Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Vikwazo vyote vya kiuchumi, kifedha na kibenki vinapaswa kuondolewa mara tu baada ya kusainiwa makubaliano ya nyuklia

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo Jumanne ameonana na viongozi wa mihimili mitatu ya dola na viongozi waandamizi wa nchi ambapo mbali na kubainisha matunda, changamoto na njia za kufikia uchumi wa kimapambano, ameainisha masuala kadhaa muhimu kuhusu mwenendo wa mazungumzo ya nyuklia. Amebainisha mistari myekundu katika mazungumzo hayo na kusisitiza kuwa: Wamarekani wanataka kuangamiza sekta ya nyuklia ya Iran; mkabala wake viongozi wote wa Iran wanasisitiza mistari myekundu ambayo haipaswi kuvukwa na wanataka makubaliano mazuri kwa maana ya makubaliano yenye insafu, ya kiadilifu, yenye izza na yanayolinda maslahi na manufaa ya Iran.

Mwanzoni mwa mkutano huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mwezi wa Ramadhani kuwa ni mwezi wa takwa na uchamungu. Amebainisha aina mbili za takwa ambazo ni takwa na uchamungu wa mtu binafsi na ule wa kijamii na akasema: Takwa ya mtu binafsi ni hali na mlinzi wa daima anayemlinda mwanadamu na dharba kali za kiroho na kuwa na taathira muhimu katika masuala yake ya kidunia.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa takwa na uchamungu wa jamii unaweza kuenezwa zaidi katika masuala ya kiuchumi. Amesisitiza kuwa takwa ya jamii katika masuala ya uchumi ndiyo uchumi wa kimapambano unaoilinda nchi mbele ya mitetemeko inayosababishwa na matukio mbalimbali ya kimataifa au mbele ya mishale yenye sumu ya siasa za wapinzani duniani.

Amekumbusha tahadhari zake za mara kwa mara alizotoa katika miaka iliyopita kuhusu udharura wa kuimarishwa nchi mkabala wa mitetemeko ya kiuchumi inayosababishwa na madola makubwa na kusema kuwa, katika miaka hiyo viongozi wa nchi wamefanya juhudi kubwa kulingana na uwezo wao lakini maudhui ya uchumi wa kimapambano unapaswa kufikiwa kwa kutumia uwezo na suhula zote.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema vigezo vya uchumi wa kimapambano vimetumika katika baadhi ya nchi na taathira zake nzuri zimeonekana na kusema: Nukta muhimu katika uchumi wa ina hii ni kutilia mkazo uzalishaji wa ndani na kuangalia ndani zaidi. Amesisitiza kuwa uzalishaji wa ndani hauna maana ya kujitenga bali ni kutegemea zaidi suhula na uwezo wa ndani ya nchi sambamba na kuangalia nje.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa utayarishaji wa sera za uchumi wa kimapambano ni matunda ya akili ya jamii na mashauriano ya muda mrefu. Ameongeza kuwa baada ya kuwasilishwa sera za uchumi wa kimapambano wataalamu wengi wa masuala ya uchumi waliuunga mkono na hivi ssa uchumi w akimapambano umeingia katika utamaduni wa uchumi hapa nchini.

Amesema mtindo wa uchumi wa kimapambano unakabiliana na mtindo wa zamani ambao nchi za ulimwengu wa tatu zilitwishwa na madola makubwa na kuongeza kuwa, mtindo huu wa zamani unategemea kuangalia nje ya nchi lakini mtindo wa uchumi wa kimapambano ni kigezo cha kisasa na kinachotegemea uwezo wa ndani ya nchi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, yumkini baadhi ya watu wakadhani kwamba mtindo wa uchumi wa kimapambano ni mzuri lakini hauwezi kutekelezeka; lakini sisi tunasisitiza kuwa inawezekana kabisa kutekeleza na kufikiwa uchumi wa kimapambano katika mazingira ya sasa hapa nchini na kwa kutilia maanani uwezo na suhula zilizopo.

Baada ya utangulizi huo Ayatullah Khamenei amebainisha baadhi ya suhula na uwezo mkubwa wa Iran ambao unaweza kuwa uwanja nzuri wa kutekelezea sera za uchumi wa kimapambano. Nguvu ya vijana wenye ujuzi na elimu na wenye kujiamini ndiyo uwezo wa kwanza ulioashiriwa na Kiongozi Muadhamu. Amesema kuwa kuwepo kwa idadi hiyo kubwa ya vijana wenye elimu na ujuzi hapa nchini ni miongoni mwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu kwa sharti kwamba siasa zisizo sahihi zisipelekee kuzeeka kwa jamii na kupungua nguvu ya vijana.

Ayatullah Khamenei ameashiria suala la kuwepo wahitimu milioni 10 wa vyuo vikuu na zaidi ya wanachuo milioni nne wanasoma katika vyuo vikuu kwa sasa hapa nchini ambao ni asilimia 25 zaidi ya kipindi cha mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Idadi hiyo kubwa ya wasomi vijana na wenye ujuzi ni miongoni mwa fahari za utawala wa Kiislamu na fursa kubwa.

Amesema kuwa nafasi ya kiuchumi ya Iran ni miongoni mwa uwezo na suhula na kuongeza kuwa: Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashika nafasi ya 20 katika uchumi wa dunia na iwapo uwezo wa nchi ambao haujatumika utatumiwa vizuri kuna uwezekano ikashika nafasi ya 12 ya uchumi duniani.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja nafasi ya kwanza ya Iran katika kuwa na akiba kubwa zaidi ya mafuta na gesi kwa ujumla duniani kuwa ni sehemu ya uwezo wa nchi hii. Vilevile ameashiria nafasi nzuri ya kijiografia ya Iran kama nukta inayounganisha kaskazini na kusini na mashariki na magharibi na akasema: Kuwa jirani na nchi 15 zenye jamii ya watu milioni 370 ambalo ni soko la kigeni la karibu sana na vilevile kuwa na jamii ya watu milioni 70 ambalo ni soko kubwa la ndani ni uwezo mwingine na iwapo soko hili la ndani pekee litazingatiwa, basi hali ya uzalishaji itabadilika kabisa.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa miundombinu mikubwa hapa nchini katika sekta ya nishati, usafirishaji, mawasiliano, vituo vya umeme na mabwawa na vilevile uzoefu mkubwa wa masuala ya utawala hapa nchini ni sehemu ya uwezo wa nchi hii. Ameongeza kuwa, uwezo huu unapaswa kutumiwa kwa njia sahihi na inayofaa kwani tatizo la nchi si kukosekana mipango sahihi wala utaalamu, bali suala kuu linalokaririwa pia kati ya wasomi na watu wenye nafasi za juu hapa nchini ni kutotumiwa ipasavyo mipango na sera sahihi.

Amesema kuwa baadhi ya matatizo yanatokana na changamoto za ndani ya nchi. Akibainisha sehemu ya changamoto hizo amesema kuwa: Changamoto kubwa ya nchi yetu ni upuuzaji katika kazi na kutoyapa uhumimu mambo mbalimbali.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, mijada ya maneno na ya kifikra haiwezi kufua dafu bali utatuzi wa matatizo unahitajia harakati, kupiga hatua na ufuatiliaji wa mambo wa muda mrefu.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa kufikia natija kwa baadhi ya miradi mikubwa huwenda kunahitaji muda mrefu kiasi cha kupita kizazi na ameongeza kuwa: Wakati kulipokuwa kukizungumziwa harakati kubwa ya elimu hapa nchini katika vyuo vikuu huwenda hakuna mtu aliyekuwa akiamini kwamba baada ya kupita miaka 10 au 15 kutapatikana harakati kubwa ya sasa ya sayansi na elimu kwa hima na juhudi za walimu na vijana wenye vipawa, lakini hii leo ikilimganishwa na miaka hiyo, tunashuhudia maendelea makubwa bali maendeleo ya kustaajabisha katika baadhi ya nyanja.

Njia sambamba na nyepesi na wakati huo huo zenye madhara makubwa ni miongoni mwa changamoto za ndani zilizoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ameweka wazi zaidi suala hilo kwa kusema: Wakati mwingi kudhamini baadhi ya mahitaji na bidhaa kunawezekana kupitia njia mbili. Njia moja ni ya kupitia Ulaya na nyepesi, na nyingine si ya kupitia Ulaya na ni ngumu. Njia ya kwanza inamuweka mwanadamu katika mbinyo na inawadhoofisha marafiki zake na kuwapa nguvu maadui zake.

Ayatullah Khamenei amesema changamoto nyingine ya ndani ambayo ni kosa kubwa sana na la kimsingi ni kudhani kuwa kujitenga na misingi ya kiitikadi na nguzo za utawala wa Kiislamu kunapelekea kufunguka njia zote.

Amesema: Viongozi katika serikali inayohudumia wananchi ni watu wenye imani na itikadi thabiti kwa misingi na nguzo za Mapinduzi ya Kiislamu na mimi silalamikii lolote dhidi ya viongozi hawa; hata hivyo katika majmui ya maafisa kuna watu wanaodhani kwamba, kulegeza kamba katika misingi na nguzo kunaweza kufungua milango, wakati ambapo matokeo ya makosa haya makubwa tumeyaona katika miaka ya hivi karibu katika baadhi ya nchi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa njia pekee ya maendeleo ni kusimama kidete na kushikamana barabara na misingi na nguzo zetu.

Ayatullah Khamenei amesema changamoto nyingine ya ndani ni baadhi ya watu kudhani kwamba wananchi hawatawezi kustahamili matatizo.          

Amesema iwapo wananchi wataelezwa ukweli wa mambo na kwa njia sahihi watasimama kidete na kupambana.

Amesema, kuwa na shaka juu ya uwezo wa ndani ya nchi ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Iran na kuongeza kuwa: Tunapaswa kuwa na imani na wasomi wetu vijana na makundi mbalimbali ya wananchi katika masuala ya uchumi na tutumie vyema uwezo wao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa sharti kuu la kuwa na uchumi wa kimapambano ni kuwa na azma thabiti na kubwa na kujiepusha na upuuzaji na uzembe, na vilevile kutegemea uendeshaji wa kijihadi. Amesisitiza kuwa kuendesha mambo kijihadi kuna maana ya kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutumia tadbiri na busara sambamba na kufanya kazi kwa azma kubwa na bila ya woga.

Ayatullah Khamenei amesema, ni jambo la dharura kueneza utamaduni unaooana na uchumi wa kimapambano sambamba na kutumia uendeshaji wa kijihadi. Amesema: Shirika la Utangazaji la Iran (IRIB) vyombo vya habari, maafisa, maimamu wa Swala za Ijumaa na wale wote ambao maneno na matamshi yao yana taathira baina ya wananchi wanapaswa kuwa waenezaji wa utamaduni wa uchumi wa kimapambano.

Amesema kuwa, kubana matumizi, utumiaji wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi hususan katika taasisi za serikali, kukabiliana ipasavyo na uingizaji bidhaa usiokuwa wa kimantiki kutoka nje ya nchi, kupambana na magendo, kutiliwa maanani karakana na viwanda vidogo vidogo na vya kati vya uzalishaji na kutazama upya sera na shughuli za mfumo wa benki ni miongoni mwa mambo ya dharura kwa ajili ya kutekeleza siasa za uchumi wa kimapambano. Amesisitiza kuwa sharti la kutimia haya yote ni mshikamano na ushirikiano wa ndani ya nchi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema watu wote wanapaswa kuisaidia serikali na maafisa wake na kuongeza kuwa: Haikubaliki kwa mtu yeyote kuzusha masuala yasiyo na msingi na kuna ulazima wa kujiepusha na mambo hayo.

Akikamilisha mjadala wa masuala yanayohusiana na uchumi wa kimapambano, Ayatullah Khamenei amesema: Tunaweza kufanya kazi kubwa katika uwanja wa uchumi na kuvuka salama kipindi hiki nyeti.

 

Katika hotuba yake muhimu sana kuhusu maudhui ya nyuklia na kabla ya kuweka wazi baadhi ya mambo yanayohusiana na mazungumzo ya nyuklia, matakwa na mistari myekundu katika uwanja huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza na kutilia mkazo mambo matatu:

Kwanza ni kwamba, kile kinachosemwa na Kiongozi katika vikao vya umma ndicho hicho hicho anachosema katika vikao makhsusi kwa Rais wa Jamhuri na maafisa wengine husika; kwa msingi huo propaganda zisizo sahihi zinazosambazwa kwamba baadhi ya mistari myekundu (katika masuala ya nyuklia) imepuuzwa na kufumbiwa macho katika vikao makhsusi si kweli na ni uongo mtupu.

Suala la pili lililotajwa na Ayatullah Khamenei kama utangulizi wa mjadala wa masuala ya nyuklia ni uaminifu, ghera, ushujaa na kushikamana na dini kwa wanachama wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia.

Amesema kuwa timu hiyo inafanya kazi kwa ghera ya kitaifa, umakini mkubwa na kwa lengo la kufumbua matatizo na kupeleka mbele kazi za nchi mkabala wa wazungumzaji wengi wa upande wa pili na inabainisha misimamo kwa ushujaa.

Ayatullah Khamenei amesema mtu yeyote anayejua habari za ndani za mazungumzo haya ya nyuklia anaelewa ukweli wa haya yanayosemwa kuhusu timu ya mazungumzo ya nyuklia Iran, pamoja na hayo yumkini wakakosea katika kuainisha baadhi ya mambo lakini hapana shaka kuwa ni watu wanaoshikamana na dini na wenye ghera.

Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu ameelekeza maneno yake kwa wakosoaji wa mazungumzo ya nyuklia.

Amesema: Sipingi ukosoaji na ninautambua kuwa ni jambo la lazima na linaosaidia, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, kukosoa ni sahali na rahisi zaidi, kwa sababu ni rahisi mtu kuona aibu na nakisi za mwingine lakini ni vigumu kuweza kuelewa mashaka na wasiwasi wake.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Maneno yangu haya hayapaswi kuzuia ukosoaji lakini tunapaswa kuelewa kuwa, timu ya mazungumzo ya nyuklia inajua vyema baadhi ya mambo yanayosemwa na wakosoaji lakini udharura unailazimisha kuchukua baadhi ya hatua.

Ayatullah Khamenei ameeleza historia fupi ya mwenendo wa mazungumzo na Wamarekani suala ambalo linasaidia sana kuelewa vyema mwenendo wa mazungumzo ya sasa.

Amesema: Maudhui ya mazungumzo na Wamarekani inahusiana na kipindi cha serikali iliyopita baada ya (Wamarekani) kutuma mjumbe hapa Tehran wakiomba kufanya mazungumzo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameweka wazi zaidi kwa kusema: Wakati huo mheshiwa mmoja katika eneo hilo (Mashariki ya Kati) alikuja kukutana nasi kama wasita na mjumbe na akasema waziwazi kwamba Rais wa Marekani amemuomba aje Tehran na kuwasilisha ombi la Wamarekani la kutaka kufanya mazungumzo na Iran. Wamarekani walimwambia mjumbe huyo kwamba, wanataka kuitambua rasmi Iran kama nguvu ya nyuklia, kuhitimisha suala hilo na kuondoa vikwazo katika kipindi cha miezi sita. Tulimwambia mjumbe huyo kwamba hatuna imani na Wamarekani na maneno yao, lakini alisisitiza, nasi tukakubali kujaribu tena suala hilo na kuanza mazungumzo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha nukta mbili muhimu kwa kusema: Katika kila mpambano wa kidiplomasia kuna medani mbili ambazo zinapaswa kupewa mazingatio. Medani ya kwanza na asili ni ile ya uhakika wa mambo, kazi na uzalishaji, na medani ya pili ni ile ya udiplomasia na siasa ambayo huwa uwanja wa kubadili mazao na mapato na kuyafanya nukta chanya na karata ya turufu na kudhamini maslahi ya taifa.

Ameongeza kuwa: Nchi yoyote inapokuwa mikono mitupu katika medani ya kwanza suala hilo hubana uwanja wa kufanya manuva na harakati za nchi husika katika medani ya pili, na kwa kutilia maanani mantiki hiyo, Iran iliingia katika mazungumzo ya nyuklia ikiwa na hazina kubwa na muhimu na sehemu ya hazina hiyo ni kuwa kwake na uwezo wa kuzalisha nishati ya nyuklia iliyorutubishwa kwa kiwango cha daraja 20.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, madola yote makubwa ya nyuklia yalikataa kuiuzia Iran nishati ya nyuklia iliyorutubishwa kwa daraja 20 kwa ajili ya kutengeneza dawa katika kituo cha Tehran na vilevile yalizuia kununuliwa nishati hiyo kutoka nchi nyingine; hata hivyo vijana wasomi wa Iran walifanikiwa kuzalisha nishati hiyo na kuifanya sinia nyuklia, suala ambalo liliuacha bumbuazi upande wa pili.

Ameongeza kuwa mbali na nishati ya nyuklia iliyorutubishwa kwa daraja 20, Iran ina mafanikio na matunda mengine halisi na katika medani na kwa hakika stratijia ya kusimama kidete Iran mbele ya mashinikizo ilifanikiwa na wakati huo Wamarekani walielewa kwamba, vikwazo havina taathira waliyoikusudia na kwamba kuna ulazima wa kutafuta njia nyingine.

Ayatullah Khamenei ameashiria mtazamo wa shaka wa Iran kwa Marekani na kusema: Licha ya hayo Iran ilikuwa tayari kulipa gharama iwapo Wamarekani wangeshikamana na ahadi yao waliyotoa kupitia mjumbe wao wa kieneo (waliyemtuma Tehran), kwa sababu katika mazungumzo inawezekana kulegeza kamba kwa mujibu wa akili na mahesabu makhsusi; hata hivyo muda mfupi baadaye walianza kutaka makuu na kuvunja ahadi yao.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa makubaliano mazuri katika mtazamo wa Iran ni makubaliano ya kiadilifu na yenye insafu na kuongeza kuwa: Wakati wa mazungumzo Wamarekani kwanza walibadilisha miezi sita waliyotoa kwa ajili ya kufuta vikwazo na kuifanya mwaka mmoja na baadaye wakarefusha zaidi mazungumzo hayo kwa kutaka makuu zaidi, bali walitishia kuweka vikwazo zaidi na kutoa vitisho vya mashambulizi ya kijeshi na kwamba machaguo yote yako mezani.

Ayatullah Khamenei amekamilisha mjadala huo kuhusu mazungumzo ya nyuklia kwa kusema: Uchunguzi wa kina kuhusu mwenendo wa matakwa ya Wamarekani unaonesha kuwa lengo lao ni kung’oa kabisa sekta ya nyuklia nchini Iran, kutokomeza utambulisho wa nyuklia hapa nchini na kuufanya kama kibonzo na bango lisilokuwa na maana.


 

Vilevile ameashiria namna utafiti wa kina unavyoonesha kuwa Iran inahitajia megawati 20 elfu za umeme utokanao na nishati ya nyuklia na kuongeza kuwa: Mbali na Wamarekani kufanya njama za kuangamiza miradi ya nyuklia na kutaka kuizuia Iran isinufaike na faida nyingi zilizomo kwenye sekta hiyo, wanataka pia kuendeleza kwa namna fulani mashinikizo na vikwazo vyao dhidi ya Iran.

Ameongeza kuwa: Kama Wamarekani wataweza kufikia malengo yao kwenye mazungumzo, basi watakuwa wamepata ushindi mkubwa kwani watakuwa wamelipigisha magoti taifa la Iran linalopigania uhuru na kujitegemea na kuishinda nchi ambayo inaweza kuwa kigezo na ruwaza njema kwa nchi nyingine duniani na kwamba ahadi zote mbaya za Wamarekani na kuzungusha zungusha kwao mambo kunafanyika kwa ajili ya kufanikisha malengo yao hayo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia pia matakwa ya kimantiki ya Iran tangu mwanzoni kabisa mwa mazungumzo hayo hadi hivi sasa na kuongeza kuwa: Sisi tangu awali kabisa tulisema kuwa, tunataka mashinikizo na vikwazo vya kidhulma vilivyowekwa dhidi yetu viondolewe, ambapo tab'an katika mkabala wa jambo hilo, tuko tayari kutoa baadhi ya vitu kwa sharti kwamba sekta ya nyuklia nchini Iran isisimame na wala isipate madhara yoyote yale.

Ayatullah Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuchora kwa uwazi kabisa mistari myekundu ya nyuklia ya Iran. Amesema kuhusu mstari mwekundu wa kwanza kabisa kwamba: Sisi, tofauti na wanavyong'ang'ania Wamarekani, hatukubaliani na mpaka wa muda mrefu wa miaka 10 na 12 na tayari tumeshawaeleza muda tunaoukubali sisi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuendelea kazi za utafiti na ustawishaji wa miradi ya nyuklia ya Iran hata katika wakati na muda huo wa utekelezaji wa makubaliano yanayotarajiwa, kuwa ni mstari wa pili mwekundu wa Iran na kuongeza kuwa: Wamarekani wanasema tusifanye kazi yoyote katika kipindi chote hicho cha miaka 12 lakini hayo ni maneno ya kibeberu kupindukia na ghalati kupita kiasi.

Akitolea ufafanuzi mstari wa tatu mwekundu wa nyuklia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwa kusisitiza kwamba: Vikwazo vya kiuchumi, kifedha na kibenki, viwe ni vile vilivyowekwa na Baraza la Usalama (la Umoja wa Mataifa) au vile vilivyowekwa na Kongresi ya Marekani au vile vilivyowekwa na serikali ya Marekani, lazima vyote viondolewe mara baada ya kutiwa saini makubaliano na vikwazo vinginevyo viondolewe katika kipindi cha muda unaokubalika.

Vile vile amesema: Wamarekani wanatoa fomula tata, yenye tabaka kadhaa na ya ajabu mno kuhusu vikwazo, na haijulikani kitu gani kitatokea baadaye, lakini sisi tunatangaza waziwazi matakwa yetu bila ya kupindisha maneno.

Ayatullah Khamenei ameendelea na mada hiyo kuhusu mitari myekundu ya nyuklia ya Iran kwa kusema: Suala la kuondolewa vikwazo halipaswi kushurutishwa na kutekeleza Iran ahadi zake yaani wasije wakasema kuwa, kwanza wewe tekeleza ahadi zako baada ya hapo wakala wa IAEA utoe ripoti ya kuthibitisha kuwa umetekeleza ahadi zako hapo ndio vikwazo viondolewe. Sisi hatuwezi kabisa kukubaliana na suala hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mchakato wa kuondolewa vikwazo nao inabidi uende sambamba na utekelezaji wa Iran wa ahadi ulizotoa.

Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesisitiza kuwa: Sisi tunapinga suala la kuakhirisha utekelezaji wa ahadi za upande wa pili hadi pale wakala wa IAEA utakapotoa ripoti na kuthibitisha kutekeleza Iran ahadi zake kwani wakala huo umethibitisha mara nyingi sana kwamba hauko huru na hauna uadilifu, hivyo sisi tuna mtazamo mbaya kuhusu wakala huo na hatuna imani nao.

Ameongeza kuwa: Wanasema inabidi Wakala upate yakini kuhusu kutekeleza Iran ahadi zake. Maneno gani hayo yasiyoingilika akilini! Vipi inataka kupata yakini? Hivi kwani si wakala huo huo unaofanya ukaguzi wake katika kila kona ya Iran?

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Iran inakataa na kupinga vikali ukaguzi usio wa kawaida, au kusailiwa shakhsia wa Iran au kukaguliwa maeneo ya kijeshi ya Iran na kulitaja suala hilo kuwa ni mstari mwengine mwekundu wa nyuklia wa Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kwa uwazi kwamba: Watu wote nchini Iran nikiwemo mimi, Serikali, Bunge, Mahakama na taasisi nyingine za kiusalama na kijeshi na taasisi nyinginezo zote, kila mtu anataka kufikiwe makubaliano mazuri, makubaliano ambayo yatalinda heshima ya Iran, yatakuwa ya kiinsafu na kiuadilifu na yatakayoendana na maslani na manufaa ya Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ijapokuwa tunapigania kuondolewa vikwazo, lakini katika upande fulani tunavihesabu vikwazo kuwa ni fursa nzuri kwetu kwani vimetufanya tuzingatie zaidi nguvu na uwezo wetu wa ndani.

Mwanzoni mwa hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia wajibu wa kuzitumia vizuri baraka za mwezi Mtukufu wa Ramadhani hususan faida zilizomo kwenye dua za mwezi huu na maana zake pana na kusema: Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa khushuu na unyenyekevu, ni mwezi wa istighfari na kurejea kwa Mwenyezi Mungu na ni mwezi wa kujijenga kiimani na kimaadili na kuitakasa nafsi.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa hotuba fupi na ndani yake ameshiria kuanza kazi za Serikali ya 11 ya Iran miezi 22 iliyopita na kuutaja mkakati wa serikali yake katika masuala ya ndani kuwa ni kuleta kuaminiana, miamala ya amani, kupunguza mianya baina ya matabaka ya wananchi na kujiweka mbali na misimamo mikali na ya kufurutu ada.

Vilevile amesema: Msimamo wa serikali yake katika siasa za nje ni kuamiliana kwa njia bora na mataifa mengine duniani kwa kuchunga mstari mwekundu ambao ni kulinda uhuru, heshima na ghera ya taifa la Iran na katika upande wa masuala ya kiutamaduni ni kuandaa mazingira yaliyo wazi kwa watu wote wanaohusiana na masuala ya kiutamaduni na sanaa sambamba na kuchunga mstari mwekundi wa kimaadili na wa hukumu za dini tukufu ya Kiislamu.

Rais Rouhani amesema kuwa, suala la kutatuliwa kadhia ya mazungumzo ya nyuklia katika kalibu ya kufanikisha haki za nyuklia za Iran na kudhamini mahitaji yake ya kijamii ni vipaumbele viwili vikuu vya serikali yake na kuongeza kuwa: Jambo ambalo limeyalazimisha madola makubwa kuja kwenye meza ya mazungumzo ni muqawama na kusimama kidete taifa la Iran mbele ya mashinikizo ya wanaolitakia mabaya taifa hili na kufanikiwa taifa la Iran kuvishinda vikwazo vya watu hao.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, kamwe vikwazo havitafanikiwa kufikia malengo yake na kwamba hata kama vikwazo vitaendelea kuwepo, taifa Iran litaweza kuendesha vizuri na kutatua masuala yake yote ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni na kuongeza kuwa: Tumefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei kwa msaada wa wananchi licha ya kuwa vikwazo dhidi ya nchi yetu bado vipo na tumefanikiwa kutoka katika uzorotaji wa kiuchumi na kukuza uwekezaji licha ya kwamba bado tumo ndani ya vikwazo.

Rais Rouhani amelitaja suala la kuongezeka akiba ya bidhaa za kiistratijia, kuondoa vizuizi vya kusafirisha nje bidhaa, kuwasilisha mkakati wa kutoka kwenye uzorotaji wa uchumi, kupunguza kiwango cha bidhaa zinazoagiziwa kutoka nje ya nchi, kubadilisha kigezo cha ukulima na upandaji mimea, kupanua wigo wa huduma za tiba, kuwasaidia wananchi wa matabaka ya kipato cha chini na kutoa ruzuku kwa ajili ya bidhaa, kupungua utegemezi wa mafuta katika bajeti, kubana matumizi katika mambo mbali mbali, kufungua viwanda elfu nane vya uzalishaji wa bidhaa za kila namna na kupigwa hatua nzuri katika masuala ya kulinda mazingira kuwa ni miongoni mwa hatua za maendeleo zilizopigwa na serikali yake licha ya Iran kuwa bado imo ndani ya vikwazo.

Rais Rouhani amelitaja suala la kupunguza serikali utegemezi wa pato litokanalo na mafuta kuwa ni hatua muhimu mno iliyochukuliwa na serikali mwaka huu na kuongeza kuwa: Ni lazima kufanyike bidii na jitihada kubwa zaidi za kujiletea maendeleo sambamba na kulindwa umoja, mshikamano na maelewano ili tuweze kuvuuka vizuri kwenye kipindi cha matatizo na kwamba jambo hilo halitowezekana bila ya kuweko msaada wa wananchi.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza pia kuwa, hatupaswi kuruhusu kutokea mivutano isiyo ya lazima katika jamii hususan kwenye kipindi hiki nyeti na muhimu. Amesema, kama upande wa pili wa mazungumzo ya nyuklia utaachana na siasa zake za kujivutia kila kitu upande wake, basi kuna uwezekano mkubwa wa kufikia makubaliano na kuvuuka vizuri kwenye kipindi hiki muhimu cha historia.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake hiyo, Rais Hassan Rouhani amebainisha kuwa, mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati leo hii yako chini ya mashinikizo makubwa sana kutokana na uingiliaji wa baadhi ya nchi na makundi ya kigaidi kwenye masuala ya eneo hili na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko mstari wa mbele katika kupambana na ugaidi na kuyaunga mkono mataifa ya eneo hili suala ambalo amesema, Iran itaendelea nalo.

 

700 /