Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Adui anataka kubadili itikadi za jamii na kuwa na ushawishi nchini Iran

 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo asubuhi (Jumatano) ameonana na maelfu ya makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kulitaja jeshi hilo kuwa ni neema kubwa ya Mwenyezi Mungu na ni la walinzi waliomacho na wenye welewa mkubwa na ni jicho la Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya ndani na nje ya Iran.
Amebainisha mambo ya lazima na vielelezo vya kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Adui ambaye ana matumaini hewa ya kumalizika Mapinduzi ya Kiislamu, anafikiria kujipenyeza nchini Iran hususan kujipenyeza kisiasa na kiutamaduni. Amesema kuwa, kuzijua vyema njama za adui, kuimarisha na kuitia nguvu roho na moyo wa kimapinduzi na kuendelea na harakati bila ya kusita kuelekea kwenye ufanikishaji wa malengo matakatifu ndiyo mambo ambayo yatazishinda njama hizo za adui.
Katika mkutano huo, Ayatullah  Khamenei amebainisha nafasi muhimu ya watumishi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na majukumu yao hatari hivi sasa na katika mustakbali wa nchi na baada ya hapo ameanza kuchanganua na kutolea ufafanuzi maneno "Sepah - Jeshi," "Pasdaran - Walinzi," "Mapinduzi" na "Kiislamu" pamoja na vipengee, sifa na mambo ya lazima kwa maneno hayo manne ya "Sepahe Pasdarane Enqelabe Islami."
Amesema neno "SEPAH" lina maana ya kuwa na taasisi, muundo, nidhamu na utaratibu mzuri na kuongeza kuwa: Hakuna taasisi wala chombo chochote kilichopewa jukumu la kitaasisi kama ilivyopewa Sepah kwa ajili ya kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu ambayo ni tukio azizi zaidi katika historia ya zamani na ya hivi sasa ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja sifa za Sepah za kutozeeka na kujadidika daima kupitia kustawi, kukua na kuimarika na vile vile kulea vijana wapya, wenye maana na welewa wa mambo kuwa ni katika mambo ya lazima ya taasisi ya Sepah na kuongeza kuwa: Mbali na Sepah yenyewe kulea vijana wake wapya, ina uhusiano pia na watu wengine wanaotoa huduma katika taasisi nyenginezo na inazisaidia pia majimui na taasisi hizo na kulea watu muhimu na wenye ushawishi katika jamii.
Ayatullah  Khamenei amesisitiza pia kuwa, sifa nyengine ya kipekee ya muundo wa kitaasisi wa Sepah ni kupatikana nguvu katika medani, nguvu za kisiasa, utambulisho wa nchi na kuliletea heshima taifa na kuongeza kuwa: Miongoni mwa sifa za muundo wa kitaasisi wa Sepah, ni kuvutia kwake vijana na kustafidi na uzoefu wa nguvu kazi ya zamani na inayotambua vyema majukumu yake na inabidi hali hiyo ilindwe na iendelezwe, ili isije ikatokezea hata mara moja kuweko pengo la kizazi cha hivi sasa na cha zamani ndani ya taasisi hiyo.
Baada ya hapo Ayatullah  Khamenei amechambua maneno "Pasdar - kulinda" na "kuyalinda Mapinduzi" na kusema kuwa maneno hayo ni nembo ya uwepo na utambulizo wa kimapinduzi na kusisitiza kuwa: Wakati tunaposema kuyalinda Mapinduzi tuna maana ya kuwa na irada na nia thabiti ya kimapinduzi isiyosita na Mapinduzi maana yake ni kuendelea kuwa imara na kuwa na nguvu zilizo hai na makini wakati wote kwani kama Mapinduzi hayatakuwa hai, basi hakutakuwa na maana ya kuyalinda.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja kipengee kingine cha maana ya "Kuyalinda Mapinduzi" kuwa ni kutokana na vitisho vinavyoyakabili Mapinduzi hayo na kusisitiza kuwa: Lau kama kusingelikuwa na vitisho dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu, basi kusingelikuwa na ulazima wa kuyalinda, hivyo kwa vile vitisho dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu vipo, inabidi tuvitambue vyema na kukabiliana vilivyo na vitisho hivyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, moja ya majukumu makuu ya Sepah ni kuwa macho wakati wote katika kufuatilia masuala ya ndani, ya kieneo na ya kimataifa kwa lengo la kutambua na kugundua vitisho vinavyoyakabili Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH si taasisi iliyoinamisha kichwa chini na wala si taasisi iliyozongwa na shughuli za kiofisi na kiidara, bali ni mwangalizi aliye macho, anayeona mbali na anayeyajua vizuri masuala ya ndani na ya nje ya nchi.
Ameutaja umuhimu wa kitengo cha usalama na ukusanyaji taarifa cha Sepah kuwa ni mkubwa sana na kuongeza kwamba, kitengo hicho katika taasisi ya Sepah kinapaswa wakati wote na bila ya kusita, kifuatilie na kuangalia kwa karibu na kwa kina vitisho vyote vinavyoyakabili Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja kipengee kingine cha neno "Kulinda Mapinduzi" kwamba ni kuwa macho na makini wakati wote na kusisitiza kuwa: Sisi kamwe hatujawahi na hatutawahi kuwa wa mwanzo wa kuanzisha vita, lakini kwa vile Mapinduzi ya Kiislamu yanakabiliwa na vitisho vya maadui wakati wote, umakini na mwamko wa daima wa Sepah na kuwa kwake tayari kikamilifu wakati wote kwa ajili ya kuyalinda Mapinduizi ya Kiislamu, ni jambo la dharura kabisa.
Ayatullah Khamenei amegusia pia kipengee kingine cha neno "Kulinda Mapinduzi" yaani kuyahifadhi na kuyaenzi Mapinduzi na kusema: Jambo la lazima katika kuyaenzi na kujua umuhimu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ni kuwa na maarifa ya kutosha, yaliyo wazi na ya kila upande kuhusu Mapinduzi hayo na inabidi ihakikishwe kuwa, maarifa na utambuzi wa namna hiyo unakuwepo katika vitengo, daraja na hatua zote za Sepah.
Ameashiria pia kuwa, moja ya njia za kuweza kujipenyeza na kueneza ushawishi wake adui ni kutia shaka katika imani za watu na kuongeza kuwa: Njia ya kuweza kukabiliana na ushawishi na kujipenyeza huko, ni kujiimarisha Sepah na kujipamba kwa mantiki madhubuti ya Mapinduzi ya Kiislamu kupitia kuongeza uwezo wake wa ukinaishaji, mantiki na ubainishaji wa masuala yanayohusiana na Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah  Khamenei amelitaja suala la kumtambua vyema adui kuwa ni kipengee kingine cha "Kulinda Mapinduzi" na kuongeza kwamba: Tunaposema adui tunakusudia uistikbari na ubeberu wa kimataifa, na dhihirisho kamili la ubeberu huo ni Marekani ambapo tawala za kiimla na zenye mawazo finyu pamoja na watu wenye nafsi dhaifu ndio vibaraka wa beberu huyo.
Ameongeza kuwa: Jambo lililo la lazima katika kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu ni kuelewa nukta dhaifu zinazotumiwa na adui na kuwaelimisha watu ambao hadi leo hii hawajawa na welewa unaotakiwa kuhusiana na adui.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza kuzungumzia nukta kadhaa za udhaifu na zenye migongano na za kimsingi za maadui akisema: Maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu ni watu ambao tangu miaka mingi nyuma walizuka na kaulimbiu ya kupigania usalama, kupambana na ugaidi, kuleta demokrasia na kuleta amani katika eneo la Mashariki ya Kati lakini hivi sasa matokeo ya kuweko kwao kwenye eneo hili ni kukosekana amani na kudhihiri ugaidi wa kinyama na wa kikatili mno pamoja na kuwasha moto wa vita katika eneo hili.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Makelele yanayopigwa na Wamarekani ya kuleta demokrasia katika eneo hili hivi sasa yamekuwa ndilo tatizo kubwa na ndiyo nukta ya udhaifu wao kwani leo hii tawala zenye mawazo finyu kabisa na za madikteta wakubwa katika eneo hili, zinaendelea na jinai zao kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye hotuba yake imejikita kwenye kubainisha maneno manne yanayounda ibara ya "Sepahe Pasdarane Enqelabe Islami - Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu" baada ya kubainisha maana ya maneno ya "Sepah" na "Pasdar" ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia maana halisi ya neno Mapinduzi.
Amesema, maana ya Mapinduzi halisi, Mapinduzi ya kubakia milele na ya kudumu ni kuwa Mapinduzi hayo na sifa isiyosita ya kunawiri, kubadilika na kuimarika. Ameongeza kuwa: Tofauti na madai na fikra za madola ya kibeberu madai ambayo kuna watu wanayakariri pia humu nchini; Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran si kitu kinachoweza kwisha au kubadilika kuwa Jamhuri ya Kiislamu kwa maana wanayoifikiria wao maadui.
Ayatullah  Khamenei, amelitaja suala la kuchorwa malengo matukufu na ya kimsingi kuwa ni hatua ya kwanza kabisa iliyochukuliwa na Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Msingi na malengo makuu matukufu kamwe hayabadiliki, tofauti na njia na mbinu za kufanikishia malengo hayo hubadilika kulingana na wakati na mazingira.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametumia matamshi na ibara ya Qur'ani Tukufu kutolea ufafanuzi na maana ya malengo matukufu akisema kuwa ndiyo hayo yanayoitwa maisha mema na Qur'ani Tukufu. Ameongeza kuwa: Maisha mema yanajumuisha masuala yote ambayo taifa fulani linayahitajia kwa ajili ya kupata ufanisi na saada ya kweli.
Amesema, heshima ya taifa; istikilali kwa maana ya kujikomboa taifa kutokana na dhulma, ukandamizaji na kudhibitiwa na madola ya kibeberu duniani; kupiga hatua za kimaendeleo na umaanawi katika elimu na ustaarabu wa kimataifa; kuwa na uadilifu, ustawi, ubunifu wa Kiislamu pamoja na kuishi katika mtindo wa maisha wa Kiislamu ni miongoni mwa sifa za maisha bora na kuongeza kuwa, kufanya harakati kuelekea kwenye jamii inayokusudiwa na Uislamu, kuwa na harakati ya kudumu na kwa hakika kuwa na mageuzi na mabadiliko ya kudumu kuelekea kwenye kujikurubisha kwa Mola Muumba ni miongoni mwa sifa za maisha hayo bora.
Amelitaja suala la kuwa na imani ya Mwenyezi Mungu na kumkufuru taghuti kuwa ni sifa nyengine ya kipekee ya maisha ya furaha na kuongeza kwamba: Wamagharibi katika propaganda zao ambazo hata ndani ya Iran kuna baadhi ya watu wanazikariri; wanadai kuwa wananchi wa Iran wameanza pole pole kuacha kuwachukia mabeberu na kwamba si lazima kila mtu anayemwamini Mwenyezi Mungu amkufuru pia taghuti, lakini kuwa na imani na Mwenyezi Mungu na kumkufuru taghuti ni sifa moja ya kipekee iliyoshikamana vizuri katika maisha mema yaliyokusudiwa na Qur'ani Tukufu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kujaribu kuitoa aidiliolojia katika udiplomasia na siasa za ndani ya nchini ni mhimili mwengine wa propaganda za sasa hivi za Wamagharibi na kusisitiza kuwa: Wanatutaka tusiingize misingi yetu mikuu katika siasa za nje, lakini uhakika wa mambo ambao wanajaribu kuukwepa ni kuwa, fikra na akida na aidiolojia ni muongozo muhimu mno katika nyuga zote.
Ayatullah Khamenei ameendelea kubainisha migongano ya dhati katika misimamo ya maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu na ambayo imekuwa ikikaririwa sana katika kipindi cha hivi karibuni. Amesema, maadui katika upande mmoja wanasema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ina nguvu, ushawishi na taathira kubwa katika eneo hili na katika upande wa pili wanatutaka tuachane na moyo na fikra ya kimapinduzi kama tunataka kuivutia na kuiridhisha jamii ya kimataifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mambo hayo mawili yanagongana kwani nguvu na ushawishi wetu unatokana na kuwa na moyo na misimamo ya kimapinduzi na ni jambo lililo wazi kuwa kama tutaachana na moyo na misimamo hiyo, basi tutadhoofika.
Ameongeza kuwa: Lengo na shabaha kuu ya maadui ni kuliona taifa la Iran linaachana na fikra ya kimapinduzi ili lipoteze nguvu zake na limezwe na kudhibitiwa ndani ya makucha ya madola machache ya kibeberu ambayo yamejipachika jina la jamii ya kimataifa.
Baada ya kujadili vipengee tofauti vya neno "Mapinduzi," Ayatullah Udhma Khamenei ameanza kubainisha sifa maalumu za neno la nne linalounda istilahi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, yaani Uislamu.
Amesisitiza kuwa: Uislamu ndio msingi na ndiyo chemchemu na nguzo kuu ya Mapinduzi (ya nchini Iran). Hata hivyo kuna baadhi ya watu wanaogopa kusikia tu neno Uislamu na badala ya kusema Mapinduzi ya Kiislamu utawasikia wanasema Mapinduzi ya mwaka 1979.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Uislamu asili umeenea kwenye kila kipengee ya Mapinduzi (ya nchini Iran) na amekosoa vikali fikra za kimaamuma, potofu na za kipumbavu na makundi ya kitakfiri akiongeza kuwa: Uislamu umesimama juu ya msingi wa akili na nukulu na kwamba Qur'ani na mafundisho ya Bwana Mtume na Ahlul Bayt Alayhimus Salaam ndio msingi wa Mapinduzi yetu msingi ambao unaweza kutangazwa na kutetewa katika nyuga na sehemu zote duniani kwa mantiki ya hali ya juu.
Ayatullah Khamenei amegusia pia ushawishi na namna Mapinduzi ya Kiislamu yalivyoweza kupenya kwenye fikra na nyoyo za mataifa ya Waislamu duniani na kusisitiza kuwa: "Uislamu unaoishia kwenye vitendo vya mtu binafsi tu," "Uislamu wa kisekula" na "Uislamu usio na fikra ya jihadi wala shahada" na wala usio na suala la kuamrishana mema na kukatazana mabaya, kamwe hauwezi kukubaliwa na taifa la Iran na kwamba Uislamu wa kimapinduzi unaweza kuonekana waziwazi katika Qur'ani Tukufu na kwenye wasia wa Imam (Khomeini) rahimahullah na katika hotuba na maandishi yake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa muhtasari wa matamshi yake hadi hapo kwa kuwakhutubu askari wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH akiwasisitizia kwa kuwaambia: Nyinyi ni Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa maana na mafuhumu hiyo pana na ya kina na mnapaswa muendelee na kazi yenu ya ulinzi kwa kuwa macho kikamilifu na kwa uwezo na nguvu zenu zote.
Vilevile ameyakosoa matamshi na maandishi ambayo kwa kujua au kutojua yanajaribu kulidhoofisha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni neema kubwa ya Mwenyezi Mungu na kila mmoja wetu anapaswa kujua thamani ya neema hiyo.
Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kujua thamani ya kuwepo jeshi la Sepah kuwa linapaswa kuwemo ndani ya jeshi hilo kabla ya sehemu nyingine yoyote na amewasisitizia hadhirina akiwaambia: Kujiimarisha kila leo kimaanawi, kifikra na kivitendo, kujiepusha kikamilifu na suala la kutafuta visingizio na kuwalaumu wengine, kujiweka mbali kikamilifu na masuala ambayo yanaweza kutia doa heshima ya Sepah na kufanya harakati ndani ya njia iliyonyooka ya Mapinduzi ya Kiislamu katika nyuga za kiuchumi, kifedha na kisiasa ndiyo hadhi na shakhshia ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na mnapaswa kujua thamani ya jambo hilo na kuilinda.
Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia udharura wa kuzingatia kikamilifu Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu vitisho vyote vinavyoikabili Iran na kuongeza kuwa: Njama za adui za kutaka kujipenyeza ni moja ya vitisho vikubwa vinavyolikabili taifa la Iran.
Ameongeza kuwa: Kujipenyeza kiuchumi na kiusalama ndiyo hatari kubwa zaidi yenye madhara makubwa, lakini kujipenyeza adui kisiasa na kiutamaduni ndiyo hatari kubwa zaidi ambayo kila mtu nchini Iran anapaswa kuwa macho mbele ya hatari hiyo.
Ayatullah Ali Khamenei amekumbushia pia hatari inayotokana na uwekezaji mkubwa wa maadui kwa ajili ya kujipenyeza kiutamaduni na kubadilisha pole pole imani za wananchi wa Iran na kuongeza kuwa: Katika upande wa kisiasa pia, mabeberu wanafanya njama za kujipenyeza kwenye vituo vikuu vya uchukuaji maamuzi nchini na kama watashindwa, basi wajipenyeze kwenye vituo vikuu vya utengenezaji maamuzi na iwapo njama hiyo itafanikiwa, basi misimamo, maamuzi na harakati ya umma nchini Iran itakuwa inapangiliwa na kutekelezwa kwa mujibu wa matakwa na maamuzi ya mabeberu, suala ambalo ni hatari sana kwa taifa.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia udharura wa kuweko mwamko wa wananchi wote mbele ya njama na hila za maadui na kuongeza kuwa: Maadui wanasubiri taifa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ichukuliwe na usingizi ili wapate kufanikisha malengo yao, lakini taifa na viongozi wa Iran kamwe hawatoruhusu hilo kutokea na kwamba ndoto za kishetani za mabeberu kuhusiana na kulala wananchi na taifa la Iran, zitabakia vivyo hivyo bila ya kuaguliwa.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Inabidi misingi ya kifikra na moyo wa kimapinduzi uwe mkubwa na imara kiasi kwamba kusiwe na kitu chochote kitakachoweza kutia doa katika harakati ya kuendelea na njia hiyo inayong'aa na kwamba watu wote wenye vipaji ndio wenye jukumu kubwa zaidi katika suala hilo la kimsingi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia umuhimu na nafasi ya mwezi wa Mfunguo Tatu, Dhulhija, na kuwataka wananchi wote kujinufaisha kimaanawi na saa na siku muhimu za mwezi huu mtukufu hususan siku kubwa ya Arafa. Amesema: Inabidi tujue vizuri thamani ya siku ya Arafa na tusome dua za siku hiyo zenye maana pana na za kina, kwa taamuli na mazingatio makubwa na ili tupate matayarisho mazuri ya kuingia katika njia nzito na ya muda mrefu ya maisha na kuweza kupata nguvu na nishati inayotakiwa kwa ajili ya kuendelea na harakati katika njia hiyo.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Saidi, mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyyul Faqih) katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Sepah ametoa ripoti fupi kuhusiana na hatua za kiutamaduni zilizochukuliwa hadi hivi sasa na jeshi hilo.
Vilevile Meja Jenerali Muhammad Ali Jaafari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amegusia kupatikana nusra ya Mwenyezi Mungu katika medani mbali mbali za muqawama katika kona zote za eneo la Mashariki ya Kati na kusema kwa kusisitiza kuwa: Tutalinda vilivyo misingi, matukufu na mafanikio yote ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa nguvu zetu zote na kamwe hatutatoa nafasi kwa wapinzani wa njia hii ya Mwenyezi Mungu kufungua njia ya kupenya ushawishi wa maadui nchini.
Meja Jenerali Jaafari amegusia pia mikakati mipya ya maadui ya kutaka kujipenyeza nchini Iran na kukumbusha kuwa: Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Sepah linaamini kwamba katika kupambana na hila na njama mpya za maadui, jeshi hilo linapaswa kuongeza uwezo na umakini wa kupiga shabaha wa makombora yake, kuongeza jitihada za kufanikisha malengo matakatifu ya Uislamu na kuchunga vigezo vinavyotakiwa na Mapinduzi ya Kiislamu.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tunatangaza kwa kujiamini kwamba, hakuna wakati wowote ambapo Iran ya Kiislamu imewahi kuwa na nguvu na uwezo wa kiulinzi na kiusalama na vikosi vilivyo imara na vilivyo tayari kufanya kazi na kutekeleza vilivyo majukumu yake katika nyuga tofauti za kijamii kama ilivyo leo hii.
 
700 /