Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Ali Khamenei:

Qarii wa Qur’ani anapaswa kuwa na imani ya kweli ya maana ya aya za kitabu hicho

Katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwezi ambao imeshushwa ndani yake Qur'ani, alasiri ya leo (Alkhamisi) kumefanyika mahafali ya Qiraa ya Qur'ani Tukufu hapa mjini Tehran yaliyohudhuriwa na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika mahafali hayo yaliyojaa nuru na kuhinikiza manukato na umaanawi wa Qur'ani, maqari na mahafidh 15 wa Qur'ani Tukufu pamoja na wahadhiri wa Qur'ani kutoka kona zote za Iran, wamesoma baadhi ya aya tukufu za maneno hayo ya Mwenyezi Mungu na kikundi cha kasida nacho kimepata fursa ya kusoma kasida za kumshukuru na kumhimidi Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Katika mahfali hayo, Ayatullah Ali Khamenei amesifu maendeleo yanayozidi kuongezeka na kustawi kila uchao na ambayo yanashuhudiwa waziwazi kati ya maqarii wa Kiirani na ameitaja sauti nzuri ya kusoma Qur'ani Tukufu kuwa ni utangulizi wa kuziandaa vizuri nyoyo za wasikilizaji kwa ajili ya kufikia kwenye malengo makuu ya maneno hayo ya Mwenyezi Mungu. Amesisitiza kuwa: Bado kuna nafasi kubwa na pana sana ya kuweza kuenea taathira zaidi za Qur'ani Tukufu katika jamii, na kwamba jambo la lazima la kuweza kutoa athari kubwa zaidi Qur'ani Tukufu katika jamii ni qiraa ambapo qarii mwenyewe mbali na kutakiwa kufikisha vizuri - kwa walengwa - mafundisho ya aya za Qur'ani Tukufu, yeye mwenyewe pia ni lazima awe na imani ya kweli na ya kina kuhusu maneno hayo ya Mwenyezi Mungu.

Ameongeza kuwa: Maqarii wa Qur'ani Tukufu wanaweza- kwa ajili ya kufikisha vizuri mafundisho ya Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu- kusoma kwa kusisitiza baadhi ya maneno ya Qur'ani na kuyasoma kwa kuyakariri mara kadhaa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametahadharisha pia kuhusu ubaya wa kuchupa mipaka katika kukariri kusoma baadhi ya aya na amesema: Miongoni mwa mambo yanayokifanya kisomo cha Qur'ani Tukufu kiwe na taathira kubwa ni kuchunga mizani za sauti wakati wa kusoma aya za Qur'ani.

Ayatullah Udhma Khamenei ametoa nasaha nyingine muhimu kwa maqarii na kwa watu wote wanaofanya kazi za Qur'ani Tukufu kwamba hakuna haja ya kurefusha kusoma baadhi tu ya maneno au aya za Qur'ani, kama ambavyo kushangilia kupita kiasi nako si jambo jema, bali ni jambo lisilo na udharura wowote ule.


 

700 /