Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Ali Khamenei:

Siasa zetu Mashariki ya Kati zinakabiliana kikamilifu na zile za Marekani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo (Jumamosi) amehutubia hadhara ya maafisa wa nchi, mabalozi wa nchi za Kiislamu na matabaka mbalimbali ya wananchi akisema kuwa umoja na mshikamano ndiyo dawa mujarabu ya ulimwengu wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa, vita vya kimadhehebu na kikaumu vinavyoendelea sasa katika Mashariki ya Kati vimepangwa na kutwishwa kwa shabaha ya kuyafanya mataifa ya Waislamu yaghafilike na utawala wa Kizayuni wa Israel. Ameongeza kuwa, siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo zinakabiliana kikamilifu na siasa za ubeberu unaoongozwa na Marekani, na Iran haiiamini hata kidogo Marekani kwa sababu wanasiasa wa nchi hiyo si wakweli wala hawana insafu kabisa.
Amewapa Waislamu mkono wa Idil Fitr na kuashiria hali ya kusikitisha ya ulimwengu wa Kiislamu na ukosefu wa umoja na mshikamano na akasema: Mifarakano na hitilafu za sasa katika eneo la Mashariki ya Kati si za kawaida na ni za kutwishwa, na maulama, wasomi, viongozi wa nchi, wanasiasa na shakhsia wa ulimwengu wa Kiislamu wanapaswa kuchunguza kwa makini mikono ya watu wanaousaliti Umma wa Kiislamu katika mifarakano na hitilafu hizo.
Kuhusu sababu za kutokuwa za kawaida hitilafu hizo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria historia ya muda mrefu ya kuishi kwa pamoja kwa amani Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni katika nchi za eneo hili na kusema: Kama Umma wa Kiislamu ungekuwa na umoja na kusisitiza zaidi juu ya mambo yanayowakutanisha pamoja Waislamu, hapana shaka kuwa ungekuwa nguvu ya aina yake katika medani ya siasa za kimataifa; lakini madola makubwa yanautwisha Umma wa Kiislamu hitilafu hizo kwa ajili ya kulinda maslahi yao na kuulinda utawala wa Kizayuni wa Israel.  
Ayatullah Khamenei ameashiria chuki iliyopo baina ya Waislamu dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel licha ya mielekeo ya baadhi ya watu katika nchi za Waislamu kwa utawala huo haramu na akasema: Madola ya kibeberu yakishirikiana na watu waovu katika baadhi ya nchi za Kiislamu yamepanga vita vya kimadhehebu na kuunda makundi kama al Qaida na Daesh kwa shabaha ya kuyasahaulisha mataifa ya Kiislamu utawala wa Kizayuni. 
Amekumbusha hatua za baadhi ya maafisa wa Marekani ya kukiri kuhusu nafasi ya serikali ya Marekani katika kuanzisha na kupanua kundi la Daesh na kusema, kuundwa muungano dhidi ya Daesh ni jambo lisiloweza kusadikika. Amesisitiza kuwa siasa za madola ya kibeberu katika eneo hili ni za kihaini na watu wote wanapaswa kuizingatia maudhui hiyo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati zinakabiliana na siasa za ubeberu. Amezungumzia maudhui ya Iraq na kusema: Siasa za ubeberu nchini Iraq ni kuiondoa madarakani serikali iliyochaguliwa kwa kura za wananchi, kuanzisha mapigano kati ya Shia na Suni na hatimaye kuigawa nchi hiyo, lakini siasa za Jamhuri ya Kiislamu kuhusu Iraq ni kuhami na kuimarisha serikali iliyochaguliwa, kusimama kidete mkabala wa wanaoanzisha vita vya ndani na hitilafu na kulinda umoja wa ardhi yote ya Iraq.
Kuhusu Syria, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, siasa za ubeberu huko Syria ni kutwisha irada na matakwa ya nje juu ya matakwa ya taifa na kuiondoa madarakani serikali ambayo imesimama kidete kukabiliana na Wazayuni, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitambua serikali ambayo kaulimbiu, lengo na nia yake ni kukabiliana na Wazayuni, kuwa ni ghanima na neema kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Amesisitiza kuwa katika masuala ya Mashariki ya Kati kama Iraq, Syria, Yemen, Lebanon na Bahrain, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haifuatilii maslahi yake binafsi bali inaamini kuwa, wananchi ndio wachukuaji maamuzi wakuu katika nchi hizo na watu wengine hawana haki ya kuingilia mambo yao na kuchukua maamuzi (kuhusu nchi hizo).
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameashiria mpambano baina ya siasa za ubeberu na zile za Jamhuri ya Kiislamu kuhusu Lebanon na kusema: Mfumo wa ubeberu ukiongozwa na Marekani ulinyamaza kwa miaka mingi na kuridhia kitendo cha utawala ghasibu wa Israel cha kukalia kwa mabavu sehemu kubwa ya ardhi ya Lebanon, lakini pale kundi la wanamapambano waumini na wenye kujitolea ambalo ndilo kundi sharifu zaidi kati ya makundi ya mapambano ya kitaifa duniani, liliposimama kupambana na wavamizi wa Kizayuni na kuwafukuza katika ardhi ya Lebanon, kundi hilo liliitwa kuwa la kigaidi na mfumo wa ubeberu unafanya juhudi za kuliangamiza.
Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza kuwa, sababu ya himaya na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa muqawama na wanamapambano wa Lebanon ni ushujaa, kujitolea na kusimama kwao kidete mbele ya wavamizi. Ameongeza kuwa: Wamarekani wanawaita wanamapambano wa Lebanon kuwa ni magaidi na wanaitambua Iran kuwa inaunga mkono ugaidi kwa sababu ya kuihami Hizbullah; wakati gaidi halisi ni Wamarekani wenyewe ambao wameanzisha kundi la Daesh na wanawaunga mkono Wazayuni habithi na wanapaswa kuhukumiwa kwa kuunga mkono ugaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia Yemen na mpambano wa siasa za ubeberu na zile za utawala wa Kiislamu nchini Iran na kusema: Nchini Yemen, Marekani inamuunga mkono rais ambaye alijiuzulu na kukimbia nchi yake katika kipindi nyeti na muhimu sana kwa lengo la kuzusha mgogoro wa kisiasa na kuitaka nchi nyingine iwashambulie wananchi wake na anaunga mkono mauaji yanayofanywa dhidi ya watu wasio na hatia na watoto wa Yemen, na vilevile inanyoosha mkono wa urafiki kwa utawala wa kidikteta zaidi ambao hauwaruhusu wananchi hata kusikia jina la uchaguzi; na wakati huo huo inaituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imekuwa ikiitisha uchaguzi mara kwa mara kuwa ni utawala wa kidikteta!
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, wanasiasa wa Marekani wanakiuka kabisa insafu katika matamshi yao na kukana uhakika usiopingika wa mambo kwa jeuri kamili.
Ameongeza kuwa, hii ndiyo sababu inasemwa kwamba Wamarekani hawawezi kuaminika kwani si wakweli hata kidogo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Katika majaribio magumu ya mazungumzo ya nyuklia ambapo Rais wa Jamhuri na maafisa husika wamefanya kazi kubwa, tumeshuhudia mara kwa mara tabia hiyo ya kutokuwa na ukweli kwa Wamarekani lakini kwa bahati nzuri maafisa wetu walikabiliana nao na wakati mwingine walipambana nao kimapinduzi; sasa tunapaswa kusubiri na kuona hatima ya maudhui hii itakuwa vipi.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa dawa mujarabu ya kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu na matatizo ya kila moja kati ya nchi za Waislamu ni kulinda umoja na mshikamano. Ameongeza kuwa: Taifa la Iran pia linapaswa kuwa na umoja, na kadhia ya nyuklia haipasi kuzusha mgawanyiko nchini, kwa sababu maudhui hiyo inafuatiliwa na maafisa husika na viongozi wanataka kudhamini maslahi ya taifa.
Ameashiria pia njama zinazofanywa na vyombo vya habari vya kigeni kwa lengo la kuzusha hitilafu na mgawanyiko hapa nchini na kusema: Njia pekee ya kukabiliana na njama hizo ni kuwa na taqwa na uchamungu wa umma na kinga ya ndani ya nafsi sambamba na kuzidisha uwezo wa ndani ya nchi kupitia njia ya kuimarisha imani, elimu na viwanda na utamaduni.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu Hujjatul Islam Walmuslimin Hassan Rouhani alitoa hotuba fupi akiwapongeza Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa sikukuu ya Idil Fitr. Amesema mwezi wa Ramadhani ulikuwa mwezi wa mtihani wa imani na kusimama kidete, kupambana na kuwa na uvumilivu. Ameongeza kuwa, Ramadhani ya mwaka huu ulikuwa mwezi wa mshikamano na kuwa na sauti moja na mwezi wa kurejea katika maumbile safi ya mwanadamu.
Rais Rouhani amesema kuwa, katika mwezi wa Ramadhani wa mwaka huu na kwa dua za kheri za wananchi, mapambano ya miaka 12 ya taifa la Iran yamezaa matunda. Amesema: Serikali kwa kufuata ramani ya njia iliyochorwa na irada na mapambano ya taifa la Iran, na kutokana na mwongozo wa busara wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, himaya ya taasisi na mihimili yote na vilevile kutokana na kujitolea kwa watoto wa taifa hili katika medani ya udiplomasia, imeweza kudhamini haki za taifa kubwa la Iran.
Rais Rouhani amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu imewadhihirishia walimwengu nguvu nyingine mpya inayoitwa uwezo wa kidiplomasia na nguvu ya mazungumzo. Vilevile ameashiria matukio ya eneo la Mashariki ya Kati na kwamba mwezi Ramadhani mwaka huu umepita kwa mashaka makubwa kwa nchi jirani na za eneo hili kama Iraq, Syria, Yemen hadi Palestina, Lebanon, Afghanistan na Pakistan na akasema: Jamhuri ya Kiislamu imeazimia kuwatetea watu wote wanaodhulumiwa na kupambana na madhalimu wote. 

               
700 /