Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Lengo la vikwazo ni kulizuia taifa la Iran lisifike kwenye nafasi yake stahiki

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo (Jumamosi) amekutana na maelfu ya wahadhiri na wanachama wa jumuiya za kielimu za vyuo vikuu kutoka nchini kote. Katika hadhara hiyo Ayatullah Khamenei amesema kuwa walimu wana nafasi isiyo na mbadala katika kufunza na kulea kizazi chenye bidii, imani na maendeleo. Amesisitiza umuhimu wa kujiepusha na michezo ya kisiasa katika mazingira ya kielimu na kusema: Kasi ya kielimu hapa nchini haipaswi kupungua kwa sababu yoyote ile.
Katika mkutano huo ulioendelea kwa kipindi cha zaidi ya masaa mawili, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema baada ya kusikiliza mitazamo na mapendekezo ya idadi kadhaa ya walimu wa vyuo vikuu kwamba, ushawishi na taathira ya walimu katika nyoyo na roho za wanafunzi ni fursa ya kipekee na kuongeza kuwa: Tumieni wenzo huo mkubwa sana kwa ajili ya kulea vijana wenye kushikamana na dini, wenye ghera ya kitaifa, ari, wanamapinduzi, wenye kijituma, wenye maadili, mashujaa na wenye kujiamini na wenye matumaini na mustakbali na leeni na kufundisha watu imara na wenye nguvu kwa ajili ya maendeleo ya Iran azizi .
Amekutaja kutowahitajia wageni , kujua vyema nafasi na mwelekeo wa nchi, na kusimama imara dhidi ya jambo lolote linaloharibu uhuru na kujitawala nchi kuwa ni miongoni mwa sifa makhsusi za lazima za kizazi cha vijana. Ameongeza kuwa: Waheshimiwa wahadhiri wanapaswa kulea kizazi kama hicho kwa kutumia mbinu zao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataja wahadhiri wa vyuo vikuu kuwa ni makamanda wa vita laini na kuwaambia:  Kama walivyokuwa makamanda wa jeshi katika vita vya miaka minane vya kujitetea kutakatifu, shirikini nyinyi wenyewe katika mapambano haya muhimu sana na makubwa na waongozeni wanachuo vijana mbao ni askari katika vita laini; na medani hii pia ni medani ya kujitetea kutakatifu.
Ameeleza kufurahishwa kwake na kuwepo wajumbe elfu 70 wa kamati za kielimu katika vyuo vikuu na akasema: Sehemu kubwa ya wahadhiri hawa ni watu wenye imani, wanaoshikamana na dini na wanaoamini misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu na suala hili muhimu ni fahari kwa nchi hii.
Ayatullah Khamenei amewataka viongozi wa Wizara za Sayansi, Uhakiki na Teknolojia na Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Udaktari kuwathamini na kuwakirimu wahadhiri wenye imani na wanamapinduzi na kusema: Watu wasioogopa hujuma za propaganda zenye maudhi na zinazofanyika mara nyingi kwa siri na wanaendelea kutekeleza majukumu yao muhimu wanapaswa kuzingatiwa na kuenziwa.
Amesema kuwa Iran kupata nafasi ya 16 ya kielimu duniani ni matokeo ya juhudi zisizosimama za miaka 10 hadi 15 iliyopita katika vyuo vikuu na vituo vya elimu. Ameongeza kuwa: Kasi ya elimu iliyotia shauku kubwa ambayo ndiyo iliyoipatia Iran fahari hiyo, imepungua na maafisa wanapaswa kufanya hima na juhudi kubwa zaidi ili harakati ya maendeleo ya kielimu hapa nchini isibakie nyuma na iende kwa kasi kulingana na mahitaji ya nchi.
Akizungumzia kwa nmna moja au nyingine sababu za kupungua kasi ya maendeleo ya kielimu hapa nchini, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa vikali tabia ya kujishughulisha  na masuala ya pembeni na michezo ya kisiasa katika mazingira ya elimu na kusema kuwa, mazingira ya vyuo vikuu yanapaswa kuwa mazingira ya uelewa wa siasa, maarifa na kujua siasa lakini michezo ya kisiasa na kujishughulisha na masuala ya pembeni vinatoa pigo kubwa kwa kazi asili za vyuo vikuu yaani juhudi na maendeleo ya kielimu.
Akitoa mfano wa kielelezo cha michezo ya kisiasa katika vyuo vikuu, Ayatullah Khamenei ameashiria makelele yaliyozushwa kuhusu udhamini wa nafasi za masomo (scholarships) na kutaja kitendo hicho kuwa ni miongoni mwa makosa makubwa yaliyofanywa katika miaka ya hivi karibuni.
Ayatullah Khamenei amesema uchunguzi makini unaonesha kuwa, suala la udhamini wa nafasi za masomo halikuwa kama ilivyochezewa katika magazeti,  na kama lilikuwepo basi ilibidi fursa zilizotolewa kwa baadhi ya watu kinyume cha sheria zifutwe kupitia njia za kisheria, na si kuzusha makelele.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, michezo ya kisiasa ni sumu ya mazingira ya elimu. Ameeleza kusikitishwa na kwamba katika maudhui hii ya udhamini wa nafasi za masomo kumefanyika dhulma dhidi ya baadhi ya watu na kuongeza kuwa, sumu iliyomwagwa katika vyuo vikuu katika maudhui hii imetokana na fikra za michezo ya kisiasa, na inasikitisha kuwa suala hilo ni kinyume na sheria, tadbiri na maadili.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Ayatullah Khamenei ametilia mkazo udharura wa viongozi kufanyika jitihada kubwa za mageuzi katika sayansi za jamii .
Amesema mageuzi hayo ya dharura yanahitaji harakati ya ndani katika vyuo vikuu na vituo kama Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni na Baraza la Mageuzi ya Sayansi za Jamii na pia yanahitaji himaya kutoka nje ya taasisi husika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kwa baraka za Mwenyezi Mungu, harakati ya ndani ipo na kuna ulazima kwa taasisi husika kufanyia kazi juhudi za kinadharia zilizofanyika katika uwanja wa mageuzi kwenye sayansi za jamii na kutimiza maazimio ya Baraza la Mageuzi katika Sayansi za Jamii.
Suala la nne lililozungumziwa katika hotuba ya Kiongozi Muadhamu ni kuzingatiwa sehemu ya utafiti katika bajeti ya taifa.
Ameashiria sisitizo lake la mara kwa mara katika miaka iliyopita katika uwanja huo na kueleza masikitiko yake kutokana na kutotimizwa sehemu iliyokusudiwa ya bajeti ya utafiti. Ameongeza kuwa: Katika hati ya maendeleo ya Iran katika kipindi cha miaka 20 ijayo kumetengwa asilimia 4 katika bajeti ya taifa kwa ajili ya utafiti wa kielimu, suala ambalo haliwezi kutimia katika kipindi kifupi, lakini kuna ulazima wa karibu asilimia 2 ya bajeti ya utafiti kutolewa katika bajeti ya taifa. Ameongeza kuwa bajeti hiyo na vyanzo vya fedha vya sehemu ya utafiti wa kielimu vinapaswa kutumiwa vyema na mahala pake.
Nukta nyingine iliyoelezwa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa maafisa wa elimu na wahadhiri wa vyuo vikuu ni udharura wa kufanyiwa kazi ramani kamili ya elimu hapa nchini.
Ayatullah Khamenei amesema ramani pana ya elimu hapa nchini imepasishwa na wataalamu na kuongeza kuwa, hatua ya kwanza ya kufanyiwa kazi hati hiyo muhimu ni kujadiliwa kwake. Amesema kuwa, kama ambavyo mjadala wa maendeleo ya kielimu yamekuwa suala linalojadiliwa kote nchini na kuwa mwenendo wa kielimu, kuna ulazima pia wahadhiri, wakurugenzi na wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini wakajua vyema ramani pana ya elimu na hati hiyo muhimu ifanyiwe mjadala unaokubalika.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia hati ya maandalizi ya elimu ya juu. Ameashiria ulazima wa kukamilishwa na kufanyiwa kazi hati hiyo na kusema: Matayarisho ya kielimu nchini yana maana ya kutambua na kuchukua maamuzi kuhusu uwezo wa vyuo vikuu na mitaala ya masomo na kisha kuainisha vipaumbele ambavyo kuna uwezekano wa kuweka vitega uchumi makhsusi kwa ajili ya maendeleo yake ya kimsingi.
Ayatullah Khamenei amesema, kuwa na mtazamo mpana kuhusu suala la ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu katika masomo ya juu ni faida ya kipekee na miongoni mwa nyanja zinazopaswa kushughulikiwa na Wizara ya Sayansi. Ameongeza kuwa, kwa mtazamo mpana, mipango na ratiba sahihi na mwongozo jumla, Wizara ya Sayansi inapaswa kuelekeza jitihada za wanafunzi wa vyuo vikuu katika elimu ya juu upande wa kutatua matatizo ya nchi, la sivyo rasilimali na uwezo wa nchi utapotea bure. 
Ameitaja nafasi ya wahadhiri wa vyuo vikuu na taasisi za uongozi wa kielimu nchini katika kukabiliana na njama za maadui kuwa ni muhimu na kuongeza kuwa: Lengo la vikwazo vya maadui (dhidi ya Iran) si suala la nyuklia wala masuala kama haki za binadamu na ugaidi, kwa sababu wao wenyewe ndiyo vituo vikuu vya kulea ugaidi na dhidi ya binadamu; bali lengo lao ni kulizuia taifa la Iran kufika kwenye nafasi linayostahiki ya ustaarabu. Amesisitiza kuwa, kuna udharura wa kudumisha harakati yenye fahari kubwa ya nchi hii kwa kutambua vyema nafasi yetu, na katika mkondo huo wahadhiri wa vyuo vikuu na vituo vya elimu wana mchango na nafasi kubwa sana.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu, wahadhiri saba wa vyuo vikuu hapa nchini walieleza mitazamo na maoni yao kuhusu masuala mbalimbali ya vyuo vikuu na harakati ya elimu na sayansi hapa nchini.                

 

 
700 /