Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi aliambia baraza la mawaziri:

Uadui wa Marekani haujapungua, inafanya jitihada za kupenya Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo (Jumatano) amekutana na baraza la mawaziri likiongozwa na Rais Hassan Rouhani ambako amesema kuwa falsafa ya siku hizi za kukumbuka tukio la kuuawa shahidi Mohammad Ali Rajaei na Mohammad Javad Bahonar (Rais na Waziri Mkuu wa zamani wa Iran) kupewa jina la Wiki ya Umoja ni kubakisha hai vigezo vya kifikra, kimwenendo na kishakhsia vya mashahidi hao mawili azizi. Amesifu juhudi za serikali ikiwa ni pamoja na katika kupunguza ughali wa maisha, kutuliza na kuimarisha uchumi, na katika sekta ya afya na kuhitimisha mazungumzo ya nyuklia na akasema: Katika mwenendo wa harakati kuu ya nchi viongozi wanapaswa kutilia maanani kikamilifu suala la kuendelea uhasama wa maadui, kuwa macho mbele ya mikakati ya wageni ya kutaka kupenya na kuingia Iran, kujiepusha na masuala yasiyo ya msingi, kulinda kasi ya ustawi wa kielimu nchini, usimamiaji wa sekta ya kiutamaduni kwa mujibu wa misingi na nara za Imam Khomeini na Mapinduzi ya Kiislamu, kutilia maanani uadilifu katika njia ya ustawi, usimamiaji halisi wa biashara ya nje, na kutayarisha ratiba yenye muda maalumu kwa ajili ya kufikia uchumi ngangari.
Katika kikao hicho kilichofanyika kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Serikali, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelipongeza taifa kwa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Ridha (as) na kusema kukutana kwa maadhimisho ya siku hiyo na Wiki ya Serikali ni tukio lenye baraka. Ameongeza kuwa: Kuwepo kwa Haram tukufu ya Imam Ridha (as) nchini Iran ni miongoni mwa fahari za nchi hii na inabidi tufanye kila tunachoweza kuadhimisha nafasi ya mtukufu huyo.
Ayatullah Khamenei amewakumbuka mashahidi Mohammad Ali Rajaei na Mohammad Javad Bahonar na kusema: Miongoni mwa malengo ya kuainishwa Wiki ya Serikali katika siku hizi ni kuweka wazi vigezo vya sifa za kimwenendo na kimaadili za mashahidi hao kwa ajili ya viongozi wa serikali. Amesema miongoni mwa sifa kuu za mashahidi Rajaei na Bahonar ni kuwa na imani na malengo ya Imam Khomeini, ikhlasi, moyo wa kuhudumia wananchi, kujitolea kwa ajili  ya wananchi, kuwa pamoja nao, kutofanya cheo kama wasila na chombo cha kudhamini mali kwa ajili ya mustakbali wao na kushikamana barabara na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, viongozi na maafisa wa serikali wanapaswa kuelewa kuwa mienendo, maisha na mahusiano yao vinatengeneza utamaduni katika jamii.
Baada ya utangulizi huo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amemshukuru Rais na baraza lake la mawaziri kutokana na juhudi na bidii yao kubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Ameashiria ripoti zilizotolewa na mawaziri kadhaa katika kikao hicho na kusema: Ripoti zilizotolewa leo ni nzuri na zinazofaa na zinapaswa kuwasilishwa kwa wananchi. Hata hivyo amesisitiza kuwa, ripoti zinazotolewa na maafisa wa serikali zinapaswa kuwa kwa namna ambayo zitasadikiwa na wananchi kwa kutilia maanani uhakika wa mambo katika maisha yao.
Ayatullah Khamenei ameendelea kwa kuashiria baadhi ya kazi nzuri zilizofanywa na serikali na kusema: Kupungua mfumuko wa bei, utulivu na uthabiti wa wastani katika medani ya uchumi na kudhibitiwa hali hiyo ni miongoni mwa hatua nzuri za serikali ambazo zinapaswa kudumishwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Hatuko radhi kuona mfumuko wa bei na ughali wa gharama za maisha zikifikia tarakimu mbili na mfumuko huo kwa kila mwaka unapaswa kuwa chini ya asilimia kumi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, juhudi za serikali kwa ajili ya kuondoka katika kwamo wa kiuchumi, mradi wa marekebisho katika sekta ya afya, mipango ya kudumisha harakati ya kielimu nchini, kudhibiti maji na jitihada za kusimamia vyema utumiaji wake katika sekta ya kilimo na miradi ya umwagiliaji ni miongoni mwa hatua nzuri zilizofanywa na serikali. Ameashiria pia maudhui ya nyuklia na akasema: Kumalizika mazungumzo ya nyuklia ni miongoni mwa kazi muhimu sana zilizofanyika na tuna matarajio kwamba, kama kuna baadhi ya masuala na matatizo katika uwanja huu yatatuliwe.
Wakati huo huo katika suala hili la nyuklia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa miongoni mwa mambo yanayomtia wasiwasi ni uwezekano wa kutotiliwa maanani malengo ya maadui na akaongeza kuwa, tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu hadi hii leo uadui wa Wazayuni na Wamarekani dhidi ya Mapinduzi na Jamhuri ya Kiislamu haujapungua na uhakika huo haupaswi kupuuzwa kwa njia yoyote ile katika fikra za maafisa wa serikali.
Amesema kuwa, mbinu zinazotumiwa na adui na mapigo yake yumkini yakawa mapya lakini viongozi wote wa masuala ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni wanapaswa kuelewa kuwa, hawapaswi kushiriki katika mipango iliyobuniwa na adui na kusaidia utekelezaji wa njama za wageni kwa kutaka au bila ya kutaka.
Ayatullah Khamenei amesema malengo ya kihasama na ya wazi ya maadui yanaonekana katika matamshi na maandishi yao na mtu yeyote hapaswi kusahau kuwa kambi ya adui imesimama mbele ya taifa ikiwa na silaha iliyo tayari kutumiwa; hivyo sisi pia tunapaswa kuchukua maamuzi na kuchukua hatua mbele ya maadui kwa kupanga safu yetu vizuri.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, udharura wa kutambua uadui usiokoma wa Wazayuni na Wamarekani si makhsusi kwa viongozi wa serikali bali wananchi wote hususan wapenzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wanapaswa kuzingatia uhakika huo, japokuwa wadhifa wa viongozi wa serikali katika uwanja huo ni mkubwa zaidi.
Ayatullah Khamenei amesema, kuna udharura kwa kila mtu kuwa macho mbele ya jitihada zinazofanywa na adui kwa ajili ya kupenya na kuingia taratibu nchini na kuongeza kuwa: Kuna ulazima wa kuchukua misimamo ya kimapinduzi waziwazi katika mazingira yote na kutangaza misimamo ya Mapinduzi na misingi ya Imam Khomeini mbele ya adui tena waziwazi, bila ya kuona haya wala woga.
Amesema iwapo tutaghafilika, tutashtuka kwa kuona adui amepenya na kuingia katika baadhi ya maeneo na kuanza kazi hatari za kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa; kwa msingi huo tunapaswa kuwa macho kikamilifu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kulinda mshikamano na umoja wa wananchi ni miongoni mwa mambo ya dharura na kuongeza kuwa, hata katika maandamano ya tarehe 22 Bahman (11 Februari kwenye maadhimisho ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini) wananchi wote si kutoka kundi na mrengo mmoja, lakini mwelekeo wao ni mmoja; hivyo kuna ulazima wa kulindwa kikamilifu mshikamano na umoja huo katika jamii.
Ameongeza kuwa ili kuweza kulinda umoja huo katika jamii kuna ulazima wa kujiepusha na mambo yasiyo ya msingi na kujitenga na migawanyiko na vilevile kujiepusha na maneno na hotuba zinazovuruga umoja na mshikamano.
Baada ya hapo Ayatullah Khamenei ameeleza vipaumbele vya kipindi cha sasa hapa nchini kwa kusisitiza udharura wa kulindwa kasi ya sasa na maendeleo ya kielimu. Amesema elimu ndiyo msingi halisi wa maendeleo ya nchi na kadiri tunavyowekeza katika uwanja huo, basi huo ni uwekezaji kwa ajili ya mustakbali wa Iran. Amesema kuwa ratiba na jitihada zinapaswa kufanyika kwa ajili ya kudumisha kasi ya maendeleo ya kielimu katika muongo wa pili wa mpango wa maendeleo ya taifa, na kwa matashi yake Mwenyezi Mungu, tuweze kuwa kati ya nchi 10 bora duniani katika medani ya elimu na sayansi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mwenendo wa harakati ya kielimu hapa nchini kubadilika na kuwa mjadala wa watu wote katika muongo mmoja wa hivi karibuni ni dhamana ya kudumishwa ustawi wa kielimu na kuongeza kuwa, mjadala huo wenye msisimko na unaotia nishati unapaswa kudumishwa na kuimarishwa.
Ametilia mkazo udharura wa kutegemea mashirika ya kuzalisha elimu na mabustani ya elimu na teknolojia ambayo pia yanatayarisha nafasi za kazi na akasema: Fanyeni mikakati kwa njia ambayo wanafunzi wa vyuo vikuu wataweza kuingia katika soko la kazi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa utamaduni ni kipaumbele kingine katika kipindi cha sasa na kuongeza kuwa, matatizo ya kiuchumi hayaparaganyishi fikra lakini matatizo ya kiutamaduni wakati mwingine humnyima mtu usinguzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa uzalishaji wa bidhaa zinazofaa za kiutamaduni na kuzuia uzalishaji wa bidhaa zenye madhara ya kiutamaduni ni nyadhifa mbili kuu za viongozi wa serikali. Ameongeza kuwa, katika nchi zote duniani kuna usimamizi wa masuala ya kiutamaduni, kwa msingi huo kama baadhi ya bidhaa hizo- sawa ziwe za maonyesho (filamu na kadhalika) au za maandishi- zinapingana na misingi na sheria, zizuiyeni bila ya kuona haya.  
Amepinga suala la kuachiwa hivihivi (bila ya mipaka) sekta ya utamaduni na kusema: Medani ya utamaduni inapaswa kusimamiwa kwa mujibu wa misingi na kaulimbiu za Imam Khomeini na Mapinduzi ya Kiislamu na zizalishwe bidhaa salama za kiutamaduni kwa ajili ya jamii.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa uchumi ndio unaopaswa kupewa kipaumbele zaidi hapa nchini na amekumbusha nukta kadhaa katika uwanja huo. Nukta ya kwanza ni maendeleo yanayokwenda sambamba na uadilifu. Amesema kuna ulazimia wa kuwa macho katika harakati za kiuchumi ili kusiwepo ufa wa kimatabaka na haki za mafukara sizipotee.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kulifanya suala la kufanya kazi na bidii kuwa mjadala wa wananchi wote na kutangazwa uzembe na kutofanya kazi kuwa ni kitu kibaya na kisichofaa katika utamaduni wa jamii ni miongoni mwa mambo muhimu katika kupanga ratiba. Ameongeza kuwa, sambamba na kulingania na kuhamasisha ujasiriamali na uzalishaji wa utajiri nchini, kuna ulazima wa kuanzishwa maeneo sahihi ya kazi na kuwaonesha wananchi njia za kutafuta kazi kupitia vyombo vya habari. Amesema baadhi ya vipindi vya redio na televisheni vimefanya kazi nzuri katika uwanja huu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria uwezo mkubwa wa nchi hii kwa ajili ya kupata ustawi mkubwa wa kiuchumi na akasema: Suala la usimamizi mzuri wa biashara ya nje lina umuhimu mkubwa. Vilevile amesisitiza suala la kuwepo mabadilishano ya kiadilifu ya biashara na Iran kutofanywa soko la bidhaa za kigeni.
Ayatullah Khamenei ametilia mkazo uchumi ngangari na kusema, suala hilo linapaswa kuzingatiwa kikamilifu na serikali katika ratiba na mipango yote. Ametoa shukrani kwa ripoti zilizowasilishwa kwake na taasisi mbalimbali katika uwanja huo na kusema: Baadhi ya kazi zilizofanyika ni za msingi na utangulizi, baadhi hazihusiani na uchumi ngangari na baadhi nyingine ni kazi za kila siku za taasisi hizo ambazo zimeorodheshwa katika harakati na shughuli za uchumi ngangari.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa uchumi ngangari ni kifurushi kamili na chenye uwiano na ni matunda ya akili na fikra za kundi la watu, hivyo ili kufanishwa, kunahitajika pia mipango ya utekelezaji yenye uwiano na mlingano. Ameongeza kuwa, katika mipango hiyo kuna ulazima wa kuainishwa hisa na sehemu ya utekelezaji ya kila asasi na wakati wa utekelezaji wake, na sambamba na kuondolewa matatizo na vizuizi, shughuli za asasi na taasisi mbalimbali katika uwanja huo zifuatiliwe na kuchunguzwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa baada ya kubuniwa ratiba hiyo ya kiutekelezaji, hatua ya pili ya kufanikisha uchumi ngangari ni kuundwa kamati madhubuti ya uongozi, angavu na yenye mamkala ambayo itatayarisha uwanja mzuri wa kutekelezwa ratiba hiyo na kutoa ripoti kwa wananchi kwa kukagua na kuchunga shughuli hizo, kuchukua hatua za kutatua matatizo na kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati mwafaka.
Ayatullah Khamenei ameliambia baraza la mawaziri kwamba: Msijishughulishe na mpango wowote wa kiuchumi usiooana na sera za uchumi ngangari na tayarisheni haraka Mpango wa Sita wa Ustawi kwa msingi huo.
Amesema ni jambo la dharura pia kutumia uwezo wa sekta zisizo za serikali kama makundi ya kujitolea ya Basuj na kufaidika na wataalamu wa uchumi na wadau wa sekta hiyo kwa ajili ya kufanikisha uchumi ngangari.
Ayatullah Khamenei amesema, kama utekelezaji wa sera za uchumi ngangari unahitajia masuala ya kisheria na mahakama, Bunge na Idara ya Mahakama pia ziko tayari kutoa ushirikiano katika uwanja huo.
Ameashiria maudhui ya mdororo wa uchumi na ripoti ya Rais iliyosema kuwa uchumi umestawi kwa asilimia tatu na kusema: Ustawi huo ni ishara ya harakati ndogo ya kuondoka kwenye mdodoro, lakini iwapo hakutakuwepo mapambano makubwa dhidi ya mdodoro huo, ustawi wa sasa wa uchumi pia utakabiliwa na hatari, na ughali wa gharama za maisha utaanza tena kupanda juu.
Akiashiria makampuni ya kiuchumi yaliyokumbwa na matatizo kutokana na mdororo wa uchumi, Kiongozi wa Mapinduzi amesema: Baadhi ya vituo hivyo vya uzalishaji vina matatizo ya kifedha, hivyo benki zinawajibika kuingia katika medani kuhusu suala hilo, lakini makampuni mengine hayana matatizo ya fedha na yamepokea mikopo yao lakini yameitumia katika maeneo mengine; hivyo kuna udharura wa kukabiliana nayo ipasavyo.
Ayatullah Khamenei amesema ili kuweza kuondoa matatizo ya mdororo, baadhi ya miradi inapaswa kukabidhiwa kwa sekta ya watu binafsi.
Amezungumzia baadhi ya takwimu za kuwepo miradi yenye thamani ya bilioni arubaini elfu ambayo haijakamilika na akasema kuwa: Iwapo asilimia kumi ya miradi hiyo itatolewa kwa sekta ya binafsi, basi tumani bilioni elfu arubaini zitaingia katika mzunguko wa uchumi nchini na jambo hilo litakuwa na taathira kubwa katika kuondoa mdororo huo.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesisitiza udharura wa kupewa mazingatio zaidi sekta ya kilimo. Amesisitiza suala la kufanyika mikakati ya kujitosheleza katika bidhaa muhimu na akasema: Tunapaswa kutumia teknolojia ya kisasa katika sekta ya kilimo sambamba na kutumia uwezo wa wahandisi vijana katika mikoa mbalimbali.
Ayatullah Khamenei amesema ni muhimu kuzuia uagiza ovyo wa matunda mutoka nje ya nchi na akaongeza kuwa, tunapaswa kutilia maanani ipasavyo vijiji na viwanda vinavyobadili bidhaa ghafi (za sekta ya kilimo, ufugaji, uvuvi.. au process industries) na kutumia uwezo wa viwanda vya vijijini.
Amesema sekta ya madini pia ni miongoni mwa maeneo yenye uwezo mkubwa kwa nchi. Ameongeza kuwa sekta ya mafuta ambayo imeporomoka kutoka dola mia moja (kwa pipa) hadi dola arubaini kutokana na ishara tu ya madola ya kibeberu na baadaye hatua za watu waovu katika eneo hili la Mashariki ya Kati, haiwezi kutegemewa, kwa msingi huo kuna ulazima wa kufikiria njia mbadala inayofaa, na njia bora zaidi ya mbadala ni sekta ya madini. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema tunapaswa kutumia uwezo wa sekta binafsi katika madini na kujiepusha na kuuza madini ghafi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa maudhui ya maji na utumiaji wake kwa njia sahihi na vilevile marekebisho ya umwagiliaji katika sekta ya kilimo vina umuhimu mkubwa.
Mwanzoni mwa mkutano huo Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa ripoti kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali katika nyanja mbalimbali katika miaka miwili iliyopia.
Rais Rouhani amesema kuleta utulivu katika anga ya kiuchumi na kijamii hapa nchini ndiyo matunda makubwa zaidi na mtaji muhimu wa serikali katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Ameongeza kuwa serikali yake imefanya juhudi kubwa kuhakikisha kwamba inatekeleza ahadi ilizotoa ikiwa ni pamoja na kupunguza mfumuko wa bei na ughali wa gharama za maisha.
Rais Rouhani amesema kuiondoa nchi katika mgogoro ni miongoni mwa hatua zilizochukulwia na serikali kwa ajili ya kutekeleza ahadi zake na kuongeza kuwa, kuondoka katika mporomoko wa uchumi na kufikia ustawi wa asilimia 3 wa uchumi katika mwaka 1393 (uliomalizika Machi mwaka huu wa 2015) ni ishara ya wazi ya kuondoka katika mdororo na tinatarajia kwamba ustawi huo utaendelea katika mwaka huu.
Amesisitiza kuwa serikali inalipa umuhimu suala la utekelezaji wa sera za uchumi ngangari na kusema: Kuzidisha asilimia 19 ya bidhaa zisizo za mafuta zinazouzwa nje ya nchi na kuleta mlingano baina ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na zile zinazuzwa nje ya nchi ni miongoni mwa ishara za harakati katika njia ya kuelekea kwenye uchumi ngangari. Amesema, katika kipindi cha miaka miwli iliyopita serikali imekumbana na vizingiti vikubwa kikiwemo kile cha kutoa ruzuku ya fedha kwa wananchi.
Amesisitiza udharura wa kufutwa hatua kwa hatua ruzuku ya fedha zinazotolea kwa wananchi na kusema kuwa mradi wa ujenzi wa nyumba wa Maskane Mehr ni miongoni mwa vizingiti vikubwa vinavyoikabili serikari ya awamu ya 11. Ameongeza kuwa, madeni yaliyoachwa na serikali uliyopita ni kizingiti kingine mbele ya serikali ya sasa.
Akitoa tathminbi kuhusu utendaji wa serikali katika masuala ya uchumi, Rais Hassan Rouhani amesema kuwa umekuwa na mafanikio ya wastani. Ameongeza kuwa: Katika kipindi kipya cha baada ya vikwazo tunahitajia mipango mipya ili pamoja na kuzidisha uzalishaji wa ndani, tuweze kuvutia mitaji na uwekezaji mpya wa kigeni na vilevile teknolojia mpya.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na serikali yake ni kujali zaidi haki za raia na kuchunga haki na kamu na madhehebu zote. Ameashiria nafasi ya 15 ya Iran katika masuala ya sayansi na elimu duniani na akasema kuwa: Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kumeanzishwa mfuko wa uvumbuzi na kuchanua kwa vipawa na mwaka huu kumetengwa mkopo wa tumani bilioni 1500 kwa ajili ya mashirika yanayozalisha elimu.
Kuhusu utendaji wa serikali ya awali ya 11 katika sekta ya siasa za nje, Rais Rouhani amesema kuwa mapatano ya nyuklia yaliyofikiwa chini ya mwongozo wa Kiongozi Muadhamu ndio matunda muhimu zaidi katika uwanja huo. Amesema kuwa timu ya Iran katika mazungumzo hayo haikutetereka na ilitetea maslahi ya taifa, heshima ya nchi na uwezo wa kujihami wa Iran kwa uhuru na ushujaa na imefanya kazi kubwa.
Rais Rouhani amesema kuwa kulinda teknolojia ya nyuklia na kuifanya ya kibiashara, kufutwa maazimio ya awali ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Iran, kuondolewa vikwazo vya kifedha na kiuchumi baada ya utekelezaji wa makubaliano na kuondolewa faili la Iran katika Baraza la Usalama baada ya miaka kumi ijayo ni miongoni mwa matunda ya mazungumzo ya nyuklia.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ameashiria hatua zilizochuliwa na serikali yake katika nyanja za utamaduni, jamii na afya na akasema: Miongoni mwa changamoto zinazoikabili serikali ni kusimamia uchaguzi wa Bunge na Najisi ya Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu katika mwezi Esfand mwaka huu (mwanzoni mwa mwaka ujao wa 2016). Amesema kuwa serikali inawajibika mbele ya sheria na inaheshimu taasisi zote zinazohusiana na masuala ya uchaguzi.
Baada ya hotuba fupi na Bwana Is’haq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais, Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran pia alitoa ripoti kuhusu utendaji wa wizara hiyo. Amesema kuwa sekta ya viwanda imestawi kwa asilimia 6.7 na kwamba uwekezaji katika sekta hiyo umeongezeka. Vilevile Waziri Neematzadeh amesema kuwa uuzaji nje wa bidhaa zisizo za mafuta umeongezeka kwa asilimia 19 na kuongeza kuwa: Serikali imezuia uagizaji wa magari ya kifahari na imebana uagizaji wa bidhaa zisizo za dharura na inafanya jitihada za kutayarisha bidhaa zinazohitajiwa na taasisi za serikali hapahapa ndani ya nchi.
Kutayarishwa asilimia 80 ya ardhi hapa nchini kwa ajili ya kuvumbua madini na kukamilisha myororo wa uzalishaji wa madini ni miongoni mwa mafanikio mengine ya Wizara ya Viwanda, Madini na Biashara yaliyotajwa na Bwana Neematzadeh.
Katika ripoti yake kwenye kikao hicho pia Waziri wa Nishati, Bwana Hamid Chitchian amesema changamoto kubwa inayoikabili wizara hiyo ni ufa mkubwa uliopo baina ya mapato na matumizi yake, rundo kubwa la madeni, ukame, mabadiliko ya hali ya hewa na utumiaji ovyo na kinyume cha sheria wa malisili za chini ya ardhi.
Waziri wa Nishati amesema kuwa uzinduzi wa vutuo 29 vya umeme vyenye uwezo wa kuzalisha megawati 4000, mipango ya kupunguza hasara za mtandao wa kusambaza umeme, utumiaji wa teknolojia 17 mpya katika sekta ya umeme kwa kutegemea uwezo wa ndani ya nchi na uuzaji nje huduma za uhandisi zenye thamani ya mabilioni ya dola ni miongoni mwa kazi zilizofanywa na wizara hiyo katika sekta ya umeme.
Kwa upande wake Waziri wa Mafuta wa Iran, Bijan Zangeneh amesema kuwa mipango ya serikali katika medani za mafuta zinazomilikiwa kwa pamoja kati ya Iran na nchi jirani ni kuzidisha uzalishaji. Amesema kuwa katika medani hizo za pamoja za mafuta, uzalishaji wa bidhaa hiyo umeongezeka kutoka mapipa 70 elfu kwa siku hadi mapipa laki moja katika mwaka huu, na katika mwaka ujao uzalishaji huo utaongezeka na kufikia mapipa laki mbili na 60 elfu.
Waziri wa Mafuta ameashiria ongezeko la asilimia 12 la uzalishaji wa gesi katika mwaka uliopita na akasema kukamilishwa awamu 25 kati ya 27 za mradi wa gesi wa Pars Kusini hadi kufikia mwishoni mwa kipindi cha serikali ya sasa na kusambaza gesi kwa kaya milioni 2.5 nchini miongoni mwa mipango ya Wizara ya Mafuta hadi mwishoini mwa kipindi cha serikali ya sasa.
Waziri wa Mafuta ameashiria suala la kuongezeka uuzaji nje mafuta kwa asilimia 15 katika miezi minne ya mwanzoni mwa mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka uliopita na kusema: Sekta ya mafuta ilikuwa miongoni mwa taasisi kuu zilizolengwa kwa vikwazo vya maadui lakini tumeweza kupeleka mbele kwa nguvu mipango na ratiba zetu katika mazingira hayo.
Vilevile Mawaziri wa Jihadi ya Kilimo na Afya wametoa ripoti kuhusu utendaji wa wizara zao katika kikao hicho.
                                                    
        
          
         

700 /