Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Mapambano dhidi ya ubeberu hayatasimama

Katika mkutano huo ambao umeanza saa 12 jioni kwa saa za Tehran na kuendelea baada ya Swala na futari, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza masikitiko yake kwa kuona siku za mwezi mtukufu wa Ramadhani zinamalizika na kuongeza kuwa: Mtu yeyote anayeuunganisha moyo wake na msimu wa machipuo ya kimaanawi na unyofu na kuruhusu athari za mvua ya rehema na neema za Mwenyezi Mungu ziusafishe moyo wake, bila ya shaka yoyote atanufaika na matunda ya mmea huo unaong'ara wa kimaanawi anaoupanda kwenye msimu huu wa neema (mwezi mtukufu wa Ramadhani).
Akijibu swali la mara kwa mara la vijana kuhusiana na njia za kuweza kukwea daraja za juu za kiroho, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Nimesikia kutoka kwa watu wakubwa kwamba jambo muhimu zaidi la kufanya kwa ajili ya kujiimarisha kiroho na kimaanawi ni kujipamba kwa taqwa na kujiepushe na maasi.
Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kutekeleza faradhi za dini hususan kusali Swala mwanzo mwa wakati wake, kwa unyenyekevu na kuuhudhurisha moyo na kuhakikisha mtu anasali Swala za jamaa kwa kadiri anavyoweza, kuwa kunakamilisha suala la kujiepusha na maasi na kuongeza kuwa: Inawirisheni majimui hiyo yenye thamani kubwa kwa kuhakikisha kuwa, kila siku mnasoma aya japo chache za Qur'ani Tukufu.
Baada ya kusisitizia wajibu wa kutekeleza ipasavyo faradhi za kidini, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza kuzungumzia majukumu na mambo ya wajibu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini. Amelitaja tabaka la wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran kuwa ni tabaka bora na kusisitiza kuwa, jukumu kubwa zaidi la wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ni kulinda msimamo wao wa kupigania malengo matakatifu.
Ayatullah Khamenei ameipinga fikra inayosema kuwa, kupingania malengo matakatifu kunakinzana na suala zima la kuangalia mambo katika uhalisia wake na kusisitiza kuwa: Kupigania ufanikishaji wa malengo matakatifu ni kinyume na fikra ya uhafidhina na si kinyume na kuangalia mambo katika uhalisia wake.
Ametoa ufafanuzi zaidi akisema, maana ya uhafidhina ni kusalimu amri mbele ya kila ukweli wa mambo na kuongeza kuwa, kupigania malengo matakatifu kuna maana ya kutumia kwa njia sahihi kila tukio chanya na kusimama imara kukabiliana na kila tukio hasi katika jitihada za kufikia kwenye lengo kubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kujenga jamii ya Kiislamu na kuhuisha fikra ya Uislamu wa kisiasa kuwa ni katika malengo muhimu zaidi matukufu na kuongeza kwamba: Kuwa na malengo matakatifu kumelizawadia taifa la Iran sifa ya kujiamini na kushikamana na itikadi yake ya kwamba "tunaweza" na kumetoa mchango mkubwa katika jitihada za kuistawisha jamii na nchi.
Kupamba na mfumo wa kibeberu na wa kiistikbari ni lengo la tatu tukufu lililogusiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Sababu kuu inayoyapelekea madola ya kibeberu yalifanyie uadui taifa la Iran, ni upinzani wa Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya mfumo uliosimama kwenye misingi ya kibeberu na kiistikbari.
Vilevile ameyataja masuala ya kupigania uadilifu, kupigania mtindo wa Kiislamu wa maisha, kupigania uhuru wa kweli na sio wa Kimagharibi, ustawi wa kielimu, uchapaji kazi na kujituma pamoja na kujiweka mbali na uvivu na ugoigoi na kuvifanya vyuo vikuu kuwa na sura ya Kiislamu, kuwa ni miongoni mwa malengo matakatifu ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele na jumuiya za wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa majibu ya dukuduku na wasiwasi wa kiistratijia wa wanachuo wanaopenda kujua ni vipi inawezekana kuathiri maamuzi ya viongozi nchini kupitia fikra ya kulinda na kupigania malengo matakatifu?
Majibu ya Kiongozi Muadhamu kwa swali hilo muhimu yalikuwa ya wazi na yenye msisitizo mkubwa. Amesema, yakaririni mara kwa mara malengo matakatifu, simameni imara kuyatetea malengo hayo bila ya kutetereka hadi yawe fikra iliyoenea na kukita mizizi baina ya wanachuo na baadaye baina ya watu wote nchini, wakati huo viongozi na vyombo vya kiserikali vitaathirika na kuzidi kuchukua maamuzi kwa kuzingatia malengo hayo matakatifu.
Baada ya kubainisha njia za kuweza jamii ya wanachuo kuathiri misimamo ya taasisi tofauti nchini, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia mambo ya lazima yanayopaswa kuzingatiwa, kufanyiwa kazi na kupewa umuhimu mkubwa na jumuiya hizo za wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran.
Amelitaja suala la kujiepusha na mitazamo finyu na kufanyia kazi kwa kina mafundisho ya Uislamu kuwa ni jambo la kwanza la lazima ambalo jumuiya za wanachuo nchini zinapaswa kulizingatia na kulifanyia kazi.
Ayatullah Khamenei amekosoa pia baadhi ya nara na kaulimbiu pamoja na matamshi yanayotolewa kuhusu suala hilo ambayo kidhahiri na kijuujuu yanaonekana kuwa ni ya Kiislamu, lakini ndani yake ni kitu kingine kabisa. Ametolea mfano wa wazi suala hilo akisema kuwa ni istilahi ya Uislamu wa rehema iliyoenea hivi sasa na kusisitiza kwamba, istilahi hiyo imeundwa na maneno mawili mazuri sana ya "Uislamu" na "rehema," lakini je tumewahi kujiuliza maana ya istilahi hiyo ni nini? Je maana yake si kwenda kinyume na mafundisho ya Qur'ani Tukufu yanayomgawa mwanadamu baina ya muumini na kafiri, adui na rafiki? Je, kwa istilahi hiyo wanataka kuwaangalia watu wote kwa jicho la rehema? Je wale watu ambao wanaufanyia uadui Uislamu na taifa la Iran, wote waangaliwe kwa jicho la rehema, mapenzi na kutokuwa wazito kwao, tofauti na mafundisho ya Mwenyezi Mungu?
Amesema mambo kama hayo inabidi yazingatiwe na kuangaliwa kwa kina, na yasiangaliwe kwa mtazamo finyu na wa juu juu kwani kufanya hivyo ni makosa na ni kupotea njia. Ameongeza kuwa: Je, istilahi ya Uislamu wa rehema haitokani na fikra ya kiliberali ya Magharibi? Kama itakuwa hivyo, basi istilahi hivyo si ya Uislamu na wala hiyo si rehema na upole kwani msingi wa mtazamo wa kiliberali ni fikra ya "Humanism" inayopingana na mafundisho ya Mwenyezi Mungu na masuala ya kiroho na kimaanawi na iliyojengeka kwenye kulinda na kupigania manufaa ya makundi yenye nguvu na ushawishi.
Ayatullah Khamenei ameendelea kujadili suala hilo kwa kukosoa masuala ambayo yameanzishwa na kupewa majina kwa kuzingatia thamani za Kimarekani na kuongeza kuwa: Wizi na uporaji wa mfumo wa kiistikabari unatokana na thamani hizo hizo za Kimarekani kama ambavyo nukta nzuri kwenye thamani hizo nazo zimetupwa kwenye lindi la kusahuliwa kutokana na vitendo vya kibeberu na kiistikbari vya viongozi wa Marekani.
Amesema, kama Uislamu wa rehema unakusudia mambo kama hayo, basi bila ya shaka yoyote istilahi hiyo ni malosa mia kwa mia na haina mfungamano wowote na Uislamu halisi.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza kuzungumzia jambo jengine la lazima la kuzifanya jumuiya za wanafunzi wa vyuo vikuu kuwa na taathira na kuongeza mvuto wao.
Amepinga kikamilifu kutumiwa njia zisizo sahihi kama vile kuwekwa kambi zinazowachanganya pamoja wanachuo wa kike na kiume na matamasha ya miziki kwa ajili ya kuzidisha mvuto wa wanachuo na kusisitiza kuwa, watu wanaowatumia wanachuo wa kike na kiume kwa ajili ya kuvutia watu wengine kwa kutumia njia mbalimbali zisizo sahihi kama vile kuweka kambi zinazowachanganya pamoja wanachuo barani Ulaya kwa mfano, wajue vyema kuwa wanayasaliti mazingira ya vyuo vikuu nchini bali wanakisaliti kizazi cha baadaye cha Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja njia sahihi za kuweza kuongeza nguvu za mvuto za jumuiya za wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kwa kugusia suala la kutoa fikra mpya za kidini, kisiasa na kijamii na kuongeza kuwa: Kuifanyia utafiti wa kina Qur'ani Tukufu na Nahjul Balagha, ndiko kunakomuwezesha mtu kuja na maneno na fikra mpya na zenye mvuto. Kutumia mbinu nzuri za kisanii kama vile tamthilia za wanachuo, vibonzo, vichekezo, athari za sauti, matamasha ya kusoma mashairi na mbinu nyinginezo kama hizo, ni njia nyengine zilizotajwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu suala hilo.
Baada ya hapo, Ayatullah Khamenei amebainisha jambo la tatu la lazima kwa ajili ya kuweza jumuiya za wanafunzi wa vyuo vikuu kuwa na mvuto mkubwa zaidi, kwamba ni pamoja na kukinaisha watu kifikra na kujiepusha kutumia nguvu na kutwisha mambo akisisitiza kuwa: Fikra za kidini haziwezi kusambazwa kwa watu wengine isipokuwa kwa njia ya kuwakinaisha watu hao kwa hoja. Ameongeza kuwa yumkini inawezekana baadhi ya fikra za dini zikakubaliwa kutokana na jazba na hamasa bila ya kukinai kifikra, lakini imani kama hiyo haidumu kutokana na kutokinaika kifikra.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia historia ya makundi ya Kimaksi na Kikomunisti ya kutumia mbinu zisizo za kukinaisha watu bali za kutwisha na kupandikiza fikra zao na kuongeza kuwa: Kama taarifa zinazosema kuwa, fikra za Kimaksi zimeanza kujijenga upya katika baadhi ya vyuo vikuu zitakuwa za kweli, basi bila ya shaka yoyote fedha za Wamarekani zitakuwa ndizo zinazosaidia mrengo huo kwa lengo la kuwachanganya na kuwaparaganya wanachuo.
Ayatullah Khamenei ametoa nasaha za kutumiwa wahadhiri wanaojali thamani katika vyuo vikuu na kujiepusha kutumia watu wasioaminika kwa mfumo wa Kiislamu, nchi na kwa wananchi na kuziambia jumuiya za wanafunzi wa vyuo vikuu kwamba: Watu kama wale waliozusha matukio ya mwaka 2009 na kuipinga wazi wazi sifa ya Uislamu na Jamhuri ya mfumo unaotawala nchini Iran si watu wa kuaminika hata kidogo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la udharura wa kuyafahamu na kuyaelewa vizuri matukio ya Iran kuwa ni jambo jengine la lazima la kuweza jumuiya za wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuyatumia kwa ajili ya kuongeza nguvu zao za mvuto na taathira zao. Ameongeza kwamba: Kuwa na matarajio ya kuwaona viongozi nchini wanafanya kazi kwa bidii kubwa na kujituma zaidi ni jambo zuri lakini wakati huo huo inabidi pia kuzingatiwe uhalisia wa mambo ulivyo na kutazama mambo kwa mtazamo chanya.
Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kuzidi kuwa makubwa malengo matukufu na kushindwa njama za baadhi ya watu za kujaribu kusahaulisha na kuyaweka pembeni malengo matakatifu ya Imam Khomenini -Mwenyezi Mungu amrehemu - kwamba ni katika matukio yanayopaswa kuzingatiwa sana nchini.
Amekumbusha kuwa, baada ya kufariki dunia Imam Khomeini – Mwenyezi  Mungu amrehemu - kuna baadhi ya watu, kutokana na fikra zao zisizo sahihi waliweka wazi malengo yao ya siri ya kutaka kuweka kando malengo makubwa ya Imam lakini hivi sasa kwa sababu ya kukomaa, hawatangazi tena hadharani malengo yao hayo, lakini wanaendelea na njama zao za kuyafanikisha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Licha ya kuweko njama zisizosita za kundi la watu hao ndani na nje ya Iran lakini nishati na uhai wa thamani umestawi zaidi hapa nchini kutokana na kutumia mbinu za kifikra, kisiasa na kisanii, na vijana ambao hawakuwepo wala kuyaona matukio ya kuvutia ya kipindi cha Imam Khomeini na vita vya kujihami kutakatifu, wamevutwa na kuathiriwakikamilifu na thamani za Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu kwa dhati.
Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kuweko ushawishi wa kustaajaribisha wa kimaanawi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati kuwa ni uhakika mwingine ambao jumuiya za wanachuo nchini zinapaswa kuutilia maanani.
Ameongeza kuwa: Tuna taarifa kuwa Wamarekani na vibaraka wao katika eneo hili wanajadiliana kwa huzuni kubwa katika vikao vyao vya siri kuhusu ushawishi wa Iran, lakini hawawezi kufanya lolote kuzuia ushawishi huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mashambulizi ya zaidi ya siku mia moja sasa huko nchini Yemen na kuendelea kuuliwa kinyama watu wasio na hatia na madhulumu wa nchi hiyo na kuongeza kuwa: Mfumo wa kiliberali wa Magharibi unaodai kupigania uhuru, haufungui hata kinywa kukemea jinai hizo za Wasaudia, na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo limetoa moja ya maazimio yake maovu kabisa ambalo badala ya kuwalaani wanaopiga watu mabomu, limelaani watu wanaopigwa mabomu huko Yemen.
Amesema, sababu kuu ya kushambuliwa makazi ya raia na watu wasio na hatia huko Yemen ni hamaki na chuki za Wasaudia na waungaji mkono wao baada ya kuona wameshindwa kukabiliana na ushawishi wa Iran katika eneo hili na kuongeza kuwa: Kinyume kabisa na madai yanayotolewa na baadhi ya watu kuhusu sababu za ushawishi huo wa Tehran, ushawishi wa Iran ya Kiislamu katika eneo hili ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na si jambo lililotokana na kutumia nguvu, mabavu na silaha, na sisi kama ambavyo shahid Beheshti alivyokuwa akiwaambia maadui wa taifa hili, tunawaambia hivyo hivyo maadui kuwa kufeni na chuki na ghadhabu zenu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vilevile amezipa nasaha jumuiya za wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran kwamba ziyafanyie kazi masuala ya kieneo na kimataifa yakiwemo masuala ya Yemen, Iraq na Syria na kulitaja suala la kuundwa jumuiya za wanachuo kwa ajili ya kutumika wakati wa uchaguzi kuwa ni aina fulani ya kuidunisha na kuidhalilisha jamii ya wanachuo nchini. Ameongeza kwamba: Ukiweka mbali jumuiya kama hizo za kupita na za kutumiwa mara moja na baadaye kutupwa, jumuiya za Kiislamu zenye mapenzi na dini tukufu ya Kiislamu na uchungu na nchi zinaweza kuwa na faida na taathira kubwa katika harakati kuu ya taifa.
Katika sehemu ya kwanza ya hotuba yake baada ya kusikiliza maoni, dukuduku na mapendekezo ya wawakilishi 9 wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, Ayatullah Khamenei amegusia matamshi ya mmoja wa wanachuo hao kuhusu kutokuwa na faida kaulimbiu zisizoambatana na vitendo na kusema: Kaulimbiu zenye maama na madhumuni zinazoakisi hakika inayoweza kuenezwa, zinaweza kuwavutia watu katika medani ya mapambano na kutoa mwelekeo hamasa.
Kubanwa uundaji wa jumuiya za kimapinduzi za wanachuo ni jambo jengine lililolalamikiwa na mmoja wa wanafunzi waliozungungumza mbele ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na katika kujibu dukuduku hilo. Kiongozi Muadhamu amewaambia mawaziri wa Sayansi na Afya nchini kwamba: Matamshi ya jumuiya hizo za kimapinduzi na Kiislamu za wanachuo ndiyo maneno na matakwa yatu  na watu ambao wamepewa jukumu la kusimamia kazi muhimu katika vyuo vikuu hawapaswi kwa namna yoyote ile kuzuia kuundwa jumuiya kama hizo na wala kubana kazi na mazingira ya harakati za jumuiya hizo.
Ayatullah Khamenei vilevile amesema kuwa, ni dukuduku la mahala pake la wanachuo wanaolalamikia kuenezwa baadhi ya mambo yanayokwamisha maendeleo ya kielimu katika vyuo vikuu kama kufanya matamasha ya muziki na kusema: Mambo kama hayo yanayofanyika kwa madai ya kuleta uchangamfu katika mazingira ya wanachuo, ni miongoni mwa makosa makubwa kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuwatumbukiza vijana kwenye anga hizo zisizo salama kuwa ni katika mipango ya maadui wa taifa la Iran na kusisitiza kuwa: Watu walioko mstari wa mbele katika harakati iliyojaa fakhari ya kielimu nchini leo hii na hasa katika taaluma nyeti na muhimu kama teknolojia ya nyuklia na teknolojia ya nano, ni vijana waumini na wanamapinduzi na ndiyo maana maadui hawataki kuona vyuo vikuu nchini Iran vinalea watu waumini na wanamapinduzi kama vile Dk Shahriyar na Dk Chamran.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Mawaziri wote wawili wa Sayansi na wa Afya ni watu wa kuaminika, lakini inabidi wawe macho watu wa chini yao wasije wakawaweka mbali wanachuo na misimamo ya kimapinduzi na ya Kiislamu kupitia baadhi ya mambo na ratiba zenye makosa na zisizo sahihi.
Kuanzishwa jukwa na mijada huru ya kifikra kwa maana halisi ya neno hilo ni nukta nyengine iliyokuwemo kwenye matamshi ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Iran ambapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusiana na suala hilo kwamba: Mimi kwa upande wangu ninaunga mkono kikamilifu jambo kama hilo na inabidi kijana mwanachuo Muislamu, mwanamapinduzi na mfuasi wa "wilaya" aweze kubatilisha hoja za mpinzani kwa utulivu wa moyo na nguvu ya maantiki na hoja, na uwezo huo upo (hapa nchini).
Katika kujibu swali la mwanafunzi mwengine kuhusiana na matamshi yanayotolewa na baadhi ya wawakilishi na watu wanaonasibishwa kwa Kiongozi Muadhamu na kuenezwa misimamo ya watu hao kwa jina la mitazamo ya Kiongozi Muadhamu, Ayatullah Khamenei amesema: Matamshi ya watu hao ni matamshi yao binafsi na maneno yangu mimi yasikilizeni kutokwa kwangu.
Ameongeza kuwa: Watu wanaoteuliwa na Kiongozi Muadhamu wanaweza kuwa na misimamo tofauti na Kiongozi Muadhamu katika baadhi ya masuala ya kisiasa na kijamii na jambo hilo halina tatizo lolote kwani suala muhimu ni misimamo mikuu na ya kimapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kama atatokezea mtu akasema jambo ambalo ni kinyume na ukweli wa mambo, mtu huyo ataonywa na kutakiwa kurekebisha jambo hilo.
Hali ya mapambano dhidi ya ubeberu baada ya mazungumzo ya nyuklia lilikuwa ni swali jingine lililoulizwa na mmoja wa wanafunzi wa vyuo vikuu waliozungumza mbele ya Ayatullah Khamenei. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu swali hilo kwa kusisitiza kwamba: Mapambano dhidi ya ubeberu na dhidi ya mfumo wa kiistikbari ni jambo ambalo msingi wake ni Qur'ani Tukufu na si jambo la kuachwa wala kusimamishwa na kwamba leo hii Marekani ndiye nembo na dhihirisho kamili zaidi la ubeberu duniani.
Ameongeza kuwa: Tumewaambia pia maafisa wa (timu ya Iran ya) mazungumzo ya nyuklia kwamba, wana ruhusa ya kufanya mazungumzo kuhusu kadhia ya nyuklia tu na wakati Wamarekani wanapoingiza masuala ya kieneo kama vile Syria na Yemen kwenye mazungumzo hayo, maafisa wetu huwaeleza kuwa masuala hayo hayana uhusiano na kadhia ya nyuklia na wala hawazungumzii mambo hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kupambana na ubeberu ni moja ya misingi mikuu ya Mapinduzi ya Kiislamu na ni katika kazi za kimsingi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hivyo jiwekeni tayari kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya ubeberu.
Mmoja wa wanachuo amemuomba Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu awatake wazazi kuwepesesha suala la ndoa na kuoana vijana nchini. Ayatullah Udhma Khamenei ameitikia ombi hilo kwa kuwataka wazazi nchini kutofanya uzito katika suala la ndoa za watoto wao na kuongeza kuwa: Mwenyezi Mungu Mtukufu ametoa ahadi katika Qur'ani tukufu kwamba atawatajirisha vijana kwa fadhila Zake baada ya kuoana, na atawatatulia matatizo yao.
Amesema, desturi na ada ya kuchumbishia na kutumia washenga kwa ajili ya kurahisisha kuoana vijana ni ada nzuri. Ameongeza kuwa: Kutatuliwa suala la ndoa za vijana kuna manufaa kwa nchi na kwa jamii, duniani na Akhera.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia suala muhimu la kuongeza idadi ya watu na kuashiria baadhi ya ripoti za kutokelezwa kwsa njia sahihi sheria inayohusiana na kukabiliana na suala la kuzuia ujauzito nchini. Amemtaka Waziri wa Afya alifuatilie kwa kina suala hilo.
Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea furaha yake kubwa ya kwa kuweza kuonana na wanafunzi wa vyuo vikuu na namna wanachuo wa Iran wanavyoshiriki kwa hamasa kubwa na kwa mafanikio makubwa katika masuala tofauti nchini na kusema kuwa, suala hilo ni muhimu sana. Ameashiria pia baadhi ya ripoti za maadui wa taifa la Iran zinazodai kuwa eti vijana wa Iran ni watu waliokata tamaa na kusema: Ripoti hizo za uongo na za kiafiriti zinatumiwa kama silaha ya kueneza fikra za uhuru mchafu na usio na heshima nchini.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, vijana wa Iran ni miongoni mwa vijana watanashati na wenye harakati nyingi zaidi duniani. Wakati huo huo ameashiria takwimu za kiwango kikubwa cha vijana wanaojiua barani Ulaya na kusema kuwa, huo ni ushahidi wa wazi wa namna vijana wa ulimwengu wa Magharibi walivyokata tamaa na maisha.
Amekitaja kitendo cha kijana mmoja wa barani Ulaya aliyeua watoto karibu 80 miaka michache iliyopita na pia wimbi kubwa la vijana wa Ulaya wanaojiunga na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kwa ajili ya kwenda kujiua kupitia mashambulio ya kujilipua kuwa ni mfano mwengine wa kuweko kiwango kikubwa cha kukata tamaa vijana wa Ulaya na kusema: Katika upande wa pili, vijana wa Iran, wakiwa katika saumu na ambao usiku wa kabla yake walikesha kwa ibada katika usiku wa Laylatul Qadr, hawakuonesha uchovu wala kukata tamaa bali walijitokeza kwa wingi wa kustaajabisha katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani) tena katika mazingira ya joto kali, jambo ambalo ni ushahidi wa wazi wa jinsi uchangamfu na hamasa ilivyomea na kukita mizizi kati ya vijana wa Iran na jinsi vijana hao walivyombali kabisa na kukata tamaa ya maisha.
Mwanzoni mwa mkutano huo, wawakilishi 9 wa jumuiya za wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali vya Iran wamepata fursa ya kutoa maoni, dukuduku, maombi, ukosoaji na mapendekezo yao mbele ya Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Wanachuo hao ni pamoja na mabwana:
- Ali Pahlavan Kashi - Katibu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Wanachuo.
- Kivan Asem Kaffash - Katibu Mkuu wa Baraza la Jumuiya za Kiislamu za Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Azad.
- Vahid Zaree - Mjumbe wa Baraza la Kubainisha Misimamo ya Basiji ya Wanachuo.
- Hadi Zolfekar - Katibu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Allama Tabatabai.
- Mikael Dayati - Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Jumuiya za Kiislamu za Wanachuo Huru.
- Ali Mahdiyan Far - Mkuu wa Basiji ya Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Azad Kaskazini.
- Husain Shahbazi Zadeh - Katibu wa Harakati ya Kupigania Uadilifu wa Wanachuo.
Pamoja na mabibi:
- Zaynab Sadat Husaini - Mjumbe wa Baraza Kuu la Ofisi ya Kuimarisha Umoja.
- Saba Karam - Mkuu wa Kundi la Jihadi ya Afya ya Kituo cha Najaf.
Miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa na wawakilishi hao tisa wa jumuiya za wanafunzi wa Vyuo vikuumbali mbali vya Iran ni pamoja na:
- Udharura wa kuweko mawasiliano zaidi kati ya viongozi wa mihimili ya dola na wanafunzi wa Vyuovikuu.
- Kuundwa ofisi ya fikra kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu matatizo ya kiutamaduni nchini.
- Kufuta mitazamo na ushawishi wa kisiasa katika masuala ya utamaduni.
- Kupewa nafasi zaidi vijana katika Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni nchini na vile vile kuzingatiwa nafasi ya jumuiya za wanafunzi wa Vyuo vikuukwenye baraza hilo.
- Ulazima wa kukabiliana kisheria na watu wanaofanya makosa katika suala zima la udhamini wa masomo.
- Udharura wa kufanyika juhudi zisizosita za kuzuia kufifia nafasi ya kielimu ya Iran kimataifa.
- Ulazima wa kufanyika juhudi za ziada za Chombo cha Mahakama nchini kwa ajili ya kukabiliana na ufisadi wa kifedha.
- Kuunga mkono juhudi za timu ya nyuklia ya Iran kwa ajili ya kusimama kidete kulinda manufaa ya taifa na kukabiliana na tabia ya Marekani ya kujivutia kila kitu upande wake.
- Kuzingatia uchumi unaotokana na elimu msingi.
- Udharura wa kutolewa watu waliohusika na fitna za mwaka 2009 kwenye nafasi za utendaji nchini.
- Ulazima wa kuzuia kukumbwa na wasiwasi nyoyo za watu katika jamii kupitia kujizuia kukuza tofauti za mitazamo ya kisiasa.
- Kutumia vizuri minbar za Sala ya Ijumaa na kujiepusha maimamu wa Sala za Ijumaa nchini kujiingiza kwenye mambo madogo madogo.
- Udharura wa kutegemea uwezo wa ndani ya nchi na uongozi na usimamiaji mambo kijihadi kwa ajili ya kukabiliana na matatizo ya kiuchumi.
- Udharura wa kuzuia kupotoshwa njia ya Imam (Khomeini - quddisa sirruh) katika nyuga za kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi.
- Kufungiwa na kutoruhusiwa kazi za mirengo isiyo salama inayojipenyeza kwenye masuala ya kiutamaduni ya Vyuo vikuunchini.
- Udharura wa kurithishwa vizazi vipya, uzoefu wa uongozi wa kizazi cha awali cha Mapinduzi ya Kiislamu.
- Kukosolewa suala la kuzibana shughuli za kidiplomasia nchini na kuzifanya zijikite tu katika suala la nyuklia na mazungumzo na Marekani pekee.
- Kukosoa utabikishaji na ufananishaji usio sahihi wa hali ya hivi sasa ya Iran na mazingira ya kukubali suluhu Imam Hasan al Mujtaba Alayhis Salaam.
- Ulazima wa viongozi kulipa uzito wa hali ya juu suala la kutatua matatizo ya watu dhaifu na wenye suhula chache nchini.

 
700 /