na magendo na akasema: Ufunguo wa matatizo ya kiuchumi ya wananchi na matatizo ya jamii ya wafanyakazi uko katika kuimarishwa na kustawishwa uzalishaji wa ndani ya nchi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewapongeza Waislamu kwa mnasaba wa kukaribia maadhimisho ya maulidi na kuzaliwa kwa Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) na Imam Jawad (as) na akasema lengo la kukutana na wafanyakazi ni kuenzi kazi na wafanyakazi na kuonesha zaidi thamani ya kazi katika fikra za maafisa wa serikali na jamii. Amesisitiza kuwa hatua ya Mtume Muhammad (saw) ya kubusu mkono wa mfanyakazi haikuwa ya kimaonyesho bali ilichukuliwa ili kuielimisha na kuifunza jamii kuhusu umuhimu wa kazi na thamani ya mfanyakazi.

Ayatullah Ali Khamenei amepongeza umadhubuti, kuwa macho na ustahifu wa jamii ya wafanyakazi hapa nchini mkabala wa harakati za mara kwa mara za ndani na nje ya nchi katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita na akasema: Majmui ya wafanyakazi imepasi mtihani katika jitihada za maendeleo ya Iran ya Kiislamu licha ya kustahamili mashaka na matatizo mengi. Amesema maafisa wa serikali wanapaswa kushukuru na kuthamini kujitolea huko kwa jamii ya wafanyakazi kwa kufanya jitihada zaidi za kutatua matatizo yao.

Ayatullah Ali Khamenei ameashiria matatizo ya sekta ya wafanyakazi kama ya kufukuzwa, ukosefu wa ajira, kucheleshwa na matatizo yao ya kimaisha na akasema: Matatizo haya hayawezi kutatuliwa kwa maneno bali kwa kuchukua hatua za kivitendo na ubunifu.

Amesema kuwa kuimarishwa uzalishaji wa ndani ndiyo uti wa mgongo wa utatuzi wa matatizo ya nchi na kutimia uchumi wa kimapambano na akaongeza kuwa: Baadhi wanasema kuwa, katika mazingira ya vikwazo na mashinikizo haiyumkini kupatikana ustawi katika uzalishaji wa ndani; hapana shaka kuwa vikwazo vya kidhalimu vimechangia katika kutokea matatizo lakini pia tunapaswa kuelewa kuwa, vikwazo na mashinikizo haviwezi kuzuia juhudi za umma zilizopangiliwa vyema kwa ajili ya ustawi wa uzalishaji wa ndani.

Ili kuthibitisha udhaifu wa vikwazo na kutoweza kwake kuzuia jitihada za ndani ya nchi, Ayatullah Khamenei ameashiria maendeleo makubwa ya kushangaza ya Iran katika nyanja za viwanda vya kijeshi, bioteknolojia, ujenzi wa mabwawa, teknolojia ya nano, elimu msingi, teknolojia ya nyuklia na kadhalika na kusema: Katika baadhi ya nyanja hizo mashinikizo ya vikwazo yalikuwa makubwa zaidi lakini hayakuweza kuzuia njia ya juhudi na maendeleo ya ndani ya nchi.

Ameongeza kuwa kama vikwazo visingekuwepo kuna uwezekano kwamba tungepata maendeleo makubwa zaidi katika baadhi ya nyanja lakini pia kuna uwezekano kuwa, wakati huo tungeendelea kutegemea fedha ya mafuta na tusingepata maendeleo haya ya sasa.  

Ayatullah Khamenei amesema kuwa kuzingatiwa na kupewa umuhimu uzalishaji mbali na kutatua matatizo ya kiuchumi, kutaleta hisi ya heshima na kujitosheleza kitaifa na akaongeza kuwa, kuimarika muundo wa ndani wa nguvu ikiwa ni pamoja na nyanja za uchumi, kunaimarisha timu ya mazungumzo ya Iran katika meza ya mazungumzo, la sivyo upande unaokabiliana na Iran utakuwa ukiweka masharti na kusema maneno ya kipuuzi.

Baada ya kubainisha udharura wa kutiliwa maanani suala la kustawishwa uzalishaji wa ndani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza udharura wa kutimizwa lengo hilo kubwa la kitaifa.

Amesema ushirikiano na mshikamano wa taasisi zote zinazohusika na masuala ya uzalishaji wa ndani utatayarisha uwanja mzuri wa kuondolewa kikwazo kikubwa katika njia ya maendeleo ya nchi. Ameongeza kuwa, wawekezaji wa ndani ambao ni miongoni mwa nguzo muhimu za kuimarisha uzalishaji wa ndani, wanapaswa kutumia suhula na mitaji yao katika uwanja huu.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, uwekezaji katika sekta ya uzalishaji wa ndani unaofumbia macho faida zaidi za kidalali na masuala yasiyo ya kiuzalishaji, huwa ni ibada.

Ametaja suala la kuchapakazi sawasawa na kwa nguvu zote katika uzalishaji wa ndani kuwa ndiyo mchango wa wafanyakazi katika kuimarisha sekta ya uzalishaji na akaongeza kuwa: Watumiaji wenye insafu pia wanapaswa kujua vyema maslahi ya taifa na kuacha kutumia bidhaa zilizotengenezwa nje ya nchi na hivyo kuwasaidia wafanyakazi wenzao kwa kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema serikali ndiyo mtumiaji mkubwa zaidi wa bidhaa na amemtaka Waziri wa Kazi kutilia mkazo katika vikao vya serikali, udharura wa asasi zote za serikali kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na kuitaka serikali ipige marufuku utumiaji wa bidhaa za nje ambazo mfano wake unazalishwa hapa nchini.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, mapambano makali na ya kivitendo dhidi ya magendo ni suala jingine lenye taathira katika kuimarisha uzalishaji wa ndani ya nchi. Amesema suala la uagizaji wa baadhi ya bidhaa kutoka nje ya nchi liko mikononi mwa sekta ya binafsi lakini serikali inaweza kuzuia madhara yoyote dhidi ya sekta ya uzalishaji wa ndani kwa kusimamia na kuongoza kazi ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Amesema harakati zaidi za vyombo vya habari katika kuwahimiza wananchi watumie bidhaa zilizozalishwa ndani ya nchi na majukumu ya Bunge ya kuimarisha sheria za uwekezaji ni sababu nyingine ya kustawisha uzalishaji.

Sehemu nyingine muhimu ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imegusia suala la kupambana na ubadhirifu na ufisadi. Amekosoa maneno matupu yasiyoandamana na vitendo yanayotolewa mara kwa mara kuhusu suala la kupambana na ubadhirifu na ufisadi na akasema: Kupiga makelele ya "mwizi" "mwizi" peke yake hakuwezi kumzuia mwizi kuiba, bali lazima zichukuliwe hatua za kivitendo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, viongozi wa nchi si magazeti yanayozungumzia mara kwa mara masuala ya ufisadi, bali wanapaswa kuchukua hatua za kivitendo na kuzuia ufisadi kwa maana yake halisi.

Ayatullah Khamenei amemalizia kwa kusema: Ufumbuzi wa matatizo ya kiuchumi hauko Lausanne, Geneva wala New York bali upo hapa nchini, na wananchi wote wanapaswa kutekeleza majukumu yao ya kuimarisha na kustawisha uzalishaji wa ndani kama njia ya kutibu matatizo ya kiuchumi.

Amesema, kwa matakwa yake Mwenyezi Mungu na kwa kuchapakazi zaidi, suala la uzalishaji wa ndani litapatiwa ufumbuzi, kama viongozi wa nchi na wananchi walivyoweza kutatua matatizo makubwa zaidi katika miongo mitatu iliyopita.

Mwanzoni mwa mkutano huo Waziri wa Kazi, Muawana na Huduma za Jamii amewapongeza wananchi kwa mnasaba wa kuadhimisha maulidi ya Imam Jawad na Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) na vilevile kwa mnasaba wa Wiki ya Wafanyakazi hapa nchini na akasema: Maafisa wa jamii ya wafanyakazi hapa nchini wameazimia kufanya kila wawezalo kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wenye kipato cha chini na kulinda matunda ya utawala wa Kiislamu.

Bwana Rabei amelitaja suala la kutumia vizuri fursa ya kuwepo nguvu kazi kubwa na yenye thamani kama ambavyo amezungumzia pia namna jumuiya ndogo ndogo za uzalishaji zinavyoungwa mkono pamoja na taasisi za elimu za kimsingi kuelekea kwenye uchumi wa ndani ya nchi kikamilifu. Vile vile amebainisha ajenda kuu na misimamo ya Wizara ya Kazi, Ushirikia na Ustawi wa Kijamii katika masuala mbali mbali.

Bw. Rabei amelitaja suala la kupewa bima Wairani wote, kuongezwa bima ya watu wa vijijini na kufanywa nyongeza za mishahara ya wafanyakazi kuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na kiwango cha mfumuko wa bei kuwa ni miongoni mwa kazi muhimu zilizofanywa na serikali ya kumi na moja ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameongeza kuwa, kutiliwa nguvu misingi ya uadilifu wa kijamii na kuondolewa madhara yanayoweza kuyakumba makundi mbalimbali ya kijamii nchini kuwa ndilo jukumu kuu la wizara yake.

700 /