Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kuna ulazima wa kuundwa kamati ya kuchunguza tukio la Mina

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran asubuhi ya leo (Jumatano) amehudhuria shughuli ya kuapishwa na kupandishwa vyeo wanafunzi wa vyuo vikuu vya maafisa wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Chuo Kikuu cha Masuala ya Jeshi la Majini cha Imam Khomeini huko Bushehr, kusini mwa Iran.
Ayatullah Khamenei ameashiria tukio la kusikitisha la Mina huko Saudi Arabia na kusema tukio hilo ni msiba halisi kwa taifa la Iran kutokana na kufariki dunia maelfu ya mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu hususan mamia ya mahujaji wa Kiirani. Ameashiria udharura wa kuundwa kamati ya kutafuta ukweli kuhusu tukio hilo itakayoshirikisha nchi za Kiislamu ikiwemo Iran na kusema: Serikali ya Saudi Arabia haitekelezi majukumu yake katika suala la kusafirisha miili mitoharifu ya mahujaji wa Iran waliofariki dunia na hadi sasa Jamhuri ya Kiislamu imelinda heshima ya udugu katika ulimwengu wa Kiislamu kwa kuonesha uvumilivu na adabu ya Kiislamu; lakini pia wanapaswa kutambuwa kwamba, utovu wa heshima wa aina yoyote ile kwa makumi ya maelfu ya mahujaji wa Iran walioko Makka na Madina na kutotekeleza majukumu yao kwa ajili ya kusafirisha miili mitoharifu ya mahujaji wa Iran kutakabiliwa na jibu kali na la kuumiza.
Ameashiria vifo vya kidhulma vya wahujaji walioaga dunia wakiwa na kiu katika tukio la Mina na vilevile makiwa ya familia zao zilizokuwa zikiwasubiri kwa hamu kubwa na akasema: Hadi sasa idadi kamili ya mahujaji wa Iran waliofariki dunia katika tukio hilo haijulikani na kuna uwezekano idadi hiyo ikaongezeka kwa mamia ya watu wengine, na kwa hakika tukio hili ni msiba mkubwa kwa taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amezungumzia baadhi ya ripoti zinazosema, kuna uwezekano mahujaji zaidi ya elfu tano wamefariki dunia katika tukio la Mina na kusema: Wakati Qur’ani Tukufu inasema kuwa Nyumba ya Mwenyezi Mungu ni eneo la usalama na inaitambua ibada ya Hija kuwa ni mahala pa amani na usalama inatupasa kuuliza kwamba je, huu ndio usalama?
Ayatullah Khamenei ametilia mkazo udharura wa kuundwa kamati ya kutafuta ukweli itakayoshirikisha nchi za Kiislamu ikiwemo Iran na kuongeza kuwa: Kwa sasa hatutaki kutoa hukumu mapema kuhusu sababu za tukio hilo lakini tunaamini kuwa, serikali ya Saudi Arabia haikutekeleza majukumu yake kuhusu majeruhi wa tukio hilo la Mina na iliwaacha hivihivi wakiwa na kiu.
Ameashiria matatizo yaliyojitokeza katika kusafirisha miili mitoharifu ya mahujaji waliofariki dunia huko Mina na juhudi zinazoendelea kufanywa na maafisa husika wa Iran na amesisitiza ulazima wa kudumishwa jitihada hizo. Amesema katika suala hili serikali ya Saudi Arabia haitekelezi wajibu na majukumu yake na wakati mwingine inafanya maudhi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: Hadi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonesha uvumilivu na kulinda adabu za Kiislamu na heshima ya udugu katika ulimwengu wa Kiislamu, lakini pia inapasa kueleweka kwamba, mkono wa Iran una nguvu kuliko wengi na una suhula nyingi zaidi, na kama itataka kutoa jibu kwa wale wanaofanya maudhi basi hali yao haitakuwa nzuri na hawataweza mpambano katika medani yoyote ile.
Ayatullah Khamenei amesema jibu la Iran ya Kiislamu litakuwa kali na la kuumiza na kuongeza kuwa: Katika kipindi cha vita vya miaka 8 ya kujihami kutakatifu (vita vya Saddam dhidi ya Iran), madola ya mashariki na magharibu na nchi jrani zilimsaidia mtu habithi na muovu lakini hatimaye wote walipata kipigo na kwa msingi huo wanaitambua Iran na kama hawaitambua basi sasa wanapaswa kuijua vyema.
Ameashiria makumi ya maelfu ya mahujaji wa Iran walioko Makka na Madina na kutahadharisha kuwa, kitendo chochote kile cha kuwavunjia heshima mahujaji wa Kiirani na vilevile serikali ya Saudi Arabia kutotekeleza majukumu yake kuhusu miili mitoharifu ya mahujaji waliofariki dunia kitafuatiwa na jibu la Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Jamhuri ya Kiislamu si dhalimu lakini pia haikubali kudhulumiwa na yeyote, kwa msingi huo hainyooshei mkono haki ya mtu au taifa lolote sawa liwe la Waislamu au la, lakini kama mtu atataka kuchukua haki za taifa na nchi ya Iran, atakabiliwa na jibu kali, na kwa rehma zake Mwenyezi Mungu uwezo huo upo na taifa la Iran liko imara na madhubuti.  
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Ayatullah Khamenei amesema mambo matatu ambayo ni ‘imani kubwa’, ‘ushujaa’ na ‘elimu’ yana umuhimu katika kuunda utambulisho wa jeshi. Ameongeza kuwa: Kama hakutakuwepo imani katika jeshi basi kutajitokeza moyo wa kukandamiza na kuua dhaifu, na kama hakutakuwepo ushujaa, jeshi halitaweza kutekeleza majukumu yake wakati wa hatari, na kama hakutakuwepo elimu na ujuzi, zana za jeshi zitakuwa butu mbele ya zana za upande wa pili.
Amesema kuwa mashambulizi yanayofanywa dhidi ya nyumba za raia, masoko na hata sherehe za harusi huko Yemen ni kielelezo cha kuua na kukandamiza watu dhaifu na ukosefu wa moyo wa ushujaa katika jeshi. Amewaagiza vijana wa jeshi la Iran kuimarisha imani, ushujaa na uvumbuzi katika uhakiki na elimu na akasema: Hii leo mfumo wa Kiislamu hapa nchini unahitaji suhula na zana ngumu na laini za kivita kwa sababu dunia ya sasa inayodhibitiwa na nguvu ya shetani ni hatari sana kwa watu wanaofuata mafundisho ya Mwenyezi Mungu na kwa hivyo kuna udharura wa kijizatiti na kuwa tayari siku zote.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa sababu kuu ya uadui wa madola ghasibu duniani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na taifa shukaa na la kimapinduzi ya Iran ni kusimama imara kwa taifa hilo mbele yao, kulinda kwake utambulisho na misingi yake na kutoyeyuka katika mifumo ya kibeberu. Ameongeza kuwa: Kuwa tayari kwa vikosi vya jeshi kuanzia Jeshi la Iran, Sepah, vikosi vya kijitolea vya wananchi na kadhalika hakuna maana ya kuwa tayari kwa ajili ya kupata ushindi mbele ya adui tu bali utayarifu huo unapaswa pia kujumuisha kujihami na kujilinda.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia vitisho vinavyotolewa na madola ya kibeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na akasema: Katika kipindi chote cha miongo minne ya Mapinduzi ya Kiislamu hususan kipindi cha miaka 8 ya kujihami kutakatifu, taifa la Iran limeonesha kuwa lina nguvu, uwezo na utambulisho na linasimama imara kupambana na wanaolitakia mabaya.
Amesisitiza kuwa, taifa la Iran limethibitisha kuwa, ni ngangari, hodari na lenye kuona mbali katika kukabiliana na mabeberu na linaheshimu utambulisho wake na wanadamu. Ameongeza kuwa linasimama kidete mbele ya ubeberu na kuheshimu wanadamu na mataifa yote.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hali ya maadui na kusema, daima ngumi imara ya wanadamu wenye imani inaweza kuwalazimisha kurudi nyuma.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia vijana wa jeshi la Iran kudurusu kwa makini masuala ya kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu, mipango ya operesheni za kijeshi na kutembelea maeneo ya vita kwa mtazamo wa kijeshi na vilevile kustafidi na uzoefu wa wakongwe wa medani hiyo. Amewaambia: Mnapaswa kuwa ngome imara ya nchi na utawala wa Kiislamu kwa maana halisi ya neno hilo.
Mwanzoni mwa shughuli hiyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehudhuria kwenye makumbusho ya mashahidi na kutoa heshima kwa mashujaa hao. Baada ya hapo Amir Jeshi Mkuu amekagua gwaide la vikosi vya jeshi vilivyokuwa hapo.   
                           
 
       

700 /