Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Siasa zetu za kukabiliana na ubeberu wa Marekani kamwe hazitabadilika

Wananchi wanaompwekesha Mwenyezi Mungu na wenye imani na umoja wa Iran leo wamefanya sijda za shukrani katika pembe zote za nchi hii yenye fahari, kwa ajili ya kumshukuru Mola wao kwa kuwawezesha kufunga, kufanya ibada na kujitakasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.  Huku wakiwa kwenye swala ya Idul- Fitr wamemwomba Mwenyezi Mungu wao Mkarimu awawezeshe kudumu kwenye wongofu na saada ya humu duniani na huko Akhera. Katika kitovu cha fahari hii ya kihistoria, wananchi wakazi wa mji mkuu Tehran, wameswali Swala ya Idi kwa uimamu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika uwanja wa Muswala wa mjini Tehran.
Katika hotuba ya kwanza ya swala hiyo, Ayatullah Khamenei amelipongeza taifa la Iran na Waislamu wote duniani kwa mnasaba wa kuwadia Idi hii tukufu na kuongeza kuwa mwezi huu, kwa maana yake halisi umekuwa mwezi wa kunyesha baraka za Mwenyezi Mungu kwa taifa la Iran. Amesema kufunga saumu katika siku zenye joto kali na ndefu katika msimu wa joto, mahafali nyingi za Qur'ani, vikao vya kupendeza vya usomaji dua na kutawasali, kuandaliwa kwa futari za kawaida (zisizo za kifahari) misikitini na barabarani na hatimaye maandamano makubwa ya Siku ya Kimataifa ya Quds ni miongoni mwa baraka hizo za mbinguni.
Kiongozi Muadhamu ameendelea kusema kuwa, njia sahihi ya kulifahamu taifa la Iran ni kuzingatia masuala kama hayo, masuala ambayo yanathibitisha kwamba taifa hufanya hivi katika uwanja wa ibada na pia kuyaonyesha njia mataifa mengine katika uwanja wa kupambana na istikbari (matifa yenye kiburi). Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria nara ya 'Mauti kwa Israel' na 'Mauti kwa Marekani' ya wananchi wa Iran katika Siku ya Kimataifa ya Quds na kusema: 'Mielekeo mikubwa ya harakati yao inapaswa kutathminiwa katika nara hizo na wala sio kupitia ndimi za wageni walio na malengo binafsi (ya chuki) ambayo kwa masikitiko yanakaririwa na baadhi ya watu wasioelewa mambo ndani ya nchi.'
Katika hotuba ya pili ya swala, Ayatullah Khamenei ameashiria matukio ya kusikitisha katika eneo na kusema: 'Kwa bahati mbaya mikono miovu na myeusi imeufanya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa mchungu na mgumu kwa mataifa mengi katika eneo, yakiwemo ya Yemen, Bahrain, Palestina na Syria, jambo ambalo ni muhimu kwa wananchi wa Iran.'
Sehemu kubwa ya hotuba ya pili ya Ayatullahil Udhma Khamenei imehusu nukta kadhaa kuhusiana na suala la nyuklia. Kwanza kabisa amewashukuru wahusika wa mazungumzo hayo marefu na magumu na hasa zahma na juhudi kubwa zilizofanywa na timu ya mazungumzo hayo. Amesema: 'Ili kupasishwa kwa matini iliyotayarishwa (kwenye mazungumzo), hatua zote za kisheria zilizopitishwa zinapaswa kupitiwa. Matini hiyo ipasishwe au la, bila shaka malipo ya waliofanya mazungumzo hayo yatalipwa (na Mwenyezi Mungu) Inshallah.'
Akiwahutubu maafisa husika watakaochunguza (matini iliyotayarishwa ya nyuklia) Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba: 'Fanyeni kazi zenu kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia maslahi ya taifa ili muweze kuwasilisha matokeo ya uchunguzi huo kwa taifa na Mwenyezi Mungu, mkiwa vifua mbele (mnajivunia kazi zenu).'
Amesisitiza juu ya udharura wa Jamhuri ya Kiislamu kukabiliana na kila aina ya utumiwaji mbaya (wa matini iliyotayarishwa) na kuongeza: 'Matini iliyotayarishwa iwe itapitishwa au la, hatutamruhusu mtu yeyote kudhuru misingi mikuu ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran.' Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mazingira yaliyopo ya vitisho na adui kulenga masuala ya ulinzi ya Iran, na kusema: 'Kwa uwezo wake Mweyezi Mungu, uwezo wa kiulinzi na maeneo ya usalama nchini yatalindwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitasalimu amri mbele ya matakwa ya kibabe (yasiyo ya kimantiki) ya maadui.'
Kuendelea kwa uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa marafiki zake katika eneo ni nukta nyingine iliyobainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu suala la nyuklia. Ayatullah Khamenei amesema: 'Iwe kwamba matini iliyotayarishwa baada ya kupitia hatua za kisheria ndani ya nchi itapitishwa au la, taifa la Iran halitaacha kuyaunga mkono mataifa madhlumu ya Palestina, Yemen, Bahrain na mataifa na serikali za Syria na Iraq na mujahidina wakweli wa Lebanon na Palestina. Huku akisisitiza kuwa kwa vyovyote vile siasa za taifa na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kamwe hazitabadilika kuhusiana na Marekani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza: 'Sisi hatutakuwa na  mazungumzo yoyote na Marekani kuhusiana na masuala ya pande mbili, kieneo wala kimataifa isipokuwa katika masuala maalumu kama vile suala la nyuklia, jambo ambalo limewahi kutokea pia huko nyuma.' Ayatullah Khamenei amekosoa vikali siasa za Marekani za kuunga mkono serikali ya kigaidi na inayoua watoto ya Kizayuni na wakati huohuo kuwataja kuwa magaidi mujahidina wanaojitolea wa Hizbullah wa nchini Lebanon na kusema: 'Siasa zatu na Marekani katika eneo zinahitilafiana kwa digrii (nyuzi) 180, kwa hivyo ni vipi tunaweza kufanya nao mazungumzo.' Katika kuendeleza tahadhari na nukta zake kuhusu maudhui ya nyuklia, Ayatullah Khamenei ameashiria majitapo na majigambo ya hivi karibuni ya Wamarekani na kuongeza: 'Viongozi wa kiume na kike wa Marekani siku hizi wamelazimika kujitapa ili kutatua matatizo ya ndani ya nchi hiyo lakini majitapo hayo ya ziada hayana ukweli wowote.'
Ameashiria moja ya majitapo hayo ya viongozi wa Marekani kuwa wamezuia uzalishaji wa silaha za nyuklia nchini Iran na kusema: Sisi tulitoa fatwa ya kuharamisha uzalishaji wa silaha za nyuklia miaka mingi iliyopita, kwa misingi ya Kiislamu. Sisi tuna kizuizi cha kisheria (kidini) kinachotuzuia kuzalisha silaha hizi lakini pamoja na kuwa Wamarekani (wenyewe) mara nyingine hukiri umuhimu wa fatwa hii, lakini bado husema uongo katika propaganda na majitapo yao na kudai kuwa vitisho vyao ndivyo vimeizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: 'Maafisa wa hivi sasa wa Marekani wanazungumzia suala la taifa la Iran kusalimu amri (katika hali ambayo) bila shaka marais wao watano wa zamani pia walikuwa na matarajio kama hayo baada ya (ushindi) wa Mapinduzi ya Kiislamu lakini ima wamekwishakufa au wametoweka kwenye historia, na nyinyi pia mtaona kusalimu amri kwa Iran kwenye ndoto tu, kama walivyokuwa wao.
Ayatullah Khamenei ameashiria kukiri kwa rais wa hivi sasa wa Marekani kuhusiana na makosa kadhaa yaliyofanywa na nchi hiyo kuhusiana na Iran yakiwemo ya mapinduzi ya tarehe 28 Mordad 1332 (August 19, 1953) na uungaji mkono wake kwa Saddam Hussein (wa Iraq) na kusema: 'Hii ni sehemu ndogo tu ya makosa; kuna makosa mengine mengi ambayo Wamarekani bado hawataki kuyakiri.' Amewanasihi viongozi wa Marekani waache kufanya makosa wanayoendelea kuyafanya sasa ili kutowalazimu viongozi wa baadaye wa nchi hiyo kukiri makosa yao hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya nguvu zinazozidi kuongezeka kila siku za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: 'Ni karibu miaka 12 sasa ambapo nchi sita kubwa duniani zinafanya juhudi za kuizuia Iran kufuatilia teknolojia ya nyuklia na kama walivyosema wengine, wafungue kabisa nati na bolti (masuala ya msingi) za nyuklia za Iran, lakini leo wamelazimika kukubali na kustahamili mzunguko wa maelfu kadhaa ya mashinepewa (centrifuge) na kuendelea utafiti na ustawi nchini Iran, na jambo hili halina maana nyingine ghairi ya nguvu ya taifa la Iran.'
Amesema kuwa uwezo na nguvu hii inayoendelea kuongezeka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatokana na kusimama imara na mapambano ya taifa pamoja na ujasiri na uvumbuzi wa wataalamu wapendwa (wa Iran). Amesifu na kuwaenzi wataalamu wa nyuklia waliouawa shihidi pamoja na wafuasi na familia zao na kuongeza: 'Rehema ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya taifa kama hili linalosimama imara kutetea kauli (msimamo) yake.'
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake ya pili ya swala ya Idi ya heri ya Fitr, Ayatullah Khamenei ameashiria maneno yaliyotamkwa hivi karibuni na rais wa sasa wa Marekani kuwa nchi hiyo ina uwezo wa kuliangamiza kabisa jeshi la Iran na kusema: Watu wa kale (wahenga) walikuwa wakiyataja maneno kama hayo kuwa ni 'majitapo mbele ya wageni' (yaani majigambo ya wapumbavu mbele ya watu wasiowajua vizuri – wasioelewa vyema historia yao mbovu).' Akiwahutubu viongozi wa Marekani, kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza: 'Sisi hatukaribishi vita vyovyote wala hatutakuwa wa kwanza kuvianzisha lakini vikitokea, atakayeshindwa kwenye vita hivyo atakuwa Marekani mchokozi na mtenda jinai.'
700 /