Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Baada ya maafa ya Mina, Kiongozi Muadhamu atangaza situ tatu za maombolezo ya taifa, asema:

Serikali ya Saudi Arabia inapaswa kubeba dhima kubwa ya tukio hilo chungu

Kufuatia maafa yaliyosababisha msiba mkubwa hii leo huko Mina, Saudi Arabia, ambapo idadi kubwa ya Wageni wa Mwenyezi Mungu wameaga dunia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ametoa ujumbe akieleza mshikamano wake na watu waliopatwa na msiba katika tukio hilo la kusikitisha na kutoa mkono wa taazia kwa familia zao. Amesisitiza kuwa: Serikali ya Saudi Arabia inawajibika kukubali jukumu lake zito katika tukio hili chungu na kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni za haki na insafu, sambamba na kutilia maanani uendeshaji mbaya na hatua zisizofaa zilizosababisha maafa haya.
Vilevile Ayatullah Ali Khamenei ametangaza siku tatu za maombolezo ya taifa nchini Iran.
Ujumbe kamili wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni huu ufuatao:
Bismillahir Rahmanir Rahim
Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake Yeye tutarejea.
Maafa yaliyosababisha msiba mkubwa leo huko Mina ambapo idadi kubwa ya Wageni wa Rahman na waumini waliohajiri kwenda kwa Mwenyezi Mungu kutoka nchi mbalimbali wameaga dunia, yamesababisha huzuni kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu na kuibadili sikukuu ya Idi kuwa maombolezo. Katika nchi yetu azizi pia makumi ya familia zilizokuwa zikisubiri kwa shauku kubwa ndugu zao wapendwa waliokwenda kuhiji, sasa zinaomboleza vifo vyao.
Kwa moyo uliojaa huzuni na mshikamano na waliopatwa na maafa, ninatoa mkono wa taazia kwa roho iliyotakasika ya Mtume Mtukufu (saw) na kwa Walii Mkubwa wa Mwenyezi Mungu, Imam wa Zama (roho zetu ziwe mhanga kwake) ambaye ndiye haswa mwenye msiba huu, na kwa jamaa wote wa wahanga na waombolezaji wote kote duniani, hususan nchini Iran kutokana na tukio hili la kuhuzunisha.
Ninawaombea wageni hawa wa Rahmani rehma makhsusi za Mwenyezi Mungu Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu na Mwenye kushukuru. Vilevile nawaombea shufaa ya haraka waliopatwa na madhara na majeruhi wa tukio hilo.
Ninapenda kukumbusha mambo kadhaa:
1- Maafisa wa ofisi ya mwakilishi wangu na Jumuiya ya Hija ambao kutwa nzima wamekuwa wakifanya jitihada kubwa za kutambua waliofariki dunia, kutibu majeruhi, kuwarejesha nchini na kupasha habari haraka, wanapaswa kuendelea na kazi hizo, na watu wote wenye uwezo wanawajibika kuwasaidia.
2- Maafisa hao wanapaswa pia kutoa msaada kwa mahujaji wa nchi nyingine na kutekeleza haki ya udugu wa Kiislamu.
3- Serikali ya Saudi Arabia inawajibika kukubali jukumu lake zito katika tukio hilo chungu na kutenda kwa mujibu wa haki na insafu. Uendeshaji mbaya na hatua zisizofaa zilizosababisha maafa haya pia zinapaswa kutiliwa maanani.
4- Waliofariki dunia katika tukio hili Inshaallah watakuwa kielelezo cha maneno haya yenye nuru ya Qur’ani inayosema: “Na mwenye kutoka nyumbani kwake ili kuhamia kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti basi yamethibiti malipo yake kwa Mwenyezi Mungu..”; suala hili ni pozo na tulizo kubwa kwa wafiwa. Mahujaji hao wamekimbilia kwa Mola wao baada ya kufanya twawafu, kufanya saayi (baina ya Swafa na Marwa) na baada ya masaa yenye baraka tele ya kusimama Arafa na Mash’ar wakiwa katika kutekeleza amali nyingine za Hija; na Inshaallah watapata rehma za Mwenyezi Mungu.
Ninatoa tena mkono wa pole kwa waliopatwa na msiba na ninatangaza siku tatu za maombolezo ya taifa hapa nchini.
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Sayyid Ali Khamenei
02/ Mehr/1394 (24/09/15)        
   

700 /