Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Rasilimali adhimu ya watu wa Iraq ni chanzo cha kutegemewa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Ali Khamenei leo jioni (Jumatano) ameonana na Waziri Mkuu wa Iraq Bw. Haider al Abadi, na ujumbe alioandamana nao katika ziara yake nchini Iran na kulitaja suala la kuwa macho kwa ajili ya kulinda umoja na mshikamano wa kisiasa na kitaifa wa Iraq kuwa ni jambo la dharura mno. Huku akiashiria nia ya kweli, hima na ushujaa wa vijana wa Iraq katika kupambana na magaidi amesisitiza kuwa: Nguvu na uwezo mkubwa wa vikosi vya kujitolea vya wananchi ni jambo lenye taathira kubwa na muhimu mno kwa ajili ya mustakbali na maendeleo ya Iraq katika nyuga tofauti.

Vilevile amesisitiza kuwa, kusimama kidete taifa na serikali ya Iraq katika kukabiliana na magaidi ni dhamana ya kupatikana amani na usalama nchini humo na katika nchi zote za eneo hili la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa: Moja ya sifa muhimu za wananchi wa Iraq ambayo imedhihirika kwa uwazi zaidi katika mapambano ya wananchi hao dhidi ya magaidi, ni ushujaa, nia ya kweli na nguvu za vikosi vya kujitolea vya wananchi na vya makabila yanayohamahama yenye ghera katika kupambana na adui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuwepo magaidi nchini Iraq kuwa ni jambo la muda na la kupita tu na kuongeza kuwa: Rasilimali kubwa na adhimu ya vikosi vya kujitolea vya wananchi ni chemchemi ya kuaminika na inayofaa kutegemewa katika nyuga tofauti ambazo hazihusiani tu na medani za mapigano.

Ayatullah Khamenei amesema: Uzoefu wa wananchi wa Iraq wa siku za huko nyuma kuanzia wakati wa ukoloni wa Uingereza hadi katika kipindi cha hivi sasa cha njama za kibeberu za kupenda kujitanua Wamarekani unaonesha kuwa, madola yanayolitakia mabaya taifa la Iraq hayapendi kuona nguvu adhimu ya wananchi wa nchi hiyo katika medani ya mapambano, hivyo kuna wajibu wa kuilinda rasilimali hiyo ya wananchi kwa nguvu zote.

Amesema kwamba moja ya malengo ya mashirika ya kiusalama na kijasusi ya nchi za Magharibi huko Iraq ni kuvunja nguzo za umoja na mshikamano wa kitaifa na kisiasa nchini humo na kusisitiza kuwa: Ni wajibu kuwa macho na kupambana vilivyo na kwa uangalifu mkubwa na njama za maadui hao za kueneza mifarakano na isiruhusiwe kutiwa doa umoja na mshikamano wa Waislamu wa Kishia na Kisuni na mshikamano wa Wakurdi na Waarabu nchini Iraq.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono umoja na mshikamano wa makundi ya wanamapamno na wanamapinduzi wa Iraq na kwamba wananchi na viongozi wa Iraq wanapaswa kuwa macho mbele ya njama za kueneza fitna, mizozo na mifarakano zinazofanywa na maadui wa taifa lao.

Ayatullahil Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inauhesabu usalama na maendeleo ya Iraq kuwa ni sawa na usalama na maendeleo yake na kuongeza kuwa: Wanachotaka Wamarekani ni kuona kuwa kwa upande mmoja wanapora utajiri wa Iraq kama wanavyofanya katika baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo hili, na kwa upande wa pili wanataka kuwatwisha Wairaq matakwa yao kama walivyofanya huko nyuma, na inabidi kufanyike juhudi kubwa za kuizuia Marekani kufikia malengo yake hayo.

Aidha amesisitizia uungaji mkono wa pande zote wa Iran kwa serikali iliyoko madarakani kihalali nchini Iraq na kuongeza kuwa: Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuiunga mkono serikali na wananchi wa Iraq.

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia sifa ya kupenda wageni na ukarimu ya wananchi wa Iraq katika kuwapokea wafanya ziara wa Arubaini ya Imam Husain AS na kusema kuwa, hiyo ni sifa nyingine nzuri sana ya wananchi wa Iraq.  Ameongeza kwamba: Miamala na tabia hiyo ya mapenzi na ya kimaanawi ni muhimu mno katika ulimwengu wa leo ambao watu wanathamini zaidi mambo ya kimaada na kidunia na kwa hakika hadi hivi sasa ukubwa na kina cha tabia hizo njema za wananchi wa Iraq hakijajulikana ipasavyo.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Bw. Eshaq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bw. Haider al Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq ameelezea kufurahishwa kwake na kupata fursa ya kuonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa, kuendelea kuwepo uungaji mkono wa pande zote wa Iran kwa Iraq na ushirikiano wa kidugu wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ndugu zao wa Iraq ni jambo linaloonesha kuwa kuna uhusiano wa kina baina ya mataifa haya mawili ndugu na kuongeza kuwa: Maadui wa Iraq wanatumia uwezo wao wote kwa ajili ya kuzusha mifarakano na mizozo na kikaumu na kimadhehebu nchini Iraq lakini wananchi na serikali ya Iraq imesimama imara kukabiliana na njama hizo na kulinda umoja na mshikamano wao wa kitaifa.

Vilevile amesisitiza kuwa, makundi ya kigaidi na kitakfiri katika nchi za Iraq na Syria hayatofautishi hata chembe baina ya Waislamu wa Kisuni na Kishia na kuongeza kuwa: Kusimama kidete serikali na wananchi wa Iraq leo hii kimekuwa kizuizi na kinga kubwa katika kukabiliana na kupanuka wigo wa kundi la Daesh katika nchi nyingine za eneo hili, lakini hilo halitoshi bali nchi zote za eneo hili zinapaswa kuungana kwa ajili ya kupambana kikweli na kwa nguvu kubwa zaidi na mgaidi hao.

Vilevile Bw. Haider al Abadi ameishukuru sana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na misaada yake mbalimbali kwa serikali na wananchi wa Iraq katika kupambana na ugaidi.


 

700 /