Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Viongozi wa serikali wanapaswa kujibu rasmi matamshi mabaya ya maafisa wa Marekani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo (Alkhamisi) amekutana na wawakilishi wa Baraza la Wataalamu na kulitaja baraza hilo kuwa ni dhihirisho kamili la demokrasia ya Kiislamu na sababu ya sakina na utulivu katika jamii. Amewausia maafisa wote hapa nchini kufanya harakati na juhudi katika fremu ya mfumo wa fikra wa Kiislamu na kuchunga wasije kutumbukia katika sera za mfumo wa kibeberu au kuwa bamba lake la kupigia muhuri. Amesema kuwa wadhifa muhimu zaidi wa maulama wa dini, wasomi wa vyuo vikuu  na maafisa wa utawala ni kuwa macho zaidi kuhusu mipango ya adui, kuitambua na kueleza mustakbali unaotia matumaini na wenye maendeleo ya nchi katika fremu ya vigezo vya mfumo wa kifikra wa Uislamu, kwa kutumia uwezo na vipawa vya vijana na uwezo wa taifa.
Vilevile Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia nukta kadhaa kuhusu makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei ameashiria baadhi ya aya za Qur'ani Tukufu zinazohusu kuteremshwa sakina na utulivu wa Mwenyezi Mungu kwenye nyoyo za waumini kupitia njia ya kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu na kuwa na dhana nzuri kwa ahadi zake. Amesema Majlisi ya Wataalamu inatayarisha uwanja mzuri wa kuteremshwa sakina na utulivu katika jamii. Akieleza sababu ya suala hilo, Ayatullah Khamenei amesema: Majlisi ya Wataalamu ndiyo majlisi pekee kunakofanyika chaguzi mbili, uchaguzi wa wawakilishi wa majlisi hiyo unaofanywa na wananchi na ule wa kumchagua Kiongozi Mkuu unaofanywa na Majlisi ya Wataalamu.
Amesema kuwa kwa mujibu wa chaguzi hizo mbili Majlisi ya Wataalamu kwa upande mmoja ni dhihirisho kamili la demokrasia ya kidini na demokrasia ya Kiislamu, na kwa upande wa pili ni kielelezo cha utawala wa thamani na sheria za Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: Wakati inapoundwa majlisi ya wataalamu yenye sifa hizo za kipekee, hudhirisha wawakilishi wake, uhuru wao wa kifikra na umakini wao na suala hilo hutayarisha uwanja wa sakina na utulivu katika jamii.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, katika chaguzi zote mbili za Majlisi ya Wataalamu kuna ulazima wa kuchungwa umakini ipasavyo na kuwa na uhuru wa kifikra na kuongeza kuwa, uhuru wa kifikra una maana ya wawakilishi wa Majlisi ya Wataalamu kutokuwa mateka na mabamba ya chapa na sera za ubeberu.
Ayatullah Khamenei amesema maagizo haya si kwa ajili ya wawakilishi wa Baraza la Wataalamu pekee bali maafisa wote na nguzo za utawala hapa nchini na shakhsia wa kisiasa, kijamii na kidini wanapaswa kuwa macho ili wasije kutumbukia katika fasihi na kuwa mabamba ya chapa ya mfumo wa ubeberu.
Ameashiria juhudi na propaganda kubwa zinazofanywa na ubeberu kwa ajili ya kuwatwisha fasihi na maneno yao bandia viongozi, wachukuaji maamuzi na watengenezaji maamuzi katika nchi mbalimbali na akasema: Katika fasihi ya mfumo wa ubeberu, vitu kama ugaidi na haki za binadamu vina maana makhsusi na katika fasihi hiyo mashambulizi mfululizo ya miezi sita dhidi ya watu wa Yemen na kuuliwa watu wasio na hatia wa Gaza si ugaidi; vilevile ukandamizaji unaofanywa dhidi ya wananchi wa Bahrain kwa sababu tu ya kudai haki zao hauhesabiwi kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu!
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, katika fasihi ya mfumo wa ubeberu, kujitetea kwa wanamapambano wa Lebanon na Palestina kunatambuliwa kuwa ni ugaidi, lakini hatua za nchi za kidikteta na washirika wa Marekani katika Mashariki ya Kati si ukiukaji wa haki za binadamu!
Ayatullah Khamenei amesema: Katika fasihi hiyo mauaji ya wataalamu wa nyuklia ambayo Wazayuni wamekiri karibu waziwazi kuwa ndio walioyafanya na baadhi ya nchi za Ulaya zimekiri kuwa zilihusika katika mauaji hayo, hayahesabiwi kuwa ni ugaidi!
Amesema kubuni maana kama hizo na kutarajia kwamba watu wote watazungumza katika fremu ya fasihi hiyo ni miongoni mwa alama kubwa za ubeberu. Ameongeza kuwa, mkabala wa hali hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ina mfumo wa kifikra wa Kiislamu ambao ungali na mvuto na upya.
Akifafanua zaidi vipengee vya mfumo huo wa kifikra, Ayatullah Khamenei ametaja vita na upinzani dhidi ya dhulma, ubeberu na udikteta, hadhi na heshima ya kitaifa na Kiislamu na kujitegemea kifikra, kisiasa na kiuchumi kuwa ni sehemu ya mfumo huo. Kuhusu umuhimu wa kujitegemea na mchango wake katika kujiamini na maendeleo ya taifa, amesema kuwa: Kujitegemea ni sehemu ya uhuru, kwa msingi huo wale wanaopinga suala la kujitegemea na kujitawala kwa hakika wanapinga uhuru.
Amesema kaulimbiu ya "Kujitawala, Uhuru na Jamhuri ya Kiislamu" inaonesha mfungamano wa kimantiki wa mambo hayo matatu na kuongeza kuwa: Kujitawala katika pande zote na uhuru wa kifikra na kivitendo yote mawili yamo katika mfumo wa kifikra wa Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, na mfumo kama huo wa kifikra unatayarisha uwanja mzuri wa kujiamini na harakati na maendeleo ya taifa lolote.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mtindo wa maisha wa Kiislamu, uvumbuzi na muawana, na mshikamano wa kitaifa ni sehemu nyingine za mfumo wa kifikra wa Kiislamu. Ameongeza kuwa katika kipindi chote cha miaka 36 iliyopita taifa la Iran liliweza kupata maendeleo makubwa kupitia harakati yake kwenye fremu ya mfumo huu wa kifikra licha ya kuwepo vizuizi vingi.
Ayatullah Khamenei amesema upeo unaokusudiwa na mfumo wa Kiislamu hapa nchini ni Iran yenye maendeleo katika upande wa elimu na viwanda, yenye jamii ya watu milioni 150 hadi 200, yenye masuala ya kimaanawi na kiroho, iliyojitenga na ubeberu lakini inayokabiliana na madhalimu na mabeberu. Amesema Jamhuri ya Kiislamu kupata nafasi hii ni jambo zito na linayoiumiza sana kambi ya ubeberu, na sababu ya njama na hila zote zinazofanyika dhidi ya utwala wa Kiislamu hapa nchini ni kuzia harakati ya kupatikana mustakbani kama huo.
Amesisitiza kuwa kudhihiri kwa nchi kama hiyo ya Kiislamu kutatayarisha uwanja wa kukunjwa jamvi la ubeberu na ukafiri na kuongeza kuwa taifa la Iran hususan vijana, maulama wa dini na wasomi wa vyuo vikuu wanapaswa kudumisha harakati yao katika fremu ya mfumo wa kifikra wa Kiislamu na watu wote wakiwemo vongozi wanalazimika kuwa macho na makini kuhusu mipango na njama za adui.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, hatupaswi kuhadaiwa na adui kutokana na tabasamu yake au wakati mwingine msaada wake wa muda mfupi katika maudhui makhsusi, bali daima tunapaswa kutaka kujua mipango na njama zake.
Ayatullah Khamenei amesisitiza tena kwamba adui na ubeberu wa kimataifa si ngano isiyo na msingi bali ni uhakika, na kielelezo chake kikubwa zaidi ni serikali ya Marekani na makampuni na mashirika ya kiuchumi ya kizayuni yanayoisaidia.
Ameashiria uwezo na vipawa vya vijana wenye imani na vilevile uwezo mkubwa, utajiri na maliasi za nchi, utamaduni mkubwa wa Kiislamu na utamaduni wa Ahlul Bait (as) kati ya wananchi na kusema: Maafisa wote na shakhsia wenye maneno yenye taathira katika jamii wanapaswa kuwafafanulia zaidi wananchi kuhusu mustakbali huo wa wazi, na sambamba na kuwapa matumaini ya mustakbali mwema, watayarishe uwanja mzuri wa kuwepo sakina na utulivu hapa nchini.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia masuala muhimu kuhusu mapatano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1, masuala ya baada yake na maudhui ya utekelezaji wa sera za uchumi ngangari.
Ayatullah Khamenei ameashiria mjadala wa siku hizi kuhusu nafasi ya majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) katika kuchunguza mapatano ya nyuklia kati ya Iran na 5+1 na kusema: "Kuhusu upande wa kisheria wa maudhui hii, weledi na wataalamu wa sheria wanapaswa kutoa maoni yao, lakini kwa mtazamo jumla mimi naamini – na pia nimemwambia Rais wa Jamhuri- kwamba si maslahi kuitenga Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu katika uchunguzi wa mapatano hayo."
Amesisitiza ulazima wa Bunge kuingia katika mjadala wa mapatano hayo na wakati huo huo amesema: "Mimi sitia nasaha zozote kuhusu namna ya kujadili mapatano hayo na kwamba je Bunge liyakubali au lisiyakubali, bali ni wabunge wenyewe waliochaguliwa na wananchi ndio wanaopaswa kuchukua maamuzi kuhusu suala hilo."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusiana na masuala ya baada ya mapatano hayo ya nyuklia kwamba: Mimi nimeshazungumza na ndugu zangu wapenzi serikalini kuhusiana na baadhi ya nukta zinazohusiana na suala hilo na hivi sasa napenda kubainisha nukta hizo mbele ya wajumbe wa Baraza la Wataalamu na mbele ya wananchi wote.
Ayatullah Khamenei ameashiria nchi sita zilizofanya mazungumzo na Iran kuhusu kadhia hiyo na nafasi ya Marekani kati ya nchi hizo sita na kuongeza kuwa: Kwa hakika, upande mkuu tunaokabiliana nao katika mazungumzo hayo ni Marekani, lakini inasikitisha kuona kuwa viongozi wa Marekani wanatoa maneno mabaya sana kuhusu suala hilo na inabidi tuainishe msimamo wetu mkabala wa matamshi hayo.
Ameashiria matamshi ya viongozi wa Marekani wanaoshikilia msimamo wa kubakishwa fremu ya vikwazo na kusema kuwa: Kama wamekusudia kubakisha fremu ya vikwazo, basi kwa nini sisi tulifanya mazungumzo nao? Jambo hilo kwa hakika linapingana kikamilifu na sababu zilizoifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenda kwenye meza ya mazungumzo hayo kwani lengo la mazungumzo lilikuwa kuondolewa vikwazo vyote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kama kwenye mazungumzo hayo tumelegeza kamba kidogo katika baadhi ya mambo, kimsingi tumefanya hivyo ili vikwazo viondolewe, la sivyo kulikuwa na ulazima gani wa kufanya mazungumzo? Sisi tungeweza kuendelea na kazi zetu kama kawaida na kuzidisha idadi ya mashinepewa 19 elfu tulizo nazo hadi mashinepewa elfu khamsini hadi elfu sitini, na tungeendelea na urutubishaji wetu wa urani kwa asilimia 20 na kuzidisha kasi kwenye suala la utafiti na kupanua zaidi miradi yetu ya nyuklia.
Ayatullah Khamenei amesisitiza pia kuwa: Kama imekusudiwa kutoondolewa vikwazo, basi hakuna haja ya kuwa na muamala wowote ule, hivyo suala hili linapaswa kuwekwa wazi.
Amewaambia viongozi nchini kwamba: Msiseme kuwa Wamarekani wametoa matamshi hayo ili kuwaridhisha wapinzani wao ndani ya Marekani, hata hivyo mimi ninaamini kuwa, mizozo ya ndani ya Marekani ni jambo lisilo na chembe ya shaka, naamini kuwa kuna hitilafu kubwa baina yao na sababu ya hitilafu hizo ziko wazi kwetu, lakini kinachosemwa rasmi, kinapaswa kujibiwa na kama hakitajibiwa basi maneno yanayotolewa na upande wa pili yatathabitishwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vilevile amegusia matamshi yanayotolewa na viongozi wa Marekani kuhusiana na kusitishwa vikwazo na kusisitiza kuwa: Tangu mwanzoni suala halikuwa hilo, sisi tumekuwa tukisisitiza kuwa vikwazo viondolewe na si kusimamishwa.
Ayatullah Ali Khamenei ameongeza kuwa: Tulivyotaka sisi ni kuondolewa mara moja vikwazo hivyo, lakini marafiki hapa wamelifafanua suala hilo na sisi hatukupinga, lakini vikwazo vyote lazima viondolewe kikamilifu. Kama itakuwa ni kusimamishwa kwa muda tu vikwazo, basi na sisi kwa upande wate tutaishia tu kusimamisha kwa muda masuala tunayotakiwa kuyafanya na si kuchukua hatua za kimsingi.
Ameongeza kuwa: Upande wa pili unasema kuwa, baadhi ya vikwazo hivyo haviko mikononi mwa serikali ya Marekani, na sisi tunasema: Hivyo hivyo vikwazo vilivyoko mikononi mwa serikali ya Marekani na mikononi serikali za Ulaya, vinapaswa kuondolewa.
Ayatullah Khamenei ametaja sehemu nyingine ya maneno mabaya yanayotolewa na viongozi wa Marekani kwamba ni matamshi yao yasiyo na uhusiano hata kidogo na kadhia ya nyuklia. Ameongeza kuwa, viongozi wa Marekani wanazungumza kama walivyokuwa wakizungumza Waingereza katika karne ya 19 kuhusiana na Iran, inaonekana viongozi wa Marekani wako nyuma ya dunia ya sasa na historia kwa karne mbili. Hawajui kuwa dunia imebadilika na madola ya kibeberu hivi sasa hayana tena uwezo na nguvu wa kufanya yanachotaka, na yanasahu kuwa katika upande wa pili kuna Jamhuri ya Kiislamu yenye uwezo na nguvu zinazotambulika na zisizotambulika ambazo zitaonekana wakati wa vitendo. Iran nayo si sawa na nchi fulani iliyobaki nyuma wanayozungumza nayo vyovyote wanavyotaka.
Akitoa mfano wa moja kati ya matamshi ya kibeberu ya viongozi wa Marekani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Viongozi wa Marekani wanasema wanatarajia kuwaona viongozi na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ikifanya mambo tofauti!
Ameongeza kuwa: Mambo tofauti katika mtazamo wa Wamarekani ni mambo yanayokwenda kinyume na misimamo ya awali ya Jamhuri ya Kiislamu, kupuuza thamani na matukufu ya Kiislamu na kuacha kushikamana na sheria za Kiislamu, lakini wajue kuwa jambo hilo kamwe halitatokea. Si serikali itafanya hivyo, si Bunge na si kiongozi yeyote yule wa Jamhuri ya Kiislamu, na kama atatokezea mtu akataka kufanya jambo hilo, basi wananchi wa Iran na Jamhuri ya Kiislamu kamwe hawatomruhusu kufanya hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia moja kati ya mambo yanayotarajiwa na Wamarekani kutoka kwa Iran akisema: Miongoni mwa siasa za Marekani katika eneo hili la Mashariki ya Kati, ni kuvifuta na kuviangamiza kikamilifu vikosi vya mapambano na kuzidhibiti kikamilifu nchi za Syria na Iraq na wanatarajia kuwa Jamhuri ya Kiislamu nayo itaungana nao katika hilo, jambo ambalo kwa hakika kamwe haliwezi kutokea.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia matamshi mengine yanayozusha hisia kali na ambayo yanatolewa na viongozi wa Marekani na kusema: Wamarekani wanasema mapatano ya nyuklia yameipatia Marekani fursa ndani ya Iran na nje ya Iran na katika eneo zima la Mashariki ya Kati.
Amewaambia viongozi wa serikali na taasisi nyingine akisema: Viongozi serikalini na katika taasisi nyingine mbalimbali hapa nchini hawapaswi kuruhusu kwa namna yoyote kufanikiwa siasa hizo za Marekani ndani ya Iran, na kuhusu nje ya Iran pia inabidi zifanyike jitihada za kutoipa Marekani fursa hizo, kwani kadiri Wamarekani wanavyokaribia kwenye fursa wanazotaja, ndivyo mataifa ya dunia yanavyozidi kudhalilishwa, kuingizwa katika matatizo na kuzidi kukandamizwa.
 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia sisitizo lake  kwa viongozi wote nchini Iran, -wa siasa za nje na wale wa taasisi nyenginezo- kuwa, ni marufuku kabisa kufanya mazungumzo na Marekani isipokuwa tu katika kadhia ya nyuklia na kuongeza kuwa: Sababu ya upinzani huo ni misimamo ya Marekani ambayo inakinzana kikamilifu na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia kadhia muhimu ya uchumi nchini Iran na kusema: Sera za Uchumi ngangari ni majimui iliyo kamili ambayo vipengee vyake haviwezi kutenganishwa na utekelezaji wake unalazimu kuweko mpango madhubuti wa kiutekelezaji, hivyo tumemtaka mheshimiwa Rais na serikali yake kuandaa mpango madhubuti, wenye manufaa na unaotekelezeka kwa ajili ya kufanikisha sera hizo za uchumi ngangari na ni matumaini yetu kuwa hilo litatendeka.
Kuhusu umuhimu wa kufanikishwa uchumi ngangari amesema kwamba: Kama uchumi ngangari utafanikiwa, basi hakutakuwa tena na umuhimu wa kujua kwamba fedha za Iran (zinazoshikiliwa nje) zitakazorejeshwa nchini ni dola bilioni 5 au dola bilioni 100; hata hivyo fedha ambazo tunadai duniani na ambazo zimezuiwa kidhulma lazima zirejeshwe na zitumika nchini, lakini uchumi ngangari haupaswi kuegemezwa kwenyesuala la  kurejeshwa fedha hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo ulazima wa kuundwa kamati maalumu na amilifu ya kusimamia utekelezaji wa siasa za uchumi huo na kusema: Kamati hiyo inapaswa kuundwa ndani ya serikali na kuanzisha harakati kubwa katika upande huo kwa kuainishwa mipaka ya kazi ya kila taasisi na kuandaliwa muda wa ufuatiliaji.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake Ayatullah Khamenei ameihutubu nguvu kazi ya watu wenye imani thabiti kote nchini Iran na kusema: Harakati kuu iliyopo nchini hivi sasa ni kuelekea kwenye thamani na malengo makuu ya Kiislamu na kwamba nguvu kazi ya watu wenye imani madhubuti na waumini wa kweli inayounda sehemu kubwa ya jamii ya Iran, inabidi sambamba na kuwa na matumaini kwa ahadi za Mwenyezi Mungu, iwe tayari kwa ajili ya kuchapa kazi katika medani tofauti za kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa na kusimama imara katika kukabiliana na njama mbalimbali za adui.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Yazdi, Mkuu wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu ametoa hotuba fupi na kusema kuwa sababu ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ni uongozi imara na wa busara wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) na ushujaa wa wananchi wa Iran kama ambavyo pia amegusia nukta kadhaa kuhusiana na kikao cha hivi karibu cha baraza hilo.
Vilevile Ayatullah Hashemi Shahroudi, Naibu wa Mkuu wa baraza la hilo ametoa ripoti kuhusiana na kikao cha kumi na nane cha baraza hilo na kusema kuwa ajenda ya kikao hicho ilikuwa kufanyia marekebisho kanuni na utaratibu wa idadi ya wajumbe wa baraza hilo.
Naibu wa Mkuu wa Baraza la Wataalamu ameashiria pia namna kikao hicho kilivyojadili hali ilivyo katika eneo la Mashariki ya Kati hivi sasa na fitna ya makundi ya kitakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu na kusema kuwa, kumejadiliwa pia suala la mazungumzo ya nyuklia kupitia kuita wageni mbali mbali mbele ya kikao hicho ili kutoa maelezo kuhusu mazungumzo hayo. Ameongeza kuwa: Kutolewa mapendekezo kuhusu njia za utatuzi wa masuala mbali mbali nchini, daghadagha na wasiwasi wa wajumbe wa Baraza la Wataalamu kuhusiana na masuala ya kiutamaduni, kuenziwa nafasi aali na tukufu ya mashahidi na harakati yenye thamani kubwa ya kiutamaduni ya taifa la Iran katika mazishi ya mashahidi hao, kuzingatia umuhimu wa uchaguzi ujao wa Baraza la Wataalamu na jukumu zito la Baraza la Kulinda Katiba kwa ajili ya kulinda nafasi na heshima ya baraza hilo na ulazima wa kuainishwa watu wenye sifa za kugombea kwa mujibu wa sheria pamoja na kutoa ripoti kuhusu maendeleo yaliyopatikana baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran katika mikoa iliyokuwa imebakishwa nyuma kimaendeleo hususan maeneo ya Waislamu wa Kisuni, ni miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa na kuzungumziwa kwenye kikao hicho cha Baraza la Wataalamu.
Vilevile Ayatullah Hashemi Shahroudi ameongeza kuwa: Wajumbe wa Baraza la Wataalamu wamesisitiza kuwa, mapatano ya nyuklia hayana maana ya kuwa na uhusiano wa kawaida na Marekani.

700 /