Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Wanaoficha sura mbaya ya Marekani wanalisaliti taifa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alasiri ya leo (Jumamosi) amekutana na familia za mashahidi wa tukio la tarehe 7 Tir na familia zenye mashahidi kadhaa katika mkoa wa Tehran ambapo amesema kuwa nchi na taifa la Iran ni wadaiwa na mashahidi na familia za mashahidi hao. Ameashiria ujumbe unaotia matumaini, unaofichua na wenye kutia furaha ya kimaanawi na azma kubwa ya mashahidi katika kila kipindi na akasema: Hii leo Iran inahitajia azma kubwa, kumjua vyema adui na kujitayarisha kwa ajili ya kukabiliana naye katika medani za vita laini kama nyanja za utamaduni, siasa na maisha ya kijamii. Ameongeza kuwa, wale wanaofanya jitihada za kuficha sura mbaya ya kutisha ya adui habithi kwa kutumia propaganda na vyombo vya habari anakwenda kinyume na maslahi ya taifa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema miongoni mwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu ni kuhuisha maarifa ya kimsingi ya Kiislamu na kutekelezwa kwake kivitendo katika jamii. Ameongeza kuwa miongoni mwa maarifa hayo ni yale yanayohusiana na kufa shahidi ambayo yamepatikana katika jamii ya Iran kwa kadiri kwamba, mashahidi waliingia katika medani za vita kwa nishati na ari na jitihada zao zenye ikhlasi ziliambatana na ujira mkubwa wa Mwenyezi Mungu wa kufa shahidi na kuharakia kukutana na Mola Muumba bila ya huzuni wala woga wowote. Amesisitiza kuwa athari za kimaanawi za kuuawa kwao shahidi zimeonekana katika jamii.

Ayatullah Khamenei amesema, hisi za izza katika familia za mashahidi na furaha na nishati ya kiroho na azma kubwa inayopatikana kati ya wananchi ni miongoni mwa baraka za mashahidi katika jamii. Ameashiria tukio la tarehe 7 Tir 1360 (Juni 1981) na kusema:   Tukio kubwa kama hili la 7 Tir ambamo Ayatullah Beheshti, aliyekuwa kiongozi wa Mahakama Kuu, mawaziri, wawakilishi wa Bunge na wanaharakati wa kisiasa na kimapinduzi waliuawa shahidi, kwa kawaida lingepelekea kushindwa Mapinduzi ya Kiislamu; hata hivyo kwa baraka za damu ya mashahidi hao, mambo yalikwenda kinyume na baada ya tukio hilo taifa la Iran liliungana, na Mapinduzi ya Kiislamu yakashika mkondo wake halisi na sahihi.  

Amesema kuwa miongoni mwa baraka za damu ya mashahidi wa 7 Tir ni kufichuka sura za watenda jinai hiyo. Ameongeza kuwa baada ya tukio hilo sura halisi ya watekelezaji wa moja kwa moja wa jinai hiyo kubwa ambao kwa miaka mingi walikuwa wakijiarifisha visivyo, ilifichuka mbele ya wananchi na vijana, na baadaye magaidi hao walikimbilia hifadhi kwa Saddam na kuungana naye kwa ajili ya kukabiliana na taifa la Iran na wananchi wa Iraq.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kufichuka kwa sura za mikono ya nyuma ya pazia za ndani na nje ya nchi ya tukio 7 Tir na vilevile sura za wale walionyamaza kimya sambamba na kuridhia, ni miongoni mwa baraka za damu ya mashahidi wa tukio hilo. Ameongeza kuwa baada ya tukio la 7 Tir Imam Komeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) alitumia vyema tukio hilo kuyaokoa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yalikuwa katika hali ya kuondolewa katika mkondo wake wa asili na kulionesha taifa harakati halisi ya Mapinduzi.

Akiashiria fajara ya kiroho ya jamii baada ya tukio la tarehe 7 Tir, Ayatullah Khamenei amesema kuwa: Tukio hilo liliwadhihirishia maadui nguvu na kukita mizizi Mapinduzi ya Kiislamu katika jamii na walitambua kuwa mienendo ya kikatili dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu haiwezi kufaulu.

Amesema kuwa kufichuliwa sura halisi ya madola ya kibeberu yanayodai kutetea haki za binadamu ni katika baraka za damu ya mashahidi wa tarehe 7 Tir na kuongeza kuwa: Wale waliofanya jinai ya tarehe 7 Tir wanaendesha shughuli zao kwa uhuru kamili huko Ulaya na Marekani na wanakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hizo na hata wanatayarishiwa vikao vya hotuba zinazozungumzia haki za binadamu!

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mienendo kama hiyo ni alama ya kilele cha unafiki, undumakuwili na uhabithi wa wale wanaodai kutetea haki za binadamu. Ameongeza kuwa: Nchi yetu ina mashahidi elfu 17 wa mauaji ya kigaidi na aghlabu yao ni wananchi wa kawaida kama wafanyabiashara, wakulima, wafanyakazi, wahadhiri wa vyuo vikuu na hata wanawake na watoto wadogo, lakini watekelezaji wa mauaji hayo yote wanaishi kwa uhuru katika nchi zinazodai kutetea haki za binadamu. Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa miongoni mwa baraka za damu ya mashahidi ni kutia moyo wa kusimama kidete na uthabiti katika jamii na kutia nguvu katika roho ya wananchi. Ameashiria shughuli ya kusindikiza miili ya mashahidi 270 iliyofanyika siku chache zilizopita mjini Tehran na hamasa kubwa ya wananchi iliyoambatana na tukio hilo na akasema: Tukio hilo adhimu, harakati, utayarifu, hamasa, mapenzi na moyo wa kuenzi thamani na matukufu uliotokana na tukio hilo vinakabiliana na kuvunjia moyo, kukosa matumaini na kupooza.

Ameeleza kusikitishwa na udhaifu na uzembe uliopo katika kuwaarifisha mashahidi ikiwa ni pamoja na kutoarifishwa ipasavyo mashahidi wa tarehe 7 Tir kama dhihirisho la adhama na kusimama kidete kwa taifa la Iran na akaasema: Vijana katika kambi yenye imani ya kiutamaduni, wanamapinduzi na wenye kujitolea wanapaswa kudhihirisha sura adhimu ya shakhsia hawa wakubwa kwa kutumia lugha ya sanaa ya picha na nyenzo za kisasa.

Ayatullah Khamenei ameashiria pia haki ya mashahidi na familia zao kwa taifa la Iran na akasema: Familia za mashahidi zinaeneza moyo na azma yao kubwa katika jamii, na moyo na azma hiyo ndiyo kitu kinachohitajiwa na nchi yetu kwa sasa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa moja kati ya mahitaji ya kimsingi ya kipindi hiki ni kumtambua adui. Ametahadharisha kuhusu baadhi ya njama za kusafisha sura ya utenda jinai ya adui kwa kutumia propaganda na vyombo vya habari na akaashiria baadhi ya mifano ya ugaidi wa Marekani na vibaraka wake dhidi ya taifa la Iran. Amesema tukio la tarehe 7 Tir 1366, mashambulizi ya mabomu ya kemikali katika eneo la Sardasht hapa nchini hapo tarehe 7 Tir 1366, mauaji ya kigaidi dhidi ya Shahid Saduqi tarehe 11 Tir 1361 na kutunguliwa ndege ya abiria ya Iran hapo tarehe 12 Tir 1367 ni mifano ya hatua za kigaidi za Marekaani na vibaraka wake. Ameongeza kuwa baadhi ya watu wanaamini kwamba, siku hizi za mwezi wa Tir zinapasa kupewa jina la “Wiki ya Haki za Binadamu za Kimarekani”.

Ayatullah Ali Khamenei ametilia mkazo tena udharura wa kumtambua adui na akasema: Taifa la Iran linapaswa kutambua kwa undani uadui wa adui wake kwa ajili ya kujitayarisha kukabiliana naye katika medani za vita laini ikiwa ni pamoja na kukabiliana naye katika medani za utamaduni, siasa na masuala ya kijamii.

Amewakosoa watu wanaofanya jitihada za kutetea sura ya kikatili, ya kutisha na mbaya ya Marekani na akasema: Wale wanaofanya jitihada za kufunika uadui habithi wa Marekani na baadhi ya vibaraka wake kwa kutumia propaganda na vyombo vya habari kwa hakika wanalisaliti taifa na nchi ya Iran.

Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema taifa la Iran linahitaji ujumbe unaotia matumaini, unaofichua na uliojaa furaha ya mashahidi. Ameongeza kuwa, Taifa la Iran ni mdaiwa wa mashahidi na familia zao, na wale wanaokana ukweli huo hawajui maslahi ya taifa, bali kwa hakika ni watu ajnabi na wageni licha ya kuwa na vitambulisho vya Kiirani.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islamu Walmuslimin Shahidi Mahallati ambaye ni mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika Taasisi ya Shahidi na Masuala ya Walemavu wa Vita amewakumbuka mashahidi wa tarehe 7 Tir na akasema: Kumbukumbu ya mashahidi hawa itabakia milele hapa nchini licha ya matakwa ya maadui wa Uislamu na Mapinduzi.

Naibu Rais wa Jamhuri na Mkuu wa Taasisi ya Shahidi ameongeza kuwa, historia ya Mapinduzi ya Kiislamu imethibitisha kwamba tukio la tarehe 7 Tir, matukio mengine mfano wake na mauaji ya kigaidi dhidi ya maelfu ya wasaidizi bora wa Mapinduzi ya Kiislamu si tu kwamba hayakuwa sababu ya kudhoofika bali pia yalikuwa wenzo wa istiqama, kusimama kidete na uthabiti wa taifa la Iran.     

   

 

700 /