Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Vyombo vya kipropaganda vya mfumo wa ubeberu vinanyamazia kimya jinai zinazofanywa dhidi ya watu wa Yemen

Wadau wa masuala ya utamaduni, magwiji wa mashairi na fasihi ya Kifarsi, washairi vijana na wakongwe wa taaluma hiyo hapa nchini na washairi kutoka nchi za India, Pakistan, Afghanistan, Tajikistan na Azerbaijan wamekutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei katika usiku wa kukumbuka tukio la kuzaliwa Karimu wa Ahlul Bait, Imam Hassan al Mujtaba (as).
Katika mkutano huo Ayatullah Khamenei amewapongeza Waislamu kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib (as) na akasema, mashairi yana taathira kubwa katika kutayarisha uwanja mzuri wa mshairi kubeba majukumu mazito. Amesisitiza udharura wa mashairi kutetea waziwazi kambi ya haki mkabala wa kambi ya batili na udhibiti wa vyombo vyake vya propaganda duniani na akasema: Mashairi ya mapinduzi ni mashairi ambayo yako katika upande huo na yanayohudumia malengo ya mapinduzi, yaani uadilifu, ubinadamu, umoja, hadhi ya kitaifa, maendeleo ya pande zote ya nchi na yanayomjenga mwanadamu.
Ayatullah Khamenei ameashiria kwamba, yumkini wenzo wenye taathira kubwa wa mashairi ukatumiwa katika pande zote mbili za kumwelekeza msikilizaji wake upande wa uongofu au kumtumbukiza katika upotofu na akasema: Hii leo na kutokana na kupanuka nyenzo za kisasa za vyombo vya habari, kuna baadhi ya mikono inayotaka kupotosha mashairi ya vijana na kuyatoa katika anga safi ya hisia za hamasa na za kimapinduzi na kuyatumia katika kuhudumia utamaduni uliochupa mipaka, uliombali na ubinadamu na ulioathirika na matamanio ya kingono, maslahi ya kibinafsi na kusifu dhulma.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza kusimama kidete kwa baadhi ya washairi vijana mbele ya anga hiyo yenye sumu na akasema: Kusimama huko imara ni alama ya kutambua wajibu na hii leo kila shairi linalosemwa dhidi ya dhulma na katika kutetea malengo ya Umma wa Kiislamu kama kuhusu Yemen, Bahrain, Lebanon, Ghaza, Palestina na Syria ni kielelezo cha mashairi yenye hikima.
Katika uwanja huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, wito unaomtaka mshairi kutosimama upande wowote katika mpambano baina ya haki na batili hauna maana na kuongeza kuwa: Iwapo mshairi na msanii hatakuwa na upande wowote wakati wa vita vya haki na batili basi kivitendo atakuwa amepoteza kipawa na neema aliyotunukiwa na Mwenyezi Mungu, na kama atasimama katika upande unaohudumia kambi ya batili basi atakuwa amefanya hiana na usaliti.
Ayatullah Khamenei ameashiria kumbukumbu ya tukio la kushambuliwa eneo la Sardasht (kaskazini magharibi mwa Iran) kwa mabomu ya kemikali na akasema kuwa: Dhulma nyingi zilizofanywa dhidi ya taifa la Iran ni mfano muhimu na wa kutisha unaoweza kuakisiwa duniani kwa kutumia lugha ya mashairi. Amesema kuwa vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na Marekani, Uingereza na uzayuni ambavyo wakati mwingine huzusha makelele mengi ya kipropaganda kwa ajili ya kutaka kuokoa maisha ya mnyama, vimenyamaza kimya kifidhuli mbele ya jinai hizo na mfano wake, kama mashambulizi ya mabomu yanayofanywa katika siku hizi dhidi ya Yemen na hujuma za miaka iliyopita dhidi ya Ghaza na Lebanon.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewauliza washairi kwamba, mwanadamu mwenye sharafu anapaswa kufanya nini mbele ya mpambano na uhabithi kama huo?
Ametaja radiamali na jibu la haraka la washairi vijana kwa matukio mbalimbali kuwa ni jambo zuri sana na lenye thamani. Amesema: Tuna matarajio kwamba mashairi ya mapinduzi ambayo kwa hakika yanahudumia malengo na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu yaani uadilifu, ubinadamu, umoja, heshima ya kitaifa, maendeleo ya pande zote ya nchi na yenye kumjenga mwanadamu, yatapanda daraja na kustawi zaidi siku baada ya siku.
Ayatullah Ali Khamenei ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya wazi ya mashairi hapa nchini katika kipindi cha baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa, uwezo wa mashairi wa Iran kwa kutilia maanani historia yake inayong’ara na nukta zake adhimu za kihistoria, ni mkubwa zaidi ya hali ya sasa. Ameongeza kuwa taasisi husika kama asasi za serikali, kitengo cha sanaa na Shirika la Utangazaji la Iran (IRIB) vinapaswa kutekeleza majukumu yao katika uwanja huu.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka watu wote kufaidika na baraka za mwezi wa Ramadhani na kuondoa uchafu katika nyoyo zao kwa kumnyenyekea na kumtaradhia Mwenyezi Mungu na kutafakari kwa kina katika dua za mwezi wa Ramadhani.
Mwanzoni mwa mkutano huo zaidi ya washairi 20 walisoma mashairi yao mbele ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.   

 
700 /