Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu katika hadhara ya wasimamizi wa Hija:

Uzoefu wa umoja wa taifa la Iran upelekwe Hija

Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran leo asubuhi (Jumamosi) amezungumza mbele ya hadhara ya wasimamizi na wafanyakazi wa Taasisi ya Hija na Ziara za Maeneo Matakatifu na kusema kuwa hija inadhamini 'kudumu kwa Uslamu' na ni nembo ya 'umoja na utukufu' wa Umma wa Kiislamu. Amesisitiza juu ya uzingatiaji sambamba upande wa kijamii na wa mtu binafsi wa ibada hiyo kubwa na kusema kuwa kuhamishiwa katika mkusanyiko adhimu wa hija, uzoefu wa umoja wa taifa la Iran kutauletea Umma wa Kiislamu mshikamano, umoja na nguvu zaidi. Ameashiria sifa za kipekee za hija zikilinganishwa na sifa za ibada nyinginezo za faradhi za Kiislamu na kusema: Hija ina pande mbili tofauti za mtu binafsi na kijamii ambapo kuzingatiwa kwa pande zote mbili kuna athari za kipekee katika saada ya hapa duniani na ya huko Akhera kwa mahujai na mataifa ya Kiislamu. Kiongozi wa Mapinduzi amesema kuwa ziara ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu na amali za hija ni fursa ya kipekee kwa ajili ya kutakasa roho, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kutayarisha masurufu ya umri mzima wa maisha. Amewahutubu mahujaji wanaozuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu kwa kusema: Tambueni thamani ya kila amali ya hija na kuzitakasa pamoja na kukata kiu ya roho na nafsi zenu kwenye chemchemi ya neema hii kubwa.
Katika kubainisha athari za kijamii za ibada ya hija, Ayatullah Khamenei pia ameashiria mahudhurio sambamba ya mataifa yote huko Madina na Makka licha ya tofauti zao za rangi, madhehebu, utamaduni na za kidhahiri na kuongeza: Hija ni dhihirisho na fursa halisi ya 'umoja wa Kiislamu.'
Amewakosoa vikali watu wanaodunisha uhakika na umuhimu wa Umma wa Kiislamu kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo ya kusifu kupita kiasi maana ya utaifa na kuongeza: Hija ni mfano wenye maana kubwa wa kubuniwa Umma wa Kiislamu na fursa kubwa sana kwa ajili ya Waislamu wa ulimwengu kuwa na umoja, maelewano na kuhurumiana.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kudhihirishwa kwa utukufu wa Umma wa Kiislamu na fursa ya kubadilishana uzoefu ni nukta nyingine muhimu ya athari za kijamii za hija na kuongeza: Kubainishwa na kuakisiwa uzoefu wenye manufaa wa mataifa mengine ya Kiislamu huimarisha Umma wa Kiislamu. Kuhusu suala hili ameashiria uzoefu wenye athari kubwa na unaofaa wa taifa la Iran katika kumtambua adui, kutomwamini adui na kutomchanganya rafiki na adui na kusema: Watu wetu kutokana na utambuzi wa kusifika, wametambua kwamba uistikbari wa kimataifa na uzayuni ndiye adui halisi na mkaidi wa taifa la Iran na Umma wa Kiislamu na ndiyo maana taifa likawa linapiga nara dhidi ya Marekani na uzayuni katika mikutano yote ya kitaifa na Kiislamu. Ayatullah Khamenei ameendelea kusema: Katika miaka 36 iliyopita, baadhi ya wakati uistikbari umefuatilia uadui wake dhidi ya Iran kupitia ndimi na mienendo ya nchi nyingine lakini taifa la Iran daima limekuwa likitambua kwamba nchi hizo zimehadaika na ni vibaraka tu na kwamba adui wake halisi ni Marekani na Israel. Kiongozi Muadhamu ameashiria uzoefu uliofeli wa kuingia madarakani baadhi ya makundi ya Kiislamu katika baadhi ya nchi na kusema: Kinyume na lilivyokuwa taifa la Iran, wao walichanganyikiwa kuhusu rafiki na adui na hivyo kupata pigo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa umoja ni uzoefu mwingine wa taifa la Iran unaoweza kuhamishwa kwenye mataifa mengine katika msimu wa hija na kuongeza: Watu wa Iran licha ya kuwa na tofauti zote za 'kiitikadi, kifikra, kisiasa na kikabila' lakini wamelinda umoja wao wa kitaifa na wanafahamu vyema thamani ya neema hiyo ya Mwenyezi Mungu, na uzoefu huu wenye thamani kubwa unapaswa kuhamishiwa katika mataifa mengine ya Kiislamu. Amesema mapigano ya ndani katika baadhi ya nchi kwa zisingizio vya madhehebu, siasa na hata vyama ni matokeo ya kutotambua thamani ya neema ya umoja na kuongeza: Mwenyezi Mungu si jamaa wa taifa lolote na iwapo watu hawatatambua thamani ya umoja na maelewano basi atawasababishia hitilafu, mapigano na umwagaji damu.
Ayatullah Khamenei amekumbusha njama za kidhalimu za kimataifa dhidi ya Uislamu, Iran na mfumo wa Kiislamu na kuongeza: Kwa hakika wao hawako dhidi ya Shia wala Iran bali wanafanya njama dhidi ya Qur'ani kwa sababu wanafahamu kwamba Qur'ani na Uislamu ndiyo kitovu cha mwamko wa mataifa. Huku akiashiria juhudi zisizokoma za waistikbari kwa ajili ya kupata njia mbalimbali za kupenya na kutoa pigo kwa Waislamu, Kiongozi wa Mapinduzi amesema: Kwa kutegemea uungaji mkono usio na kikomo wa kifedha wa uistikbari, makumi ya ya vituo vya kifikra na kisiasa nchini Marekani, Ulaya, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na nchi tegemezi, vinatalii na kuchunguza Uislamu na Ushia ili kupata njia za kukabiliana na mambo yanayouletea mwamko na nguvu umma wa Kiislamu. Ameendelea kusema: Watumiaji mabavu duniani, wanafuatilia kwa karibu suala la kuanzisha utumiaji nguvu na hitilafu kwa jina la Uislamu na kwa kuichafua dini tukufu ya Kiislamu wanafanya juhudi za kuyapiganisha mataifa na hata kuzua mapigano ndani ya taifa moja ili kudhoofisha umma wa Kiislamu, ambapo kuhamishiwa uzoefu wa taifa la Iran kuhusu umoja na kutambuliwa adui katika mataifa mengine, katika siku za hija kunaweza kuvunja njama hii.
Kiongozi Muadhamu amesema: Bila shaka kuna wale wanaopinga kuhamishwa kwa uzoefu huu wenye manufaa baina ya mataifa katika msimu wa hija, lakini kwa vyovyote vile njia ya kufanikisha jambo hili inapasa kupatikana.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameashiria tena ulazima wa kuzingatiwa sambamba pande za mtu binafsi na kijamii za ibada ya hija na  kusisitiza kwamba: Waheshimiwa mahujaji hawapasi kupoteza fursa ya kipekee ya kupumua katika mji wenye uturi wa Mtume na uwepo wa kiibada na wa kuvutia katika mji mtakatifu wa Makka na Nyumba ya Mwenyezi Mungu, kwa kujishughulisha na matembezi ya sokoni na ununuzi wa bidhaa, na hivyo kujuta katika umri wao wote kwa kutonufaika kikamilifu na fursa ya kipekee na ya kusisimua ya kuwepo katika Masjidul Haram na Masjidu an-Nabi.
Kiongozi wa Mapinduzi vilevile amesema katika hotuba yake kwamba juhudi za maandalizi ya hija ni moja ya majukumu bora na ya kufana zaidi. Huku akiwashukuru wasimamizi wa hija kwa juhudi zao amesema: Fanyeni jitihada zenu zote kwa ajili ya kuanda hija inayofaa.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadamu, Hujjatul Islam wal Muslimeen Qadhi Askar, Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu na Msimamizi wa Mahujaji wa Kiirani alimpongeza Kiongozi Muadhamu kwa mnasaba wa kuwadia Siku Kumi za Heshima na kusema kuwa kauli mbiu ya hija ya mwaka huu ni: 'Hija, Umaanawi, Mwamko na Maelewano ya Kiislamu.' Amesema: Kubuniwa kwa stratijia kumi na mpango wa ustawi wa hija, kuinuliwa viwango vya elimu ya nguvukazi, kutolewa mafunzo ya maarifa kwa ajili ya mahujaji na wanazuoni wanaoongoza misafara, kufanyika vikao vya kielimu na kunufaika na vipawa vya mahujai pamoja na waratibu wa hija ni miongoni mwa shughuli na mitazamo itakayozingatiwa katika maandalizi ya amali za hija. Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu na Msimamizi wa Mahujaji wa Kiirani amesema: Hija ya mwaka huu mbali na kulinda utukufu na heshima ya taifa la Iran inapasa kuwa kitovu cha umoja wa Waislamu duniani.
Bwana Saeed Ohadi, Mkuu wa Taasisi ya Hija na Ziara pia ametoa ripoti kuhusiana na shughuli za taasisi hiyo na kusema kuwa kusahilishwa taratibu za kusajiliwa majina ya mahujaji na kusafirishwa asilimia 62 ya mahujaji kwa ndege za moja kwa moja kuelekea Madina, kuwasilishwa vyakula tofauti katika ratiba ya chakula, kudhaminiwa sehemu kubwa ya mahitaji ya mahujaji ndani ya nchi, kupunguzwa kwa bei ya huduma na kupashwa habari kwa mfumo erevu ni miongoni mwa hatua na mipango iliyotekelezwa na taasisi hiyo kwa lengo la kufanikisha hija ya mwaka huu. Amesema: Mipango ya lazima imetekelezwa kwa madhumuni ya kusafirisha mahujaji 64,000 nchini kwenda hija kupitia misafara 455.
Kabla ya kufanyika kikao hicho, Kiongozi wa Mapinduzi pia alitembelea maonyesho ya picha na vitabu vinavyohusiana na hija.

700 /