Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Taifa la Iran litajibu uchokozi wa aina yoyote wa adui

Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatano) ameonana na waziri na maafisa wa Wizara ya Elimu na Malezi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na idadi kubwa ya walimu nchini na sambamba na kubainisha nafasi isiyo na mbadala ya Wizara ya Elimu na Malezi na vilevile nafasi muhimu mno na yenye taathira kubwa ya mwalimu katika kulea kizazi chenye imani thabiti, chenye welewa mpana wa mambo, chenye muono wa mbali, kinachojiamini na chenye nishati kubwa na matumaini, amelitaja suala la kufanikisha malengo hayo makuu matukufu kuwa linaweza kupatikana tu kwa kutekelezwa kikamilifu na kwa mshikamano wa kada zote; hati ya mabadiliko ya kimsingi ya Wizara ya Elimu na Malezi. Amesisitiza kuwa: Viongozi serikalini na hususan wale wanaohusika na masuala ya kiuchumi wanapaswa kulipa uzito wa hali ya juu na wa kipekee suala la Wizara ya Elimu na Malezi na maisha ya walimu na kulipa kipaumbele kikubwa zaidi kuliko hata taasisi nyingine suala hilo na wajue kuwa kuwekeza kwa namna yoyote ile katika taasisi na majimui hiyo ya elimu na malezi, ni kuwekeza kwa ajili ya mustakbali wa taifa na kuongeza tija na faida kwa nchi.

Vilevile ameashiria vitisho vya hivi karibuni vya viongozi rasmi wa Marekani vilivyotolewa sambamba na kuendelea kufanyika mazungumzo ya nyuklia na kusisitiza kuwa: Mimi siungi mkono mazungumzo yanayofanyika chini ya mzimu wa vitisho. Maafisa wetu wa siasa za kigeni na wale wanaofanya mazungumzo hayo wanapaswa kuzingatia vizuri mistari myekundu na mikuu ya taifa na kwamba sambamba na kuendelea na mazungumzo, wana wajibu pia wa kutilia maanani na kulinda adhama na haiba ya taifa la Iran na wasikubali kusalimu amri mbele ya mashinikizo, mabavu, udhalilishaji na vitisho vyovyote vile.

Mwanzoni mwa hotuba yake hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kukumbuka siku alipouawa shahidi mwanafikra maarufu na mkubwa wa Iran, Ayatullah Mutahhari na kusema kuwa moja ya sifa bora za mwanafikra huyo ni kuwa kwake mwalimu aliyefanya kazi zake kwa ikhlasi na bidii zisizochoka.

Aidha amegusia nafasi isiyo na mbadala ya Wizara ya Elimu na Malezi katika kujenga mustakbali wa nchi na kuongeza kuwa: Katika suala la elimu na malezi, mwalimu ni kiungo muhimu mno na chenye taathira kubwa sana katika kuzifinyanga na kuzipa sura bora shakhsia za kifikra na kiroho za wanafunzi na kizazi cha baadaye cha nchi kwa namna ambayo hata baba au mama au mazingira anayokulia mtoto hayawezi kuwa na taathira kubwa kama ya mwalimu.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kwa kuzingatia nafasi ya Wizara ya Elimu na Malezi na walimu katika mustakbali wa nchi, kutoa gharama zozote kwa ajili ya kuimarisha sekta hiyo kwa hakika ni uwekezaji bora kabisa.

Pia amesisitiza kuwa inabidi kuliangalia suala la kiuchumi la Wizara ya Elimu na Malezi kwa jicho hilo hilo kama ambavyo amegusia pia nafasi ya mwalimu katika kulea watu wakubwa na shakhsia bora na kuongeza kuwa: Jukumu la mwalimu ni kulea kizazi cha watu waliojengeka kiimani, watambuzi, wanaojiamini, wenye matumaini mazuri na mustakbali, wenye nishati, wenye muono mpana, wenye irada madhubuti na wenye afya na siha ya kimwili na kiroho.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Jukumu la mwalimu kwa hakika ni kujenga jamii bora ya wanadamu wenye sifa tukufu na kwa kweli kazi ya mwalimu ni muondelezo wa jukumu la Manabii yaani kuwaelimisha watu na kuzitakasa nafsi zao.

Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kufanikishwa risala ya kweli ya walimu kuwa lina mambo yake ya lazima na ya dharura na kuongeza kuwa: Moja ya mambo hayo ya lazima ni kuzingatiwa suala la maisha ya walimu. Viongozi serikalini na hususan wale wanaohusika na masuala ya uchumi, wana wajibu wa kuiangalia kwa mtazamo wa kipekee Wizara ya Elimu na Malezi na hali ya kiuchumi ya walimu licha ya kuwepo vizuizi hivi na vile na kulifanya suala hilo kipaumbele chao kikuu.

Vilevile amesisitiza kuwa kama suala la maisha ya walimu litadharauliwa, basi adui atalitumia vibaya suala hilo na kuongeza kuwa: Tab’an walimu ni watu waumini, waungwana na weledi wa mambo na wanazijua vyema njama za maadui na za watu wenye chuki na mfumo wa Jamhri ya Kiislamu ambao wanataka kutumia suala la maisha ya walimu kueneza fitna na kujengea hoja na kuwekea sera zao za kisiasa ili kuutia kwenye matatizo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amelitaja suala la Chuo Kikuu cha walimu kuwa ni muhimu sana katika upande wa kuandaa na kuwaongezea elimu walimu na kusisitiza kwamba: Michakato yote katika Chuo Kikuu hicho hususan mchakato wa kuchunguza watu wenye sifa za kujiunga na chuo hicho, aina za masomo na kuteua wahadhiri na wajumbe wa jopo la wahadhiri wa chuo hicho, yote inapaswa kuwa salama na iendane na vigezo vya Kiislamu na vya Mapinduzi.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia hati ya mabadiliko ya kimsingi katika Wizara ya Elimu na Malezi na kuungwa mkono kwake na wataalamu mahiri na magwiji na kuongeza kuwa: Jambo la wajibu la kuifanya hati hiyo izae matunda ni kutekelezwa vipengee vyake kiukamilifu na kwa mshikamano wa kada zote, na iwapo hati hiyo ya mabadiliko ya kimsingi itatekelezwa sehemu yake moja tu na Wizara ya Elimu na Malezi na kudharauliwa sehemu nyingine, basi hati hiyo haitokuwa na taathira zinazotakiwa na hakuna mabadiliko yoyote yatakayotokea.

Aidha amesisitizia wajibu wa kueleweshwa Wizara ya Elimu na Malezi pamoja na walimu yote yaliyomo kwenye hati hiyo na kuongeza kuwa: Vyombo na vya upashaji habari na hususan Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB navyo vinapaswa kuisaidia Wizara ya Elimu na Malezi katika jambo hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ni jambo la dharura kutumia vizuri mpango wa sita wa maendeleo ambao siasa zake kuu Inshaallah zitatangazwa katika siku za usoni na ambao utakuwa na mtazamo maalumu kuhusiana na hati hiyo ya mabadiliko ya kimsingi katika Wizara ya Elimu na Malezi na ameitumia fursa hiyo kuwaambia maafisa wa Wizara ya Elimu na Malezi kwamba: Kuweni macho ili ratiba zisizo za muono wa kina na mambo ya kila siku yasije yakachukua nafasi ya mabadiliko ya kimsingi katika Wizara ya Elimu na Malezi.

Ayatullah Udhma Khamene ameitaja hali ilivyo nchini Iran hivi sasa kuwa ni nzuri kwa ajili ya kufanyika mabadiliko ya kimsingi katika Wizara ya Elimu na Malezi na kuongeza kuwa: Kwa bahati nzuri leo hii nchi yetu ina utulivu na usalama na viongozi wa serikali wanafanya kazi kwa mapenzi makubwa na kwa kuzingatia jambo hilo, hivyo huu ni wakati mzuri wa kuweza kuongeza ubora katika Wizara ya Elimu na Malezi na kuifikisha kwenye daraja inayotakiwa.

Mwishoni mwa sehemu hiyo ya hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amewashukuru tena walimu na kusema: Ninaitumia fursa hii kuwashukuru na kuwapa salamu zangu walimu wote nchini.

Katika sehemu ya pili ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia miamala ya hivi karibuni ya viongozi rasmi wa Marekani kuhusiana na taifa la Iran sambamba na kuendelea na mazungumzo ya nyuklia na kutaja nukta kadhaa muhimu katika sehemu hiyo ya hotuba yake.

Awali ya yote, Ayatullah Udhma Khamenei amegusia uhakika usiopingika kwa kusema: Katika kipindi chote hiki cha miaka 35 iliyopita, maadui wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu licha ya kufanya makeke makubwa na kupiga makelele mengi lakini mara zote wamekabiliwa na uadhama na haiba ya taifa la Iran na ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Amesisitiza kuwa: Haiba na adhama hiyo si kitu cha dhahania na cha kufikirika bali ni ukweli usio na shaka kwani nchi kubwa ya Iran yenye watu zaidi ya milioni sabiini ina utamaduni mkongwe na historia ya kale na kubwa na ni nchi ya waty wenye ushujaa na nia na azma ya kupigiwa mfano.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa taifa hili daima limekuwa likilinda vizuri utambulisho wake na kuongeza kuwa: Katika kipindi cha miaka minane ya vita vya kujihami kutakatifu (vita vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) madola makubwa duniani yalifanya njama za kila namna za kujaribu kulipigisha magoti taifa hili lakini yalishindwa, hivyo inabidi adhama na haiba hiyo ilindwe.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Viongozi wa kisiasa wa nchi mbalimbali wamekuwa wakikiri hadharani na pia kwa siri kwamba lau kama vikwazo ambavyo limewekewa taifa la Iran hivi sasa vingeliwekwa dhidi ya nchi nyingine yoyote ile, basi bila ya shaka yoyote nchi hiyo ingeliangamia na kusambaratika kabisa, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama kidete na imara kukabiliana vilivyo na vikwazo hivyo.

Amesisitiza kuwa: Suala hili si kadhia ndogo hata chembe, lakini vyombo vya kipropaganda duniani vinaeneza propaganda za kuwafanya watu wa nchi nyinginezo wasijue uhakika wa mambo ulivyo nchini Iran. Hata hivyo lakini mataifa mengi duniani yanaujua uhakika huo na viongozi wa kisiasa duniani nao wanautambua vyema uhakika huo ijapokuwa hawaukiri kwa maneno na wanautamka kwa sura nyingine.

Baada ya kutoa utangulizi huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaelekea viongozi nchini hususan maafisa wa siasa za kigeni wa Iran na vilevile watu wenye vipawa katika jamii akiwaambia: Jueni kuwa, iwapo taifa fulani litashindwa kulinda adhama na utambulisho wake mbele ya mabeberu, basi bila ya shaka yoyote taifa hilo litaporomoka hivyo tambueni thamani ya kuweza taifa la Iran hivi sasa kujitambua na kulinda vilivyo utambulisho wake.

Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia vitisho vya kijeshi vilivyotolewa na viongozi wawili rasmi wa Marekani katika siku za hivi karibuni dhidi ya Iran sambamba na kuendelea na mazungumzo ya nyuklia na kuongeza kuwa: Kufanya mazungumzo chini ya mzimu wa vitisho hakuna maana na kwamba taifa la Iran haliwezi kukubaliana na mazungumzo yanayofanyika chini ya kivuli cha vitisho.

Amegusia tena matamshi ya viongozi rasmi wa Marekani ya siku za hivi karibuni ambao wamesema kuwa kama kutatokezea kitu fulani basi wataishambulia kijeshi Iran na kuwaelekea viongozi wa Marekani akiwaonya kwa kuwaambia: Kwanza tambueni kuwa mnajidanganya. Pili kama nilivyosema wakati wa utawala wa rais aliyepita wa Marekani ni kwamba zama za kupiga na kuondoka zimeisha na kwamba yeyote atakayejaribu kulichokoza taifa la Iran, taifa hili kamwe halitamuacha vivi hivi.

Kwa mara nyingine, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, viongozi wote nchini na hususan wale wanaofanya mazungumzo, wanapaswa kulizingatia vyema jambo hilo. Ameongeza kuwa: Wanaofanya mazungumzo ya nyuklia wanapaswa wakati wote kuchunga mistari myekundu na masuala ya kimsingi na Inshaallah hawatoivuuka mistari hiyo.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, ni jambo lisilokubalika kabisa kuuona upande wa pili muda wote unatoa vitisho dhidi yetu sambamba na kufanya mazungumzo nasi. 

Ameongeza kuwa: Wamarekani wanayahitajia sana mazungumzo hayo kuliko tunavyoyahitajia sisi na hata kama watasema kiwango cha kuhitajia kwao mazungumzo hayo hakizidi chetu basi kitakuwa ni sawa na kiwango chetu cha kuhitajia mazungumzo hayo. Sisi tunapenda kuona mazungumzo hayo yanazaa matunda na vikwazo dhidi yetu vinaondolewa, lakini hii haina maana ya kwamba kama vikwazo havitaondolewa basi tutashindwa kuendesha nchi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Hivi sasa imewathibitikia watu wote ndani ya nchi kuwa si sahihi kuamini kwamba utatuzi wa matatizo yetu ya kiuchumi unafungamana na kuondolewa vikwazo, bali matatizo yetu ya kiuchumi yanapaswa kuondolewa kwa tadibiri, irada ya kweli na uwezo wetu wenyewe, ni sawa kuwe na vikwazo au kusiwe na vikwazo.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tab’an kama vikwazo havitakuwepo huenda utatuzi wa matatizo ya kiuchumi ukawa rahisi kupatikana lakini inawezekana pia kutatuliwa matatizo yaliyopo ya kiuchumi licha ya kuendelea kuwepo vikwazo.

Vilevile amesisitiza kuwa huo ndio msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusiana na mazungumzo ya nyuklia na katika kubainisha sababu zinazoifanya serikali ya Marekani kuhitajia mno mazungumzo hayo amesema: Kwa ajili ya kutia nguvu utendaji kazi wao na kuonesha kuwa kuna jambo la maana wamefanya, viongozi wa serikali ya Marekani wanahitajia mno kuwa na kisingizio cha kuwawezesha kudai kuwa “Sisi tumeiburuza Iran kwenye meza ya mazungumzo na kuitwisha baadhi ya mambo tuliyotaka.”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwa kusisitiza kwamba: Mimi sikubaliani na mazungumzo yanayofanyika chini ya mzimu wa vitisho.

Aidha ameielekea timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kuiambia: Endeleeni na mazungumzo hayo kwa kuchunga mistari mikuu ya nchi na kama mtaweza kufikia makubaliano kwa kuchunga mistari hiyo ni jambo jema, lakini msikubali kwa hali yoyote ile kusalimu amri mbele ya mashinikizo, mabavu, kudhalilishwa na kutishwa.

Aidha amsisitiza kuwa hivi sasa serikali ya Marekani ndiyo serikali iliyopoteza heshima kabisa duniani na kutaja moja ya sababu za serikali ya Marekani kupoteza heshima na itibari yake kuwa ni namna Washington inavyounga mkono jinai zinazofanywa na serikali ya ukoo wa Aal Saud huko Yemen.

Serikali ya Aal Saud inafanya mauaji ya watu wasio na hatia wanawake na watoto huko Yemen pasi na kujali chochote na kwa kisingizio tu kwamba kwa nini wananchi wa Yemen hawamtaki mtu fulani kuwa rais wao, na Wamarekani nao wanaunga mkono hadharani jinai hizo kubwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa Marekani haina heshima wala itibari yoyote katika fikra za wananchi wa nchi za eneo hili na kuongeza kuwa: Wamarekani hata hawaoni haya wanapojitokeza hadharani na kuunga mkono mauaji ya wananchi wa Yemen, lakini wakati huo huo  inaituhumu Iran kuwa inatuma silaha na kuingilia masuala ya ndani ya Yemen wakati inachofanya Tehran ni kujaribu kadiri inavyowezekana kuwatumia wananchi wa Yemen misaada ya madawa na chakula.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Taifa la wanamapambano na wanamapinduzi la Yemen halina haja na msaada wa silaha kwani kambi na maghala yote ya silaha yako mikononi mwao, bali wanachohitajia wananchi wa Yemen ni misaada ya kibinadamu ya madawa, chakula na nishati kutokana na kuzingirwa kila upande na maadui wa taifa hilo, lakini wavamizi wa nchi hiyo hawaruhusu hata kuingia Yemen misaada hiyo ya kibinadamu ya shirika la Hilal Nyekundu (la Iran).

Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa njia ambayo taifa la Iran limejichagulia ni njia madhubuti, makini na yenye mustakbali mzuri na kuongeza kuwa: Kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na kwa “upofu wa jicho la adui” njia hiyo itafikia malengo yaliyokusudiwa na watu wote wataona namna adui atakavyoshindwa kufanikisha malengo yake maovu kuhusiana na taifa la Iran.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Bw. Fani, Waziri wa Elimu na Malezi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kukumbuka kuuawa shahidi mashahidi Rajai, Bahonar na Mutahhari na vilevile kwa mnasaba wa maadhimisho ya wiki ya mwalimu nchini Iran amesema kuwa: Kuundwa kamati ya utendaji na kuandaliwa muongozo wa hati ya mabadiliko ya kimsingi ya mfumo wa elimu na malezi nchini Iran, kuongeza idadi ya safari za kielimu za wanafunzi wanaotembelea maeneo ya vita vya kujihami kutakatifu, kutekelezwa kivitendo ratiba ya kuhifadhisha Qur’ani Tukufu kwa njia ya maudhui mashuleni, kuongeza safari za malezi na utafiti kwa lengo la kuwasomesha wanafunzi mtindo wa maisha ya Kiirani-Kiislamu, kuandaa mashindano ya michezo ndani ya shule mbalimbali kwa kuzingatia misingi mitatu mikuu; mafunzo, melezi na michezo, kulipa mazingatio maalumu suala la wanafunzi wa maeneo yaliyo nyuma kimaendeleo, kufanyia marekebisho msimamo wa ratiba za masomo uliosimama juu ya msingi wa siasa za idadi ya watu na uchumi wa kusimama kidete, kuongeza kiwango cha kushiriki watu wanaojitolea kwenye mambo ya kheri katika ujenzi wa shule na kuongeza kiwango cha elimu ya walimu, kuwa ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Elimu na Malezi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika duru yake hii mpya.

 

 

 

700 /