Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Jamhuri ya Kiislamu inazinyooshea mkono wa urafiki serikali za Kiislamu

Akizungumza Leo asubuhi (Jumatatu) mbele ya hadhara ya wanazuoni, wananadharia, na wageni wa kikao cha Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait (as) na vilevile wageni wa kikao cha Muungano wa Redio na Televisheni za Kiislamu, Ayatullahil Udhma Khamenei Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mapambano dhidi ya njama za uistikbari katika eneo (Mashariki ya Kati) ni misdaki ya wazi (kusudio halisi) ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Ameashiria makabiliano ya dhati na (juhudi za Marekani za kutumia vibaya matokeo ya mazungumzo ya nyuklia na satwa ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni nchini Iran) na lusema: Mbinu za mfumo wa kibeberu katika eneo zimesimama juu ya misingi miwili ya kuleta hitilafu na kuwa na satwa (kujipenyeza) ambapo tunapasa kutumia mbinu sahihi za hujuma na ulinzi ili kupambana kwa makini na bila kusita na mbinu hizo (za maadui).
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kufanyika kwa kikao cha sita cha Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait (as) na kusema kuwa kuwafuata Ahlul Bait wa Mtume (saw) kunalazimu kuenezwa maarifa ya Kiislamu, kusimamishwa sheria za Mwenyezi Mungu, kufanya jihadi (jitihada) katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa nguvu zetu zote na kupambana na dhulma na dhalimu na kusisitiza kuwa: Kufanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu hakuna maana ya vita vya kijeshi tu, bali kunajumuisha mapambano ya kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa.
Ayatullah Khamenei amesema: Leo misdaki na kielelezo bora zaidi ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kutambua vyema mbinu (njama) za uistikbari katika eneo la Kiislamu na hasa katika eneo la kistratijia na nyeti la magharibi mwa Asia na kuweka mipango ya kupambana nazo ambapo mapambano hayo yanapasa kujumuisha makabiliano ya kiulinzi na kihujuma. Kiongizo wa Mapinduzi ameashiria njama za uistikbari katika eneo katika kipindi cha miaka mia moja iliyopita na kusema: Hata kama njama za uistibari katika eneo la Kiislamu zina historia ndefu, lakini mashinikizo na njama ziliongezeka tokea wakati wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ili kuzuia kukaririwa kwa uzoefu huo (Mapinduzi ya Kiislamu) katika nchi nyingine. Amesema: Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu tokea miaka 35 iliyopita umekuwa shabaha ya vitisho, vikwazo, mashinikizo ya kiusalama na njama mbalimbali za kisiasa, na taifa la Iran limeyazoea mashinikizo haya.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza: Ni wazi kuwa njama za maadui katika eneo la magharibi mwa Asia zimeongezeka zaidi kutokana na kuchanganyikiwa adui kufuatia mwamko wa Kiislamu ambao ulianza miaka kadhaa iliyopita kaskazini mwa Afrika. Ayatullah Khamenei amesema: Wanadhani kuwa wameweza kukandamiza mwamko wa Kiislamu lakini harakati hii haiwezi kukandamizwa na bado inaendelea na hivi karibuni au baadaye kidogo ukweli wake utadhihiri. Ayatullah Khamenei amesema, mfumo wa ubeberu ukiongozwa na Marekani ni misdaki halisi na dhihirisho kamili la 'maana ya adui' na kusisitiza: Marekani haina uelewa (haijanufaika) wowote ule  wa maadili ya kiutu na hutekeleza ukatili na jinai bila kujali lolote na kwa kutumia maneno matamu (ya kuvutia) na kwa kutabasamu. Kisha Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mbinu zinzotumiwa na adui katika mazingira ya hivi sasa na kuongeza: Mbinu hizi zimesimama juu ya misingi miwili ya 'kuzua hitilafu' na 'kujipenyeza.' Kuhusu mpango wa adui wa kuzua hitilafu Ayatullah Khamenei amesema: Kuzua hitilafu miongoni mwa serikali na hatari zaidi kuliko hilo, miongoni mwa mataifa, kumewekwa katika ajenda ya uistikbari. Ameashiria kwamba katika hali ya hivi sasa ibara kama Shia na Suni zinatumika kwa ajili ya kuleta hitilafu miongoni mwa mataifa na kusema kwamba Waingereza ni wataalamu wa kuzua hitilafu nao Wamarekani ni wanafunzi wao na kuongeza: Makundi ya kikatili, yanayovunjia heshima matukufu na ya kijabari ambayo Marekani imekiri kushiriki katika uundwaji wake ni chombo muhimu zaidi kinachotumiwa kuzusha hitilafu ambazo kidhahiri zinaonekana kuwa za kidini  miongoni mwa mataifa, njama na mbinu ambazo kwa bahati mbaya baadhi ya Waislamu wenye fikra finyu wamehadaika nazo na kutumbukia kwenye mpango wa adui kwa kutokuwa na mwamko. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mfano wa wazi kuhusiana na maudhui hiyo ni suala la Syria na kuongeza: Wakati tawala za kitaghuti nchini Tunisia na Misri zilipopinduliwa kwa nara za Kiislamu, Wamarekani na Wazayuni walichukua uamuzi wa kutumia fomula hiyo kuzitokomeza nchi za mapambano za Kiislamu na hiyo ndio maana waliiendea Syria. Ayatullah Khamenei amesema: Baada ya kuanza tukio la Syria, baadhi ya Waislamu wasio na mwamko walitumbukia kwenye njama ya mpango huo na kuanza kujaza jedwali la mafumbo la adui, na hivyo kuifikisha Syria katika hali hii. Amesisitiza yale yanayojiri leo huko Iraq, Syria, Yemen na maeneo mengine na juhudi zinazofanyika ili kuyadhihirisha kuwa ni 'vita vya kimadhehebu' kwa vyovyote vile si vita vya kimadhehebu bali ni vita vya kisiasa. Kiongozi Mudhamu amesema: Jukumu muhimu zaidi hii leo ni kufanya juhudi za kuondoa hitilafu hizi.
Ayatullah Khamenei amesema: Sisi tumesema wazi na hadharani kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inazinyooshea mkono wa urafiki serikali zote za Kiislamu za eneo na wala hatuna tatizo lolote na serikali za Kiislamu. Ameongeza: Jamhuri ya Kiislamu ina uhusiano wa kirafiki na nchi nyingi jirani, bila shaka baadhi ya nchi pia zina hitilafiana na sisi na zinafanya ukaidi na uhabithi lakini Iran imesimamisha msingi wake juu ya uhusiano mzuri na majirani na serikali za Kiislamu na hasa mataifa ya eneo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Msingi wa mwenendo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni misingi ambayo Imam mpendwa (MA) alifungamana nayo na hivyo kufanikiwa kuyaletea ushindi Mapinduzi ya Kiislamu na kuyafikisha katika hatua ya uthabiti.
Ayatullah Khamenei amesema, 'wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao' ni moja ya misingi imara ya mfumo wa Kiislamu na kusisitiza: Sisi kwa msingi wa darsa ya mpendwa Imam (MA) na sera ya wazi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hatufanyi mapatano na uistikbari lakini tuna urafiki na ndugu Waislamu. Amesema: Sisi hatuzingatii madhehebu katika kutetea na kuunga mkono mtu anayedhulumiwa na uungaji mkono uleule tulioutoa kwa ndugu zetu Mashia nchini Lebanon ndio uleule tulioutoa kwa ndugu zetu Masuni katika Ukanda wa Gaza, na tunalichukulia suala la Palestina kuwa suala la ulimwengu wa Kiislamu.
Katika kumalizia suala la 'kuzua hitilafu' Ayatullah Khamenei amesema suala hilo ndiyo nguzo ya kwanza ya njama za adui katika eneo la Kiislamu la magharibi mwa Asia na kuongeza: Kuongezwa hitilafu katika ulimwengu wa Kiislamu ni marufuku na sisi tunapinga kila aina ya mwenendo  na harakati inayozusha hitilafu hata ikiwa itatoka kwa baadhi ya makundi ya Kishia, na tunalaani kuvunjiwa heshima matukufu ya Ahlu Suna.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema 'upenyaji' katika nchi za eneo ni mbinu ya pili ya kikorofi inayotumiwa na Marekani na kusisitiza: Marekani inataka kuhuisha satwa yake ya makumi ya miaka na heshima yake iliyotoweka katika eneo. Ayatullah Khamenei ameashiria juhudi zinazofanywa na Washington kwa ajili ya kutumia vibaya matokeo ya mazungumzo ya nyuklia na kuongeza: Wamarekani wanataka kutumia mapatano ambayo taklifu yake haijajulikana sio Iran tu bali hata Marekani kwenyewe na haijulikani iwapo yatapitishwa au la, kama chombo cha kujipenyeza nchini Iran lakini sisi tumeifunga kabisa njia hii. Tutatumia nguvu zetu zote kutowaruhusu Wamarekani kuwa na ushawishi wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni au kuwepo kisiasa nchini Iran. Amesema siasa za kieneo za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinagongana moja kwa moja na siasa za kieneo za Marekani na kuongeza: Wao wanataka kuzigawa nchi za eneo na kubuni nchi ndogondogo tegemezi lakini sisi kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu hatutaruhusu hilo kutimia. Kiongozi Muadhamu amekumbusha onyo alizotoa huko nyuma kuhusiana na juhudi zinazofanywa na Marekani kwa ajili ya kuigawa Iraq na kuongeza: Baadhi walikuwa wakishangazwa na maneno hayo lakini leo Wamarekani wanazungumzia waziwazi suala la kuigawa Iraq. Ayatullah Khamenei ameongeza: Kugawanywa Iraq na wakiweza Syria ni lengo lililo wazi la Wamarekani lakini umoja wa ardhi za nchi za eneo zikiwemo Iraq na Syria una umuhimu mkubwa kwetu sisi.
Katika kuendelea kufafanua mkabiliano uliopo kati ya siasa za kieneo za Jamhuri ya Kiislamu na siasa za utawala wa Marekani, Kiongozi Muadhamu ameongeza: Iran inatetea kikamilifu mapambano katika eneo yakiwemo mapambano ya Palestina na itaendelea kumuunga mkono kila mtu anayepambana na Israel na kuuponda utawala wa Kizayuni.
 Amesema kuwa kukabiliana na siasa za kuzusha mifarakano za Marekani na vituo vya kuzusha hitilafu ni miongoni mwa siasa za kimsingi za Iran na kuongeza kuwa: Ushia ambako kituo chake cha matangazo kiko London na kazi yake ni kuutayarishia njia ubeberu, sisi hatuutambui kuwa ni Ushia.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha sera za Iran za kutetea watu wote wanaodhulumiwa wakiwemo wananchi wa Bahrain na Yemen na kuongeza kuwa: Kinyume na madai yasiyo na msingi, Iran haiingilii masuala ya ndani ya nchi hizo lakini itaendelea kuwatetea na kuwasaidia wananchi hao wanaodhulumiwa.
Amekosoa vikali mauaji yanayoendelea kufanywa dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Yemen na kuharibiwa nchi hiyo na akasema: Kufuatilia baadhi ya malengo ya kisiasa tena kwa kutumia mbinu za kipumbavu ndiyo sababu ya kuendelea kwa jinai zinazofanywa dhidi ya watu wa Yemen.
Ayatullah Khamenei amekamilisha sehemu hii ya hotuba yake kwa kusema: Katika maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu ikiwemo Pakistan na Afghanistan kunajiri matukio ya kuumiza, na Waislamu wanapaswa kutibu matatizo hayo kwa umakini na uangalifu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa Muungano wa Redio na Televisheni za Kiislamu ni kituo chenye umuhimu mkubwa kwa ajili ya kukabiliana na mfumo hatari na mafia tata ya vyombo vya habari vya Kimarekani na Kizayuni. Ameongeza kuwa harakati hiyo inabidi iimarishwe na kupanuliwa zaidi.
Amekumbusha suala la masafa makubwa yaliyopo baina ya vyombo vya habari katika nchi nyingi za Kiislamu na matakwa ya wananchi Waislamu na vilevile suala la vyombo hivyo vya habari kufuata siasa hatari za ubeberu na kusema: Mamlaka kubwa ya vyombo vya habari vya madhalimu ambavyo vinadai kutopendelea upande wowote inahudumia malengo ya madhalimu wa kimataifa kwa kupotosha, kusema uongo na kwa kutumia mbinu tata za aina mbalimbali.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, licha ya majigambo ya ubeberu na vibaraka wao, hapana shaka kuwa izza na nguvu ya Uislamu iko wazi na imedhaminiwa kwa baraka za wanaume, vijana na wanawake wapigana jihadi, na mustakbali mwema utakuwa wa eneo la Mashariki ya Kati na mataifa ya Waislamu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait Hujjatul Islamu Walmuslimin Muhammad Hassan Akhtari alitoa ripoti kuhusu mkutano wa sita wa jumuiya hiyo na kusema: Mkutano huo umehudhuriwa na maulama na shakshia kutoka zaidi ya nchi 30 duniani.
Vilevile Katibu Mkuu wa Muungano wa Redio na Televisheni za Kiislamu, Hujatul Islam Karimiyan alitoa ripoti akisema kuwa, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na muungano huo ni pamoja na kufanya jitihada za kuanzisha lugha mpya katika medani ya vyombo vya habari kwa kutumia vigezo vya Kiislamu, kuvutia imani ya watu, kulea nguvu kazi inayofaa na kuanzisha mbinu ya kuzalisha, kusambaza na kutangaza habari.

700 /