Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Kushikamana na masuala ya kiroho ndiyo sababu kuu ya kutatuliwa matatizo yote

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo alikutana na Rais na baraza la mawaziri katika mfululizo wa vikao vyake kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Katika kikao hicho Ayatullah Khamenei ametoa ufafanuzi wa barua ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib kwa Malik al Ashtar (aliyemteua kuwa gavana wake nchini Misri) na akasema: Hazina ya kiroho, kimaanawi na kifikra ndiyo sababu ya kutatuliwa matatizo yote. Amesema kutadabari na kutafakari kwa kina katika kitabu cha Nahjul Balagha cha Bwana wa Wachamungu, Imam Ali (as), kunamtayarishia mtu hazima kama hiyo.
Akiashiria matamshi yaliyotolewa na Rais Hassan Rouhani mwanzoni mwa kikao hicho kuhusu matokeo ya mazungumzo ya nyuklia (kati ya Iran na kundi la 5+1), Kiongozi Muadhamu ameishukuru timu ya Iran katika mazungumzo hayo kwa kazi na juhudi zake kubwa katika mazungumzo hayo.
Baada ya hapo ameashiria sifa makhsusi za shakhsia na nafasi maalumu ya Malik al Ashtar kwa Amirul Muuminin na akasema: Imam Ali bin Abi Twalib (as) alitoa amri hiyo kwa mtu mkubwa kama huyu, suala ambalo lenyewe ni nukta ya kutiliwa maanani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha majukumu ya viongozi katika amri ya Amirul Muuminin kwa Malik al Ashtar na kusema: Kukusanya ushuru na haki za serikali kwa wananchi, kulinda wananchi na nchi yao, kuielekeza jamii katika mambo ya kheri na ufanisi na kujenga na kustawisha nchi ni majukumu manne makuu yanayoainishwa na Amirul Muuminin kwa ajili ya watawala katika barua yake kwa Malik.
Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kuwausia watawala wa Kiislamu kuwa na taqwa na kumcha Mwenyezi Mungu katika kila hali na nafasi, kufanya jitihada kubwa katika kutekeleza faradhi za wajibu, suna na mustahabu, kumnusuru Mwenyezi Mungu kwa moyo, ulimi na matendo na kuidhibiti nafsi mbele ya matamanio ya aina zote kuwa ni katika amri muhimu ambazo Bwana wa Wachamungu alimuusia Malik al Ashtar katika uwanja wa kuijenga na kuitakasa nafsi.
Suala jingine lililosisitizwa na Kiongozi Muadhamu kwa kutegemea baadhi ya vipengee vya amri ya Imam Ali (as) kwa Malik al Ashtar ni umuhimu wa kutoa maamuzi yenye insafu kuhusu viongozi waliotangulia.
Ametaja amali njema kuwa ndiyo akiba bora zaidi ya kipindi cha uongozi wa kila mtu na kuongeza kuwa: Wananchi huwa hawakosei katika kutoa maamuzi yanayoambatana na fikra, kutaamali na yaliyozingatia mambo yote; kwa msingi huo, kutokana na maamuzi na hukumu kama hizo za wananchi inawezekana kujua kiongozi yupi mwema na yupi si mwema.
Nasaha nyinyine mbili zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wakati anasoma amri ya kiserikali ya Amirul Muuminin kwa Malik al Ashtar ni kuichunga vilivyo nafsi ili isipotoke njia sahihi na kupotea na kuweka mbele na kutanguliza taklifu na maamrisho ya Mwenyezi Mungu kuliko jambo lolote jingine. Amesema hayati Imam Khomeini alikuwa dhihirisho la utekelezaji wa nasaha hizo za Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa amri nyingine za Imam Ali (as) kwa Malik al Ashtar ni kuwapenda kwa dhati wananchi na kuamiliana nao kwa upendo na upole. Ameongeza kuwa: Kwa mujibu wa amri ya Amirul Muuminin, kiongozi anapaswa kusamehe makosa na kuteleza kwa wananchi isipokuwa pale makosa hayo yapohusiana na kuchupa mipaka ya Mwenyezi Mungu au kupiga vita Uislamu na serikali ya Kiislamu.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameitaja amri ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) kwa Malik al Ashtar kuwa ni miongoni mwa hazina kubwa za kiutamaduni. Amepongeza tena juhudi zinazofanywa na viongozi wa serikali na kuwaombea taufiki ya Mwenyezi Mungu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu Hujjatul Islam Walmuslimin Hassan Rouhani amezungumzia matokeo ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 na akamshukuru Kiongozi Muadhamu kwa himaya na miongozo yake kwa serikali na timu ya Iran katika mazungumzo hayo. Amesema anatarajia kwamba, suala hilo litatayarisha uwanja mzuri wa kukomeshwa mashinikizo na kuondolewa tuhuma za maadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kuanzisha harakati mpya katika njia ya maendeleo ya nchi.
Vilevile ametoa ripoti kuhusu utendaji na hatua zilizochukuliwa na serikali. Ameashiria mafanikio na matatizo yaliyoikumba serikali katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kutaja uhusiano wa karibu na nchi jirani na kutilia maanani mazungumzo ya nyuklia kuwa ni katika hatua zilizochukuliwa na serikali katika medani ya siasa za nje. Ameongeza kuwa, katika hali ambayo eneo la Mashariki ya Kati limekumbwa na machafuko na ugaidi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikizihami nchi zinazosumbuliwa na tatizo la ugaidi na itadumisha njia hiyo.
Katika uwanja wa masuala ya uchumi, Rais Rouhani amekutaja kuvuka salama kipindi cha mdororo wa kiuchumi, kuondoa ustawi wa uchumi katika hali hasi na kuifanya kuwa chanya, kudhibiti mfumuko wa bei na ughali wa maisha, kupungua kiwango cha uagizaji wa ngano kutoka nje na kuongezeka uuzaji nje bidhaa zisizo za mafuta kuwa ni miongoni mwa mafanikio ya serikali. Amesema: Ili kuweza kuvuka matatizo ya ajira na ustawi wa kiuchumi tunahitajia uwekezaji na teknolojia.
Rais Rohani amesema, deni kubwa la serikali kwa Benki Kuu na mashirika binafsi, matatizo yanayosababishwa na ruzuku ya fedha, ukosefu wa ajira, shughuli za taasisi za fedha zisizo halali, uhaba wa maji, ukame, masuala ya mazingira na kupungua kwa bei ya mafuta ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili serikali.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesisitiza kuwa serikali yake itatumia uwezo wake wote kwa ajili ya kuondoa matatizo ya wananchi na taifa na kusema: Ili kuweza kutatua matatizo hayo kunahitajika ushirikiano wa mihimili mitatu mikuu ya dola ili tuweze kupiga hatua zilizosalia kwa kasi kubwa zaidi.  

 
700 /