Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Si mantiki kwa baadhi ya nchi za Ulaya kufuata kibubusa sera za Marekani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alasiri ya leo alimkaribisha ofisini kwake Rais Heinz Fischer wa Austria aliyeko safarini hapa nchini. Katika mazungumzo yake na mgeni huyo, Ayatullah Ali Khamenei ameashiria uadui wa serikali ya Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu kutokana na Washington kupoteza maslahi yake hapa nchini Iran na kusisitiza kuwa, si jambo la mantiki kwa baadhi ya nchi za Ulaya kufuata kibubusa sera za kihasama za Marekani dhidi ya Iran. Hata hivyo amesema Austria si miongoni mwa nchi hizo na kuna ulazima kwa viongozi wa nchi hizi mbili kuweka mipango ya kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili.
Katika mazungumzo hayo Ayatullah Khamenei amesema lengo kuu la Mapinduzi ya Kiislamu ni kudhamini kheri na saada kwa ajili ya wananchi wa Iran na wanadamu wote chini ya kivuli cha kufuata njia ya Mwenyezi Mungu, utawala wa akili na imani sambamba na kuchapakazi. Ameongeza kuwa: Hata hivyo mwenendo wetu huo wa kuwatakia kheri wanadamu una maadui pia katika uga wa kimataifa wanaotaka kuzusha vita na mapigano baina ya mataifa mbalimbali; lakini Iran ina marafiki wengi wazuri na wa kweli kati ya serikali na mataifa mbalimbali.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria uadui usio wa kimantiki wa baadhi ya nchi za Ulaya dhidi ya Iran baada ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: Mapinduzi ya Kiislamu yaliwanyang’anya Wamarekani Iran ambayo walikuwa wakiidhibiti kikamilifu, na suala hilo ndiyo sababu ya uadui wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu; pamoja na hayo mwenendo wa baadhi ya nchi za Ulaya wa kuifuata kibubusa Marekani si wa kimantiki wala hauna msingi, hata hivyo Austria si miongoni mwa nchi hizo.
Amesisitiza umuhimu wa kufanyika mipango ya kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na kujibu swali la Rais Heinz Fischer wa Austria alimeiliza kuhusu kustakbali wa uhusiano wa Iran na nchi za Ulaya kwa kusema: Hadi sasa kumekuwepo matamshi kutoka upande wa serikali za nchi za Ulaya lakini inatupasa tusubiri athari za kivitendo za matamshi hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia vitendo na uharibifu unaofanywa na makundi potofu katika Mashariki ya Kati kwa kutumia jina la Uislamu na kusema: Kinachoarifishwa na makundi haya si Uislamu, bali Uislamu umesimama juu ya misingi imara ya kimantiki, kiimani na kiakili.
Katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Rais Hassan Rouhani, Bwana Heinz Fischer, Rais wa Austria ameishukuru Iran kwa ukarimu wake na kusema kuwa mazungumzo yake na maafisa wa serikali hapa nchini ni mazuri. Amesema kuna udharura wa kutiliwa mkazo mambo yote na kufanyiwa kazi yaliyozungumzwa ili kufikiwa mapatano.
Rais wa Austria ameeleza kufurahishwa kwake na mtazamo chanya wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu nchi yake na kusema: Mazungumzo yangu na Bwana Rouhani yalikuwa mazuri na sisi tuna matumaini ya mustakbali mzuri.
Ameongeza kuwa, sasa kumejitokeza fursa mpya kwa ajili ya ushirikiano.                

700 /