Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Utawala wa Kizayuni wa Israel hautakuwepo tena baada ya miaka 25

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo asubuhi (Jumatano) amehutubia mjumuiko mkubwa wa maelfu ya wananchi wa matabaka mbalimbali ambapo ameonya kuhusu njama za Marekani za kutaka kujipenyeza katika baadhi ya masuala ndani ya Iran.  Ameutaja uchumi wenye nguvu na ngangari, maendeleo na ustawi endelevu wa kielimu na kulindwa na kuimarishwa moyo wa kimapinduzi hususan baina ya vijana kuwa ni mambo matatu muhimu ya kuweza kukabiliana kwa umakini na kwa nguvu zote na uadui usio na mwisho wa Shetani Mkubwa, Marekani. Vilevile amebainisha nukta kadhaa kuhusiana na uchaguzi wa mwezi Esfand 1394 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia - mwezi Machi 2016) na kuongeza kuwa: Matokeo ya kila uchaguzi ni haki ya watu kama ilivyo kila kura ya mwananchi, na kwamba haki hiyo ya taifa italindwa kwa nguvu zote.
Ayatullah Khamenei amegusia pia siku zilizojaa baraka za mwezi wa Mfunguo Pili Dhulqa'ada na umuhimu wa kutumia vizuri fursa hiyo yenye thamani kubwa na ameutaja mwezi wa Shahrivar (mwaka wa Kiirani) kuwa ni mwezi wenye kumbukumbu zenye maana kubwa. Ameongeza kuwa: Katika matukio yote ya mwezi huu (wa Shahrivar) yakiwemo ya kuuliwa watu wasio na hatia na utawala wa Kipahlavi hapo tarehe 17 Shahrivar 1357 (8 Septemba 1978), kuuliwa Rais na Waziri Mkuu (wa Iran) tarehe 8 Shahrivar 1360 (30 Agosti 1981), kuuliwa kigaidi Ayatullah Quddusi na shahid Ayatullah Madani katika mwezi huo huo pamoja na uvamizi wa Saddam nchini Iran tarehe 31 Shahrivar 1359 (22 Septemba 1980), kunashuhudiwa mkono wa Marekani kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kwenye matukio hayo.
Vilevile ameelezea wasiwasi wake kutokana na kuanza kusahauliwa pole pole kumbukumbu hizo zenye mazingatio makubwa hususan kati ya vijana nchini na kuzilaumu taasisi husika kwa kutotekeleza inavyotakiwa majukumu yao katika suala hilo.
Ameongeza kuwa: Matukio kama hayo yenye kutoa ibra hayapaswi kusahauliwa katika kumbukumbu za kihistoria za taifa kwani kama kizazi cha vijana kitasahau matukio kama hayo na sababu za kutokea kwake, basi vizazi vijavyo vitashindwa kujua njia sahihi za kutatua matatizo kama hayo na kizazi hicho kinaweza kufanya makosa katika mustakbali.
Ayatullah Khamenei amekumbushia pia baadhi ya ushahidi wa namna Wamarekani walivyokuwa na udhibiti mutlaki wa masuala ya Iran katika kipindi cha utawala wa Kipahlavi na kuongeza kuwa: Nguzo zote za utawala wa taghuti ikiwemo serikali na Baraza la Mawaziri na hata Shah mwenyewe, wote walikuwa mikononi mwa Marekani, na viongozi wa Marekani kupitia kwa vibaraka wao, wakawa mithili ya Firauni wakiliendesha taifa la Iran kidhulma; lakini Imam wetu mtukufu kama Musa wa zama hizi, alitumia uungaji mkono wa wananchi wa Iran na kukunja jamvi la Wamarekani katika ardhi hii yenye historia kongwe.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kufungwa mirija ya maslahi haramu ya Wamarekani nchini Iran kuwa ndiyo sababu kuu inayowafanya Wamarekani waifanyie uadui usio na mwisho Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran.
Ayatullah Khamenei pia ameitaja hatua ya kihistoria ya Imam Khomeini ya kuiita Marekani kuwa ni Shetani Mkubwa kwamba ni harakati yenye maana kubwa sana na kuongeza kuwa: Mkuu wa mashetani wote duniani ni Ibilisi, lakini kazi pekee ya Ibilisi ni kuwalaghai na kuwadanganya watu wakati ambapo Marekani inalaghai, inaua, inaweka vikwazo, inahadaa na inafanya ria.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewalaumu vikali watu ambao wanajaribu kumfanya ibilisi Marekani aonekane kwa sura nzuri na ya malaika mwokozi na kusema: Hata tukiweka pembeni mafundisho ya kidini na msimamo wa kimapinduzi, hata suala la kuwa waaminifu kwa maslahi ya nchi na akili tu, haliruhusu kufanya kitu kama hicho. Akili gani na dhati gani ya nafsi inayoweza kuruhusu kumfanya mtenda jinai kama Marekani aonekana mzuri na rafiki awezaye kuaminiwa?
Vilevile ameonya kwa mara nyingine kuhusiana na siasa na mbinu zinazotumiwa na Marekani kwa ajili ya kujipenyeza nchini Iran na kuongeza kuwa: Shetani ambaye amefukuzwa na taifa la Iran anafanya njama za kurejea kupitia dirishani, nasi hatupaswi hata chembe kuruhusu jambo hilo kutokea.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa uadui wa Wamarekani dhidi ya taifa la Iran hauna mwisho na ametoa mfano wa uhakika huo akisema: Hata katika siku hizi za baada ya kufikiwa mwafaka wa nyuklia (baina ya Iran na kundi la 5+1) mwafaka ambao hadi hivi sasa haujajulikana hatima yake nchini Iran na Marekani, Wamarekani katika baraza la Congress wameshughulika kufanya njama na kuandaa muswada wa kuiwekea vizuizi Iran.
Amesema, njia pekee ya kuweza kumaliza njama hizo za Wamarekani ni kwa Wairani kuwa imara kitaifa na kuongeza kuwa: Tunapaswa kuwa na nguvu na kuwa imara kiasi kwamba shetani mkubwa aweze kukata tamaa na kuvunjika moyo kuhusu kufanikiwa njama na uadui wake kwetu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha pia njia za kuweza kupata nguvu na uimara wa kitaifa kwa kusisitizia nukta tatu kuu ambazo ni: "Kuwa na uchumi wenye nguvu na usiotetereka," "kuwa na elimu iliyopiga hatua na inayozidi kustawi kila uchao" na "kulindwa na kutiwa nguvu moyo wa kimapinduzi hususan kati ya vijana."
Amesema kuhusu nukta ya kwanza kwamba: Uchumi wenye nguvu na usiotetereka utaweza tu kupatikana kupitia utekelezaji wa kina na wa bila ya kuchelewesha muda wa siasa zilizowasilishwa za uchumi wa kusimama kidete na wa kimuqawama ambapo tab'an tayari serikali imeanza kulishughulikia suala hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema pia kuwa, suala la ustawi wa kielimu sambamba na kulindwa na kuhifadhiwa kasi ya maendeleo ya kielimu nchini ni jambo muhimu sana na kuongeza kuwa: Kutia nguvu moyo wa kimapinduzi na kusimama kidete kati ya wananchi ni miongoni mwa njia bora kabisa za kujiimarisha taifa na kwamba viongozi nchini wanapaswa kuwaenzi na kujua umuhimu wa vijana wanamapinduzi.
Ayatullah Khamenei amegusia pia njama za adui za kueneza tabia ya kutojali na kutoshughulishwa na masuala muhimu baina ya vijana nchini Iran na kuongeza kuwa: Maadui wanataka kuua moyo wa hamasa na wa kimapinduzi wa vijana wetu na cha kusikitisha ni kuona kuwa ndani ya Iran pia kuna baadhi ya watu utawasikia wakiwapachika majina mabaya vijana wanamapinduzi kama vile kuwaita watu wenye misimamo mikali, suala ambalo kwa kweli ni kosa kubwa sana.
Baada ya kubainisha njia za kuweza kupata nguvu za kitaifa zinazoongezeka kila leo na kumvunja moyo pamoja na kumkatisha tamaa adui, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Wamarekani hivi sasa kwa namna fulani wamegawana kazi na wanaamiliana kindumilakuwili na Iran. Baadhi yao wanaichekea na kuionesha tabasamu Iran na baadhi yao wamo katika kuandaa muswada dhidi ya Iran.
Ameutaja muamala wa Wamarekani kuhusiana na mazungumzo na Iran kuwa ni kisingizio cha kutaka kujipenyeza White House na kutwisha siasa zake ndani ya Iran na kusisitiza kuwa: Sisi tumeruhusu kufanyika mazungumzo kati yetu na Marekani kuhusu kadhia ya nyuklia tu tena kwa sababu maalumu zilizotangazwa hadharani na Alhamdulillah timu yetu ya mazungumzo nayo imefanya kazi nzuri katika mazungumzo hayo, lakini sisi hatufanyi mazungumzo na Marekani katika maudhui yoyote nyengine.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Tab'an sisi tunafanya mazungumzo na tuna maelewano na nchi nyingine zote katika ngazi tofauti za kiserikali, za kikaumu na za kidini, ukitoa shetani mkubwa Marekani.
Vilevile amegusia uhakika wa kuwa pandikizi utawala wa Kizayuni wa Israel na kuongeza kuwa: Baadhi ya Wazayuni wamesema kuwa, kutokana na matokeo ya mazungumzo ya nyuklia, wamepata utulivu wa moyo wa miaka 25, lakini sisi tunawaambia, kwanza kabisa ni kuwa hiyo miaka 25 hamtaiona kamwe na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, wakati huo hakutakuwa tena na kitu kinachoitwa utawala wa Kizayuni katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Katika kipindi cha hivi sasa pia, moyo wa mapambano ya Kiislamu na moyo wa kihamasa na kijihadi daima utaendelea kuwasakama Wazayuni na hautaupa raha hata kidogo utawala huo dhalimu.
Sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameihusisha na kuzungumzia nukta muhimu kuhusiana na uchaguzi wa mwezi Isfand 1394 (mwezi Machi 2016).
Aidha amewalaumu wale watu ambao tangu mwaka mmoja na nusu kabla ya uchaguzi wamekuwa wakijiandaa na kujishughulisha na uchaguzi huo na kusema kuwa: Kufanya hivyo si kwa maslahi ya nchi yetu kwani wakati anga ya ushindani na mchuano wa uchaguzi inapofanywa kuwa jambo la asili, hupelekea mambo ya asili kuwekwa pembeni na jambo hilo halina faida kwa wananchi na wala kwa nchi, lakini hivi sasa umewadia wakati wa kugusia baadhi ya nukta kuhusiana na uchaguzi huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, suala la uchaguzi ni muhimu mno na ni dhihirisho la ushiriki wa wananchi katika maamuzi ya nchi yao kama ambavyo ni dhihirisho la imani ya wananchi kwa mfumo wao wa utawala na ni nembo ya kutawala mfumo wa demokrasia ya kweli ya kidini nchini Iran.
Ameongeza kuwa: Ni kutokana na umuhimu wake huo mkubwa usio na mbadala ndio maana suala la kufanyika chaguzi nchini Iran halijawahi kucheleweshwa hata kwa siku moja katika kipindi chote hiki cha miaka 37 iliyopita na hakuna sababu wala hali yoyote iwayo iliyozuia kufanyika chaguzi hizo hata katika nyakati ngumu kabisa. Tab'an kuna baadhi ya watu wenye muono finyu wa kisiasa walitaka wakati fulani kuakhirisha uchaguzi lakini hawakupewa fursa ya kufanya hivyo.
Ayatullah Khamenei amekumbushia propaganda zisizosita za Marekani na vitimbakwiri vyake dhidi ya chaguzi za nchini Iran na kuongeza kuwa: Maadui hao katika vipindi vyote vya utawala wa taghuti nchini Iran (kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu) hawakulalamikia uchaguzi hata mmoja uliofanyika nchini Iran licha ya kuwa chaguzi zote hizo zilikuwa za kimaonyesho tu na hivi sasa pia Wamarekani wanazinyamazia kimya tawala za kidikteta na za kurithishana za eneo la Mashariki ya Kati bila ya kuonesha upinzani wowote ule, lakini inapofika suala la Iran na licha ya kuwa nchini humo mumefanyika makumi ya chaguzi za kidemokrasia kikamilifu, siku zote utawasikia Wamarekani wanalalamikia chaguzi hizo na kuziangalia kwa mtazamo hasi.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, chaguzi zote zilizofanyika nchini Iran katika kipindi cha miaka 37 iliyopita ni chaguzi salama kabisa na kuongeza kuwa: Chaguzi nchini Iran zinafanyika kwa viwango vinavyotambuliwa kimataifa na kwa mujibu wa viwango hivyo, chaguzi hizo za Iran ni miongoni mwa chaguzi salama na zilizofikia viwango vya juu vya ubora, lakini cha kusikitisha ni kuwa, kuna baadhi chache ya watu ndani ya Iran wanajaribu kutia dosari chaguzi hizo kwa hatua zao ghalati kiasi kwamba watu hao wanadai hata kabla ya kufanyika uchaguzi kuwa eti wana wasiwasi na usalama na kuheshimiwa haki katika uchaguzi huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislaamu amekutaja kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran katika chaguzi zote za miongo mitatu iliyopita kuwa ni uthibitisho wa jinsi wananchi hao wanavyouamini na kuukubali mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuhoji kwa kusema: Kwa nini kuna baadhi ya watu wanajifanya kuwa na wasiwasi ili - Mungu apishie mbali - waitiea doa imani hiyo ya wananchi?
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Ni jambo lililo wazi kwamba katika suala la usalama wa uchaguzi ni kuwa, kuna sheria na usimamiaji mzuri na makini katika chaguzi zinazofanyika nchini Iran na mtu yeyote haruhusiwa kufanya mambo yatakayoutia dosari uchaguzi huo, sasa cha kujiuliza kuwa, wanaosema maneno hayo wana malengo gani?
Ameendelea kuzungumzia namna uchaguzi nchini Iran unavyofanyika kwa usalama, uwazi na haki ya hali ya juu kwa kugusia nafasi muhimu ya sheria na Baraza la Kulinda katiba na kuongeza kuwa: Moja ya baraka kubwa za kuwepo Baraza la Kulinda Katiba ni kusimamia na kuzuia kutokea kosa au dosari yoyote ile na tab'an ziko na taasisi na vyombo vingine vinavyofanya kazi hiyo ili kuhakikisha chaguzi zinakuwa za wazi, salama na za haki kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kubainisha uwazi na usalama wa chaguzi za nchini Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuongeza kuwa: Tab'an katika baadhi ya chaguzi kuliwahi kuwasilishwa ripoti ya kutokezea hitilafu fulani katika uchaguzi, na hapo hapo ikatolewa amri ya kufanyika uchunguzi wa kina kuhusu madai hayo na ikathibitika kwamba madai hayo hayakuwa na ukweli wowote. Aidha kumewahi kuwa na maneno ya hapa na pale kuhusiana na kuweko matatizo au hitilafu katika uchaguzi fulani lakini kamwe dosari hizo ndogo ndogo hazijawahi kuwa na taathira hasi katika chaguzi hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kura za wananchi ni haki ya watu kwa maana halisi ya neno na kusisitiza kwamba: Kulindwa kila kura ya mwananchi ni wajibu wa kisheria na Kiislamu na hakuna mtu yeyote aliye na haki ya kupora haki hiyo kama ambavyo matokeo ya kura za wananchi pia ni dhihirisho kamili la haki za watu na kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anayachunga na kuyalinda.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kusimama kidete katika kukabiliana na ung'ang'anizi wa baadhi ya watu walioshikilia kuwa kulifanyika udanganyifu katika uchaguzi wa mwaka 2009, ni mfano bora wa kuwa salama na kuheshimiwa kikamilifu matokeo ya kura za wananchi na kulindwa haki hizo za watu nchini Iran. Ameongeza kuwa: Watu milioni 40 walijitokeza kwa wingi mno katika medani hiyo, hivyo matokeo ya uchaguzi huo bila ya kujali ushindi wa mgombea fulani maalumu, tuliyalinda kikamilifu na hali ni hiyo hiyo kwa chaguzi nyengine zote, ninasimama kidete kulinda matokeo ya kura za wananchi zozote ziwazo na kamwe siruhusu kuingia doa katika jambo hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia matamshi yasiyo ya kimantiki yanayotolewa kuhusiana na Wizara ya Mambo ya Ndani na Baraza la Kulinda Katiba kuhusu uchaguzi na kusisitiza kuwa: Baraza la Kulinda Katiba ndiye mlinzi wa uchaguzi na hilo si jambo la ajabu kwani katika sehemu zote duniani ziko taasisi za namna hiyo japo kwa majina tofauti.
Ameongeza kuwa: Usimamiaji wa Baraza la Kulinda Katiba katika uchaguzi unafanyika kwa ajili ya kuuthibitisha na kuutia nguvu uchaguzi na kazi yenye umuhimu mkubwa ya baraza hilo na usimamiaji wake huo ni sehemu ya kulindwa haki za watu na inabidi jambo hilo lihifadhiwe na liendelee.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia pia udharura wa kuainishwa watu wenye sifa za kugombea katika uchaguzi na kuongeza: Kazi inayofanywa na Baraza la Kulinda Katiba ni kuhakikisha kuwa watu wasio na sifa ambao kwa namna moja au nyengine wanaweza kujiingiza kwenye uchaguzi, wasipate nafasi ya kufanya hivyo na hiyo ni haki ya kisheria, kimantiki na kiakili kabisa ya baraza hilo.
Ayatullah Khamenei amekutaja kushiriki kwa wingi wananchi katika chaguzi mbali mbali nchini Iran kwamba kunadhamini usalama wa nchi na kuongeza kuwa: Bila ya shaka yoyote Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kupata nusra ya Mwenyezi Mungu na kuwashinda maadui wote kutokana na umoja na mshikamano wa taifa la Iran na kujiepusha na migawanyiko.

700 /