Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Ni muhimu sana kwa chombo cha mahakama kuwa huru na kutokubali kuathiriwa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri la leo amekutana na mkuu na maafisa wa Idara ya Vyombo vya Mahakama ambapo amemsifu shahidi madhlumu Muhammad Beheshti na shahidi Quddusi, mashahidi wawili wakubwa wa idara hiyo hapa nchini. Amesema: Kuwa huru na kutokubali kuathiriwa chombo hicho ni suala lenye umuhimu mkubwa na kuongeza kuwa, kuna ulazima wa kukabiliana na mambo yanayotia dosari uhuru wa mahakama ikiwa ni pamoja na vitisho, vishawishi, kuona haya na mashinikizo ya anga ya umma na kuwa na mwenendo na mbinu sahihi za kimahakama.

Amekutaja kuwa na nguvu kuwa ni miongoni mwa sababu za kuwa huru Idara ya Vyombo vya Mahakama na kuongeza kuwa: Kuwa na nguvu kwa chombo hicho si kutaka kuwa na nguvu za kisiasa na kimakundi, bali kuna maana ya kuwa imara na kusimama kidete katika kutetea haki.

Kuzingatia sheria na usafi kamili wa Idara ya Vyombo vya Mahakama ni mambo mengine mawili ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja kuwa ni muhimu kwa aliji ya kuwa huru vyombo vya mahakama. Ameongeza kuwa, kuhusu usafi wa vyombo vya mahakama kumefanyika kazi nzuri na njia hiyo inapaswa kudumishwa kwa bidii, kwa sababu ufisadi wa aina yoyote katika vyombo vya mahakama utatayarisha uwanja wa kujitokeza ufisadi mkubwa zaidi katika jamii.

Ayatullah Ali Khamenei amekutaja kuzuia jinai kuwa ni miongoni mwa masuala nyeti na muhimu ya Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini. Ameongeza kuwa, taasisi na asasi nyingine pia zinapaswa kuchukua hatua katika uwanja huo, lakini kuna ulazima kufanyika jitihada zenye mpangilio na ratiba katika sekta hiyo, la sivyo jinai zitaongezeka na kuenea zaidi na haitawezekana kuzidhibiti.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa suala la kuongezeka idadi ya wafungwa linasikitisha. Ameongeza kuwa: Suala hilo linasababisha matatizo katika pande mbalimbali za kifedha, kifamilia, kiakhlaki na kijamii na kuna ulazima wa kufikiria vilivyo tiba yake kwa kuzingatia njia mbalimbali za ufumbuzi.

Katika uwanja huo huo Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kueneza utamaduni na ada ya kufanya suhulu na mapatano katika jamii na kuimarisha mabaraza ya kutatua hitilafu kuna taathira kubwa katika kuzuia ongezeko la idadi ya wafungwa. Ameongeza kuwa, kuna ulazima wa kutafutwa mapendekezo na njia mpya za utatuzi ili kuweza kukabiliana na athari mbaya za ongezeko la idadi ya watu wanaofungwa jela kutokana na matatizo ya kifedha na wale wa dawa za kulevya hapa nchini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo udharura wa kurahisisha ndoa baina ya vijana na akaashiria baadhi ya matatizo ya mahakama za familia ikiwa ni pamoja na ‘talaka ya kuafikiana’. Amesema waheshimiwa majaji wanapaswa kupunguza masuala kama haya kwa msaada wa wakuu wa familia.

Kufanya kazi kwa ratiba na mpangilio, kurekebisha sheria na kutayarisha majaji hodari ni masuala matatu muhimu yaliyousiwa na Kiongozi Muadhamu katika hotuba yake ya leo.

Ayatullah Khamenei ametilia mkazo udharura wa kufanya kazi kwa ratiba na mpangilia katika vyombo vya mahakama na akasema: Kutegemea ratiba ya wazi na iliyoandikwa kunasaidia harakati makini katika njia ya mustakbali na kuzuia mkwamo katika shughuli za kila siku.

Kuhusu suala la kufanyia marekebisho sheria na kanuni, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa sheria zinatayarisha njia nzuri ya maendeleo ya nchi, na kama kuna sheria na kanuni zenye dosari au zinazogongana basi zinapaswa kurekebishwa. Amesisitiza kuwa yeye binafsi hakubali suala la kukwepa sheria.

Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kutayarisha nguvu kazi kuwa lina umuhimu mkubwa na kusema: Kuna nguvu kazi hodari na safi katika Idara ya Vyombo vya Mahakama na kuna udharura wa kulea na kutayarisha vizuri nguvu hiyo kwa ajili ya kazi kubwa.

Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei ametoa pongeza kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini na akawakumbuka kwa kheri mashahidi Beheshti na Quddusi. Ameashiria mchango wa shakhsia kubwa ya shahidi Ayatullah Beheshti katika kipindi cha mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu na wakati wa kuendesha masuala ya nchi baada ya mapinduzi na akasema: Ayatullah Beheshti alikuwa miongoni mwa watu wa kipekee katika zama hizi, shakhsia yenye mvuto, mudiri hodari na mwanamapinduzi ambaye maisha yake yalikuwa na faida na taathira kwa Mapinduzi ya Kiislamu na Iran. Amesema kuuliwa kwake shahidi kulileta umoja na mshikamano wa jamii na kuimarisha harakati ya mapinduzi.

Vilevile amemtaja shahidi Quddusi (mwendesha mashtaka wa kwanza baada ya Mapinduzi) kuwa alikuwa shakhsia yenye moyo laini na wakati huo huo shujaa na mtu asiyetetereka.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza harakati, azma kubwa na uendeshaji wa kijihadi wa Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini katika kutekeleza majukumu yake. Amesema idara hiyo ni moja kati ya mihimili mikuu ya nchi na mtekelezaji wa sehemu muhimu ya sheria za Kiislamu; hivyo basi ni mahala pake kuwa na matarajio ya kushuhudia jitihada, bidii na kustahamili mashaka katika idara hiyo.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini Ayatullah Amoli Larijani amepongeza shughuli ya kuwakumbuka mashahidi wa tukio la tarehe 7 Tir hususan Ayatullah Dakta Beheshti na akawasilisha ripoti ya hatua na mipango ya idara hiyo.

Ayatullah Larijani ameashiria suala la kuzidishwa usimamizi wa kazi na utendaji wa majaji na wafanyakazi wa mahakama na akasema kuwa taasisi zote za idara hiyo zimo mbioni kuzidisha usafi na usalama wa kiidara.

 

 

700 /